1 Wathesalonike 5:5-11
1 Wathesalonike 5:5-11 Biblia Habari Njema (BHN)
Nyinyi nyote ni watu mnaoishi katika mwanga, watu wa mchana. Sisi si watu wa usiku, wala wa giza. Basi, tusilale usingizi kama wengine; tunapaswa kukesha na kuwa na kiasi. Wanaolala hulala usiku, na walevi hulewa usiku. Lakini sisi ni watu wa mchana na tunapaswa kuwa na kiasi. Tunapaswa kuvaa imani na upendo kama vazi la kujikinga kifuani, na tumaini letu la wokovu kama kofia ya chuma. Maana Mungu hakututeua ili tuangamizwe na ghadhabu yake, bali tuupate wokovu kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo ambaye alikufa kwa ajili yetu, ili tuishi pamoja naye, iwe tu hai au tumekufa. Kwa hiyo farijianeni na kusaidiana nyinyi kwa nyinyi, kama mnavyofanya sasa.
1 Wathesalonike 5:5-11 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Kwa kuwa ninyi nyote mmekuwa wana wa nuru, na wana wa mchana; sisi si wa usiku, wala wa giza. Basi tusilale usingizi kama wengine, bali tukeshe, na kuwa na kiasi. Maana walalao usingizi hulala usiku, pia na walewao hulewa usiku. Lakini sisi tulio wa mchana, tuwe na kiasi, hali tukijivika kifuani imani na upendo, na chapeo yetu iwe tumaini la wokovu. Kwa kuwa Mungu hakutuweka ili tupate hasira yake, bali ili tupate wokovu, kwa Bwana wetu Yesu Kristo; ambaye alikufa kwa ajili yetu, ili tuishi pamoja naye, iwe tunakesha au tunalala. Basi, farijianeni na kujengana kila mtu na mwenzake, hakika kama mnavyofanya.
1 Wathesalonike 5:5-11 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Kwa kuwa ninyi nyote mmekuwa wana wa nuru, na wana wa mchana; sisi si wa usiku, wala wa giza. Basi tusilale usingizi kama wengine, bali tukeshe, na kuwa na kiasi. Maana walalao usingizi hulala usiku, pia na walewao hulewa usiku. Lakini sisi tulio wa mchana, tuwe na kiasi, hali tukijivika kifuani imani na upendo, na chapeo yetu iwe tumaini la wokovu. Kwa kuwa Mungu hakutuweka kwa hasira yake, bali tupate wokovu, kwa Bwana wetu Yesu Kristo; ambaye alikufa kwa ajili yetu, ili tuishi pamoja naye, kwamba twakesha au kwamba twalala. Basi, farijianeni na kujengana kila mtu na mwenzake, vile vile kama mnavyofanya.
1 Wathesalonike 5:5-11 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Ninyi nyote ni wana wa nuru na wana wa mchana. Sisi si wana wa giza wala wa usiku. Kwa hiyo basi, tusilale kama watu wengine wanavyolala, bali tukeshe na kuwa na kiasi. Kwa kuwa wote wanaolala, hulala usiku, na wale wanaolewa, hulewa usiku. Lakini kwa kuwa sisi ni wana wa mchana, basi tuwe na kiasi, tukijivika imani na upendo kama dirii kifuani na tumaini letu la wokovu kama chapeo. Kwa maana Mungu hakutuita ili tupate ghadhabu bali tupate wokovu kupitia kwa Bwana wetu Yesu Kristo. Yeye alikufa kwa ajili yetu ili hata kama tuko macho au tumelala, tupate kuishi pamoja naye. Kwa hiyo farijianeni na kujengana, kama vile mnavyofanya sasa.