1 Wathesalonike 4:1-13
1 Wathesalonike 4:1-13 Biblia Habari Njema (BHN)
Hatimaye, ndugu zangu, mmejifunza kutoka kwetu namna mnavyopaswa kuishi ili kumpendeza Mungu. Na kweli mmekuwa mnaishi hivyo. Sasa tunawaombeni na kuwasihi kwa jina la Bwana Yesu mfanye vema zaidi. Maana mnayajua yale maagizo tuliyowapeni kwa mamlaka ya Bwana Yesu. Mungu anataka nyinyi muwe watakatifu na mjiepushe kabisa na maisha ya zinaa. Kila mwanamume anapaswa kujua namna ya kuishi na mkewe kwa utakatifu na heshima, na si kwa tamaa mbaya kama watu wa mataifa mengine wasiomjua Mungu. Basi, mtu yeyote asimkosee au kumpunja mwenzake kuhusu jambo hili. Tulikwisha waambieni hayo na kuwaonya kwamba Bwana atawaadhibu wanaofanya mambo hayo. Mungu hakutuita tuishi maisha ya zinaa, bali tuishi katika utakatifu. Kwa hiyo basi, anayedharau mafundisho hayo hamdharau mtu, bali anamdharau Mungu mwenyewe anayewapeni Roho wake Mtakatifu. Hakuna haja ya kuwaandikieni juu ya kuwapenda ndugu zenu waumini. Nyinyi wenyewe mmefundishwa na Mungu namna mnavyopaswa kupendana. Na mmekuwa mkiwatendea hivyo ndugu zenu wote kila mahali katika Makedonia. Basi, ndugu, tunawaombeni mfanye hata zaidi. Muwe na nia ya kuishi maisha ya utulivu, kila mmoja ashughulikie mambo yake mwenyewe na afanye kazi kwa mikono yake mwenyewe kama tulivyowaagiza pale awali. Kwa namna hiyo mtajipatia sifa nzuri kutoka kwa wale wasio Wakristo, na hamtakuwa na lazima ya kuwategemea wengine kwa mahitaji yenu. Ndugu, twataka mjue ukweli kuhusu wale ambao wamekwisha fariki dunia, ili msipatwe na huzuni kama watu wengine wasio na matumaini.
1 Wathesalonike 4:1-13 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Iliyobaki, ndugu, tunawasihi na kuwaonya kwamba mwenende katika Bwana Yesu; kama mlivyopokea kwetu jinsi iwapasavyo kuenenda na kumpendeza Mungu, kama nanyi mnavyoenenda, vivyo hivyo mpate kuzidi sana. Kwa kuwa mnajua ni maagizo gani tuliyowapa kwa Bwana Yesu. Maana haya ndiyo mapenzi ya Mungu, kutakaswa kwenu, mwepukane na uasherati; kila mmoja wenu ajue kuuweza mwili wake katika utakatifu na heshima; si katika hali ya tamaa mbaya, kama Mataifa wasiomjua Mungu. Mtu asimpunje ndugu yake wala kumkosea katika jambo hili; kwa sababu Bwana ndiye alipizaye kisasi cha haya yote; kama tulivyowaambia kwanza, tukashuhudia sana. Maana Mungu hakutuitia uchafu, bali tuwe katika utakaso. Basi yeye anayekataa, hakatai mwanadamu bali Mungu, anayewapa ninyi Roho wake Mtakatifu. Kuhusu upendano, hamna haja niwaandikie; maana ninyi wenyewe mmefundishwa na Mungu kupendana. Kwa maana mnafanya neno hili kwa ndugu wote walio katika Makedonia yote. Lakini tunawasihi, ndugu, mzidi sana. Tena mjitahidi kutulia, na kutenda shughuli zenu, na kufanya kazi kwa mikono yenu wenyewe, kama tulivyowaagiza; ili mwende kwa adabu mbele yao walio nje, wala msiwe na haja ya kitu chochote. Lakini, ndugu, hatutaki msijue habari zao waliolala mauti, msije mkahuzunika kama na wengine wasio na matumaini.
1 Wathesalonike 4:1-13 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Iliyobaki, ndugu, tunakusihini na kuwaonya kwamba mwenende katika Bwana Yesu; kama mlivyopokea kwetu jinsi iwapasavyo kuenenda na kumpendeza Mungu, kama nanyi mnavyoenenda, vivyo hivyo mpate kuzidi sana. Kwa kuwa mnajua ni maagizo gani tuliyowapa kwa Bwana Yesu. Maana haya ndiyo mapenzi ya Mungu, kutakaswa kwenu, mwepukane na uasherati; kila mmoja wenu ajue kuuweza mwili wake katika utakatifu na heshima; si katika hali ya tamaa mbaya, kama Mataifa wasiomjua Mungu. Mtu asimpunje ndugu yake wala kumkosa katika jambo hili; kwa sababu Bwana ndiye alipizaye kisasi cha haya yote; kama tulivyowaambia kwanza, tukashuhudia sana. Maana Mungu hakutuitia uchafu, bali tuwe katika utakaso. Basi yeye anayekataa, hakatai mwanadamu bali Mungu, anayewapa ninyi Roho wake Mtakatifu. Katika habari ya upendano, hamna haja niwaandikie; maana ninyi wenyewe mmefundishwa na Mungu kupendana. Kwa maana mnafanya neno hili kwa ndugu wote walio katika Makedonia yote. Lakini twawasihi, ndugu, mzidi sana. Tena mjitahidi kutulia, na kutenda shughuli zenu, na kufanya kazi kwa mikono yenu wenyewe, kama tulivyowaagiza; ili mwenende kwa adabu mbele yao walio nje, wala msiwe na haja ya kitu cho chote. Lakini, ndugu, hatutaki msijue habari zao waliolala mauti, msije mkahuzunika kama na wengine wasio na matumaini.
1 Wathesalonike 4:1-13 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Na kuhusu mambo mengine, ndugu, tuliwafundisha jinsi ya kuishi ili kumpendeza Mungu, kama vile mnavyoishi. Sasa tunawaomba na kuwasihi katika Bwana Yesu mfanye hivi zaidi na zaidi. Kwa kuwa mnajua maagizo tuliyowapa kwa mamlaka ya Bwana Yesu. Mapenzi ya Mungu ni ninyi mtakaswe, ili mjiepushe na uasherati, na kila mmoja wenu ajifunze kuutawala mwili wake mwenyewe katika utakatifu na heshima, bali si kwa tamaa mbaya kama watu wa Mataifa wasiomjua Mungu. Katika jambo hili mtu asimkosee ndugu yake wala kumlaghai. Kwa kuwa Bwana ni mlipiza kisasi katika mambo haya yote, kama vile tulivyokwisha kuwaambia mapema na kuwaonya vikali. Kwa maana Mungu hakutuitia uchafu, bali utakatifu. Kwa hiyo, mtu yeyote anayekataa mafundisho haya hamkatai mwanadamu, bali anamkataa Mungu anayewapa ninyi Roho wake Mtakatifu. Sasa kuhusu upendo wa ndugu hamna haja mtu yeyote kuwaandikia, kwa maana ninyi wenyewe mmefundishwa na Mungu kupendana. Nanyi kwa kweli mnawapenda ndugu wote katika Makedonia nzima. Lakini ndugu, tunawasihi mzidi sana kuwapenda. Jitahidini kuishi maisha ya utulivu, kila mtu akijishughulisha na mambo yake mwenyewe na kufanya kazi kwa mikono yake, kama vile tulivyowaagiza, ili maisha yenu ya kila siku yajipatie heshima kutoka kwa watu walio nje, ili msimtegemee mtu yeyote. Lakini ndugu, hatutaki mkose kujua kuhusu wale waliolala katika mauti, ili msihuzunike kama watu wengine wasiokuwa na tumaini.