1 Wathesalonike 3:6-13
1 Wathesalonike 3:6-13 Biblia Habari Njema (BHN)
Sasa Timotheo amekwisha rudi, naye ametupa habari za kufurahisha kuhusu imani na upendo wenu. Ametuarifu kwamba mnatukumbuka daima, na kwamba mna hamu ya kutuona sisi kama nasi tulivyo na hamu ya kuwaoneni. Basi, habari za imani yenu zimetutia moyo katika taabu na mateso yetu yote, kwani sasa tunaishi kweli ikiwa nyinyi mnasimama imara katika kuungana na Bwana. Sasa tunaweza kumshukuru Mungu wetu kwa ajili yenu. Tunamshukuru kwa furaha tuliyo nayo mbele yake kwa sababu yenu. Tunazidi kumwomba Mungu usiku na mchana kwa moyo wetu wote ili atupatie fursa ya kuwaoneni uso kwa uso ili tuweze kurekebisha chochote kilichopungua katika imani yenu. Tunamwomba Mungu, Baba yetu mwenyewe, na Bwana wetu Yesu, atutayarishie njia ya kuja kwenu. Bwana awawezeshe nyinyi kupendana na kuwapenda watu wote zaidi na zaidi, kama vile sisi tunavyowapenda nyinyi. Hivyo ataiimarisha mioyo yenu, nanyi mtakuwa wakamilifu na watakatifu mbele ya Mungu na Baba yetu wakati Bwana wetu Yesu atakapokuja pamoja na wote walio wake.
1 Wathesalonike 3:6-13 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Lakini Timotheo alipotujia hivi sasa kutoka kwenu, alituletea Habari Njema za imani yenu na upendo wenu, na ya kwamba mnatukumbuka vema siku zote; mkitamani kutuona kama vile nasi tunavyotamani kuwaona ninyi. Kwa sababu hiyo, ndugu, katika dhiki na mateso yetu yote, katika habari zenu, tumefarijiwa kwa imani yenu. Kwa kuwa sasa tunaishi, ikiwa ninyi mnasimama imara katika Bwana. Maana ni shukrani gani tuwezayo kumlipa Mungu kwa ajili yenu, kwa furaha ile yote tunayoifurahia, kwa sababu yenu mbele za Mungu wetu; usiku na mchana tunapoomba kwa juhudi tupate kuwaona nyuso zenu, na kuurekebisha upungufu wa imani yenu? Basi Mungu mwenyewe, Baba yetu, na Bwana wetu Yesu, atuongoze njia yetu tufike kwenu. Bwana na awaongeze na kuwazidisha katika upendo, ninyi kwa ninyi, na kwa watu wote, kama vile sisi nasi tulivyo kwenu; apate kuifanya imara mioyo yenu iwe bila lawama katika utakatifu mbele za Mungu, Baba yetu, wakati wa kuja kwake Bwana wetu Yesu pamoja na watakatifu wake wote.
1 Wathesalonike 3:6-13 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Lakini Timotheo alipotujia hivi sasa kutoka kwenu, alituletea habari njema za imani yenu na upendo wenu, na ya kwamba mnatukumbuka vema siku zote; mkitamani kutuona sisi vile vile kama sisi kuwaona ninyi. Kwa sababu hiyo, ndugu, tulifarijiwa kwa habari zenu, katika msiba na dhiki yetu yote, kwa imani yenu. Kwa kuwa sasa twaishi, ikiwa ninyi mnasimama imara katika Bwana. Maana ni shukrani gani tuwezayo kumlipa Mungu kwa ajili yenu, kwa furaha ile yote tunayoifurahia, kwa sababu yenu mbele za Mungu wetu; usiku na mchana tunapoomba kwa juhudi tupate kuwaona nyuso zenu, na kuyatengeneza mapungufu ya imani yenu? Basi Mungu mwenyewe, Baba yetu, na Bwana wetu Yesu, atuongoze njia yetu tufike kwenu. Bwana na awaongeze na kuwazidisha katika upendo, ninyi kwa ninyi, na kwa watu wote, kama vile sisi nasi tulivyo kwenu; apate kuifanya imara mioyo yenu iwe bila lawama katika utakatifu mbele za Mungu, Baba yetu, wakati wa kuja kwake Bwana wetu Yesu pamoja na watakatifu wake wote.
1 Wathesalonike 3:6-13 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Lakini Timotheo amerejea kwetu hivi sasa kutoka kwenu, na ameleta habari njema kuhusu imani yenu na upendo wenu. Ametuambia kwamba siku zote mnatukumbuka kwa wema, na kwamba mna shauku ya kutuona kama vile sisi tulivyo na shauku ya kuwaona ninyi. Kwa hiyo, ndugu zetu, katika dhiki na mateso yetu yote tumefarijika kwa sababu ya imani yenu. Sasa kwa kuwa hakika tunaishi, kwa kuwa ninyi mmesimama imara katika Bwana. Je, tutawezaje kumshukuru Mungu kiasi cha kutosha kwa ajili yenu, kutokana na furaha tuliyo nayo mbele za Mungu wetu kwa sababu yenu? Usiku na mchana tunaomba kwa bidii ili tupate kuwaona tena na kujaza kile kilichopungua katika imani yenu. Basi Mungu wetu na Baba yetu mwenyewe na Bwana wetu Yesu atengeneze njia ya sisi kuja kwenu. Bwana na auongeze upendo wenu na kuuzidisha kati yenu na kwa wengine wote, kama vile tulivyo na upendo mwingi kwenu. Tunamwomba Mungu aimarishe mioyo yenu ili msiwe na lawama katika utakatifu mbele za Mungu wetu aliye Baba yetu wakati wa kuja kwake Bwana wetu Yesu pamoja na watakatifu wote.