1 Wathesalonike 3:1-13
1 Wathesalonike 3:1-13 Biblia Habari Njema (BHN)
Mwishowe hatukuweza kuvumilia zaidi. Basi, tuliamua kubaki kule Athene peke yetu, na kumtuma kwenu ndugu yetu Timotheo, ambaye ni mfanyakazi mwenzetu kwa ajili ya Mungu katika kuhubiri Habari Njema ya Kristo. Tulimtuma ili awaimarisheni na kuwafarijini, kusudi imani ya mtu yeyote miongoni mwenu isije ikafifia kwa sababu ya taabu hizo. Nyinyi mnajua kwamba tunapaswa kupata mateso. Maana, tulipokuwa pamoja nanyi, tuliwaambieni kwamba tutateswa; na kama mjuavyo, ndivyo ilivyotukia. Ndio maana nilimtuma Timotheo kwenu. Sikuweza kungoja zaidi, na hivyo nilimtuma nipate habari za imani yenu. Isije ikawa labda Mshawishi aliwajaribuni na kazi yote tuliyofanya miongoni mwenu ikapotea bure! Sasa Timotheo amekwisha rudi, naye ametupa habari za kufurahisha kuhusu imani na upendo wenu. Ametuarifu kwamba mnatukumbuka daima, na kwamba mna hamu ya kutuona sisi kama nasi tulivyo na hamu ya kuwaoneni. Basi, habari za imani yenu zimetutia moyo katika taabu na mateso yetu yote, kwani sasa tunaishi kweli ikiwa nyinyi mnasimama imara katika kuungana na Bwana. Sasa tunaweza kumshukuru Mungu wetu kwa ajili yenu. Tunamshukuru kwa furaha tuliyo nayo mbele yake kwa sababu yenu. Tunazidi kumwomba Mungu usiku na mchana kwa moyo wetu wote ili atupatie fursa ya kuwaoneni uso kwa uso ili tuweze kurekebisha chochote kilichopungua katika imani yenu. Tunamwomba Mungu, Baba yetu mwenyewe, na Bwana wetu Yesu, atutayarishie njia ya kuja kwenu. Bwana awawezeshe nyinyi kupendana na kuwapenda watu wote zaidi na zaidi, kama vile sisi tunavyowapenda nyinyi. Hivyo ataiimarisha mioyo yenu, nanyi mtakuwa wakamilifu na watakatifu mbele ya Mungu na Baba yetu wakati Bwana wetu Yesu atakapokuja pamoja na wote walio wake.
1 Wathesalonike 3:1-13 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi kwa hiyo, tulipokuwa hatuwezi kuvumilia zaidi, tuliona vema kuachwa Athene peke yetu. Tukamtuma Timotheo ndugu yetu, mtumishi wa Mungu katika Injili ya Kristo, ili kuwafanya ninyi imara na kuwafariji katika imani yenu; mtu asifadhaishwe na dhiki hizi; maana ninyi wenyewe mnajua ya kuwa ndizo tulizowekewa. Kwa kuwa tulipokuwapo kwenu tulitangulia kuwaambia kwamba tutapata dhiki, kama ilivyotukia, nanyi mnajua. Kwa hiyo mimi nami nilipokuwa siwezi kuvumilia tena, nilituma mtu ili niijue imani yenu, asije yule mjaribu akawajaribu, na taabu yetu ikawa haina faida. Lakini Timotheo alipotujia hivi sasa kutoka kwenu, alituletea Habari Njema za imani yenu na upendo wenu, na ya kwamba mnatukumbuka vema siku zote; mkitamani kutuona kama vile nasi tunavyotamani kuwaona ninyi. Kwa sababu hiyo, ndugu, katika dhiki na mateso yetu yote, katika habari zenu, tumefarijiwa kwa imani yenu. Kwa kuwa sasa tunaishi, ikiwa ninyi mnasimama imara katika Bwana. Maana ni shukrani gani tuwezayo kumlipa Mungu kwa ajili yenu, kwa furaha ile yote tunayoifurahia, kwa sababu yenu mbele za Mungu wetu; usiku na mchana tunapoomba kwa juhudi tupate kuwaona nyuso zenu, na kuurekebisha upungufu wa imani yenu? Basi Mungu mwenyewe, Baba yetu, na Bwana wetu Yesu, atuongoze njia yetu tufike kwenu. Bwana na awaongeze na kuwazidisha katika upendo, ninyi kwa ninyi, na kwa watu wote, kama vile sisi nasi tulivyo kwenu; apate kuifanya imara mioyo yenu iwe bila lawama katika utakatifu mbele za Mungu, Baba yetu, wakati wa kuja kwake Bwana wetu Yesu pamoja na watakatifu wake wote.
1 Wathesalonike 3:1-13 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi kwa hiyo, tulipokuwa hatuwezi kuvumilia zaidi, tuliona vema kuachwa Athene peke yetu. Tukamtuma Timotheo ndugu yetu, mtumishi wa Mungu katika Injili ya Kristo, ili kuwafanya ninyi imara na kuwafariji kwa habari ya imani yenu; mtu asifadhaishwe na dhiki hizi; maana ninyi wenyewe mnajua ya kuwa twawekewa hizo. Kwa kuwa tulipokuwapo kwenu tulitangulia kuwaambia kwamba tutapata dhiki, kama ilivyotukia, nanyi mwajua. Kwa hiyo mimi nami nilipokuwa siwezi kuvumilia tena, nalituma mtu ili niijue imani yenu, asije yule mjaribu akawajaribu, na taabu yetu ikawa haina faida. Lakini Timotheo alipotujia hivi sasa kutoka kwenu, alituletea habari njema za imani yenu na upendo wenu, na ya kwamba mnatukumbuka vema siku zote; mkitamani kutuona sisi vile vile kama sisi kuwaona ninyi. Kwa sababu hiyo, ndugu, tulifarijiwa kwa habari zenu, katika msiba na dhiki yetu yote, kwa imani yenu. Kwa kuwa sasa twaishi, ikiwa ninyi mnasimama imara katika Bwana. Maana ni shukrani gani tuwezayo kumlipa Mungu kwa ajili yenu, kwa furaha ile yote tunayoifurahia, kwa sababu yenu mbele za Mungu wetu; usiku na mchana tunapoomba kwa juhudi tupate kuwaona nyuso zenu, na kuyatengeneza mapungufu ya imani yenu? Basi Mungu mwenyewe, Baba yetu, na Bwana wetu Yesu, atuongoze njia yetu tufike kwenu. Bwana na awaongeze na kuwazidisha katika upendo, ninyi kwa ninyi, na kwa watu wote, kama vile sisi nasi tulivyo kwenu; apate kuifanya imara mioyo yenu iwe bila lawama katika utakatifu mbele za Mungu, Baba yetu, wakati wa kuja kwake Bwana wetu Yesu pamoja na watakatifu wake wote.
1 Wathesalonike 3:1-13 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Kwa hivyo tulipokuwa hatuwezi kuvumilia zaidi, tuliamua tubaki Athene peke yetu. Tukamtuma Timotheo ambaye ni ndugu yetu na mtumishi mwenzetu wa Mungu katika kuieneza Injili ya Kristo, aje kuwaimarisha na kuwatia moyo katika imani yenu, ili mtu yeyote asifadhaishwe na mateso haya. Mnajua vyema kwamba tumewekewa hayo mateso. Kwa kweli, tulipokuwa pamoja nanyi tuliwaambia mara kwa mara kwamba tutateswa na imekuwa hivyo kama mnavyojua. Kwa sababu hii niliposhindwa kuvumilia zaidi, nilimtuma mtu ili nipate habari za imani yenu. Niliogopa kwamba kwa njia fulani yule mjaribu asiwe amewajaribu, nasi tukawa tumejitaabisha bure. Lakini Timotheo amerejea kwetu hivi sasa kutoka kwenu, na ameleta habari njema kuhusu imani yenu na upendo wenu. Ametuambia kwamba siku zote mnatukumbuka kwa wema, na kwamba mna shauku ya kutuona kama vile sisi tulivyo na shauku ya kuwaona ninyi. Kwa hiyo, ndugu zetu, katika dhiki na mateso yetu yote tumefarijika kwa sababu ya imani yenu. Sasa kwa kuwa hakika tunaishi, kwa kuwa ninyi mmesimama imara katika Bwana. Je, tutawezaje kumshukuru Mungu kiasi cha kutosha kwa ajili yenu, kutokana na furaha tuliyo nayo mbele za Mungu wetu kwa sababu yenu? Usiku na mchana tunaomba kwa bidii ili tupate kuwaona tena na kujaza kile kilichopungua katika imani yenu. Basi Mungu wetu na Baba yetu mwenyewe na Bwana wetu Yesu atengeneze njia ya sisi kuja kwenu. Bwana na auongeze upendo wenu na kuuzidisha kati yenu na kwa wengine wote, kama vile tulivyo na upendo mwingi kwenu. Tunamwomba Mungu aimarishe mioyo yenu ili msiwe na lawama katika utakatifu mbele za Mungu wetu aliye Baba yetu wakati wa kuja kwake Bwana wetu Yesu pamoja na watakatifu wote.