1 Wathesalonike 2:13-20
1 Wathesalonike 2:13-20 Biblia Habari Njema (BHN)
Tena tunayo sababu nyingine ya kumshukuru Mungu: Tulipowaleteeni ujumbe wa Mungu, nyinyi mliusikia, mkaupokea, si kama vile ujumbe wa binadamu, bali kama ujumbe wa Mungu, na kweli ndivyo ulivyo. Maana Mungu anafanya kazi ndani yenu nyinyi mnaoamini. Ndugu, nyinyi mmepatwa na mambo yaleyale yaliyoyapata makanisa ya Mungu kule Yudea, mambo yaliyowapata watu walio wake Kristo Yesu. Nyinyi mlidhulumiwa na wananchi wenzenu kama vile wao walivyodhulumiwa na wenzao Wayahudi, ambao walimuua Bwana Yesu na manabii, wakatutesa na sisi pia. Watu hao wanamchukiza Mungu, tena ni maadui za kila mtu! Hata walijaribu kutuzuia kuwahubiria watu wa mataifa mengine ujumbe utakaowaletea wokovu. Ndivyo walivyokamilisha orodha ya dhambi zote walizotenda siku zote. Lakini sasa hasira ya Mungu imewaangukia. Ndugu, kuachana kwetu nanyi kulikuwa kwa muda tu, tena kuachana huko kulikuwa kwa mwili tu na si kwa roho. Kitambo kifupi baadaye, tulishikwa na hamu kubwa ya kuwaoneni tena! Kwa hiyo tuliamua kuwatembeleeni tena. Nami, Paulo, nilijaribu kuja kwenu zaidi ya mara moja, lakini Shetani alituzuia. Je, tutakaposimama mbele ya Bwana Yesu wakati atakapokuja, fahari ya ushindi wetu itakuwa nini? Itakuwa ni nyinyi wenyewe; nyinyi ndio tumaini letu na furaha yetu. Naam, nyinyi ni utukufu wetu na furaha yetu!
1 Wathesalonike 2:13-20 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Kwa sababu hiyo sisi nasi tunamshukuru Mungu bila kukoma, kwa kuwa, mlipopata lile neno la ujumbe wa Mungu mlilolisikia kwetu, mlilipokea si kama neno la wanadamu, bali kama neno la Mungu; na kwa kweli ndivyo lilivyo; litendalo kazi pia ndani yenu ninyi mnaoamini. Maana ninyi, ndugu, mlikuwa wafuasi wa makanisa ya Mungu yaliyo katika Yudea, katika Kristo Yesu; kwa kuwa mlipata mateso yale yale kwa watu wa taifa lenu wenyewe, waliyoyapata na hao kwa Wayahudi; ambao walimwua Bwana Yesu, na hao manabii, na kutuudhi sisi; wala hawampendezi Mungu, wala hawapatani na watu wowote; huku wakituzuia tusiseme na Mataifa wapate kuokolewa; ili watimize dhambi zao siku zote. Lakini hasira imewafikia hata mwisho. Lakini sisi, ndugu, tukiwa tumefarakana nanyi kwa muda, kwa uso si kwa moyo, tulizidi kutamani kwa shauku nyingi kuwaona nyuso zenu. Kwa hiyo tulitaka kuja kwenu, naam, mimi Paulo, nilitaka kuja mara kwa mara, lakini Shetani akatuzuia. Maana tumaini letu, au furaha yetu, au taji la kujionea fahari, ni nini? Je! Si ninyi, mbele za Bwana wetu Yesu, wakati wa kuja kwake? Maana ninyi ndinyi utukufu wetu, na furaha yetu.
1 Wathesalonike 2:13-20 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Kwa sababu hiyo sisi nasi twamshukuru Mungu bila kukoma, kwa kuwa, mlipopata lile neno la ujumbe la Mungu mlilolisikia kwetu, mlilipokea si kama neno la wanadamu, bali kama neno la Mungu; na ndivyo lilivyo kweli kweli; litendalo kazi pia ndani yenu ninyi mnaoamini. Maana ninyi, ndugu, mlikuwa wafuasi wa makanisa ya Mungu yaliyo katika Uyahudi, katika Kristo Yesu; kwa kuwa mlipata mateso yale yale kwa watu wa taifa lenu wenyewe, waliyoyapata na hao kwa Wayahudi; ambao walimwua Bwana Yesu, na hao manabii, na kutuudhi sisi; wala hawampendezi Mungu, wala hawapatani na watu wo wote; huku wakituzuia tusiseme na Mataifa wapate kuokolewa; ili watimize dhambi zao siku zote. Lakini hasira imewafikia hata mwisho. Lakini sisi, ndugu, tukiwa tumefarakana nanyi kwa kitambo, kwa uso si kwa moyo, tulizidi kutamani kwa shauku nyingi kuwaona nyuso zenu. Kwa hiyo tulitaka kuja kwenu, naam, mimi Paulo, mara ya kwanza, na mara ya pili, na Shetani akatuzuia. Maana tumaini letu, au furaha yetu, au taji ya kujionea fahari, ni nini? Je! Si ninyi, mbele za Bwana wetu Yesu, wakati wa kuja kwake? Maana ninyi ndinyi utukufu wetu, na furaha yetu.
1 Wathesalonike 2:13-20 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Nasi pia tunamshukuru Mungu bila kukoma kwa sababu mlipolipokea neno la Mungu mlilosikia kutoka kwetu, hamkulipokea kama neno la wanadamu, bali mlilipokea kama lilivyo hasa, neno la Mungu, linalotenda kazi ndani yenu ninyi mnaoamini. Kwa maana ninyi ndugu zetu, mlifanyika wafuasi wa makanisa ya Mungu yaliyo ndani ya Kristo Yesu katika Yudea. Mlipata mateso yale yale kutoka kwa watu wenu wenyewe kama vile makanisa hayo yalivyoteswa na Wayahudi, wale waliomuua Bwana Yesu na manabii, nasi wakatufukuza pia. Watu hao walimchukiza Mungu na tena ni adui wa watu wote, wakijitahidi kutuzuia tusizungumze na watu wa Mataifa ili wapate kuokolewa. Kwa njia hii wanazidi kujilundikia dhambi zao hadi kikomo. Lakini hatimaye ghadhabu ya Mungu imewafikia. Lakini ndugu zetu, tulipotenganishwa nanyi kwa muda mfupi (ingawa kutengana huko kulikuwa kwa mwili tu, si kwa moyo), tulizidi kuwa na shauku kubwa kuwaona uso kwa uso. Maana tulitaka kuja kwenu, hasa mimi Paulo, nilitaka kuja tena na tena, lakini Shetani akatuzuia. Kwa maana tumaini letu ni nini, au furaha yetu, au taji letu la kujisifia mbele za Bwana wetu Yesu Kristo wakati wa kuja kwake? Je, si ni ninyi? Naam, ninyi ndio fahari yetu na furaha yetu.