1 Wathesalonike 1:2-8
1 Wathesalonike 1:2-8 Biblia Habari Njema (BHN)
Tunamshukuru Mungu daima kwa ajili yenu nyinyi nyote na kuwakumbukeni daima katika sala zetu. Maana, mbele ya Mungu Baba yetu, twakumbuka jinsi mnavyoonesha imani yenu kwa matendo, jinsi upendo wenu unavyowawezesha kufanya kazi kwa bidii, na jinsi tumaini lenu katika Bwana wetu Yesu Kristo lilivyo thabiti. Ndugu, twajua kwamba Mungu anawapenda na kwamba amewateua muwe watu wake, maana wakati tulipowahubirieni ile Habari Njema haikuwa kwa maneno tu, bali pia kwa nguvu na kwa Roho Mtakatifu, tukiwa na hakika kwamba ujumbe huo ulikuwa wa kweli. Mnajua jinsi tulivyoishi pamoja nanyi; tuliishi kwa manufaa yenu. Nyinyi mlifuata mfano wetu, mkamwiga Bwana. Ingawa mliteswa sana, mliupokea ujumbe huo kwa furaha itokayo kwa Roho Mtakatifu. Kwa hiyo nyinyi mmekuwa mfano mzuri kwa waamini wote wa Makedonia na Akaya. Maana, kutokana na bidii yenu ujumbe wa Bwana umesikika si huko Makedonia na Akaya tu, bali imani yenu kwa Mungu imeenea popote. Tena hatuhitaji kusema zaidi.
1 Wathesalonike 1:2-8 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Twamshukuru Mungu siku zote kwa ajili yenu nyote, tukiwataja katika maombi yetu. Wala hatuachi kuikumbuka kazi yenu ya imani, na taabu yenu ya upendo, na subira yenu ya tumaini lililo katika Bwana wetu Yesu Kristo, mbele za Mungu Baba yetu. Kwa maana, ndugu mnaopendwa na Mungu, tunajua uteule wenu; ya kwamba Injili yetu haikuwafikia katika maneno tu, bali na katika nguvu, na katika Roho Mtakatifu, na uthibitifu mwingi; kama vile mnavyojua jinsi zilivyokuwa tabia zetu kwenu, kwa ajili yenu. Nanyi mkawa wafuasi wetu na wa Bwana, mkiisha kulipokea neno katika dhiki nyingi, pamoja na furaha ya Roho Mtakatifu. Hata mkawa kielelezo kwa watu wote waaminio katika Makedonia, na katika Akaya. Maana kutoka kwenu neno la Mungu limevuma, si katika Makedonia na Akaya tu, ila na kila mahali imani yenu mliyo nayo kwa Mungu imeenea; hata hatuna haja sisi kunena lolote.
1 Wathesalonike 1:2-8 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Twamshukuru Mungu siku zote kwa ajili yenu nyote, tukiwataja katika maombi yetu. Wala hatuachi kuikumbuka kazi yenu ya imani, na taabu yenu ya upendo, na saburi yenu ya tumaini lililo katika Bwana wetu Yesu Kristo, mbele za Mungu Baba yetu. Kwa maana, ndugu mnaopendwa na Mungu, twajua uteule wenu; ya kwamba injili yetu haikuwafikia katika maneno tu, bali na katika nguvu, na katika Roho Mtakatifu, na uthibitifu mwingi; kama vile mnavyojua jinsi zilivyokuwa tabia zetu kwenu, kwa ajili yenu. Nanyi mkawa wafuasi wetu na wa Bwana, mkiisha kulipokea neno katika dhiki nyingi, pamoja na furaha ya Roho Mtakatifu. Hata mkawa kielelezo kwa watu wote waaminio katika Makedonia, na katika Akaya. Maana kutoka kwenu neno la Mungu limevuma, si katika Makedonia na Akaya tu, ila na kila mahali imani yenu mliyo nayo kwa Mungu imeenea; hata hatuna haja sisi kunena lo lote.
1 Wathesalonike 1:2-8 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Siku zote tunamshukuru Mungu kwa ajili yenu ninyi nyote, tukiwataja kwenye maombi yetu daima. Tunaikumbuka daima kazi yenu ya imani mbele za Mungu aliye Baba yetu, taabu yenu katika upendo na saburi yenu ya tumaini katika Bwana wetu Yesu Kristo. Ndugu zetu mnaopendwa na Mungu, kwa kuwa tunajua kwamba Mungu amewachagua, kwa sababu ujumbe wetu wa Injili haukuja kwenu kwa maneno matupu bali pia ulidhihirishwa katika nguvu na katika Roho Mtakatifu, tena ukiwa na uthibitisho kamili, kama vile ninyi wenyewe mnavyojua jinsi tulivyoenenda kati yenu kwa ajili yenu. Nanyi mkawa wafuasi wetu na wa Bwana, ingawa mlipata mateso mengi, mlilipokea lile Neno kwa furaha katika Roho Mtakatifu. Hivyo ninyi mkawa kielelezo kwa waumini wote katika Makedonia na Akaya. Kwa maana kutoka kwenu neno la Bwana limesikika, si katika Makedonia na Akaya tu, bali pia imani yenu katika Mungu imejulikana kila mahali, kiasi kwamba hatuna haja ya kusema chochote juu yake.