1 Wathesalonike 1:1-5
1 Wathesalonike 1:1-5 Biblia Habari Njema (BHN)
Mimi Paulo, Silwano na Timotheo, kwa jumuiya ya kanisa la Thesalonike, ambayo ni watu wake Mungu Baba, na wa Bwana Yesu Kristo. Tunawatakieni neema na amani. Tunamshukuru Mungu daima kwa ajili yenu nyinyi nyote na kuwakumbukeni daima katika sala zetu. Maana, mbele ya Mungu Baba yetu, twakumbuka jinsi mnavyoonesha imani yenu kwa matendo, jinsi upendo wenu unavyowawezesha kufanya kazi kwa bidii, na jinsi tumaini lenu katika Bwana wetu Yesu Kristo lilivyo thabiti. Ndugu, twajua kwamba Mungu anawapenda na kwamba amewateua muwe watu wake, maana wakati tulipowahubirieni ile Habari Njema haikuwa kwa maneno tu, bali pia kwa nguvu na kwa Roho Mtakatifu, tukiwa na hakika kwamba ujumbe huo ulikuwa wa kweli. Mnajua jinsi tulivyoishi pamoja nanyi; tuliishi kwa manufaa yenu.
1 Wathesalonike 1:1-5 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Paulo, Silwano na Timotheo, kwa kanisa la Wathesalonike, lililo katika Mungu Baba, na katika Bwana Yesu Kristo. Neema na iwe kwenu na amani. Twamshukuru Mungu siku zote kwa ajili yenu nyote, tukiwataja katika maombi yetu. Wala hatuachi kuikumbuka kazi yenu ya imani, na taabu yenu ya upendo, na subira yenu ya tumaini lililo katika Bwana wetu Yesu Kristo, mbele za Mungu Baba yetu. Kwa maana, ndugu mnaopendwa na Mungu, tunajua uteule wenu; ya kwamba Injili yetu haikuwafikia katika maneno tu, bali na katika nguvu, na katika Roho Mtakatifu, na uthibitifu mwingi; kama vile mnavyojua jinsi zilivyokuwa tabia zetu kwenu, kwa ajili yenu.
1 Wathesalonike 1:1-5 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Paulo, na Silwano, na Timotheo, kwa kanisa la Wathesalonike, lililo katika Mungu Baba, na katika Bwana Yesu Kristo. Neema na iwe kwenu na amani. Twamshukuru Mungu siku zote kwa ajili yenu nyote, tukiwataja katika maombi yetu. Wala hatuachi kuikumbuka kazi yenu ya imani, na taabu yenu ya upendo, na saburi yenu ya tumaini lililo katika Bwana wetu Yesu Kristo, mbele za Mungu Baba yetu. Kwa maana, ndugu mnaopendwa na Mungu, twajua uteule wenu; ya kwamba injili yetu haikuwafikia katika maneno tu, bali na katika nguvu, na katika Roho Mtakatifu, na uthibitifu mwingi; kama vile mnavyojua jinsi zilivyokuwa tabia zetu kwenu, kwa ajili yenu.
1 Wathesalonike 1:1-5 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Paulo, Silvano na Timotheo. Kwa kanisa la Wathesalonike, ninyi mlio ndani ya Mungu Baba yetu na ndani ya Bwana Yesu Kristo. Neema iwe kwenu na amani. Siku zote tunamshukuru Mungu kwa ajili yenu ninyi nyote, tukiwataja kwenye maombi yetu daima. Tunaikumbuka daima kazi yenu ya imani mbele za Mungu aliye Baba yetu, taabu yenu katika upendo na saburi yenu ya tumaini katika Bwana wetu Yesu Kristo. Ndugu zetu mnaopendwa na Mungu, kwa kuwa tunajua kwamba Mungu amewachagua, kwa sababu ujumbe wetu wa Injili haukuja kwenu kwa maneno matupu bali pia ulidhihirishwa katika nguvu na katika Roho Mtakatifu, tena ukiwa na uthibitisho kamili, kama vile ninyi wenyewe mnavyojua jinsi tulivyoenenda kati yenu kwa ajili yenu.