1 Samueli 8:11-18
1 Samueli 8:11-18 Biblia Habari Njema (BHN)
Samueli aliwaambia, “Hivi ndivyo mfalme wenu atakayewatawala atakavyowatendea: Watoto wenu wa kiume atawafanya wawe waendeshaji wa magari yake, na wengine kuwa wapandafarasi wake, na wengine watapiga mbio mbele ya magari yake. Atajichagulia wengine wawe makamanda wa vikosi vyake vya maelfu na wengine wawe makamanda wa vikosi vya watu hamsinihamsini. Atawafanya wengine wamlimie mashamba yake na kuvuna mazao yake. Atawafanya wengine pia wamtengenezee zana za vita, na wengine wamtengenezee vipuli vya magari yake. Binti zenu atawachukua kuwa watengenezaji marashi, wengine wapishi na wengine waokaji mikate. Atayachukua mashamba yenu mazuri, mashamba ya mizeituni, na mashamba ya mizabibu na kuwapa watumishi wake. Atachukua sehemu ya kumi ya nafaka zenu na ya zabibu zenu na kuwapa maofisa wake na watumishi wake. Atachukua watumishi wenu wa kiume na wa kike na ng'ombe wenu wazuri na punda wenu wazuri kabisa na kuwafanya wamfanyie kazi zake. Atachukua sehemu ya kumi ya kondoo wenu. Na nyinyi wenyewe mtakuwa watumwa wake. Wakati huo, nyinyi mtalalamika kwa sababu ya mfalme wenu ambaye mmejichagulia nyinyi wenyewe. Lakini Mwenyezi-Mungu hatawajibu.”
1 Samueli 8:11-18 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Akasema, Mfalme atakayewatawala ninyi atakuwa na desturi hii; atatwaa wana wenu na kuwaweka kwake, katika magari yake, na kuwa wapanda farasi wake; nao watapiga mbio mbele ya magari yake. Naye atawaweka kwake kuwa wakuu juu ya maelfu, na makamanda juu ya hamsini hamsini; na wengine atawaweka walime shamba lake, na kuvuna mavuno yake, na kufanyiza zana zake za vita, na vyombo vya magari yake. Na binti zenu atawatwaa kuwa watengenezaji wa marhamu, wapishi na waokaji. Atatwaa mashamba yenu, na mashamba yenu ya mizabibu, na ya mizeituni, yale yaliyo mazuri sana, ili awape watumishi wake. Naye atawatoza ushuru wa mbegu zenu na wa mizabibu yenu, awape wakuu wake, na watumishi wake. Atawatwaa watumishi wenu na wajakazi wenu, na ng'ombe wenu walio wazuri sana, na punda wenu, naye atawatia katika kazi zake mwenyewe. Atawatoza fungu la kumi la mifugo wenu; nanyi mtakuwa watumwa wake. Nanyi mtalia siku ile kwa sababu ya mfalme wenu mliyejichagulia; BWANA asiwajibu siku ile.
1 Samueli 8:11-18 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Akasema, Mfalme atakayewamiliki ninyi atakuwa na desturi hii; atatwaa wana wenu na kuwaweka kwake, kwa magari yake, na kuwa wapanda farasi wake; nao watapiga mbio mbele ya magari yake. Naye atawaweka kwake kuwa maakida juu ya elfu, na maakida juu ya hamsini; na wengine atawaweka walime shamba lake, na kuvuna mavuno yake, na kufanyiza zana zake za vita, na vyombo vya magari yake. Na binti zenu atawatwaa kuwa wafanyaji wa marhamu, na wapishi, na waokaji. Atatwaa makonde yenu, na mashamba yenu ya mizabibu, na ya mizeituni, yale yaliyo mazuri sana, ili awape watumishi wake. Naye atawatoza ushuru wa mbegu zenu na wa mizabibu yenu, awape maakida wake, na watumishi Wake. Atawatwaa watumishi wenu na wajakazi wenu, na ng’ombe zenu walio wazuri sana, na punda zenu, naye atawatia katika kazi zake mwenyewe. Atawatoza fungu la kumi la makundi yenu; nanyi mtakuwa watumwa wake. Nanyi mtalia siku ile kwa sababu ya mfalme wenu mliyejichagulia; BWANA asiwajibu siku ile.
1 Samueli 8:11-18 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Akasema, “Hivi ndivyo atakavyowatendea mfalme atakayewatawala. Atawachukua wana wenu na kuwafanya watumike kwa magari yake ya vita na farasi, nao watakimbia mbele ya magari yake. Baadhi yao atawaweka kuwa majemadari wa jeshi wa maelfu na majemadari wa jeshi wa hamsini, wengine kulima mashamba yake na kuvuna mavuno yake, pia na wengine kutengeneza silaha za vita na vifaa kwa ajili ya magari yake ya vita. Atawachukua binti zenu kuwa watengeneza manukato, wapishi na waokaji. Atayachukua mashamba yenu yaliyo mazuri, mashamba ya mizabibu na mashamba yenu ya mizeituni na kuwapa watumishi wake. Ataichukua sehemu ya kumi ya nafaka yenu na ya zabibu zenu na kuwapa maafisa wake na watumishi wake. Atawachukua watumishi wenu wa kiume na wa kike, na ngʼombe wenu walio wazuri sana na punda kwa matumizi yake mwenyewe. Atachukua sehemu ya kumi ya makundi yenu ya kondoo na mbuzi, na ninyi wenyewe mtakuwa watumwa wake. Siku ile itakapowadia, mtalia kwa kutaka msaada kutokana na mfalme mliyemchagua, naye BWANA hatawajibu.”