1 Samueli 8:1-7
1 Samueli 8:1-7 Biblia Habari Njema (BHN)
Samueli alipokuwa mzee, aliwafanya watoto wake wa kiume kuwa waamuzi wa Israeli. Mtoto wake wa kwanza wa kiume aliitwa Yoeli, na wa pili aliitwa Abiya. Wote wawili walikuwa waamuzi huko Beer-sheba. Lakini watoto hao hawakufuata mwenendo wa baba yao. Bali walianza kujitafutia faida. Wakapokea rushwa na kupotosha haki. Basi, viongozi wote wa Israeli walikusanyika pamoja, na kumwendea Samueli mjini Rama, wakamwambia, “Tazama, wewe sasa ni mzee na watoto wako hawafuati mwenendo wako. Hivyo, tuteulie mfalme wa kututawala kama yalivyo mataifa mengine.” Lakini jambo la Waisraeli kutaka wapewe mfalme wa kuwatawala, halikumpendeza Samueli. Naye akamwomba Mwenyezi-Mungu. Mwenyezi-Mungu akamwambia, “Sikiliza kila kitu ambacho watu wanakuambia; maana hawajakukataa wewe, bali wamenikataa mimi kuwa mfalme juu yao.
1 Samueli 8:1-7 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Na Samweli alipozeeka, aliwafanya wanawe wawe waamuzi juu ya Israeli. Na jina la mwanawe mzaliwa wa kwanza lilikuwa Yoeli; na jina la wa pili Abiya; walikuwa waamuzi katika Beer-sheba. Ila wanawe hawakuenda katika njia zake, bali waliziacha, ili wapate faida; wakapokea rushwa, na kupotosha hukumu. Ndipo wazee wote wa Israeli wakakutana pamoja, wakamwendea Samweli huko Rama; wakamwambia, Angalia, wewe umezeeka, na wanao hawaendi katika njia zako; basi, tuteulie mfalme atutawale kama mataifa yale mengine yote. Lakini neno hilo likawa baya machoni pa Samweli, waliposema, Tupe mfalme atuamue. Naye Samweli akamwomba BWANA. BWANA akamwambia Samweli, Isikilize sauti ya watu hawa katika kila neno watakalokuambia; kwa maana hawakukukataa wewe, bali wamenikataa mimi, ili nisiwe mfalme juu yao.
1 Samueli 8:1-7 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Hata Samweli alipokuwa mzee, aliwafanya wanawe wawe waamuzi juu ya Israeli. Na jina la mwanawe mzaliwa wa kwanza aliitwa Yoeli; na jina la wa pili Abiya; walikuwa waamuzi katika Beer-sheba. Ila wanawe hawakuenda katika njia zake, bali waliziacha, ili wapate faida; wakapokea rushwa, na kupotosha hukumu. Ndipo wazee wote wa Israeli wakakutana pamoja, wakamwendea Samweli huko Rama; wakamwambia, Angalia, wewe umekuwa mzee, na wanao hawaendi katika njia zako; basi, tufanyie mfalme atuamue, mfano wa mataifa yote. Lakini neno hilo likawa baya machoni pa Samweli, waliposema, Tupe mfalme atuamue. Naye Samweli akamwomba BWANA. BWANA akamwambia Samweli, Isikilize sauti ya watu hawa katika kila neno watakalokuambia; kwa maana hawakukukataa wewe, bali wamenikataa mimi, ili nisiwe mfalme juu yao.
1 Samueli 8:1-7 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Samweli alipokuwa mzee, akaweka wanawe kuwa waamuzi wa Israeli. Mzaliwa wa kwanza aliitwa Yoeli, na wa pili aliitwa Abiya, nao wakatumika huko Beer-Sheba. Lakini wanawe hawakuenenda katika njia zake. Waliziacha wakageukia faida za udanganyifu nao wakapokea rushwa na kupotosha haki. Basi wazee wote wa Israeli wakakusanyika pamoja na kumjia Samweli huko Rama. Wakamwambia, “Wewe umekuwa mzee, nao wanao hawaenendi katika njia zako, sasa tuteulie mfalme wa kutuongoza, kama ilivyo kwa mataifa mengine yote.” Lakini wao waliposema, “Tupe mfalme wa kutuongoza,” hili lilimchukiza Samweli, hivyo akamwomba BWANA. Naye BWANA akamwambia: “Sikiliza yale yote watu wanakuambia. Si wewe ambaye wamekukataa, bali wamenikataa mimi kuwa mfalme wao.