1 Samueli 8:1-22
1 Samueli 8:1-22 Biblia Habari Njema (BHN)
Samueli alipokuwa mzee, aliwafanya watoto wake wa kiume kuwa waamuzi wa Israeli. Mtoto wake wa kwanza wa kiume aliitwa Yoeli, na wa pili aliitwa Abiya. Wote wawili walikuwa waamuzi huko Beer-sheba. Lakini watoto hao hawakufuata mwenendo wa baba yao. Bali walianza kujitafutia faida. Wakapokea rushwa na kupotosha haki. Basi, viongozi wote wa Israeli walikusanyika pamoja, na kumwendea Samueli mjini Rama, wakamwambia, “Tazama, wewe sasa ni mzee na watoto wako hawafuati mwenendo wako. Hivyo, tuteulie mfalme wa kututawala kama yalivyo mataifa mengine.” Lakini jambo la Waisraeli kutaka wapewe mfalme wa kuwatawala, halikumpendeza Samueli. Naye akamwomba Mwenyezi-Mungu. Mwenyezi-Mungu akamwambia, “Sikiliza kila kitu ambacho watu wanakuambia; maana hawajakukataa wewe, bali wamenikataa mimi kuwa mfalme juu yao. Tangu nilipowatoa Misri, wameniacha mimi, wamekuwa wakiitumikia miungu mingine mpaka leo. Sasa hayo matendo ambayo wamekuwa wakinitendea mimi, ndiyo wanayokutendea na wewe. Basi, wasikilize, lakini, waonye vikali, na waeleze waziwazi jinsi mfalme atakayewatawala atakavyowatendea.” Kwa hiyo, Samueli akawaambia wale watu waliokuwa wanaomba wapewe mfalme maneno yote ya Mwenyezi-Mungu. Samueli aliwaambia, “Hivi ndivyo mfalme wenu atakayewatawala atakavyowatendea: Watoto wenu wa kiume atawafanya wawe waendeshaji wa magari yake, na wengine kuwa wapandafarasi wake, na wengine watapiga mbio mbele ya magari yake. Atajichagulia wengine wawe makamanda wa vikosi vyake vya maelfu na wengine wawe makamanda wa vikosi vya watu hamsinihamsini. Atawafanya wengine wamlimie mashamba yake na kuvuna mazao yake. Atawafanya wengine pia wamtengenezee zana za vita, na wengine wamtengenezee vipuli vya magari yake. Binti zenu atawachukua kuwa watengenezaji marashi, wengine wapishi na wengine waokaji mikate. Atayachukua mashamba yenu mazuri, mashamba ya mizeituni, na mashamba ya mizabibu na kuwapa watumishi wake. Atachukua sehemu ya kumi ya nafaka zenu na ya zabibu zenu na kuwapa maofisa wake na watumishi wake. Atachukua watumishi wenu wa kiume na wa kike na ng'ombe wenu wazuri na punda wenu wazuri kabisa na kuwafanya wamfanyie kazi zake. Atachukua sehemu ya kumi ya kondoo wenu. Na nyinyi wenyewe mtakuwa watumwa wake. Wakati huo, nyinyi mtalalamika kwa sababu ya mfalme wenu ambaye mmejichagulia nyinyi wenyewe. Lakini Mwenyezi-Mungu hatawajibu.” Hata hivyo watu walikataa kumsikiliza Samueli, wakasema, “La! Sisi tutakuwa na mfalme juu yetu, ili nasi pia tuwe kama mataifa mengine. Mfalme wetu, atatuhukumu, atatuongoza na kutupigania vita vyetu.” Samueli alipokwisha sikiliza kila kitu walichosema, akaenda na kumweleza Mwenyezi-Mungu. Mwenyezi-Mungu akamwambia Samueli, “Wasikilize na wapatie mfalme.” Kisha Samueli akawaambia Waisraeli warudi nyumbani, kila mtu mjini kwake.
1 Samueli 8:1-22 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Na Samweli alipozeeka, aliwafanya wanawe wawe waamuzi juu ya Israeli. Na jina la mwanawe mzaliwa wa kwanza lilikuwa Yoeli; na jina la wa pili Abiya; walikuwa waamuzi katika Beer-sheba. Ila wanawe hawakuenda katika njia zake, bali waliziacha, ili wapate faida; wakapokea rushwa, na kupotosha hukumu. Ndipo wazee wote wa Israeli wakakutana pamoja, wakamwendea Samweli huko Rama; wakamwambia, Angalia, wewe umezeeka, na wanao hawaendi katika njia zako; basi, tuteulie mfalme atutawale kama mataifa yale mengine yote. Lakini neno hilo likawa baya machoni pa Samweli, waliposema, Tupe mfalme atuamue. Naye Samweli akamwomba BWANA. BWANA akamwambia Samweli, Isikilize sauti ya watu hawa katika kila neno watakalokuambia; kwa maana hawakukukataa wewe, bali wamenikataa mimi, ili nisiwe mfalme juu yao. Kwa kadiri ya matendo yote waliyonitenda tokea siku ile nilipowatoa katika Misri hata leo, kwa kuniacha mimi, na kwa kutumikia miungu mingine, ndivyo wanavyokutenda wewe. Basi sasa, isikilize sauti yao; lakini, uwaonye sana, na kuwaonesha desturi ya mfalme atakayewamiliki. Naye Samweli akawaambia wale watu waliotaka mfalme maneno yote ya BWANA. Akasema, Mfalme atakayewatawala ninyi atakuwa na desturi hii; atatwaa wana wenu na kuwaweka kwake, katika magari yake, na kuwa wapanda farasi wake; nao watapiga mbio mbele ya magari yake. Naye atawaweka kwake kuwa wakuu juu ya maelfu, na makamanda juu ya hamsini hamsini; na wengine atawaweka walime shamba lake, na kuvuna mavuno yake, na kufanyiza zana zake za vita, na vyombo vya magari yake. Na binti zenu atawatwaa kuwa watengenezaji wa marhamu, wapishi na waokaji. Atatwaa mashamba yenu, na mashamba yenu ya mizabibu, na ya mizeituni, yale yaliyo mazuri sana, ili awape watumishi wake. Naye atawatoza ushuru wa mbegu zenu na wa mizabibu yenu, awape wakuu wake, na watumishi wake. Atawatwaa watumishi wenu na wajakazi wenu, na ng'ombe wenu walio wazuri sana, na punda wenu, naye atawatia katika kazi zake mwenyewe. Atawatoza fungu la kumi la mifugo wenu; nanyi mtakuwa watumwa wake. Nanyi mtalia siku ile kwa sababu ya mfalme wenu mliyejichagulia; BWANA asiwajibu siku ile. Lakini hao watu wakakataa kuisikiliza sauti ya Samweli; wakasema, Sivyo hivyo; lakini tunataka kuwa na mfalme juu yetu; ili sisi nasi tufanane na mataifa yote; tena ili mfalme wetu atuamue, tena atuongoze na kupigana vita vyetu Samweli akayasikia maneno yote ya watu, akayanena masikioni mwa BWANA. BWANA akamwambia Samweli, Isikilize sauti yao, ukawateulie mfalme. Kisha Samweli akawaambia watu wa Israeli, Kila mtu aende nyumbani kwake.
1 Samueli 8:1-22 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Hata Samweli alipokuwa mzee, aliwafanya wanawe wawe waamuzi juu ya Israeli. Na jina la mwanawe mzaliwa wa kwanza aliitwa Yoeli; na jina la wa pili Abiya; walikuwa waamuzi katika Beer-sheba. Ila wanawe hawakuenda katika njia zake, bali waliziacha, ili wapate faida; wakapokea rushwa, na kupotosha hukumu. Ndipo wazee wote wa Israeli wakakutana pamoja, wakamwendea Samweli huko Rama; wakamwambia, Angalia, wewe umekuwa mzee, na wanao hawaendi katika njia zako; basi, tufanyie mfalme atuamue, mfano wa mataifa yote. Lakini neno hilo likawa baya machoni pa Samweli, waliposema, Tupe mfalme atuamue. Naye Samweli akamwomba BWANA. BWANA akamwambia Samweli, Isikilize sauti ya watu hawa katika kila neno watakalokuambia; kwa maana hawakukukataa wewe, bali wamenikataa mimi, ili nisiwe mfalme juu yao. Kwa kadiri ya matendo yote waliyonitenda tokea siku ile nilipowatoa katika Misri hata leo, kwa kuniacha mimi, na kwa kutumikia miungu mingine, ndivyo wanavyokutenda wewe. Basi sasa, isikilize sauti yao; walakini, uwaonye sana, na kuwaonyesha desturi ya mfalme atakayewamiliki. Naye Samweli akawaambia wale watu waliotaka mfalme maneno yote ya BWANA. Akasema, Mfalme atakayewamiliki ninyi atakuwa na desturi hii; atatwaa wana wenu na kuwaweka kwake, kwa magari yake, na kuwa wapanda farasi wake; nao watapiga mbio mbele ya magari yake. Naye atawaweka kwake kuwa maakida juu ya elfu, na maakida juu ya hamsini; na wengine atawaweka walime shamba lake, na kuvuna mavuno yake, na kufanyiza zana zake za vita, na vyombo vya magari yake. Na binti zenu atawatwaa kuwa wafanyaji wa marhamu, na wapishi, na waokaji. Atatwaa makonde yenu, na mashamba yenu ya mizabibu, na ya mizeituni, yale yaliyo mazuri sana, ili awape watumishi wake. Naye atawatoza ushuru wa mbegu zenu na wa mizabibu yenu, awape maakida wake, na watumishi Wake. Atawatwaa watumishi wenu na wajakazi wenu, na ng’ombe zenu walio wazuri sana, na punda zenu, naye atawatia katika kazi zake mwenyewe. Atawatoza fungu la kumi la makundi yenu; nanyi mtakuwa watumwa wake. Nanyi mtalia siku ile kwa sababu ya mfalme wenu mliyejichagulia; BWANA asiwajibu siku ile. Walakini hao watu wakakataa kuisikiliza sauti ya Samweli; wakasema, Sivyo hivyo; lakini tunataka kuwa na mfalme juu yetu; ili sisi nasi tufanane na mataifa yote; tena ili mfalme wetu atuamue, tena atoke mbele yetu na kutupigia vita vyetu. Samweli akayasikia maneno yote ya watu, akayanena masikioni mwa BWANA. BWANA akamwambia Samweli, Isikilize sauti yao, ukawafanyie mfalme. Kisha Samweli akawaambia watu wa Israeli, Enendeni kila mtu mjini kwake.
1 Samueli 8:1-22 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Samweli alipokuwa mzee, akaweka wanawe kuwa waamuzi wa Israeli. Mzaliwa wa kwanza aliitwa Yoeli, na wa pili aliitwa Abiya, nao wakatumika huko Beer-Sheba. Lakini wanawe hawakuenenda katika njia zake. Waliziacha wakageukia faida za udanganyifu nao wakapokea rushwa na kupotosha haki. Basi wazee wote wa Israeli wakakusanyika pamoja na kumjia Samweli huko Rama. Wakamwambia, “Wewe umekuwa mzee, nao wanao hawaenendi katika njia zako, sasa tuteulie mfalme wa kutuongoza, kama ilivyo kwa mataifa mengine yote.” Lakini wao waliposema, “Tupe mfalme wa kutuongoza,” hili lilimchukiza Samweli, hivyo akamwomba BWANA. Naye BWANA akamwambia: “Sikiliza yale yote watu wanakuambia. Si wewe ambaye wamekukataa, bali wamenikataa mimi kuwa mfalme wao. Kama vile walivyofanya tangu siku nilipowapandisha kutoka Misri hadi siku hii ya leo; wakiniacha mimi na kutumikia miungu mingine, ndivyo wanavyokufanyia wewe. Sasa wasikilize, lakini waonye sana, na uwafahamishe yale watakayotendewa na mfalme atakayewatawala.” Samweli akawaambia wale watu waliokuwa wakiomba wapewe mfalme maneno yote ya BWANA. Akasema, “Hivi ndivyo atakavyowatendea mfalme atakayewatawala. Atawachukua wana wenu na kuwafanya watumike kwa magari yake ya vita na farasi, nao watakimbia mbele ya magari yake. Baadhi yao atawaweka kuwa majemadari wa jeshi wa maelfu na majemadari wa jeshi wa hamsini, wengine kulima mashamba yake na kuvuna mavuno yake, pia na wengine kutengeneza silaha za vita na vifaa kwa ajili ya magari yake ya vita. Atawachukua binti zenu kuwa watengeneza manukato, wapishi na waokaji. Atayachukua mashamba yenu yaliyo mazuri, mashamba ya mizabibu na mashamba yenu ya mizeituni na kuwapa watumishi wake. Ataichukua sehemu ya kumi ya nafaka yenu na ya zabibu zenu na kuwapa maafisa wake na watumishi wake. Atawachukua watumishi wenu wa kiume na wa kike, na ngʼombe wenu walio wazuri sana na punda kwa matumizi yake mwenyewe. Atachukua sehemu ya kumi ya makundi yenu ya kondoo na mbuzi, na ninyi wenyewe mtakuwa watumwa wake. Siku ile itakapowadia, mtalia kwa kutaka msaada kutokana na mfalme mliyemchagua, naye BWANA hatawajibu.” Lakini watu wakakataa kumsikiliza Samweli wakasema, “Hapana! Tunataka mfalme wa kututawala. Kisha tutakuwa kama mataifa mengine yote, tukiwa na mfalme wa kutuongoza na kwenda mbele yetu na kutupigania vita vyetu.” Samweli aliposikia yote watu waliyosema, akarudia kuyasema mbele za BWANA. BWANA akamjibu, “Wasikilize na uwape mfalme.” Kisha Samweli akawaambia Waisraeli, “Kila mmoja arudi mjini kwake.”