Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Samueli 7:2-12

1 Samueli 7:2-12 Biblia Habari Njema (BHN)

Tangu sanduku la Mwenyezi-Mungu lipelekwe mjini Kiriath-yearimu muda mrefu ulipita, miaka ishirini hivi. Wakati huo Waisraeli wote walimlilia Mwenyezi-Mungu. Samueli akawaambia Waisraeli, “Kama mnamrudia Mwenyezi-Mungu kwa moyo wenu wote, ni lazima mwondoe kati yenu miungu ya kigeni na sanamu za Ashtarothi. Mwelekeeni Mwenyezi-Mungu kwa moyo wote, na kumtumikia yeye peke yake; naye atawaokoa kutoka mikononi mwa Wafilisti.” Hivyo, Waisraeli wakatupilia mbali sanamu za Mabaali na Maashtarothi, wakamtumikia Mwenyezi-Mungu peke yake. Kisha, Samueli akawaita Waisraeli wote wakutane huko Mizpa, akawaambia, “Huko nitamwomba Mwenyezi-Mungu kwa ajili yenu.” Hivyo, Waisraeli wote wakakusanyika huko Mizpa. Walichota maji na kuyamimina mbele ya Mwenyezi-Mungu, wakafunga siku ile yote na kusema, “Tumetenda dhambi mbele ya Mwenyezi-Mungu.” (Samueli alikuwa mwamuzi wa Waisraeli huko Mizpa). Wafilisti waliposikia kuwa Waisraeli wamekusanyika huko Mizpa, wakuu watano wa Wafilisti wakaenda kuwashambulia. Waisraeli waliposikia juu ya jambo hilo waliwaogopa Wafilisti. Basi, wakamwambia Samueli, “Usiache kumlilia Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, kwa ajili yetu. Endelea kumlilia atuokoe kutoka kwa Wafilisti.” Kwa hiyo Samueli alichukua mwanakondoo anayenyonya akamtolea Mwenyezi-Mungu kama sadaka ya kuteketezwa nzima. Kisha Samueli akamlilia Mwenyezi-Mungu kwa ajili ya Israeli, naye akajibu kilio chake. Samueli alipokuwa anatoa ile sadaka ya kuteketezwa, Wafilisti walikaribia kuwashambulia Waisraeli. Lakini Mwenyezi-Mungu akatoa sauti kubwa ya ngurumo dhidi ya Wafilisti, na kuwavuruga Wafilisti, nao wakatimuliwa mbele ya Waisraeli. Waisraeli walitoka Mizpa na kuwafuatilia Wafilisti mpaka karibu na mji wa Beth-kari, wakawaangamiza. Kisha, Samueli alichukua jiwe na kulisimamisha kati ya Mizpa na Sheni, akaliita jiwe hilo Ebenezeri akisema, “Mwenyezi-Mungu ametusaidia mpaka sasa.”

1 Samueli 7:2-12 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Ikawa, tangu sanduku lipelekwe Kiriath-yearimu, muda mrefu ulipita; maana ulikuwa miaka ishirini; na nyumba yote ya Waisraeli wakamwombolezea BWANA. Basi Samweli akawaambia nyumba yote ya Israeli, akasema, Ikiwa mnamrudia BWANA kwa mioyo yenu yote, basi, iondoleeni mbali miungu migeni, nayo Maashtorethi yatoke kwenu, mkamwelekezee BWANA mioyo yenu, mkamtumikie yeye peke yake; naye atawaokoa katika mikono ya Wafilisti. Ndipo wana wa Israeli wakayaondoa Mabaali na Maashtorethi, wakamtumikia BWANA peke yake. Samweli akasema, Wakusanyeni Waisraeli wote Mispa, nami nitawaombea ninyi kwa BWANA. Wakakusanyika huko Mispa, wakateka maji na kuyamimina mbele za BWANA; wakafunga siku ile, wakasema huko, Tumemfanyia BWANA dhambi. Samweli akawaamua wana wa Israeli huko Mispa. Hata Wafilisti waliposikia ya kuwa wana wa Israeli wamekusanyika huko Mispa, wakuu wa Wafilisti walipanda juu ili kupigana na Israeli. Nao wana wa Israeli waliposikia, wakawaogopa Wafilisti. Wana wa Israeli wakamwambia Samweli, Usiache kumlilia BWANA, Mungu wetu, kwa ajili yetu, kwamba atuokoe na mikono ya Wafilisti. Ndipo Samweli akatwaa mwana-kondoo mchanga, akamtolea BWANA sadaka ya kuteketezwa nzima; Samweli akamlilia BWANA kwa ajili ya Israeli; BWANA akamwitikia. Hata Samweli alipokuwa akiitoa hiyo sadaka ya kuteketezwa, Wafilisti wakakaribia ili kupigana na Israeli; lakini BWANA akapiga ngurumo, mshindo mkubwa sana, juu ya Wafilisti siku ile, akawafadhaisha; nao wakaangamizwa mbele ya Israeli. Nao watu wa Israeli wakatoka Mispa, wakawafuatia Wafilisti, wakawapiga, hadi walipofika chini ya Beth-kari. Ndipo Samweli akatwaa jiwe, na kulisimamisha kati ya Mispa na Sheni, akaliita jina lake Ebenezeri, akisema, Hata sasa BWANA ametusaidia.

1 Samueli 7:2-12 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Ikawa, tangu siku hiyo ambayo sanduku lilikaa Kiriath-yearimu wakati ulikuwa mwingi; kwa maana ulikuwa miaka ishirini; na nyumba yote ya Israeli wakamwombolezea BWANA. Basi Samweli akawaambia nyumba yote ya Israeli, akasema, Ikiwa mnamrudia BWANA kwa mioyo yenu yote, basi, iondoleeni mbali miungu migeni, nayo Maashtorethi yatoke kwenu, mkamtengenezee BWANA mioyo yenu, mkamtumikie yeye peke yake; naye atawaokoa katika mikono ya Wafilisti. Ndipo wana wa Israeli wakayaondoa Mabaali na Maashtorethi, wakamtumikia BWANA peke yake. Samweli akasema, Wakusanyeni Israeli wote Mispa, nami nitawaombea ninyi kwa BWANA. Wakakusanyika huko Mispa, wakateka maji na kuyamimina mbele za BWANA; wakafunga siku ile, wakasema huko, Tumemfanyia BWANA dhambi. Samweli akawaamua wana wa Israeli huko Mispa. Hata Wafilisti waliposikia ya kuwa wana wa Israeli wamekusanyika huko Mispa, mashehe wa Wafilisti walipanda juu ili kupigana na Israeli. Nao wana wa Israeli waliposikia, wakawaogopa Wafilisti. Wana wa Israeli wakamwambia Samweli, Usiache kumlilia BWANA, Mungu wetu, kwa ajili yetu, kwamba atuokoe na mikono ya Wafilisti. Ndipo Samweli akatwaa mwana-kondoo mchanga, akamtolea BWANA sadaka ya kuteketezwa nzima; Samweli akamlilia BWANA kwa ajili ya Israeli; BWANA akamwitikia. Hata Samweli alipokuwa akiitoa hiyo sadaka ya kuteketezwa, Wafilisti wakakaribia ili kupigana na Israeli; walakini BWANA akapiga ngurumo, mshindo mkubwa sana, juu ya Wafilisti siku ile, akawafadhaisha; nao wakaangamizwa mbele ya Israeli. Nao watu wa Israeli wakatoka Mispa, wakawafuatia Wafilisti, wakawapiga, hata walipofika chini ya Beth-kari. Ndipo Samweli akatwaa jiwe, na kulisimamisha kati ya Mispa na Sheni, akaliita jina lake Eben-ezeri, akisema, Hata sasa BWANA ametusaidia.

1 Samueli 7:2-12 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

Sanduku la BWANA lilibakia huko Kiriath-Yearimu kwa muda mrefu, jumla ya miaka ishirini. Nao watu wote wa Israeli wakamrudia BWANA. Naye Samweli akawaambia nyumba yote ya Israeli, “Ikiwa mtamrudia BWANA kwa mioyo yenu yote, basi iacheni miungu migeni na Maashtorethi, na kujitoa wenyewe kwa BWANA na kumtumikia yeye peke yake, naye atawaokoa ninyi kutoka kwa mkono wa Wafilisti.” Hivyo Waisraeli wakaweka mbali Mabaali yao na Maashtorethi yao, nao wakamtumikia BWANA peke yake. Kisha Samweli akasema, “Wakusanyeni Israeli wote huko Mispa, nami nitawaombea kwa BWANA.” Walipokwisha kukutanika huko Mispa, walichota maji na kuyamimina mbele za BWANA. Siku hiyo walifunga na wakaungama, wakisema, “Tumetenda dhambi dhidi ya BWANA.” Naye Samweli alikuwa kiongozi wa Israeli huko Mispa. Wafilisti waliposikia kwamba Israeli wamekusanyika huko Mispa, watawala wa Wafilisti wakapanda ili kuwashambulia. Waisraeli waliposikia habari hiyo, waliogopa kwa sababu ya Wafilisti. Wakamwambia Samweli, “Usiache kumlilia BWANA, Mungu wetu, kwa ajili yetu, ili apate kutuokoa na mikono ya Wafilisti.” Kisha Samweli akamchukua mwana-kondoo anyonyaye na kumtoa mzima kuwa sadaka ya kuteketezwa kwa BWANA. Akamlilia BWANA kwa niaba ya Israeli, naye BWANA akamjibu. Samweli alipokuwa anatoa hiyo dhabihu ya kuteketezwa, Wafilisti wakasogea karibu ili kupigana vita na Israeli. Lakini siku ile BWANA alinguruma kwa ngurumo kubwa dhidi ya Wafilisti na kuwafanya wafadhaike na kutetemeka hivi kwamba walikimbizwa mbele ya Waisraeli. Wanaume wa Israeli wakatoka mbio huko Mispa na kuwafuatia Wafilisti, wakiwachinja njiani hadi mahali chini ya Beth-Kari. Ndipo Samweli akachukua jiwe na kulisimamisha kati ya Mispa na Sheni. Akaliita Ebenezeri, akisema, “Hadi sasa BWANA ametusaidia.”