1 Samueli 6:5-13
1 Samueli 6:5-13 Biblia Habari Njema (BHN)
Lazima mfanye vinyago vya majipu na vinyago vya panya wenu, vitu ambavyo vinaangamiza nchi yenu. Ni lazima mumpe heshima Mungu wa Israeli. Labda ataacha kuwaadhibu, nyinyi wenyewe, miungu yenu na nchi yenu. Kwa nini mnakuwa wakaidi kama Wamisri na Farao? Je, Mungu alipowadhihaki Wamisri, hawakuwaacha Waisraeli waondoke, nao wakaondoka? Basi, tayarisheni gari jipya na ng'ombe wawili wakamuliwao ambao bado hawajafungwa nira; wafungeni kwenye gari hilo lakini ndama wao wasiende pamoja nao, ila wabaki zizini. Chukueni sanduku la Mwenyezi-Mungu na kuliweka katika gari hilo. Kando ya sanduku wekeni vile vinyago vya dhahabu ambavyo mnampelekea kama sadaka ya kuondoa hatia yenu. Kisha mliache liende litakakokwenda. Bali angalieni, ikiwa gari hilo linakwenda moja kwa moja kuelekea nchi yake yaani kwenye mji wa Beth-shemeshi, basi, hapo tutajua kuwa aliyetuletea tauni hii ni Mungu wa Israeli. Lakini kama haliendi huko, basi, tutajua kuwa sio mkono wake uliotupiga, bali maafa haya yametupata kwa bahati mbaya.” Walifanya kama walivyoambiwa; waliwachukua ng'ombe wawili wanaokamuliwa na kuwafunga kwenye gari, na ndama wao wakawafunga zizini. Lile sanduku la Mwenyezi-Mungu wakalitia kwenye gari hilo pamoja na lile kasha lenye vinyago vya dhahabu vya panya na vile vya majipu. Hao ng'ombe walikwenda moja kwa moja kuelekea mji wa Beth-shemeshi bila kupinda kushoto au kulia, na walikuwa wanalia walipokuwa wanakwenda. Wale wafalme watano wa Wafilisti waliwafuata hadi mpakani mwa Beth-shemeshi. Watu wa Beth-shemeshi walikuwa wanavuna ngano bondeni. Walipotazama juu na kuliona sanduku la Mwenyezi-Mungu, wakafurahi sana.
1 Samueli 6:5-13 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Kwa hiyo mtafanya sanamu za majipu yenu, na sanamu za panya wenu wanaoiharibu nchi; nanyi mtamtukuza huyo Mungu wa Israeli; huenda ataupunguza uzito wa mkono wake juu yenu, na juu ya miungu yenu, na juu ya nchi yenu. Mbona, basi, mnaifanya mioyo yenu migumu, kama vile wale Wamisri, na yule Farao, walivyoifanya mioyo yao migumu? Hata na hao, baada ya kuwadhihaki, je! Hawakuwaruhusu watu waende, nao wakaondoka? Basi sasa jifanyieni gari jipya, mtwae na ng'ombe wake wawili wakamwao, ambao hawajafungwa nira, nanyi mkawafunge hao ng'ombe garini, na kuwaondoa ndama wao na kuwatia zizini; kisha, litwaeni hilo sanduku la BWANA, na kuliweka juu ya gari; na hivyo vitu vya dhahabu, mtakavyompelekea kuwa matoleo ya kosa, mvitie katika kasha kando yake; mkalipeleke sanduku, lipate kwenda. Kisha angalieni, likikwea kwa njia ya mpakani mwake kwenda Beth-shemeshi, basi, ndiye aliyetutenda uovu huo mkuu; la, sivyo, ndipo tutakapojua ya kwamba si mkono wake uliotupiga; ilikuwa ni bahati mbaya iliyotupata. Basi watu wale walifanya hivyo; wakatwaa ng'ombe wawili wakamuliwao, wakawafunga garini, na ndama wao wakawafunga zizini; kisha wakaliweka sanduku la BWANA juu ya gari, pamoja na kasha lenye panya wa dhahabu na sanamu za majipu yao. Na hao ng'ombe wakashika njia moja kwa moja kwenda Beth-shemeshi; wakaiandama njia ya barabara, wakaenda wakilia, lakini hawakugeukia upande wa kulia wala wa kushoto; na wakuu wa Wafilisti wakawafuata hata kuufikia mpaka wa Beth-shemeshi. Nao watu wa Beth-shemeshi walikuwa wakivuna ngano yao bondeni; wakainua macho yao, wakaliona sanduku, wakafurahi sana kuliona.
1 Samueli 6:5-13 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Kwa hiyo mtafanyiza sanamu za majipu yenu, na sanamu za panya wenu waiharibuo nchi; nanyi mtamtukuza huyo Mungu wa Israeli; huenda ataupunguza uzito wa mkono wake juu yenu, na juu ya miungu yenu, na juu ya nchi yenu. Mbona, basi, mnaifanya migumu mioyo yenu, kama vile wale Wamisri, naye yule Farao, walivyoifanya migumu mioyo yao? Hata na hao, hapo alipokwisha kuwadhihaki, je! Hawakuwaruhusu watu, nao wakaenda zao? Basi sasa jifanyizieni gari jipya, mtwae na ng’ombe wake wawili wakamwao, ambao hawajafungwa nira, nanyi mkawafunge hao ng’ombe garini, na kuwaondoa ndama zao na kuwatia zizini; kisha, litwaeni hilo sanduku la BWANA, na kuliweka juu ya gari; na hivyo vitu vya dhahabu, mtakavyompelekea kuwa matoleo ya kosa, mvitie katika kasha kando yake; mkalipeleke sanduku, lipate kwenda. Kisha angalieni, likikwea kwa njia ya mpakani mwake kwenda Beth-shemeshi, basi, ndiye aliyetutenda uovu huo mkuu; la, sivyo, ndipo tutakapojua ya kwamba si mkono wake uliotupiga; ilikuwa ni ajali iliyotupata. Basi watu wale walifanya hivyo; wakatwaa ng’ombe wawili wakamwao, wakawafunga garini, na ndama zao wakawafunga zizini; kisha wakaliweka sanduku la BWANA juu ya gari, pamoja na kasha lenye panya wa dhahabu na sanamu za majipu yao. Na hao ng’ombe wakashika njia moja kwa moja kwenda Beth-shemeshi; wakaiandama njia ya barabara, wakaenda wakilia, lakini hawakugeukia upande wa kuume wala wa kushoto; na mashehe wa Wafilisti wakawafuata hata kuufikia mpaka wa Beth-shemeshi. Nao watu wa Beth-shemeshi walikuwa wakivuna ngano yao bondeni; wakainua macho yao, wakaliona sanduku, wakafurahi sana kuliona.
1 Samueli 6:5-13 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Tengenezeni mifano ya majipu na ya panya wale wanaoharibu nchi yenu, nanyi mtukuzeni Mungu wa Israeli. Labda ataondoa mkono wake kutoka kwenu na kwa miungu yenu na nchi yenu. Kwa nini ninyi mnafanya mioyo yenu migumu kama Wamisri na Farao walivyofanya? Je, alipowatendea kwa ukali, hawakuwaachia Waisraeli wakaenda zao? “Sasa basi, wekeni gari jipya la kukokotwa pamoja na ngʼombe wawili ambao wamezaa lakini ambao kamwe hawajafungwa nira. Fungieni hao ngʼombe hilo gari, lakini ondoeni ndama wao na mwaweke zizini. Chukueni hilo Sanduku la BWANA na mliweke juu ya gari la kukokotwa, na ndani ya kasha kando yake wekeni hivyo vitu vya dhahabu mnavyompelekea BWANA kama sadaka ya hatia. Lipelekeni, lakini liangalieni kwa makini. Iwapo litaenda katika nchi yake lenyewe, kuelekea Beth-Shemeshi, basi tutajua kwamba BWANA ndiye alileta haya maafa makubwa juu yetu. Lakini kama halikwenda, basi tutajua kwamba haukuwa mkono wa BWANA uliotupiga na kwamba iliyotokea kwetu ni ajali.” Basi wakafanya hivyo. Wakachukua ngʼombe wawili wa aina hiyo, wakawafungia hilo gari la kukokotwa, nao ndama wao wakawekwa zizini. Wakaliweka Sanduku la BWANA juu ya hilo gari la kukokotwa pamoja na lile kasha lenye ile mifano ya panya wa dhahabu na ya majipu ya dhahabu. Kisha hao ngʼombe wakaenda moja kwa moja kuelekea Beth-Shemeshi, wakishuka bila kugeuka kuume au kushoto, huku wakilia njia yote. Watawala wa Wafilisti waliwafuata hao ngʼombe hadi mpakani mwa Beth-Shemeshi. Wakati huu watu wa Beth-Shemeshi walikuwa wakivuna ngano yao huko bondeni, walipoinua macho yao na kuona lile Sanduku, wakafurahi kuliona.