Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Samueli 4:1-11

1 Samueli 4:1-11 Biblia Habari Njema (BHN)

Wakati huo, Wafilisti walikutana pamoja, wapigane na Waisraeli. Waisraeli walipiga kambi yao huko Ebenezeri, na Wafilisti wakapiga kambi yao huko Afeka. Wafilisti waliwashambulia Waisraeli, na baada ya mapigano makali, Waisraeli walishindwa. Waisraeli 4,000 waliuawa kwenye uwanja wa mapambano. Wanajeshi walionusurika walipowasili kambini, wazee wa Israeli walisema, “Kwa nini Mwenyezi-Mungu amewaacha Wafilisti watushinde leo? Twendeni tukalilete sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu kutoka Shilo, ili aweze kwenda nasi vitani na kutuokoa kutoka na zetu.” Hivyo, walituma watumishi huko Shilo, nao wakalileta sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu wa majeshi ambaye anakaa kifalme juu ya viumbe wenye mabawa. Wale watoto wawili wa kiume wa Eli, Hofni na Finehasi walikuja pamoja na lile sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu. Sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu lilipofika kambini Waisraeli wote walishangilia kwa furaha, hata nchi yote ikatikisika. Wafilisti waliposikia sauti hiyo ya furaha walisema “Kelele hizo zote kambini mwa Waebrania zina maana gani?” Walipojua kwamba sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu lilikuwa limewasili kambini mwa Waisraeli, Wafilisti waliogopa; wakasema, “Bila shaka, miungu imewasili kambini mwao! Ole wetu! Jambo kama hili halijawahi kutokea. Ole wetu! Ni nani atakayeweza kutuokoa kutokana na miungu hiyo yenye nguvu? Hiyo ni miungu iliyowaua Wamisri kwa kila aina ya mapigo jangwani. Sasa, enyi Wafilisti, jipeni moyo. Muwe, hodari msije mkawa watumwa wa Waebrania kama wao walivyokuwa watumwa wetu. Muwe hodari kama wanaume na kupigana.” Wafilisti walipiga vita, na Waisraeli walishindwa na kukimbia kila mtu nyumbani kwake. Siku hiyo kulikuwa na mauaji makubwa kwani askari wa miguu 30,000 wa Israeli waliuawa. Sanduku la agano la Mungu lilitekwa, na wale watoto wawili wa kiume wa Eli, Hofni na Finehasi, wakauawa.

1 Samueli 4:1-11 Swahili Revised Union Version (SRUV)

[Ikawa siku zile Wafilisti walikusanyika ili kupigana na Israeli,] nao Waisraeli wakatoka juu ya Wafilisti kwenda vitani; wakatua karibu na Ebenezeri, nao Wafilisti wakatua huko Afeki. Nao Wafilisti wakajipanga juu ya Israeli; na walipopigana, Waisraeli wakapigwa na Wafilisti; waliowaua karibu elfu nne katika uwanja wa vita. Hata watu walipofika kambini, wazee wa Israeli wakasema, Mbona BWANA ametupiga leo mbele ya Wafilisti? Twende tukalilete sanduku la Agano la BWANA kutoka Shilo hadi huku, lije kati yetu, na kutuokoa katika mikono ya adui zetu. Basi wakatuma watu kwenda Shilo, nao wakalileta toka huko sanduku la Agano la BWANA wa majeshi, akaaye juu ya makerubi; na Hofni na Finehasi, wana wawili wa Eli, walikuwako huko pamoja na sanduku la Agano la Mungu. Na sanduku la Agano la BWANA lilipoingia kambini, Israeli wote wakapiga kelele kwa sauti kuu, hata nchi ikavuma. Nao Wafilisti waliposikia mshindo wa zile kelele, walisema, Maana yake nini mshindo wa kelele hizi kubwa katika kambi ya Waebrania? Wakatambua ya kuwa sanduku la BWANA limefika kambini. Wafilisti wakaogopa, maana walisema, Mungu ameingia kambini. Wakasema, Ole wetu! Kwani halijawa jambo kama hili tangu hapo. Ole wetu! Ni nani anayeweza kutuokoa kutoka kwa miungu hawa wenye nguvu? Hawa ndio miungu waliowapiga Wamisri kwa mapigo ya kila namna jangwani. Jipeni moyo, na kufanya kiume enyi Wafilisti, msije mkawa watumwa wa Waebrania, kama wao walivyokuwa watumwa wenu; fanyeni kiume, mkapigane nao. Wafilisti wakapigana nao, Israeli wakapigwa, wakakimbia kila mtu hemani kwake; wakauawa watu wengi sana; maana katika Israeli walianguka watu elfu thelathini walioenda vitani kwa miguu. Hilo sanduku la Mungu likatwaliwa; na Hofni na Finehasi, wale wana wawili wa Eli, wakauawa.

1 Samueli 4:1-11 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

[Ikawa siku zile Wafilisti walikusanyika ili kupigana na Israeli,] nao Waisraeli wakatoka juu ya Wafilisti kwenda vitani; wakatua karibu na Ebenezeri, nao Wafilisti wakatua huko Afeki. Nao Wafilisti wakajipanga juu ya Israeli; na walipopigana, Israeli wakapigwa mbele ya Wafilisti; wakauawa watu wa jeshi lao lililokuwa uwandani wapata watu elfu nne. Hata watu walipofika kambini, wazee wa Israeli wakasema, Mbona BWANA ametupiga leo mbele ya Wafilisti? Twende tukalilete sanduku la agano la BWANA toka Shilo hata huku, lije kati yetu, na kutuokoa katika mikono ya adui zetu. Basi wakatuma watu kwenda Shilo, nao wakalileta toka huko sanduku la agano la BWANA wa majeshi, akaaye juu ya makerubi; na Hofni na Finehasi, wana wawili wa Eli, walikuwako huko pamoja na sanduku la agano la Mungu. Na sanduku la agano la BWANA lilipoingia kambini, Israeli wote wakapiga kelele kwa sauti kuu, hata nchi ikavuma. Nao Wafilisti waliposikia mshindo wa zile kelele, walisema, Maana yake nini mshindo wa kelele hizi kubwa katika kambi ya Waebrania? Wakatambua ya kuwa sanduku la BWANA limefika kambini. Wafilisti wakaogopa, maana walisema, Mungu ameingia kambini. Wakasema, Ole wetu! Kwani halijawa jambo kama hili tangu hapo. Ole wetu! Ni nani atakayetuokoa na mkono wa miungu hawa walio hodari? Hawa ndio miungu waliowapiga Wamisri kwa mapigo ya kila namna jangwani. Iweni hodari, na kufanya kiume enyi Wafilisti, msije mkawa watumwa wa Waebrania, kama wao walivyokuwa watumwa wenu; fanyeni kiume, mkapigane nao. Wafilisti wakapigana nao, Israeli wakapigwa, wakakimbia kila mtu hemani kwake; wakauawa watu wengi sana; maana katika Israeli walianguka watu thelathini elfu wenye kwenda vitani kwa miguu. Hilo sanduku la Mungu Likatwaliwa; na Hofni na Finehasi, wale wana wawili wa Eli, wakauawa.

1 Samueli 4:1-11 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

Nalo neno la Samweli likaja kwa Israeli yote. Basi Waisraeli walitoka kwenda kupigana dhidi ya Wafilisti. Waisraeli wakapiga kambi huko Ebenezeri, nao Wafilisti wakapiga kambi huko Afeki. Wafilisti wakapanga safu za majeshi yao kupambana na Israeli, wakati vita vilipoenea, Israeli wakashindwa na Wafilisti, ambao waliwaua askari wa Israeli wapatao elfu nne kwenye uwanja wa vita. Askari waliporudi kambini, wazee wa Israeli wakawauliza, “Kwa nini BWANA ameruhusu leo tushindwe mbele ya Wafilisti? Tuleteni Sanduku la Agano la BWANA kutoka Shilo, ili lipate kwenda pamoja nasi, na kutuokoa kutoka mikono ya adui zetu.” Hivyo wakawatuma watu huko Shilo, nao wakalichukua Sanduku la Agano la BWANA wa majeshi, aliyekaa kwenye kiti chake cha enzi kati ya makerubi. Nao Hofni na Finehasi, wale wana wawili wa Eli, walikuwa huko na Sanduku la Agano la Mungu. Wakati Sanduku la Agano la BWANA lilikuja kambini, Waisraeli wote wakapiga kelele kwa sauti kuu hata ardhi ikatikisika. Wafilisti waliposikia makelele, wakauliza, “Kwa nini kuna makelele haya yote katika kambi ya Waebrania?” Walipofahamu kuwa Sanduku la BWANA limekuja kambini, Wafilisti wakaogopa, wakasema, “Mungu amekuja kambini, ole wetu. Halijatokea jambo kama hili tangu hapo awali. Ole wetu! Ni nani atakayetuokoa kutoka mikononi mwa miungu hii yenye nguvu? Ni miungu ile iliyowapiga Wamisri kwa mapigo ya aina zote huko jangwani. Tuweni hodari, enyi Wafilisti! Tuweni wanaume, la sivyo mtakuwa watumwa wa Waebrania, kama wao walivyokuwa kwenu. Kuweni wanaume, mpigane!” Basi Wafilisti wakapigana, nao Waisraeli wakashindwa na kila mtu akakimbilia kwenye hema lake. Mauaji yalikuwa makubwa sana, Israeli wakapoteza askari elfu thelathini walioenda kwa miguu. Sanduku la Mungu likatekwa, na hao wana wawili wa Eli, Hofni na Finehasi, wakauawa.