1 Samueli 26:9-23
1 Samueli 26:9-23 Biblia Habari Njema (BHN)
Lakini Daudi akamwambia Abishai, “Usimwangamize; maana hakika Mwenyezi-Mungu atamwadhibu mtu yeyote atakayeunyosha mkono wake dhidi ya mteule wake aliyepakwa mafuta. Naapa kwa Mwenyezi-Mungu aliye hai, kwamba Mwenyezi-Mungu mwenyewe atamuua Sauli; ama siku yake ya kufa itafika, au atakwenda vitani na kufia huko. Lakini Mwenyezi-Mungu anakataza nisinyoshe mkono wangu dhidi ya mtu ambaye amemteua kwa kumpaka mafuta. Lakini chukua mkuki wake ulio karibu na kichwa chake pamoja na gudulia lake la maji, halafu tujiendee zetu.” Hivyo, Daudi alichukua ule mkuki na gudulia la maji karibu na kichwa cha Shauli nao wakajiendea zao. Lakini hakuna mtu aliyeona au kujua tukio hilo, wala hakuna aliyeamka, kwa kuwa Mwenyezi-Mungu aliwaletea usingizi mzito. Kisha, Daudi akaenda upande wa pili wa bonde hilo, akasimama juu mlimani mbali na kundi la Shauli. Akaliita kwa sauti jeshi la Shauli na Abneri mwana wa Neri akisema, “Abneri, je, unanisikia?” Abneri akauliza, “Ni nani wewe unayemwita mfalme?” Daudi akamjibu, “Je, wewe si mwanamume? Nani aliye sawa nawe katika Israeli? Mbona basi, hukumlinda bwana wako mfalme? Mtu mmoja wetu aliingia hapo kumwangamiza bwana wako mfalme! Ulilotenda si jambo jema. Ninaapa kwa Mwenyezi-Mungu aliye hai, kwamba unastahili kufa, kwa kuwa hukumlinda bwana wako, ambaye Mwenyezi-Mungu amempaka mafuta. Sasa hebu angalia, mkuki wa mfalme na lile gudulia la maji lililokuwa karibu na kichwa chake kama vipo!” Shauli alitambua sauti ya Daudi, akamwuliza, “Je, hiyo ni sauti yako mwanangu Daudi?” Daudi akamjibu, “Bwana wangu, mfalme, ni sauti yangu.” Halafu akaendelea kusema, “Lakini kwa nini, wewe bwana wangu unifuatilie mimi mtumishi wako? Nimefanya nini? Ni ovu gani nimekufanyia? Basi, sasa bwana wangu mfalme, usikie maneno ya mtumishi wako. Ikiwa Mwenyezi-Mungu ndiye aliyekuchochea uje dhidi yangu, basi, na apokee tambiko itakayomfanya abadili nia yake. Lakini kama ni watu, basi, Mwenyezi-Mungu na awalaani watu hao kwani wamenifukuza kutoka urithi aliotupa Mwenyezi-Mungu wakisema, ‘Nenda ukaitumikie miungu mingine.’ Usiniache nife katika nchi ya kigeni, mbali na Mwenyezi-Mungu. Kwa nini wewe mfalme wa Israeli umetoka kuyatafuta maisha yangu kama mtu anayewinda kware milimani?” Ndipo Shauli akajibu, “Mimi nimefanya makosa. Rudi mwanangu Daudi. Sitakudhuru tena kwa kuwa leo maisha yangu yalikuwa ya thamani mbele yako. Mimi nimekuwa mpumbavu na nimekosa vibaya sana.” Daudi akajibu, “Ee mfalme, mkuki wako uko hapa, mtume kijana wako mmoja aje auchukue. Mwenyezi-Mungu humtunza kila mtu kwa uadilifu na uaminifu wake. Leo Mwenyezi-Mungu alikutia mikononi mwangu, lakini mimi sikunyosha mkono wangu dhidi yako kwa kuwa wewe umeteuliwa naye kwa kutiwa mafuta.
1 Samueli 26:9-23 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Lakini Daudi akamwambia Abishai, Usimwangamize; kwani ni nani awezaye kuunyosha mkono wake juu ya masihi wa BWANA, naye akawa hana hatia? Daudi akasema, Aishivyo BWANA, BWANA atampiga; au siku yake ya kufa itampata; atashuka kwenda vitani na kupotea. Hasha! Nisiunyoshe mkono wangu juu ya masihi wa BWANA; lakini sasa tafadhali twaa hili fumo lililo kichwani pake, na hili gudulia la maji, nasi twende zetu. Basi Daudi akalitwaa lile fumo, na lile gudulia la maji, kichwani pa Sauli; nao wakaenda zao, wala hapana mtu aliyeliona jambo hili wala kulijua, wala kuamka; maana wote walikuwa wamelala; kwa kuwa usingizi mzito kutoka kwa BWANA umewaangukia. Kisha Daudi akaenda ng'ambo ya pili, akasimama juu ya kilima, mbali sana; palipokuwapo nafasi tele katikati yao; naye Daudi akawapigia kelele watu wale, na Abneri, mwana wa Neri, akasema, Abneri, hujibu? Ndipo Abneri akajibu, akasema, U nani wewe unayemlilia mfalme? Naye Daudi akamwambia Abneri, Wewe si mtu shujaa? Tena ni nani aliye sawa na wewe katika Israeli? Mbona, basi, hukumlinda bwana wako, huyo mfalme? Kwa maana mtu mmoja aliingia ili amwangamize mfalme, bwana wako? Jambo hili ulilolitenda si jema. Aishivyo BWANA, mmestahili kufa, kwa sababu hamkumlinda bwana wenu, masihi wa BWANA. Haya basi! Tazameni, liko wapi fumo la mfalme, na gudulia la maji lililokuwa kichwani pake? Naye Sauli akaitambua sauti ya Daudi, akasema, Hii ndiyo sauti yako, Daudi, mwanangu? Daudi akasema, Ndiyo, ni sauti yangu, bwana wangu, mfalme. Akasema, Bwana wangu ananiwinda mimi mtumishi wake kwa sababu gani? Nimefanya nini mimi? Ni uovu gani nilio nao mkononi mwangu? Basi sasa, nakusihi, bwana wangu, mfalme, na asikie maneno ya mtumishi wake. Ikiwa ni BWANA aliyekuchochea juu yangu, na akubali sadaka; bali ikiwa ni wanadamu, na walaaniwe mbele za BWANA; kwa sababu wamenifukuza leo, nisishikamane na urithi wa BWANA, wakisema, Nenda, ukatumikie miungu mingine. Basi sasa, isianguke damu yangu chini mbali na uso wa BWANA; maana mfalme wa Israeli ametoka ili kutafuta uhai wangu, kama vile mtu awindavyo kware mlimani. Ndipo Sauli akasema, Nimekosa; rudi, Daudi, mwanangu; maana sitakudhuru tena, kwa kuwa maisha yangu yalikuwa na thamani machoni pako leo; angalia, nimetenda upumbavu, nimekosa sana. Daudi akajibu, akasema, Litazame fumo hili, Ee mfalme! Kijana mmoja na avukie huku, alitwae. BWANA humlipa kila mtu kulingana na haki na uaminifu wake; maana BWANA amekutia mikononi mwangu leo, nami nilikataa kuunyosha mkono wangu juu ya masihi wa BWANA.
1 Samueli 26:9-23 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Lakini Daudi akamwambia Abishai, Usimwangamize; kwani ni nani awezaye kuunyosha mkono wake juu ya masihi wa BWANA, naye akawa hana hatia? Daudi akasema, Aishivyo BWANA, BWANA atampiga; au siku yake ya kufa itampata; atashuka kwenda vitani na kupotea. Hasha! Nisiunyoshe mkono wangu juu ya masihi wa BWANA; lakini sasa tafadhali twaa hili fumo lililo kichwani pake, na hili gudulia la maji, nasi twende zetu. Basi Daudi akalitwaa lile fumo, na lile gudulia la maji, kichwani pa Sauli; nao wakaenda zao, wala hapana mtu aliyeliona jambo hili wala kulijua, wala kuamka; maana wote walikuwa wamelala; kwa kuwa usingizi mzito kutoka kwa BWANA umewaangukia. Kisha Daudi akaenda ng’ambo ya pili, akasimama juu ya kilima, mbali sana; palipokuwapo nafasi tele katikati yao; naye Daudi akawapigia kelele watu wale, na Abneri, mwana wa Neri, akasema, Abneri, hujibu? Ndipo Abneri akajibu, akasema, U nani wewe unayemlilia mfalme? Naye Daudi akamwambia Abneri, Wewe si mtu shujaa? Tena ni nani aliye sawa na wewe katika Israeli? Mbona, basi, hukumlinda bwana wako, huyo mfalme? Kwa maana mtu mmoja aliingia ili amwangamize mfalme, bwana wako? Jambo hili ulilolitenda si jema. Aishivyo BWANA, mmestahili kufa, kwa sababu hamkumlinda bwana wenu, masihi wa BWANA. Haya basi! Tazameni, liko wapi fumo la mfalme, na gudulia la maji lililokuwa kichwani pake? Naye Sauli akaitambua sauti ya Daudi, akasema, Hii ndiyo sauti yako, Daudi, mwanangu? Daudi akasema, Ndiyo, ni sauti yangu, bwana wangu, mfalme. Akasema, Bwana wangu ananiwinda mimi mtumishi wake kwa sababu gani? Nimefanya nini mimi? Ni uovu gani nilio nao mkononi mwangu? Basi sasa, nakusihi, bwana wangu, mfalme, na asikie maneno ya mtumishi wake. Ikiwa ni BWANA aliyekuondokesha juu yangu, na akubali sadaka; bali ikiwa ni wanadamu, na walaaniwe mbele za BWANA; kwa sababu wamenifukuza leo, nisishikamane na urithi wa BWANA, wakisema, Enenda, katumikie miungu mingine. Basi sasa, isianguke damu yangu chini mbali na uso wa BWANA; maana mfalme wa Israeli ametoka ili kutafuta uhai wangu, kama vile mtu awindavyo kware mlimani. Ndipo Sauli akasema, Nimekosa; rudi, Daudi, mwanangu; maana sitakudhuru tena, kwa kuwa maisha yangu yalikuwa na thamani machoni pako leo; angalia, nimetenda upumbavu, nimekosa sana. Daudi akajibu, akasema, Litazame fumo hili, Ee mfalme! Kijana mmoja na avukie huku, alitwae. Naye BWANA atamlipa kila mtu haki yake, na uaminifu wake; maana BWANA amekutia mikononi mwangu leo, nami nalikataa kuunyosha mkono wangu juu ya masihi wa BWANA.
1 Samueli 26:9-23 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Lakini Daudi akamwambia Abishai, “Usimwangamize! Ni nani awezaye kutia mkono juu ya mpakwa mafuta wa BWANA na asiwe na hatia?” Daudi akasema, “Hakika kama BWANA aishivyo, BWANA mwenyewe atampiga; au wakati wake utafika, naye atakufa, au ataenda vitani na kuangamia. Lakini Mungu na apishie mbali nisije nikainua mkono juu ya mpakwa mafuta wa BWANA. Sasa chukua huo mkuki na hilo gudulia la maji vilivyo karibu na kichwa chake, tuondoke.” Hivyo Daudi akachukua huo mkuki na hilo gudulia la maji vilivyokuwa karibu na kichwa cha Sauli, nao wakaondoka. Hakuna yeyote aliyeona au kufahamu habari hii, wala hakuna hata mmoja aliyeamka usingizini. Wote walikuwa wamelala, kwa sababu BWANA alikuwa amewatia kwenye usingizi mzito. Kisha Daudi akavuka upande mwingine na kusimama juu ya kilima, mahali palipokuwa na nafasi pana kati yao. Daudi akapaza sauti kwa jeshi na kwa Abneri mwana wa Neri, akisema, “Je, Abneri, hutanijibu?” Abneri akajibu, “Nani wewe unayemwita mfalme?” Daudi akasema, “Wewe si ni mtu shujaa? Ni nani aliye kama wewe katika Israeli? Kwa nini basi hukumlinda mfalme bwana wako? Mtu mmoja alikuja kumwangamiza mfalme, bwana wako. Ulichokifanya si kizuri. Kwa hakika kama BWANA aishivyo, wewe na watu wako mnastahili kufa, kwa sababu hamkumlinda bwana wenu, mpakwa mafuta wa BWANA. Tazameni hapo mlipo. Uko wapi mkuki wa mfalme na gudulia la maji ambavyo vilikuwa karibu na kichwa chake?” Sauli akatambua sauti ya Daudi, na kusema, “Je, hiyo ni sauti yako, Daudi mwanangu?” Daudi akajibu, “Naam, hiyo ndiyo, bwana wangu mfalme.” Pia akaongeza, “Kwa nini bwana wangu anamfuatia mtumishi wake? Nimefanya nini, nalo kosa langu ni lipi nililolifanya niwe na hatia? Sasa mfalme bwana wangu na asikilize maneno ya mtumishi wake. Kama BWANA amekuchochea dhidi yangu, basi yeye na aipokee sadaka yangu. Lakini kama ni wanadamu waliofanya hivyo, walaaniwe mbele za BWANA! Wao sasa wamenifukuza kutoka sehemu yangu katika urithi wa BWANA wangu wakisema, ‘Nenda ukatumikie miungu mingine.’ Basi usiache damu yangu imwagike kwenye ardhi mbali na uso wa BWANA. Mfalme wa Israeli ametoka kutafuta kiroboto, kama vile mtu awindavyo kware katika milima.” Ndipo Sauli akasema, “Nimetenda dhambi. Rudi, Daudi mwanangu. Kwa kuwa uliyahesabu maisha yangu kuwa ya thamani leo, sitajaribu kukudhuru tena. Hakika nimetenda kama mpumbavu na nimekosa sana.” Daudi akajibu, “Mkuki wa mfalme uko hapa. Mmoja wa vijana wako na avuke kuuchukua. BWANA humlipa kila mtu kwa ajili ya haki yake na uaminifu wake. BWANA alikutia katika mikono yangu leo, lakini sikuinua mkono wangu juu ya mpakwa mafuta wa BWANA.