Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Samueli 26:1-21

1 Samueli 26:1-21 Biblia Habari Njema (BHN)

Baadhi ya wanaume kutoka mji wa Zifu walimwendea Shauli huko Gibea wakamwambia kwamba Daudi alikuwa anajificha kwenye mlima Hakila, upande wa mashariki wa Yeshimoni. Mara moja, Shauli alikwenda kwenye nyika za Zifu kumtafuta Daudi akiwa na askari waliochaguliwa 3,000 wa Israeli. Shauli akapiga kambi juu ya mlima Hakila, karibu na barabara, mashariki ya Yeshimoni. Lakini Daudi alikuwa bado huko nyikani. Daudi alipojua kwamba Shauli alikuwa amekuja nyikani kumtafuta, alituma wapelelezi, akafahamishwa kwamba ni kweli. Daudi akatoka, akaenda mahali Shauli alipopiga kambi. Akapaona mahali ambapo Shauli alikuwa amelala na Abneri mwana wa Neri, kamanda wa jeshi la Shauli, alikuwa amelala karibu na Shauli. Shauli alikuwa amelala katikati ya kambi huku akizungukwa na jeshi lake. Daudi akamwambia Ahimeleki ambaye alikuwa, Mhiti, na Abishai ndugu yake Yoabu (mama yao aliitwa Seruya), “Nani atakwenda pamoja nami kwenye kambi ya Shauli?” Abishai akamwambia; “Mimi nitakwenda pamoja nawe.” Hivyo usiku, Daudi na Abishai wakaingia kwenye kambi ya Shauli, wakamkuta Shauli amelala katikati ya kambi hiyo, na mkuki wake umechomekwa ardhini karibu na kichwa chake. Abneri pamoja na askari walikuwa wamelala kumzunguka Shauli. Abishai akamwambia Daudi, “Leo Mungu amemtia adui yako mikononi mwako. Basi, niache nimbane udongoni kwa pigo moja tu la mkuki; sitampiga mara mbili.” Lakini Daudi akamwambia Abishai, “Usimwangamize; maana hakika Mwenyezi-Mungu atamwadhibu mtu yeyote atakayeunyosha mkono wake dhidi ya mteule wake aliyepakwa mafuta. Naapa kwa Mwenyezi-Mungu aliye hai, kwamba Mwenyezi-Mungu mwenyewe atamuua Sauli; ama siku yake ya kufa itafika, au atakwenda vitani na kufia huko. Lakini Mwenyezi-Mungu anakataza nisinyoshe mkono wangu dhidi ya mtu ambaye amemteua kwa kumpaka mafuta. Lakini chukua mkuki wake ulio karibu na kichwa chake pamoja na gudulia lake la maji, halafu tujiendee zetu.” Hivyo, Daudi alichukua ule mkuki na gudulia la maji karibu na kichwa cha Shauli nao wakajiendea zao. Lakini hakuna mtu aliyeona au kujua tukio hilo, wala hakuna aliyeamka, kwa kuwa Mwenyezi-Mungu aliwaletea usingizi mzito. Kisha, Daudi akaenda upande wa pili wa bonde hilo, akasimama juu mlimani mbali na kundi la Shauli. Akaliita kwa sauti jeshi la Shauli na Abneri mwana wa Neri akisema, “Abneri, je, unanisikia?” Abneri akauliza, “Ni nani wewe unayemwita mfalme?” Daudi akamjibu, “Je, wewe si mwanamume? Nani aliye sawa nawe katika Israeli? Mbona basi, hukumlinda bwana wako mfalme? Mtu mmoja wetu aliingia hapo kumwangamiza bwana wako mfalme! Ulilotenda si jambo jema. Ninaapa kwa Mwenyezi-Mungu aliye hai, kwamba unastahili kufa, kwa kuwa hukumlinda bwana wako, ambaye Mwenyezi-Mungu amempaka mafuta. Sasa hebu angalia, mkuki wa mfalme na lile gudulia la maji lililokuwa karibu na kichwa chake kama vipo!” Shauli alitambua sauti ya Daudi, akamwuliza, “Je, hiyo ni sauti yako mwanangu Daudi?” Daudi akamjibu, “Bwana wangu, mfalme, ni sauti yangu.” Halafu akaendelea kusema, “Lakini kwa nini, wewe bwana wangu unifuatilie mimi mtumishi wako? Nimefanya nini? Ni ovu gani nimekufanyia? Basi, sasa bwana wangu mfalme, usikie maneno ya mtumishi wako. Ikiwa Mwenyezi-Mungu ndiye aliyekuchochea uje dhidi yangu, basi, na apokee tambiko itakayomfanya abadili nia yake. Lakini kama ni watu, basi, Mwenyezi-Mungu na awalaani watu hao kwani wamenifukuza kutoka urithi aliotupa Mwenyezi-Mungu wakisema, ‘Nenda ukaitumikie miungu mingine.’ Usiniache nife katika nchi ya kigeni, mbali na Mwenyezi-Mungu. Kwa nini wewe mfalme wa Israeli umetoka kuyatafuta maisha yangu kama mtu anayewinda kware milimani?” Ndipo Shauli akajibu, “Mimi nimefanya makosa. Rudi mwanangu Daudi. Sitakudhuru tena kwa kuwa leo maisha yangu yalikuwa ya thamani mbele yako. Mimi nimekuwa mpumbavu na nimekosa vibaya sana.”

1 Samueli 26:1-21 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Basi hao Wazifi wakamwendea Sauli huko Gibea, wakasema, Je! Yule Daudi hakujificha katika kilima cha Hakila, kuelekea Yeshimoni? Basi Sauli akaondoka, akashuka nyikani kwa Zifu, naye alikuwa na watu elfu tatu, wateule wa Israeli, pamoja naye, ili kumtafuta Daudi katika nyika ya Zifu. Naye Sauli akapiga hema katika kilima cha Hakila, kilichoelekea Yeshimoni, barabarani; lakini Daudi alikuwa akikaa nyikani, akaona ya kwamba Sauli amemfuata mpaka nyikani. Basi Daudi akatuma wapelelezi, akapata habari ya hakika ya kwamba Sauli amefika. Daudi akainuka, akafika mahali pale alipotua Sauli; Daudi akapaangalia mahali alipolala Sauli, na Abneri, mwana wa Neri, jemadari wa jeshi lake; naye Sauli alikuwa amelala kati ya magari, na hao watu wamepiga hema zao wakimzunguka. Ndipo Daudi akajibu, akamwambia Ahimeleki, Mhiti, na Abishai, mwana wa Seruya, ndugu yake Yoabu, akisema, Ni nani atakayeshuka pamoja nami kwa Sauli kambini? Abishai akasema, Mimi nitashuka pamoja nawe. Basi Daudi na Abishai wakawaendea watu usiku; na tazama, Sauli alikuwapo kati ya magari amelala usingizi, na fumo lake limechomekwa chini, karibu na kichwa chake; naye Abneri na watu wake wamelala wakimzunguka. Ndipo Abishai akamwambia Daudi, Mungu amemtia adui yako mikononi mwako leo; basi, niache nimpige kwa hilo fumo hadi chini kwa pigo moja, sitampiga mara ya pili. Lakini Daudi akamwambia Abishai, Usimwangamize; kwani ni nani awezaye kuunyosha mkono wake juu ya masihi wa BWANA, naye akawa hana hatia? Daudi akasema, Aishivyo BWANA, BWANA atampiga; au siku yake ya kufa itampata; atashuka kwenda vitani na kupotea. Hasha! Nisiunyoshe mkono wangu juu ya masihi wa BWANA; lakini sasa tafadhali twaa hili fumo lililo kichwani pake, na hili gudulia la maji, nasi twende zetu. Basi Daudi akalitwaa lile fumo, na lile gudulia la maji, kichwani pa Sauli; nao wakaenda zao, wala hapana mtu aliyeliona jambo hili wala kulijua, wala kuamka; maana wote walikuwa wamelala; kwa kuwa usingizi mzito kutoka kwa BWANA umewaangukia. Kisha Daudi akaenda ng'ambo ya pili, akasimama juu ya kilima, mbali sana; palipokuwapo nafasi tele katikati yao; naye Daudi akawapigia kelele watu wale, na Abneri, mwana wa Neri, akasema, Abneri, hujibu? Ndipo Abneri akajibu, akasema, U nani wewe unayemlilia mfalme? Naye Daudi akamwambia Abneri, Wewe si mtu shujaa? Tena ni nani aliye sawa na wewe katika Israeli? Mbona, basi, hukumlinda bwana wako, huyo mfalme? Kwa maana mtu mmoja aliingia ili amwangamize mfalme, bwana wako? Jambo hili ulilolitenda si jema. Aishivyo BWANA, mmestahili kufa, kwa sababu hamkumlinda bwana wenu, masihi wa BWANA. Haya basi! Tazameni, liko wapi fumo la mfalme, na gudulia la maji lililokuwa kichwani pake? Naye Sauli akaitambua sauti ya Daudi, akasema, Hii ndiyo sauti yako, Daudi, mwanangu? Daudi akasema, Ndiyo, ni sauti yangu, bwana wangu, mfalme. Akasema, Bwana wangu ananiwinda mimi mtumishi wake kwa sababu gani? Nimefanya nini mimi? Ni uovu gani nilio nao mkononi mwangu? Basi sasa, nakusihi, bwana wangu, mfalme, na asikie maneno ya mtumishi wake. Ikiwa ni BWANA aliyekuchochea juu yangu, na akubali sadaka; bali ikiwa ni wanadamu, na walaaniwe mbele za BWANA; kwa sababu wamenifukuza leo, nisishikamane na urithi wa BWANA, wakisema, Nenda, ukatumikie miungu mingine. Basi sasa, isianguke damu yangu chini mbali na uso wa BWANA; maana mfalme wa Israeli ametoka ili kutafuta uhai wangu, kama vile mtu awindavyo kware mlimani. Ndipo Sauli akasema, Nimekosa; rudi, Daudi, mwanangu; maana sitakudhuru tena, kwa kuwa maisha yangu yalikuwa na thamani machoni pako leo; angalia, nimetenda upumbavu, nimekosa sana.

1 Samueli 26:1-21 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Basi hao Wazifi wakamwendea Sauli huko Gibea, wakasema, Je! Yule Daudi hakujificha katika kilima cha Hakila, kuelekea Yeshimoni? Basi Sauli akaondoka, akashuka nyikani kwa Zifu, naye alikuwa na watu elfu tatu, wateule wa Israeli, pamoja naye, ili kumtafuta Daudi katika nyika ya Zifu. Naye Sauli akapiga hema katika kilima cha Hakila, kilichoelekea Yeshimoni, barabarani; lakini Daudi alikuwa akikaa nyikani, akaona ya kwamba Sauli amemfuata mpaka nyikani. Basi Daudi akatuma wapelelezi, akapata habari ya hakika ya kwamba Sauli amefika. Daudi akainuka, akafika mahali pale alipotua Sauli; Daudi akapaangalia mahali alipolala Sauli, na Abneri, mwana wa Neri, jemadari wa jeshi lake; naye Sauli alikuwa amelala kati ya magari, na hao watu wamepiga hema zao wakimzunguka. Ndipo Daudi akajibu, akamwambia Ahimeleki, Mhiti, na Abishai, mwana wa Seruya, ndugu yake Yoabu, akisema, Ni nani atakayeshuka pamoja nami kwa Sauli kambini? Abishai akasema, Mimi nitashuka pamoja nawe. Basi Daudi na Abishai wakawaendea watu usiku; na tazama, Sauli alikuwapo kati ya magari amelala usingizi, na fumo lake limechomekwa chini, karibu na kichwa chake; naye Abneri na watu wake wamelala wakimzunguka. Ndipo Abishai akamwambia Daudi, Mungu amemtia adui yako mikononi mwako leo; basi, niache nimpige kwa hilo fumo hata nchi kwa pigo moja, sitampiga mara ya pili. Lakini Daudi akamwambia Abishai, Usimwangamize; kwani ni nani awezaye kuunyosha mkono wake juu ya masihi wa BWANA, naye akawa hana hatia? Daudi akasema, Aishivyo BWANA, BWANA atampiga; au siku yake ya kufa itampata; atashuka kwenda vitani na kupotea. Hasha! Nisiunyoshe mkono wangu juu ya masihi wa BWANA; lakini sasa tafadhali twaa hili fumo lililo kichwani pake, na hili gudulia la maji, nasi twende zetu. Basi Daudi akalitwaa lile fumo, na lile gudulia la maji, kichwani pa Sauli; nao wakaenda zao, wala hapana mtu aliyeliona jambo hili wala kulijua, wala kuamka; maana wote walikuwa wamelala; kwa kuwa usingizi mzito kutoka kwa BWANA umewaangukia. Kisha Daudi akaenda ng’ambo ya pili, akasimama juu ya kilima, mbali sana; palipokuwapo nafasi tele katikati yao; naye Daudi akawapigia kelele watu wale, na Abneri, mwana wa Neri, akasema, Abneri, hujibu? Ndipo Abneri akajibu, akasema, U nani wewe unayemlilia mfalme? Naye Daudi akamwambia Abneri, Wewe si mtu shujaa? Tena ni nani aliye sawa na wewe katika Israeli? Mbona, basi, hukumlinda bwana wako, huyo mfalme? Kwa maana mtu mmoja aliingia ili amwangamize mfalme, bwana wako? Jambo hili ulilolitenda si jema. Aishivyo BWANA, mmestahili kufa, kwa sababu hamkumlinda bwana wenu, masihi wa BWANA. Haya basi! Tazameni, liko wapi fumo la mfalme, na gudulia la maji lililokuwa kichwani pake? Naye Sauli akaitambua sauti ya Daudi, akasema, Hii ndiyo sauti yako, Daudi, mwanangu? Daudi akasema, Ndiyo, ni sauti yangu, bwana wangu, mfalme. Akasema, Bwana wangu ananiwinda mimi mtumishi wake kwa sababu gani? Nimefanya nini mimi? Ni uovu gani nilio nao mkononi mwangu? Basi sasa, nakusihi, bwana wangu, mfalme, na asikie maneno ya mtumishi wake. Ikiwa ni BWANA aliyekuondokesha juu yangu, na akubali sadaka; bali ikiwa ni wanadamu, na walaaniwe mbele za BWANA; kwa sababu wamenifukuza leo, nisishikamane na urithi wa BWANA, wakisema, Enenda, katumikie miungu mingine. Basi sasa, isianguke damu yangu chini mbali na uso wa BWANA; maana mfalme wa Israeli ametoka ili kutafuta uhai wangu, kama vile mtu awindavyo kware mlimani. Ndipo Sauli akasema, Nimekosa; rudi, Daudi, mwanangu; maana sitakudhuru tena, kwa kuwa maisha yangu yalikuwa na thamani machoni pako leo; angalia, nimetenda upumbavu, nimekosa sana.

1 Samueli 26:1-21 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

Hao Wazifu wakamwendea Sauli huko Gibea na kusema, “Je, Daudi hakujificha katika kilima cha Hakila, kinachotazamana na Yeshimoni?” Hivyo Sauli akashuka kwenda katika Jangwa la Zifu, akiwa na wapiganaji wake elfu tatu wa Israeli waliochaguliwa, ili kumtafuta Daudi huko. Sauli akapiga kambi yake kando ya barabara juu ya kilima cha Hakila kinachotazamana na Yeshimoni, lakini Daudi alikuwa anaishi huko jangwani. Alipoona kuwa Sauli amemfuata huko, Daudi akatuma wapelelezi na akapata habari kwa hakika kwamba Sauli alikuwa amewasili. Ndipo Daudi akaondoka, akaenda hadi mahali ambapo Sauli alikuwa amepiga kambi. Akaona mahali Sauli na Abneri mwana wa Neri, jemadari wa jeshi, walipokuwa wamelala. Sauli alikuwa amelala ndani ya kambi, jeshi likiwa limemzunguka. Basi Daudi akamuuliza Ahimeleki Mhiti, na Abishai mwana wa Seruya, nduguye Yoabu, akisema, “Ni nani atakayeshuka pamoja nami kambini kwa Sauli?” Abishai akajibu, “Nitaenda pamoja nawe.” Hivyo Daudi na Abishai wakaenda kwenye jeshi wakati wa usiku, tazama Sauli, alikuwa amelala ndani ya kambi na mkuki wake umekitwa ardhini karibu na kichwa chake. Abneri na askari walikuwa wamelala kumzunguka Sauli. Abishai akamwambia Daudi, “Leo Mungu amemtia adui yako mikononi mwako. Sasa niruhusu nimchome hadi ardhini kwa pigo moja la mkuki wangu; sitamchoma mara mbili.” Lakini Daudi akamwambia Abishai, “Usimwangamize! Ni nani awezaye kutia mkono juu ya mpakwa mafuta wa BWANA na asiwe na hatia?” Daudi akasema, “Hakika kama BWANA aishivyo, BWANA mwenyewe atampiga; au wakati wake utafika, naye atakufa, au ataenda vitani na kuangamia. Lakini Mungu na apishie mbali nisije nikainua mkono juu ya mpakwa mafuta wa BWANA. Sasa chukua huo mkuki na hilo gudulia la maji vilivyo karibu na kichwa chake, tuondoke.” Hivyo Daudi akachukua huo mkuki na hilo gudulia la maji vilivyokuwa karibu na kichwa cha Sauli, nao wakaondoka. Hakuna yeyote aliyeona au kufahamu habari hii, wala hakuna hata mmoja aliyeamka usingizini. Wote walikuwa wamelala, kwa sababu BWANA alikuwa amewatia kwenye usingizi mzito. Kisha Daudi akavuka upande mwingine na kusimama juu ya kilima, mahali palipokuwa na nafasi pana kati yao. Daudi akapaza sauti kwa jeshi na kwa Abneri mwana wa Neri, akisema, “Je, Abneri, hutanijibu?” Abneri akajibu, “Nani wewe unayemwita mfalme?” Daudi akasema, “Wewe si ni mtu shujaa? Ni nani aliye kama wewe katika Israeli? Kwa nini basi hukumlinda mfalme bwana wako? Mtu mmoja alikuja kumwangamiza mfalme, bwana wako. Ulichokifanya si kizuri. Kwa hakika kama BWANA aishivyo, wewe na watu wako mnastahili kufa, kwa sababu hamkumlinda bwana wenu, mpakwa mafuta wa BWANA. Tazameni hapo mlipo. Uko wapi mkuki wa mfalme na gudulia la maji ambavyo vilikuwa karibu na kichwa chake?” Sauli akatambua sauti ya Daudi, na kusema, “Je, hiyo ni sauti yako, Daudi mwanangu?” Daudi akajibu, “Naam, hiyo ndiyo, bwana wangu mfalme.” Pia akaongeza, “Kwa nini bwana wangu anamfuatia mtumishi wake? Nimefanya nini, nalo kosa langu ni lipi nililolifanya niwe na hatia? Sasa mfalme bwana wangu na asikilize maneno ya mtumishi wake. Kama BWANA amekuchochea dhidi yangu, basi yeye na aipokee sadaka yangu. Lakini kama ni wanadamu waliofanya hivyo, walaaniwe mbele za BWANA! Wao sasa wamenifukuza kutoka sehemu yangu katika urithi wa BWANA wangu wakisema, ‘Nenda ukatumikie miungu mingine.’ Basi usiache damu yangu imwagike kwenye ardhi mbali na uso wa BWANA. Mfalme wa Israeli ametoka kutafuta kiroboto, kama vile mtu awindavyo kware katika milima.” Ndipo Sauli akasema, “Nimetenda dhambi. Rudi, Daudi mwanangu. Kwa kuwa uliyahesabu maisha yangu kuwa ya thamani leo, sitajaribu kukudhuru tena. Hakika nimetenda kama mpumbavu na nimekosa sana.”