1 Samueli 23:14-18
1 Samueli 23:14-18 Biblia Habari Njema (BHN)
Basi, Daudi alibaki ngomeni jangwani, katika nchi ya milima ya mbuga za Zifu. Shauli alimtafuta kila siku, lakini Mungu hakumtia Daudi mikononi mwa Shauli. Daudi alijua kuwa Shauli alitaka kuyaangamiza maisha yake. Daudi akawa katika mbuga za Zifu, huko Horeshi. Yonathani mwana wa Shauli alimfuata Daudi huko Horeshi akamtia moyo kwamba Mungu anamlinda. Yonathani alimwambia, “Usiogope, baba yangu Shauli hatakupata. Wewe utakuwa mfalme wa Israeli, mimi nitakuwa wa pili wako. Hata Shauli baba yangu anajua jambo hili.” Hao wote wawili, wakafanya agano mbele ya Mwenyezi-Mungu. Daudi akabaki mjini Horeshi na Yonathani akaenda zake nyumbani.
1 Samueli 23:14-18 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi Daudi alikuwa akikaa nyikani ngomeni, akakaa katika nchi ya milima milima kwenye nyika ya Zifu. Naye Sauli alikuwa akimtafuta kila siku, lakini Mungu hakumtia mikononi mwake. Daudi akaona ya kwamba Sauli ametoka nje ili kutafuta roho yake; naye Daudi akawako katika nyika ya Zifu, huko Horeshi. Ndipo Yonathani, mwana wa Sauli, akainuka akamwendea Daudi huko Horeshi, akamtia nguvu mkono wake katika Mungu. Akamwambia, Usiogope, kwa maana mkono wa Sauli, babangu, hautakupata; na wewe utakuwa mfalme juu ya Israeli; na mimi nitakuwa makamu wako; ndivyo ajuavyo hata Sauli, babangu. Na hao wawili wakafanya agano mbele za BWANA; Daudi naye akakaa huko Horeshi, na Yonathani akaenda nyumbani kwake.
1 Samueli 23:14-18 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi Daudi alikuwa akikaa nyikani ngomeni, akakaa katika nchi ya milima milima kwenye nyika ya Zifu. Naye Sauli alikuwa akimtafuta kila siku, lakini Mungu hakumtia mikononi mwake. Daudi akaona ya kwamba Sauli ametoka nje ili kutafuta roho yake; naye Daudi akawako katika nyika ya Zifu, huko Horeshi. Ndipo Yonathani, mwana wa Sauli, akainuka akamwendea Daudi huko Horeshi, akamtia nguvu mkono wake katika Mungu. Akamwambia, Usiogope, kwa maana mkono wa Sauli, babangu, hautakupata; na wewe utakuwa mfalme juu ya Israeli; na mimi nitakuwa wa pili wako; ndivyo ajuavyo hata Sauli, babangu. Na hao wawili wakafanya agano mbele za BWANA; Daudi naye akakaa huko Horeshi, na Yonathani akaenda nyumbani kwake.
1 Samueli 23:14-18 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Daudi akakaa katika ngome za jangwani na katika vilima vya Jangwa la Zifu. Siku baada ya siku Sauli aliendelea kumsaka, lakini Mungu hakumtia Daudi mkononi mwake. Daudi alipokuwa huko Horeshi katika Jangwa la Zifu, akajua kuwa Sauli alikuwa amekuja ili amuue. Naye Yonathani mwana wa Sauli akamwendea Daudi huko Horeshi na kumtia moyo kusimama imara katika imani yake kwa Mungu. Akamwambia, “Usiogope, Daudi; baba yangu Sauli hatakutia mkononi mwake. Utakuwa mfalme juu ya Israeli, nami nitakuwa wa pili wako. Hata baba yangu Sauli anajua hili.” Wote wawili wakafanya agano mbele za BWANA. Kisha Yonathani akaenda zake nyumbani, lakini Daudi akabaki Horeshi.