1 Samueli 23:1-29
1 Samueli 23:1-29 Biblia Habari Njema (BHN)
Kisha Daudi aliambiwa, “Sikiliza, Wafilisti wanaushambulia mji wa Keila na wanapora nafaka kwenye viwanja vya kupuria.” Basi, Daudi akamwomba Mwenyezi-Mungu shauri, “Je, niende kuwashambulia Wafilisti hawa?” Mwenyezi-Mungu akamjibu, “Ndiyo, nenda ukawashambulie Wafilisti na kuuokoa mji wa Keila.” Lakini watu wa Daudi wakamwambia, “Kama tukiwa hapahapa Yuda tunaogopa, itakuwaje basi, tukienda Keila na kuyashambulia majeshi ya Wafilisti?” Daudi akamwomba tena shauri Mwenyezi-Mungu, naye Mwenyezi-Mungu akamwambia, “Inuka uende Keila kwani nitawatia Wafilisti mikononi mwako.” Basi, Daudi akaenda Keila pamoja na watu wake, na huko akapigana na Wafilisti, akawaua Wafilisti wengi na kuteka nyara ng'ombe wengi. Hivyo Daudi aliwaokoa wakazi wa Keila. Abiathari, mwana wa Ahimeleki, alipokimbilia kwa Daudi huko Keila, alikwenda na kizibao cha kuhani. Shauli alipoambiwa kuwa Daudi amekwisha fika Keila, akasema, “Mungu amemtia mikononi mwangu kwani amejifungia mwenyewe kwa kuingia katika mji wenye malango yenye makomeo.” Hivyo, Shauli aliyaita majeshi yaende Keila na kufanya mashambulizi, ili kumzingira Daudi pamoja na watu wake. Daudi aliposikia mipango miovu ya Shauli dhidi yake, akamwambia kuhani Abiathari, “Kilete hapa hicho kizibao cha kuhani.” Kisha Daudi akaomba, “Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, kwa hakika mimi mtumishi wako, nimesikia kwamba Shauli anapanga kuja kuangamiza mji wa Keila kwa sababu yangu. Je, wakazi wa Keila watanitia mikononi mwa Shauli? Je, Shauli atakuja kweli kama nilivyosikia mimi mtumishi wako? Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, nakuomba unijibu mimi mtumishi wako.” Mwenyezi-Mungu akamjibu, “Shauli atakuja.” Daudi akamwuliza, “Je, wakazi wa Keila watanitia mikononi mwa Shauli, mimi pamoja na watu wangu?” Mwenyezi-Mungu akamjibu, “Watakutia mikononi mwake.” Kisha, Daudi na watu wake ambao walikuwa kama 600, waliondoka na kwenda popote walipoweza kwenda. Shauli aliposikia kwamba Daudi amekwisha kimbia kutoka Keila, akaiacha mipango yake yote. Basi, Daudi alibaki ngomeni jangwani, katika nchi ya milima ya mbuga za Zifu. Shauli alimtafuta kila siku, lakini Mungu hakumtia Daudi mikononi mwa Shauli. Daudi alijua kuwa Shauli alitaka kuyaangamiza maisha yake. Daudi akawa katika mbuga za Zifu, huko Horeshi. Yonathani mwana wa Shauli alimfuata Daudi huko Horeshi akamtia moyo kwamba Mungu anamlinda. Yonathani alimwambia, “Usiogope, baba yangu Shauli hatakupata. Wewe utakuwa mfalme wa Israeli, mimi nitakuwa wa pili wako. Hata Shauli baba yangu anajua jambo hili.” Hao wote wawili, wakafanya agano mbele ya Mwenyezi-Mungu. Daudi akabaki mjini Horeshi na Yonathani akaenda zake nyumbani. Shauli alipokuwa bado huko Gibea, Wazifu wakamwendea na kumwambia, “Daudi anajificha katika nchi yetu kwenye ngome huko Horeshi, kwenye mlima Hakila, ulio upande wa kusini wa Yeshimoni. Sasa, mfalme, njoo ili utekeleze yaliyomo moyoni mwako, na kwa upande wetu, jukumu letu litakuwa kumtia Daudi mikononi mwako.” Shauli akawajibu, “Nyinyi kweli mnanionea huruma; Mwenyezi-Mungu na awabariki. Nendeni, mkahakikishe tena, mjue mahali anapojificha, na ni nani amemwona mahali hapo; maana nimeambiwa kwamba yeye ni mjanja sana. Chunguzeni kila upande mjue mahali anapojificha, kisha mniletee habari kamili. Halafu nitakwenda pamoja nanyi na ikiwa bado atakuwa yuko huko, basi, mimi nitamsaka miongoni mwa maelfu yote ya watu wa Yuda.” Basi, wakaondoka kwenda Zifu, wakimtangulia Shauli. Wakati huo, Daudi na watu wake walikuwa katika jangwa la Maoni, katika bonde la Araba kusini mwa Yeshimoni. Shauli na watu wake wakaanza kumtafuta Daudi. Lakini Daudi alipoambiwa habari hizo, alikwenda kujificha kwenye miamba, iliyoko katika mbuga za Maoni na kukaa huko. Shauli aliposikia habari hizo, alimfuatilia Daudi huko kwenye mbuga za Maoni. Shauli na watu wake walikuwa upande mmoja wa mlima, na Daudi na watu wake walikuwa upande mwingine wa mlima. Daudi alipokuwa anaharakisha kukimbia, Shauli naye alikuwa anamkaribia kumkamata Daudi. Hapo mtu mmoja akamwendea Shauli na kumwambia, “Njoo haraka; Wafilisti wanaishambulia nchi.” Hivyo, Shauli akaacha kumfuatilia Daudi, akaenda kupigana na Wafilisti. Ndio maana mahali hapo pakaitwa “Mwamba wa Matengano.” Daudi aliondoka mahali hapo, akaenda kuishi kwenye ngome ya mji wa Engedi.
1 Samueli 23:1-29 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Kisha wakamwambia Daudi, Angalia, Wafilisti wanapigana vita juu ya Keila na kuiba nafaka katika viwanja vya kupuria. Basi Daudi akamwuliza BWANA, Je! Niende nikawapige hao Wafilisti? Naye BWANA akamwambia Daudi, Nenda ukawapige Wafilisti, na kuuokoa Keila. Ila watu wake Daudi wakamwambia, Tazama, sisi tunaogopa hapa katika Yuda; je! Si zaidi tukienda Keila juu ya majeshi ya Wafilisti? Basi Daudi akamwuliza BWANA tena, Naye BWANA akamjibu, akasema, Ondoka, ukashukie Keila; kwa kuwa nitawatia hao Wafilisti mikononi mwako. Ndipo wakaenda Keila, Daudi na watu wake, wakapigana na hao Wafilisti, wakateka nyara ng'ombe zao, na kuwaua uuaji mkuu. Hivyo Daudi akawaokoa watu wa Keila. Ikawa Abiathari, mwana wa Ahimeleki, alipomkimbilia Daudi huko Keila, alishuka na naivera mkononi mwake. Kisha Sauli aliambiwa ya kwamba Daudi amefika Keila. Sauli akasema, Mungu amemtia mkononi mwangu; kwa maana amefungwa ndani, kwa vile alivyoingia katika mji wenye malango na makomeo. Basi Sauli akawaita watu wote waende vitani, ili waishukie Keila, na kumzingira Daudi na watu wake. Naye Daudi alifahamu ya kuwa Sauli amemkusudia mabaya; akamwambia Abiathari, kuhani, Lete hapa hiyo naivera. Ndipo Daudi akasema, Ee BWANA, Mungu wa Israeli, mimi mtumishi wako nimesikia hakika ya kuwa Sauli anataka kuja huku Keila, ili kuuharibu mji kwa ajili yangu. Je! Watu wa Keila watanitoa, nitiwe mkononi mwake? Je! Sauli atashuka, kama mtumishi wako alivyosikia? Ee Bwana, Mungu wa Israeli, nakusihi, umwambie mtumishi wako. Naye BWANA akamjibu, Atashuka. Ndipo Daudi akasema, Je! Watu wa Keila watanitia mimi na watu wangu mkononi mwake Sauli? BWANA akasema, Watakutia. Basi Daudi na watu wake, ambao walikuwa kama mia sita, wakaondoka na kutoka Keila, wakaenda popote walipoweza kwenda. Kisha Sauli akaambiwa ya kwamba Daudi amekimbia toka Keila; akauacha mpango wake. Basi Daudi alikuwa akikaa nyikani ngomeni, akakaa katika nchi ya milima milima kwenye nyika ya Zifu. Naye Sauli alikuwa akimtafuta kila siku, lakini Mungu hakumtia mikononi mwake. Daudi akaona ya kwamba Sauli ametoka nje ili kutafuta roho yake; naye Daudi akawako katika nyika ya Zifu, huko Horeshi. Ndipo Yonathani, mwana wa Sauli, akainuka akamwendea Daudi huko Horeshi, akamtia nguvu mkono wake katika Mungu. Akamwambia, Usiogope, kwa maana mkono wa Sauli, babangu, hautakupata; na wewe utakuwa mfalme juu ya Israeli; na mimi nitakuwa makamu wako; ndivyo ajuavyo hata Sauli, babangu. Na hao wawili wakafanya agano mbele za BWANA; Daudi naye akakaa huko Horeshi, na Yonathani akaenda nyumbani kwake. Ndipo wale Wazifi wakakwea kwa Sauli huko Gibea, wakasema, Je! Yule Daudi hakujificha kwetu ngomeni mwa Horeshi, kilimani pa Hakila upande wa kusini wa Yeshimoni? Basi sasa, Ee mfalme, ushuke, kama utakavyo nafsini mwako kushuka; na kazi yetu itakuwa kumtia mkononi mwa mfalme. Naye Sauli akasema, Na mbarikiwe ninyi na BWANA; kwa sababu mmenihurumia. Nendeni, nawasihi, mkazidi kupata hakika, mkajue na kuona mahali pake anapojificha, tena ni nani aliyemwona huko; maana nimeambiwa ya kwamba ana ujanja mwingi. Chunguzeni basi, mkayajue maficho yake yote anapojificha; kisha njoni kwangu, tena msikose, nami nitakwenda pamoja nanyi; tena itakuwa, akiwapo katika nchi, mimi nitamtafutatafuta katika maelfu yote ya Yuda. Nao wakaondoka, wakaenda Zifu kumtangulia Sauli; lakini Daudi na watu wake walikuwapo nyikani pa Maoni, katika Araba upande wa kusini mwa jangwa. Basi Sauli na watu wake wakaenda kumtafuta. Watu wakamwambia Daudi; basi kwa hiyo akashuka mpaka mwambani, akakaa nyikani pa Maoni. Naye Sauli alipopata habari, alimwinda Daudi nyikani pa Maoni. Sauli akaenda upande huu wa mlima, na Daudi na watu wake wakaenda upande huu wa mlima; naye Daudi akafanya haraka sana ili amtoroke Sauli; kwa sababu Sauli na watu wake walikuwa wakiwazingira Daudi na watu wake ili kuwakamata. Lakini akaja mjumbe kwa Sauli, kusema, Njoo upesi, kwa kuwa Wafilisti wameishambulia nchi. Basi Sauli akarudi kutoka kumwinda Daudi, akaenda kupigana na Wafilisti; kwa hiyo wakapaita mahali pale, Selahamalekothi. Naye Daudi akakwea kutoka huko, akakaa katika ngome ya Engedi.
1 Samueli 23:1-29 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Kisha wakamwambia Daudi, kusema, Angalia, Wafilisti wanapigana vita juu ya Keila na kuiba nafaka sakafuni mwa kupuria. Basi Daudi akamwuliza BWANA, kusema, Je! Niende nikawapige hao Wafilisti? Naye BWANA akamwambia Daudi, Nenda ukawapige Wafilisti, na kuuokoa Keila. Ila watu wake Daudi wakamwambia, Tazama, sisi tunaogopa hapa katika Yuda; je! Si zaidi tukienda Keila juu ya majeshi ya Wafilisti? Basi Daudi akamwuliza Bwana tena, Naye BWANA akamjibu, akasema, Ondoka, ukashukie Keila; kwa kuwa nitawatia hao Wafilisti mikononi mwako. Ndipo wakaenda Keila, Daudi na watu wake, wakapigana na hao Wafilisti, wakateka nyara ng’ombe zao, na kuwaua uuaji mkuu. Hivyo Daudi akawaokoa watu wa Keila. Ikawa Abiathari, mwana wa Ahimeleki, alipomkimbilia Daudi huko Keila, alishuka na naivera mkononi mwake. Kisha Sauli aliambiwa ya kwamba Daudi amefika Keila. Sauli akasema, Mungu amemtia mkononi mwangu; kwa maana amefungwa ndani, kwa vile alivyoingia katika mji wenye malango na makomeo. Basi Sauli akawaita watu wote waende vitani, ili waishukie Keila, na kumhusuru Daudi na watu wake. Naye Daudi alifahamu ya kuwa Sauli amemkusudia mabaya; akamwambia Abiathari, kuhani, Lete hapa hiyo naivera. Ndipo Daudi akasema, Ee BWANA, Mungu wa Israeli, mimi mtumwa wako nimesikia hakika ya kuwa Sauli anataka kuja huku Keila, ili kuuharibu mji kwa ajili yangu. Je! Watu wa Keila watanitoa, nitiwe mkononi mwake? Je! Sauli atashuka, kama mtumwa wako alivyosikia? Ee Bwana, Mungu wa Israeli, nakusihi, umwambie mtumwa wako. Naye BWANA akamjibu, Atashuka. Ndipo Daudi akasema, Je! Watu wa Keila watanitia mimi na watu wangu mkononi mwake Sauli? BWANA akasema, Watakutia. Basi Daudi na watu wake, ambao wapata kama mia sita, wakaondoka na kutoka Keila, wakaenda po pote walipoweza kwenda. Kisha Sauli akaambiwa ya kwamba Daudi amekimbia toka Keila; akaacha kutoka nje. Basi Daudi alikuwa akikaa nyikani ngomeni, akakaa katika nchi ya milima milima kwenye nyika ya Zifu. Naye Sauli alikuwa akimtafuta kila siku, lakini Mungu hakumtia mikononi mwake. Daudi akaona ya kwamba Sauli ametoka nje ili kutafuta roho yake; naye Daudi akawako katika nyika ya Zifu, huko Horeshi. Ndipo Yonathani, mwana wa Sauli, akainuka akamwendea Daudi huko Horeshi, akamtia nguvu mkono wake katika Mungu. Akamwambia, Usiogope, kwa maana mkono wa Sauli, babangu, hautakupata; na wewe utakuwa mfalme juu ya Israeli; na mimi nitakuwa wa pili wako; ndivyo ajuavyo hata Sauli, babangu. Na hao wawili wakafanya agano mbele za BWANA; Daudi naye akakaa huko Horeshi, na Yonathani akaenda nyumbani kwake. Ndipo wale Wazifi wakakwea kwa Sauli huko Gibea, wakasema, Je! Yule Daudi hakujificha kwetu ngomeni mwa Horeshi, kilimani pa Hakila upande wa kusini wa Yeshimoni? Basi sasa, Ee mfalme, ushuke, kama utakavyo nafsini mwako kushuka; na kazi yetu itakuwa kumtia mkononi mwa mfalme. Naye Sauli akasema, Na mbarikiwe ninyi na BWANA; kwa sababu mmenihurumia. Nendeni, nawasihi, mkazidi kupata hakika, mkajue na kuona mahali pake anapojificha, tena ni nani aliyemwona huko; maana nimeambiwa ya kwamba atenda kwa hila nyingi. Chunguzeni basi, mkayajue maficho yake yote anapojificha; kisha njoni kwangu, tena msikose, nami nitakwenda pamoja nanyi; tena itakuwa, akiwapo katika nchi, mimi nitamtafuta-tafuta katika elfu zote za Yuda. Nao wakaondoka, wakaenda Zifu kumtangulia Sauli; lakini Daudi na watu wake walikuwapo nyikani pa Maoni, katika Araba upande wa kusini wa jangwa. Basi Sauli na watu wake wakaenda kumtafuta. Watu wakamwambia Daudi; basi kwa hiyo akashuka mpaka mwambani, akakaa nyikani pa Maoni. Naye Sauli alipopata habari, alimwinda Daudi nyikani pa Maoni. Sauli akaenda upande huu wa mlima, na Daudi na watu wake wakaenda upande huu wa mlima; naye Daudi akafanya haraka sana kwenda zake kwa hofu ya Sauli; kwa sababu Sauli na watu wake wakamzunguka Daudi na watu wake ili kuwakamata. Lakini akaja mjumbe kwa Sauli, kusema, Njoo upesi, kwa kuwa Wafilisti wameishambulia nchi. Basi Sauli akarudi kutoka kumwinda Daudi, akaenda kinyume cha Wafilisti; kwa hiyo wakapaita mahali pale, Selahamalekothi. Naye Daudi akakwea kutoka huko, akakaa katika ngome ya Engedi.
1 Samueli 23:1-29 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Daudi alipoambiwa, “Tazama, Wafilisti wanapigana dhidi ya Keila, nao wanapokonya nafaka katika sakafu za kupuria,” akauliza kwa BWANA, akisema, “Je, niende na kuwashambulia hawa Wafilisti?” BWANA akamjibu, “Nenda, washambulie Wafilisti na uuokoe Keila.” Lakini watu wa Daudi wakamwambia, “Hapa Yuda kwenyewe tunaogopa. Je, si zaidi tukienda Keila dhidi ya majeshi ya Wafilisti!” Daudi akauliza kwa BWANA tena, naye BWANA akamjibu akamwambia, “Shuka uende Keila, kwa kuwa nitawatia Wafilisti mkononi mwako.” Basi Daudi na watu wake wakaenda Keila, wakapigana na Wafilisti na kutwaa wanyama wao wa kutosha. Daudi akawatia hasara kubwa Wafilisti na kuwaokoa watu wa Keila. Basi Abiathari mwana wa Ahimeleki alikuwa ameleta kizibau alipokimbilia kwa Daudi huko Keila. Sauli akaambiwa kwamba Daudi alikuwa ameenda Keila, naye akasema, “Mungu amemtia mkononi mwangu, kwa kuwa Daudi amejifunga mwenyewe kwa kuingia kwenye mji wenye malango na makomeo.” Naye Sauli akayaita majeshi yake yote yaende vitani, kuishukia Keila ili kumzingira Daudi na watu wake kwa jeshi. Daudi alipojua kuwa Sauli alikuwa ana hila dhidi yake, akamwambia Abiathari kuhani, “Leta kile kizibau.” Daudi akasema, “Ee BWANA, Mungu wa Israeli, mtumishi wako amesikia kwa hakika kwamba Sauli anapanga kuja Keila na kuangamiza mji kwa ajili yangu. Je, watu wa Keila watanisalimisha kwake? Je, Sauli atateremka, kama mtumishi wako alivyosikia? Ee BWANA, Mungu wa Israeli, mwambie mtumishi wako.” Naye BWANA akasema, “Ndiyo, atashuka.” Daudi akauliza tena, “Je watu wa Keila watanisalimisha mimi pamoja na watu wangu kwa Sauli?” Naye BWANA akasema, “Ndiyo, watafanya hivyo.” Basi Daudi na watu wake wapatao mia sita wakaondoka Keila, wakawa wanaenda sehemu moja hadi nyingine. Sauli alipoambiwa Daudi ametoroka kutoka Keila, hakuenda huko. Daudi akakaa katika ngome za jangwani na katika vilima vya Jangwa la Zifu. Siku baada ya siku Sauli aliendelea kumsaka, lakini Mungu hakumtia Daudi mkononi mwake. Daudi alipokuwa huko Horeshi katika Jangwa la Zifu, akajua kuwa Sauli alikuwa amekuja ili amuue. Naye Yonathani mwana wa Sauli akamwendea Daudi huko Horeshi na kumtia moyo kusimama imara katika imani yake kwa Mungu. Akamwambia, “Usiogope, Daudi; baba yangu Sauli hatakutia mkononi mwake. Utakuwa mfalme juu ya Israeli, nami nitakuwa wa pili wako. Hata baba yangu Sauli anajua hili.” Wote wawili wakafanya agano mbele za BWANA. Kisha Yonathani akaenda zake nyumbani, lakini Daudi akabaki Horeshi. Basi Wazifu wakakwea kwa Sauli huko Gibea na kusema, “Je, Daudi hajifichi miongoni mwetu katika ngome huko Horeshi, katika kilima cha Hakila, kusini mwa Yeshimoni? Sasa, ee mfalme, uteremke wakati wowote unapoona vyema kufanya hivyo, sisi tutawajibika kumkabidhi kwa mfalme.” Sauli akajibu, “BWANA awabariki kwa kunifikiria. Nendeni mkafanye maandalizi zaidi. Mkajue mahali Daudi huenda mara kwa mara, na nani amepata kumwona huko. Wananiambia yeye ni mjanja sana. Jueni kila mahali anapojificha, kisha mrudi na kunipa taarifa kamili. Nami nitaenda pamoja nanyi; kama atakuwa katika eneo hilo, nitamsaka miongoni mwa koo zote za Yuda.” Basi wakaondoka na kwenda hadi Zifu wakimtangulia Sauli. Naye Daudi na watu wake walikuwa katika Jangwa la Maoni, katika Araba kusini mwa Yeshimoni. Sauli na watu wake wakaanza msako, naye Daudi alipoelezwa hili, akateremka hadi mwambani na kukaa katika Jangwa la Maoni. Sauli aliposikia hili, akaenda katika Jangwa la Maoni akimfuata Daudi. Sauli alikuwa akienda upande mmoja wa mlima, naye Daudi na watu wake walikuwa upande mwingine wa mlima, wakiharakisha kumkimbia Sauli. Sauli na majeshi yake walipokaribia kumkamata Daudi na watu wake, mjumbe alikuja kwa Sauli, akisema, “Njoo haraka! Wafilisti wanaishambulia nchi.” Ndipo Sauli akarudi akaacha kumfuata Daudi na kwenda kukabiliana na Wafilisti. Ndiyo sababu wanaiita sehemu hii Sela-Hamalekothi. Naye Daudi akakwea kutoka huko na kuishi katika ngome za En-Gedi.