1 Samueli 21:1-9
1 Samueli 21:1-9 Biblia Habari Njema (BHN)
Daudi alikwenda kwa kuhani Ahimeleki huko Nobu. Ahimeleki akatoka kumlaki huku akiwa anatetemeka, akamwuliza, “Kwa nini umekuja hapa peke yako?” Daudi akamjibu, “Niko hapa kutokana na amri ya mfalme. Aliniambia nisimweleze mtu yeyote juu ya kile ambacho amenituma. Nimeagana na watu wangu kwamba tukutane mahali fulani. Je, una kitu chochote? Nakuomba mikate mitano au chochote kilichoko.” Kuhani Ahimeleki akamwambia, “Hapa sina mkate wa kawaida. Ninayo tu ile mikate mitakatifu. Mnaweza kupewa mikate hiyo ikiwa watu wako hawajalala na wanawake hivi karibuni.” Daudi akamwambia, “Kwa hakika, daima ninapokwenda kwa ajili ya shughuli maalumu, wanawake wamekuwa mbali nasi! Ikiwa miili ya vijana wangu ni mitakatifu tuwapo kwenye shughuli za kawaida, je, si zaidi katika shughuli hii maalumu?” Hivyo kuhani Ahimeleki akampa mikate mitakatifu, kwani hapakuwa na mikate mingine isipokuwa hiyo ya kuwekwa mbele ya Mwenyezi-Mungu, ikabadilishwa na mikate mipya kutoka mekoni. Basi kulikuwa hapo siku hiyo mtumishi mmoja wa Shauli ambaye alikuwa amezuiliwa mbele ya Mwenyezi-Mungu. Mtumishi huyo aliitwa Doegi, Mwedomu, msimamizi wa wachungaji wa Shauli. Basi, Daudi akamwambia Ahimeleki, “Je, una upanga au mkuki ambao unaweza kunipatia? Kwa kuwa shughuli za mfalme zilinilazimu niondoke haraka, nami niliondoka bila upanga wangu wala silaha nyingine yoyote.” Ahimeleki akamjibu, “Ninao ule upanga wa Mfilisti Goliathi uliyemuua kwenye bonde la Ela; uko nyuma ya kizibao cha kuhani umefungwa katika kitambaa. Ikiwa unataka kuuchukua huo basi, uchukue kwani hakuna upanga mwingine hapa.” Daudi akamwambia, “Hakuna upanga mwingine kama huo; nakuomba unipe.”
1 Samueli 21:1-9 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi Daudi akaenda Nobu kwa Ahimeleki, kuhani. Ahimeleki akaenda kumlaki Daudi, akitetemeka, akamwambia, Kwa nini uko peke yako, wala hapana mtu pamoja nawe? Daudi akamwambia Ahimeleki, kuhani, Mfalme ameniagiza shughuli, akaniambia, Asijue mtu awaye yote habari ya shughuli hii ninayokutuma, wala ya neno hili ninalokuamuru; nami nimewaagiza vijana waende mahali fulani. Kuna nini basi, chini ya mkono wako? Nipe mkononi mwangu mikate mitano, au chochote ulicho nacho hapa. Yule kuhani akamjibu Daudi, akasema, Hapana mikate ya kawaida chini ya mkono wangu, ila mikate mitakatifu; ikiwa wale vijana wamejitenga na wanawake. Naye Daudi akamjibu kuhani, akamwambia, Hakika tumejitenga na wanawake siku hizi tatu; napo nilipotoka, vyombo vya vijana hawa vilikuwa vitakatifu, ingawa ilikuwa safari ya kawaida; basi leo je! Vyombo vyetu havitakuwa vitakatifu zaidi? Ndipo kuhani akampa ile mikate mitakatifu; kwa maana hapakuwa na mikate ila ile ya wonyesho, nayo imekwisha kuondolewa mbele za BWANA, ili itiwe mikate ya moto siku ile ilipoondolewa. Basi siku ile palikuwapo na mtu mmoja wa watumishi wa Sauli, amezuiwa hapo mbele za BWANA jina lake akiitwa Doegi, Mwedomi, mkubwa wa wachungaji wa Sauli. Tena Daudi akamwambia Ahimeleki, Na hapa chini ya mkono wako, je! Hapana mkuki, au upanga? Kwa maana sikuleta upanga, wala silaha zangu, kwa sababu ile shughuli ya mfalme ilitaka haraka. Yule kuhani akasema, Upanga wa Goliathi, yule Mfilisti, uliyemwua katika bonde la Ela, tazama, upo hapa, umefungwa ndani ya nguo nyuma ya naivera; ukipenda kuuchukua, haya! Uchukue, maana hapa hapana mwingine ila huo tu. Daudi akasema, Hapana mwingine kama ule; haya! Nipe.
1 Samueli 21:1-9 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi Daudi akaenda Nobu kwa Ahimeleki, kuhani. Ahimeleki akaenda kumlaki Daudi, akitetemeka, akamwambia, Kwani wewe kuwa peke yako, wala hapana mtu pamoja nawe? Daudi akamwambia Ahimeleki, kuhani, Mfalme ameniagiza shughuli, akaniambia, Asijue mtu awaye yote habari ya shughuli hii ninayokutuma, wala ya neno hili ninalokuamuru; nami nimewaagiza vijana waende mahali fulani. Kuna nini basi, chini ya mkono wako? Nipe mkononi mwangu mikate mitano, au cho chote ulicho nacho hapa. Yule kuhani akamjibu Daudi, akasema, Hapana mikate ya sikuzote chini ya mkono wangu, ila mikate mitakatifu; ikiwa wale vijana wamejitenga na wanawake. Naye Daudi akamjibu kuhani, akamwambia, Hakika tumejitenga na wanawake siku hizi tatu; napo nilipotoka, vyombo vya vijana hawa vilikuwa vitakatifu, ingawa ilikuwa safari ya sikuzote; basi leo je! Vyombo vyetu havitakuwa vitakatifu zaidi? Ndipo kuhani akampa ile mikate mitakatifu; kwa maana hapakuwa na mikate ila ile ya Wonyesho, nayo imekwisha kuondolewa mbele za BWANA, ili itiwe mikate ya moto siku ile ilipoondolewa. Basi siku ile palikuwapo na mtu mmoja wa watumishi wa Sauli, amezuiwa hapo mbele za BWANA jina lake akiitwa Doegi, Mwedomi, mkubwa wa wachungaji wa Sauli. Tena Daudi akamwambia Ahimeleki, Na hapa chini ya mkono wako, je! Hapana mkuki, au upanga? Kwa maana sikuleta upanga, wala silaha zangu, kwa sababu ile shughuli ya mfalme ilitaka haraka. Yule kuhani akasema, upanga wa Goliathi, yule Mfilisti, uliyemwua katika bonde la Ela, tazama, upo hapa, umefungwa ndani ya nguo nyuma ya naivera; ukipenda kuuchukua, haya! Uchukue, maana hapa hapana mwingine ila huo tu. Daudi akasema, Hapana mwingine kama ule; haya! Nipe.
1 Samueli 21:1-9 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Daudi akaenda Nobu, kwa Ahimeleki kuhani. Ahimeleki akatetemeka alipokutana naye, akamuuliza, “Kwa nini uko peke yako? Kwa nini hukufuatana na mtu yeyote?” Daudi akamjibu Ahimeleki kuhani, akisema, “Mfalme ameniagiza shughuli fulani na kuniambia, ‘Mtu yeyote asijue chochote kuhusu kazi niliyokutuma kuifanya, wala maagizo niliyokupa!’ Kuhusu watu wangu, nimewaambia mahali pa kukutana. Sasa basi, una nini mkononi? Nipatie mikate mitano au chochote unachoweza kupata.” Lakini kuhani akamjibu Daudi, “Sina mkate wowote wa kawaida kwa sasa. Hata hivyo, ipo hapa mikate iliyowekwa wakfu, iwapo watu wamejitenga na wanawake.” Daudi akajibu, “Hakika tumejitenga na wanawake kwa siku hizi chache kama kawaida ya ninapotoka kwenda kwenye shughuli. Navyo vyombo vya wale vijana huwa ni vitakatifu hata kwenye safari ya kawaida, si zaidi sana leo vyombo vyao vitakuwa ni vitakatifu?” Hivyo kuhani akampa ile mikate iliyowekwa wakfu, kwa kuwa hapakuwa na mikate mingine isipokuwa hiyo ya Wonesho, iliyokuwa imeondolewa hapo mbele za BWANA na kubadilishwa na mingine yenye moto siku ile ilipoondolewa. Basi siku hiyo palikuwepo mmoja wa watumishi wa Sauli, aliyezuiliwa mbele za BWANA; alikuwa Doegi Mwedomu, kiongozi wa wachungaji wa Sauli. Daudi akamuuliza Ahimeleki, “Je, unao mkuki au upanga hapa? Sikuleta upanga wala silaha nyingine yoyote, kwa sababu shughuli ya mfalme ilikuwa ya haraka.” Kuhani akajibu, “Upanga wa Goliathi Mfilisti, ambaye ulimuua katika Bonde la Ela, upo hapa, umefungwa katika kitambaa nyuma ya kizibau. Kama unauhitaji, uchukue, hakuna upanga mwingine hapa ila huo tu.” Daudi akasema, “Hakuna upanga mwingine kama huo. Nipatie huo.”