1 Samueli 2:1-26
1 Samueli 2:1-26 Biblia Habari Njema (BHN)
Halafu Hana aliomba na kusema: “Namshangilia Mwenyezi-Mungu moyoni mwangu. Namtukuza Mwenyezi-Mungu aliye nguvu yangu. Nawacheka adui zangu; maana naufurahia ushindi wangu. “Hakuna aliye mtakatifu kama Mwenyezi-Mungu; hakuna yeyote aliye kama yeye; hakuna aliye mwamba kama Mungu wetu. Acheni kujisifu, acheni kusema ufidhuli. Maana ajuaye ni Mwenyezi-Mungu. Yeye huyapima matendo yote. Pinde za wenye nguvu zimevunjika. Lakini wadhaifu wanaendelea kupata nguvu. Wale ambao zamani walikuwa na chakula tele, sasa wanaajiriwa ili wapate chakula. Lakini waliokuwa na njaa, sasa hawana njaa tena. Mwanamke tasa amejifungua watoto saba. Lakini mama mwenye watoto wengi, sasa ameachwa bila mtoto. Mwenyezi-Mungu huua na hufufua; yeye huwashusha chini kuzimu naye huwarudisha tena. Mwenyezi-Mungu huwafanya baadhi wawe maskini, na baadhi wawe matajiri. Wengine huwashusha, na wengine huwakweza. Huwainua maskini toka mavumbini; huwanyanyua wahitaji toka majivuni, akawaketisha pamoja na wakuu, na kuwarithisha viti vya heshima. Maana, minara ya dunia ni ya Mwenyezi-Mungu; yeye ameisimika dunia juu ya minara yake. “Maisha ya waaminifu wake huyalinda, lakini maisha ya waovu huyakatilia mbali gizani. Maana, binadamu hapati ushindi kwa nguvu zake. Maadui wa Mwenyezi-Mungu watavunjwa vipandevipande; atanguruma dhidi yao kama radi mbinguni. Mwenyezi-Mungu ataihukumu dunia yote; atampa nguvu mfalme wake ataukuza uwezo wa mteule wake.” Kisha, Elkana akarudi nyumbani Rama. Lakini mtoto Samueli akabaki Shilo kumtumikia Mwenyezi-Mungu chini ya uongozi wa kuhani Eli. Watoto wa kiume wa Eli walikuwa walaghai sana. Hawakumjali Mwenyezi-Mungu wala juu ya vitu ambavyo watu walipaswa kuwapa makuhani. Kila mara mtu alipokuwa anatolea tambiko yake, mtumishi wa kuhani alikuja na uma wenye meno matatu; na wakati nyama ikiwa bado inachemka, huyo mtumishi aliuchomeka uma huo ndani ya chungu, nyama yoyote iliyotolewa humo na uma huo, ilikuwa mali ya kuhani. Waisraeli wote waliokwenda Shilo kutolea tambiko zao walitendewa hivyo. Zaidi ya hayo, hata kabla mafuta hayajachomwa, mtumishi wa kuhani huja na kumwambia yule mtu anayetoa tambiko, “Mtolee kuhani nyama ya kubanika maana yeye hatapokea nyama yako iliyochemshwa, bali iliyo mbichi.” Na kama mtu huyo akimjibu, “Ngojea kwanza nichome mafuta halafu utachukua kiasi chochote unachotaka,” hapo huyo mtumishi wa kuhani humjibu, “La, ni lazima unipe sasa hivi. La sivyo, nitaichukua kwa nguvu.” Dhambi hii ya vijana hao wa Eli ilikuwa kubwa sana mbele ya Mwenyezi-Mungu. Maana, vijana hao walidharau matoleo ya Mwenyezi-Mungu. Wakati huo, kijana Samueli aliendelea kumtumikia Mwenyezi-Mungu, akiwa amevaa kizibao cha kitani. Kila mwaka mama yake alimfumia vazi dogo, na kumpelekea alipokuwa akienda na mumewe kutolea tambiko ya kila mwaka. Eli aliwabariki Elkana na mkewe, akisema, “Mwenyezi-Mungu na akupe wewe Elkana watoto wengine kwa mwanamke huyu ili wachukue mahali pa yule uliyempa Mwenyezi-Mungu.” Kisha wao hurudi nyumbani. Mwenyezi-Mungu alimhurumia Hana naye akajaliwa kupata watoto wa kiume watatu na mabinti wawili. Mtoto Samueli akaendelea kukua mbele ya Mwenyezi-Mungu. Wakati huo Eli alikuwa mzee sana. Aliposikia yote ambayo watoto wake wa kiume walikuwa wanawatendea Waisraeli, jinsi walivyokuwa wanalala na wanawake waliokuwa wanahudumu kwenye mlango wa hema la mkutano, aliwauliza, “Kwa nini mnafanya mambo haya? Nasikia kutoka kwa watu wote juu ya maovu mnayoyafanya. Msifanye hivyo wanangu kwa sababu mambo hayo ninayoyasikia kutoka kwa watu wa Mwenyezi-Mungu ni mabaya. Mtu akimkosea mwenzake, anaweza kuombewa kwa Mungu, ili Mungu amsamehe. Lakini mtu akimkosea Mwenyezi-Mungu nani awezaye kumwombea msamaha?” Lakini watoto hao hawakumsikiliza baba yao, kwani Mwenyezi-Mungu alikwisha kata shauri kuwaua. Mtoto Samueli aliendelea kukua, akazidi kupendwa na Mwenyezi-Mungu na watu.
1 Samueli 2:1-26 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Naye Hana akaomba, akasema, Moyo wangu wamshangilia BWANA, Pembe yangu imetukuka katika BWANA, Kinywa changu kimepanuka juu ya adui zangu; Kwa kuwa naufurahia wokovu wako; Hakuna aliye mtakatifu kama BWANA; Kwa maana hakuna yeyote ila wewe, Wala hakuna mwamba kama Mungu wetu. Msizidi kunena kwa kutakabari hivyo; Majivuno yasitoke vinywani mwenu; Kwa kuwa BWANA ni Mungu wa maarifa, Naye huyapima matendo kwa mizani. Pinde zao mashujaa zimevunjika, Na hao waliojikwaa wamepata nguvu. Walioshiba wamejikodisha ili kupata chakula, Lakini waliokuwa na njaa sasa hawana njaa tena. Naam, huyo aliyekuwa tasa amezaa watoto saba, lakini aliye na watoto wengi amehuzunika. BWANA huua, naye hufanya kuwa hai; Hushusha hadi kuzimu, tena huleta juu. BWANA hufukarisha mtu, na hutajirisha; Hushusha chini, tena huinua juu. Humwinua mnyonge kutoka mavumbini, Humpandisha mhitaji kutoka jaani, Ili awaketishe pamoja na wakuu, Wakakirithi kiti cha enzi cha utukufu; Kwa maana nguzo za dunia zina BWANA, Naye ameuweka ulimwengu juu yake. Yeye atailinda miguu ya watakatifu wake; Bali waovu watanyamazishwa gizani, Maana kwa nguvu hakuna atakayeshinda; Washindanao na BWANA watapondwa kabisa; Toka mbinguni yeye atawapigia radi; BWANA ataihukumu dunia yote; Naye atampa mfalme wake nguvu, Na kuitukuza pembe ya masihi wake. Kisha Elkana akaenda Rama nyumbani kwake. Na yule mtoto akamtumikia BWANA mbele yake Eli, kuhani. Basi, hao wana wa Eli walikuwa watu wasiofaa kitu; hawakumjali BWANA, wala haki ya makuhani ilivyokuwa kwa watu. Wakati huo mtu yeyote alipotoa dhabihu wakati wowote, ndipo huja mtumishi wa kuhani, nyama ilipokuwa katika kutokota, naye akawa na uma wa meno matatu mkononi mwake; naye huutia kwa nguvu humo chunguni, au birikani, au sufuriani, au chomboni; nyama yote iliyoinuliwa kwa huo uma kuhani huichukua mwenyewe. Ndivyo walivyofanya huko Shilo kwa Waisraeli wote waliokuja huko. Tena, kabla ya kuteketeza mafuta, huja mtumishi wa kuhani, akamwambia yule mwenye kuitoa dhabihu, Mtolee kuhani nyama ya kuoka; kwa kuwa hataki kupewa nyama iliyotokoswa, bali nyama mbichi. Tena, ikiwa mtu yule amwambia, Hawakosi wataichoma moto hayo mafuta kwanza, kisha utwae kadiri roho yako itakavyopenda; ndipo husema, Sivyo, lakini sharti unipe sasa hivi; la, hunipi, basi nitaitwaa kwa nguvu. Hivyo dhambi yao wale vijana ilikuwa kubwa sana machoni pa BWANA; kwa maana hao watu walidharau sadaka ya BWANA. Lakini Samweli alikuwa akitumika mbele za BWANA, naye alikuwa kijana aliyevaa naivera ya kitani. Tena mamaye alimshonea kanzu ndogo, na kumletea kila mwaka, hapo alipokwea pamoja na mumewe ili kutoa dhabihu kila mwaka. Naye Eli akambariki Elkana na mkewe, akasema, BWANA na akupe uzao kwa mwanamke huyu, wachukue mahali pa yule aliyemtoa kwa BWANA. Kisha wakarudi nyumbani kwao. Naye BWANA akamwangalia Hana, naye akachukua mimba, akazaa watoto, watatu wa kiume na wawili wa kike. Naye huyo mtoto Samweli akakua mbele za BWANA. Basi Eli alikuwa mzee sana; naye alisikia habari za mambo yote ambayo wanawe waliwatenda Waisraeli; na jinsi walivyolala na wanawake waliokuwa wakitumika mlangoni pa hema ya kukutania. Akawaambia, Mbona mnatenda mambo kama hayo? Maana nasikia habari za matendo yenu mabaya kwa watu hawa wote. Sivyo hivyo, wanangu, kwa maana habari hii ninayoisikia si habari njema; mnawakosesha watu wa BWANA. Mtu mmoja akimkosea mwenzake, Mungu atamhukumu; lakini mtu akimkosea BWANA, ni nani atakayemtetea? Lakini hawakuisikia sauti ya baba yao, kwa sababu BWANA amekusudia kuwaua. Na yule mtoto, Samweli, akazidi kukua akapata kibali kwa BWANA, na kwa watu pia.
1 Samueli 2:1-26 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Naye Hana akaomba, akasema, Moyo wangu wamshangilia BWANA, Pembe yangu imetukuka katika BWANA, Kinywa changu kimepanuka juu ya adui zangu; Kwa kuwa naufurahia wokovu wako; Hakuna aliye mtakatifu kama BWANA; Kwa maana hakuna ye yote ila wewe, Wala hakuna mwamba kama Mungu wetu. Msizidi kunena kwa kutakabari hivyo; Majivuno yasitoke vinywani mwenu; Kwa kuwa BWANA ni Mungu wa maarifa, Na matendo hupimwa na yeye kwa mizani. Pinde zao mashujaa zimevunjika, Na hao waliojikwaa wamefungiwa nguvu. Walioshiba wamejikodisha ili kupata chakula, Na hao waliokuwa na njaa wamepata raha. Naam, huyo aliyekua tasa amezaa watoto saba, Na yeye aliye na wana wengi amedhoofika. BWANA huua, naye hufanya kuwa hai; Hushusha hata kuzimu, tena huleta juu. BWANA hufukarisha mtu, naye hutajirisha; Hushusha chini, tena huinua juu. Humwinua mnyonge kutoka mavumbini, Humpandisha mhitaji kutoka jaani, Ili awaketishe pamoja na wakuu, Wakakirithi kiti cha enzi cha utukufu; Kwa maana nguzo za dunia zina BWANA, Naye ameuweka ulimwengu juu yake. Yeye atailinda miguu ya watakatifu wake; Bali waovu watanyamazishwa gizani, Maana kwa nguvu hakuna atakayeshinda; Washindanao na BWANA watapondwa kabisa; Toka mbinguni yeye atawapigia radi; BWANA ataihukumu miisho ya dunia; Naye atampa mfalme wake nguvu, Na kuitukuza pembe ya masihi wake. Kisha Elkana akaenda Rama nyumbani kwake. Na yule mtoto akamtumikia BWANA mbele yake Eli, kuhani. Basi, hao wana wa Eli walikuwa watu wasiofaa kitu; hawakumjali BWANA, wala haki ya makuhani ilivyokuwa kwa watu. Wakati huo mtu ye yote alipotoa dhabihu wakati wo wote, ndipo huja mtumishi wa kuhani, nyama ilipokuwa katika kutokota, naye akawa na uma wa meno matatu mkononi mwake; naye huutia kwa nguvu humo chunguni, au birikani, au sufuriani, au chomboni; nyama yote iliyoinuliwa kwa huo uma kuhani huichukua mwenyewe. Ndivyo walivyofanya huko Shilo kwa Waisraeli wote waliokuja huko. Tena, kabla ya kuteketeza mafuta, huja mtumishi wa kuhani, akamwambia yule mwenye kuitoa dhabihu, Mtolee kuhani nyama ya kuoka; kwa kuwa hataki kupewa nyama iliyotokoswa, bali nyama mbichi. Tena, ikiwa mtu yule amwambia, Hawakosi wataichoma moto hayo mafuta kwanza, kisha utwae kadiri roho yako itakavyopenda; ndipo husema, Sivyo, lakini sharti unipe sasa hivi; la, hunipi, basi nitaitwaa kwa nguvu. Hivyo dhambi yao wale vijana ilikuwa kubwa sana machoni pa BWANA; kwa maana hao watu walidharau sadaka ya BWANA. Lakini Samweli alikuwa akitumika mbele za BWANA, naye alikuwa kijana, mwenye kuvaa naivera ya kitani. Tena mamaye humfanyizia kanzu ndogo, na kumletea mwaka kwa mwaka, hapo alipokwea pamoja na mumewe ili kutoa dhabihu kila mwaka. Naye Eli akambariki Elkana na mkewe, akasema, BWANA na akupe uzao kwa mwanamke huyu, badala ya azimo aliloazimiwa BWANA. Kisha wakaenda nyumbani kwao. Naye BWANA akamwangalia Hana, naye akachukua mimba, akazaa watoto, wa kiume watatu na wa kike wawili. Naye huyo mtoto Samweli akakua mbele za BWANA. Basi Eli alikuwa mzee sana; naye alisikia habari za mambo yote ambayo wanawe waliwatenda Waisraeli; na jinsi walivyolala na wanawake waliokuwa wakitumika mlangoni pa hema ya kukutania. Akawaambia, Mbona mnatenda mambo kama hayo? Maana nasikia habari za matendo yenu mabaya kwa watu hawa wote. Sivyo hivyo, wanangu, kwa maana habari hii ninayoisikia si habari njema; mnawakosesha watu wa BWANA. Mtu mmoja akimkosa mwenzake, Mungu atamhukumu; lakini mtu akimkosa BWANA, ni nani atakayemtetea? Lakini hawakuisikia sauti ya baba yao, kwa sababu BWANA amekusudia kuwaua. Na yule mtoto, Samweli, akazidi kukua akapata kibali kwa BWANA, na kwa watu pia.
1 Samueli 2:1-26 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Kisha Hana akaomba na kusema: “Moyo wangu wamshangilia BWANA, katika BWANA pembe yangu imeinuliwa juu. Kinywa changu chajisifu juu ya adui zangu, kwa kuwa naufurahia wokovu wako. “Hakuna yeyote aliye mtakatifu kama BWANA, hakuna mwingine zaidi yako; hakuna Mwamba kama Mungu wetu. “Msiendelee kusema kwa kiburi hivyo wala msiache vinywa vyenu kunena kwa kiburi, kwa kuwa BWANA ndiye Mungu ajuaye, na yeye hupima matendo. “Pinde za mashujaa zimevunjika, lakini wale wanaojikwaa wamevikwa nguvu. Wale waliokuwa na chakula tele wamejikodisha wenyewe ili kupata chakula, lakini wale waliokuwa na njaa hawana njaa tena. Mwanamke yule aliyekuwa tasa amezaa watoto saba, lakini yule aliyekuwa na wana wengi amedhoofika. “BWANA huua na huhuisha; yeye hushusha hadi kaburini na hufufua. BWANA humfanya mtu maskini naye hutajirisha, hushusha na hukweza. Humwinua maskini kutoka mavumbini na humwinua mhitaji kutoka lundo la majivu; huwaketisha pamoja na wakuu, na kuwafanya warithi kiti cha utawala cha heshima. “Kwa kuwa misingi ya dunia ni ya BWANA; juu yake ameuweka ulimwengu. Yeye atailinda miguu ya watakatifu wake, lakini waovu watanyamazishwa kwenye giza. “Si kwa nguvu mtu hushinda; wale wampingao BWANA wataharibiwa kabisa. Atapiga radi dhidi yao kutoka mbinguni; BWANA ataihukumu miisho ya dunia. “Atampa nguvu mfalme wake, na kuitukuza pembe ya mpakwa mafuta wake.” Kisha Elkana akaenda nyumbani Rama, lakini mtoto akahudumu mbele za BWANA chini ya kuhani Eli. Wana wa Eli walikuwa watu waovu kabisa, hawakumheshimu BWANA. Basi ilikuwa desturi ya makuhani pamoja na watu kwamba kila mara yeyote anapotoa dhabihu na huku nyama ikiwa inachemshwa, mtumishi wa kuhani angekuja na uma wenye meno matatu mkononi mwake. Angeutumbukiza huo uma kwenye sufuria au birika au sufuria kubwa au chungu, naye kuhani angejichukulia chochote uma ungekileta. Hivi ndivyo walivyowatendea Waisraeli wote waliokuja Shilo. Lakini hata kabla mafuta ya mnyama hayajachomwa, mtumishi wa kuhani angekuja na kusema kwa mtu aliyekuwa akitoa dhabihu, “Mpe kuhani nyama akaoke, kwani hatapokea nyama iliyochemshwa kutoka kwako, ila iliyo mbichi tu.” Mtu yule akimwambia, “Mafuta ya mnyama na yachomwe kwanza, ndipo uchukue chochote unachotaka,” mtumishi angejibu, “Hapana, nipe sasa; kama hunipi, nitaichukua kwa nguvu.” Hii dhambi ya hawa vijana ilikuwa kubwa sana machoni pa BWANA, kwa kuwa waliitendea dhabihu ya BWANA kwa dharau. Lakini Samweli alikuwa akihudumu mbele za BWANA, kijana akivaa kizibau cha kitani. Kila mwaka mama yake alimshonea joho dogo na kumpelekea alipokwea pamoja na mumewe kutoa dhabihu ya mwaka. Eli alikuwa akiwabariki Elkana na mkewe, akisema, “BWANA na akupe watoto kwa mwanamke huyu ili kuchukua nafasi ya yule aliyekuwa amemwomba na akamtoa kwa BWANA.” Kisha wakawa wanaenda nyumbani. BWANA akawa mwenye neema kwa Hana, naye akapata mimba akazaa wana wa kiume watatu na binti wawili. Wakati huo, kijana Samweli akaendelea kukua mbele za BWANA. Basi Eli, aliyekuwa mzee sana, alisikia kuhusu kila kitu ambacho wanawe walikuwa wakiwafanyia Israeli wote na jinsi walivyokutana kimwili na wanawake waliohudumu kwenye ingilio la Hema la Kukutania. Hivyo akawaambia, “Kwa nini mmefanya mambo kama haya? Nimesikia kutoka kwa watu wote kuhusu haya matendo yenu maovu. Sivyo, wanangu, hii si habari nzuri ninayosikia ikienea miongoni mwa watu wa BWANA. Mtu akifanya dhambi dhidi ya mtu mwenzake, mtu mwingine aweza kumwombea kwa Mungu, lakini kama mtu akimfanyia Mungu dhambi, ni nani atakayemwombea?” Hata hivyo wanawe hawakusikia maonyo ya baba yao, kwa sababu BWANA alitaka kuwaua. Naye kijana Samweli akaendelea kukua katika kimo, akimpendeza BWANA na wanadamu.