1 Samueli 18:6-16
1 Samueli 18:6-16 Biblia Habari Njema (BHN)
Askari walipokuwa wanarudi nyumbani, pamoja na Daudi baada ya kumwua yule Mfilisti, wanawake kutoka kila mji katika Israeli walitoka kwenda kumlaki mfalme Shauli. Wanawake nao walikuwa wanaimba nyimbo za furaha, wakipiga matari na vinubi. Pia walikuwa wanacheza na kuimba nyimbo za kuitikiana hivi: “Shauli ameua maelfu yake, na Daudi ameua makumi elfu yake.” Shauli hakupendezwa na maneno ya wimbo huo, hivyo akakasirika sana. Akasema, “Wamempa Daudi makumi elfu, lakini mimi wamenipa maelfu tu. Lililobakia ni kumpa Daudi ufalme.” Tangu siku hiyo, Shauli akawa anamwonea kijicho Daudi. Kesho yake, roho mwovu kutoka kwa Mungu, alimvamia Shauli kwa ghafla, akawa anapayukapayuka kama mwendawazimu nyumbani kwake. Daudi alikuwa anapiga kinubi kama alivyofanya siku zote. Shauli alikuwa na mkuki mkononi mwake; basi, alimtupia Daudi mkuki mara mbili kwani alifikiri, “Nitambana Daudi ukutani.” Lakini Daudi alikwepa mara zote mbili. Shauli alikuwa anamwogopa Daudi kwa kuwa Mwenyezi-Mungu alikuwa pamoja naye, lakini Mwenyezi-Mungu alikuwa amemwacha Shauli. Hivyo, Shauli akamwondoa na kumfanya kiongozi wa wanajeshi 1,000. Naye Daudi akawaongoza vyema vitani. Daudi alifanikiwa katika kila kitu alichofanya, kwani Mwenyezi-Mungu alikuwa pamoja naye. Shauli alipoona kufanikiwa kwa Daudi, akawa anamwogopa. Lakini watu wote wa Israeli na Yuda walimpenda Daudi, kwani aliwaongoza vizuri vitani na kuwarudisha kwa mafanikio.
1 Samueli 18:6-16 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Hata ikawa, walipokuwa wakienda, hapo Daudi aliporudi baada ya kumwua yule Mfilisti, wanawake wakatoka katika miji yote ya Israeli, kwa kuimba na kucheza, ili kumlaki mfalme Sauli; wakatoka na matari, na shangwe, na vinanda. Nao wale wanawake wakaitikiana wakicheza, wakasema, Sauli amewaua elfu zake, Na Daudi makumi elfu yake. Basi Sauli akaghadhibika sana, na maneno haya yakamchukiza; akasema, Wamempa Daudi makumi elfu, na mimi wamenipa elfu tu; kuna nini tena awezayo kupata, isipokuwa ni ufalme? Sauli akamwonea Daudi wivu tangu siku ile. Ikawa siku ya pili yake, roho mbaya kutoka kwa Mungu ikamjia Sauli kwa nguvu, naye akatabiri ndani ya nyumba. Basi Daudi alikuwa akipiga kinubi kwa mkono wake kama siku zote; naye Sauli alikuwa na mkuki mkononi mwake. Mara Sauli akautupa ule mkuki; maana alisema, Nitampiga Daudi hadi ukutani. Daudi akaepa, mara mbili. Sauli akamwogopa Daudi, kwa sababu BWANA alikuwa pamoja naye, ila amemwacha Sauli. Kwa ajili ya hayo Sauli akamwondosha kwake, akamfanya awe kamanda wake juu ya askari elfu moja; naye akatoka na kuingia mbele ya watu. Naye Daudi akatenda kwa busara katika njia zake zote naye BWANA alikuwa pamoja naye. Sauli alipoona ya kwamba alitenda kwa busara sana, yeye alimwogopa. Lakini Israeli wote na Yuda wakampenda Daudi; kwa kuwa aliwaongoza wakienda na kurudi vitani.
1 Samueli 18:6-16 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Hata ikawa, walipokuwa wakienda, hapo Daudi aliporudi baada ya kumwua yule Mfilisti, wanawake wakatoka katika miji yote ya Israeli, kwa kuimba na kucheza, ili kumlaki mfalme Sauli; wakatoka na matari, na shangwe, na vinanda. Nao wale wanawake wakaitikiana wakicheza, wakasema, Sauli amewaua elfu zake, Na Daudi makumi elfu yake. Basi Sauli akaghadhibika sana, na maneno haya yakamchukiza; akasema, Wamempa Daudi makumi elfu, na mimi wamenipa elfu tu; kuna nini tena awezayo kupata, isipokuwa ni ufalme? Sauli akamwonea Daudi wivu tangu siku ile. Ikawa siku ya pili yake, roho mbaya kutoka kwa Mungu ikamjilia Sauli kwa nguvu, naye akatabiri ndani ya nyumba. Basi Daudi alikuwa akipiga kinubi kwa mkono wake kama siku zote; naye Sauli alikuwa na mkuki mkononi mwake. Mara Sauli akautupa ule mkuki; maana alisema, Nitampiga Daudi hata ukutani. Daudi akaepa, akatoka mbele yake, mara mbili. Sauli akamwogopa Daudi, kwa sababu BWANA alikuwa pamoja naye, ila amemwacha Sauli. Kwa ajili ya hayo Sauli akamwondosha kwake, akamfanya awe akida wake juu ya askari elfu; naye akatoka na kuingia mbele ya watu. Naye Daudi akatenda kwa busara katika njia zake zote naye BWANA alikuwa pamoja naye. Sauli alipoona ya kwamba alitenda kwa busara sana, yeye alimwogopa. Lakini Israeli wote na Yuda wakampenda Daudi; kwa kuwa alitoka na kuingia mbele yao.
1 Samueli 18:6-16 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Watu walipokuwa wanarudi nyumbani baada ya Daudi kumuua yule Mfilisti, wanawake wakaja kutoka pande zote za miji ya Israeli kumlaki Mfalme Sauli kwa kuimba na kucheza, kwa nyimbo za furaha na kwa matari na zeze. Walipokuwa wanacheza, wakaimba: “Sauli amewaua elfu zake, naye Daudi makumi elfu yake.” Sauli akakasirika sana; sehemu hii ya kurudia rudia ya wimbo huu ilimkasirisha sana. Akafikiri kuwa, “Wamempa Daudi makumi elfu, lakini mimi wamenipa elfu tu. Apate nini zaidi isipokuwa ufalme?” Kuanzia wakati ule na kuendelea Sauli akawa na jicho la wivu juu ya Daudi. Kesho yake roho mbaya iliyoachiwa nafasi na Mungu ikaja kwa nguvu juu ya Sauli. Alikuwa akitabiri nyumbani mwake, wakati Daudi alikuwa akipiga kinubi, kama alivyozoea. Sauli alikuwa na mkuki mkononi mwake; akautupa kwa nguvu, akijiambia mwenyewe, “Nitamchoma kwa mkuki abaki hapo ukutani.” Lakini Daudi akamkwepa mara mbili. Sauli akamwogopa Daudi, kwa sababu BWANA alikuwa pamoja na Daudi, lakini alikuwa amemwacha yeye. Kwa hiyo Sauli akamwondoa Daudi mbele yake na kumpa kuwa kiongozi wa watu elfu moja, naye Daudi akatoka na kuingia akiongoza vikosi katika vita. Katika kila kitu alichofanya, Daudi alipata mafanikio makubwa, kwa sababu BWANA alikuwa pamoja naye. Sauli alipoona jinsi alivyokuwa akifanikiwa, akamwogopa. Lakini Israeli wote na Yuda walimpenda Daudi, kwa sababu ndiye alikuwa akiwaongoza katika vita vyao.