1 Samueli 18:1-30
1 Samueli 18:1-30 Biblia Habari Njema (BHN)
Shauli alipomaliza kuzungumza na Daudi, Yonathani mwana wa Shauli, alivutiwa sana na Daudi, akampenda kwa moyo wake wote kama alivyojipenda yeye mwenyewe. Tangu siku hiyo, Shauli akamchukua Daudi nyumbani kwake, asimruhusu kurudi nyumbani kwa baba yake. Kwa kuwa Yonathani alimpenda Daudi kama roho yake, alifanya agano naye. Alivua vazi alilovaa na kumpa Daudi pamoja na silaha zake, hata upanga, upinde na mkanda wake. Kokote Daudi alikotumwa na Shauli, Daudi alifanikiwa. Hivyo, Shauli akamfanya kuwa mkuu wa jeshi lake. Jambo hilo liliwafurahisha watu wote hata watumishi wa Shauli. Askari walipokuwa wanarudi nyumbani, pamoja na Daudi baada ya kumwua yule Mfilisti, wanawake kutoka kila mji katika Israeli walitoka kwenda kumlaki mfalme Shauli. Wanawake nao walikuwa wanaimba nyimbo za furaha, wakipiga matari na vinubi. Pia walikuwa wanacheza na kuimba nyimbo za kuitikiana hivi: “Shauli ameua maelfu yake, na Daudi ameua makumi elfu yake.” Shauli hakupendezwa na maneno ya wimbo huo, hivyo akakasirika sana. Akasema, “Wamempa Daudi makumi elfu, lakini mimi wamenipa maelfu tu. Lililobakia ni kumpa Daudi ufalme.” Tangu siku hiyo, Shauli akawa anamwonea kijicho Daudi. Kesho yake, roho mwovu kutoka kwa Mungu, alimvamia Shauli kwa ghafla, akawa anapayukapayuka kama mwendawazimu nyumbani kwake. Daudi alikuwa anapiga kinubi kama alivyofanya siku zote. Shauli alikuwa na mkuki mkononi mwake; basi, alimtupia Daudi mkuki mara mbili kwani alifikiri, “Nitambana Daudi ukutani.” Lakini Daudi alikwepa mara zote mbili. Shauli alikuwa anamwogopa Daudi kwa kuwa Mwenyezi-Mungu alikuwa pamoja naye, lakini Mwenyezi-Mungu alikuwa amemwacha Shauli. Hivyo, Shauli akamwondoa na kumfanya kiongozi wa wanajeshi 1,000. Naye Daudi akawaongoza vyema vitani. Daudi alifanikiwa katika kila kitu alichofanya, kwani Mwenyezi-Mungu alikuwa pamoja naye. Shauli alipoona kufanikiwa kwa Daudi, akawa anamwogopa. Lakini watu wote wa Israeli na Yuda walimpenda Daudi, kwani aliwaongoza vizuri vitani na kuwarudisha kwa mafanikio. Shauli akamwambia Daudi, “Huyu ni Merabu, binti yangu mkubwa, nitakuoza awe mke wako kwa masharti mawili: Uwe askari wangu shupavu na mtiifu, upigane vita vya Mwenyezi-Mungu.” [Shauli alidhani kwa njia hiyo Wafilisti watamuua Daudi, ili kitendo hicho asikifanye yeye mwenyewe.] Daudi akamwambia Shauli, “Mimi ni nani hata mfalme awe baba mkwe wangu? Ukoo wangu wenyewe na hata jamaa ya baba yangu si maarufu katika Israeli.” Lakini, wakati ule ambapo Merabu binti yake Shauli angeozwa kwa Daudi, aliozwa kwa Adrieli kutoka mji wa Mehola. Hata hivyo, Mikali binti mwingine wa Shauli alimpenda Daudi. Shauli alipoambiwa alifurahi sana. Shauli alifikiri, “Ngoja nimwoze huyu ili awe mtego kwake. Na bila shaka Wafilisti watamuua.” Hivyo Shauli akamwambia Daudi mara ya pili, “Sasa nitakuwa baba mkwe wako.” Halafu Shauli aliwaamuru watumishi wake akisema “Ongea faraghani na Daudi na kumwambia, ‘Mfalme anapendezwa sana nawe, hata watumishi wake pia wote wanakupenda’. Hivyo, sasa kubali kuwa mkwewe mfalme.” Basi, watumishi hao wa Shauli walimwambia Daudi maneno hayo faraghani, naye akawaambia, “Mimi ni mtu maskini na duni. Je mnadhani mfalme kuwa baba mkwe wangu ni jambo rahisi?” Wale watumishi walimweleza Shauli kama Daudi alivyosema. Shauli akawaambia, “Mwambieni Daudi hivi: ‘Kile ambacho mfalme anataka kama mahari ya binti yake ni magovi 100 ya Wafilisti, ili ajilipize kisasi cha adui zake.’” [Hivi ndivyo Shauli alivyopanga Daudi auawe na Wafilisti.] Wale watumishi walipomweleza Daudi yale matakwa ya Shauli, Daudi alifurahi kuwa mfalme atakuwa baba mkwe wake. Kabla ya siku ya harusi, Daudi na watu wake walikwenda, wakawaua Wafilisti 200 na kuyachukua magovi yao mpaka kwa mfalme Shauli. Hapo akamhesabia idadi kamili ili mfalme awe baba mkwe wake Daudi. Hivyo, Shauli akamwoza Daudi binti yake Mikali awe mke wake. Lakini Shauli alipoona wazi kwamba Mwenyezi-Mungu alikuwa pamoja na Daudi, na kuwa Mikali binti yake alimpenda mno Daudi, alizidi kumwogopa Daudi. Shauli akawa adui wa Daudi daima. Jeshi la Wafilisti lilikwenda kupigana na Waisraeli, lakini kila mara walipopigana vita, Daudi alipata ushindi kuliko watumishi wa Shauli; hivyo jina lake Daudi likazidi kusifiwa sana.
1 Samueli 18:1-30 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ikawa Daudi alipokwisha kusema na Sauli, roho ya Yonathani, ikaambatana na roho ya Daudi, Yonathani akampenda kama roho yake mwenyewe. Sauli akamtwaa siku ile, wala hakumwacha arudi tena nyumbani kwa baba yake. Nao Yonathani na Daudi wakaahidiana, kwa kuwa alimpenda kama roho yake mwenyewe. Ndipo Yonathani akalivua joho alilokuwa amelivaa, akampa Daudi, na mavazi yake, hata na upanga wake pia, na upinde wake, na mshipi wake. Basi Daudi akatoka kwenda kila mahali alikotumwa na Sauli, akatenda kwa akili; Sauli akamweka juu ya watu wa vita; jambo hili likawa jema machoni pa watu wote, na machoni pa watumishi wa Sauli pia. Hata ikawa, walipokuwa wakienda, hapo Daudi aliporudi baada ya kumwua yule Mfilisti, wanawake wakatoka katika miji yote ya Israeli, kwa kuimba na kucheza, ili kumlaki mfalme Sauli; wakatoka na matari, na shangwe, na vinanda. Nao wale wanawake wakaitikiana wakicheza, wakasema, Sauli amewaua elfu zake, Na Daudi makumi elfu yake. Basi Sauli akaghadhibika sana, na maneno haya yakamchukiza; akasema, Wamempa Daudi makumi elfu, na mimi wamenipa elfu tu; kuna nini tena awezayo kupata, isipokuwa ni ufalme? Sauli akamwonea Daudi wivu tangu siku ile. Ikawa siku ya pili yake, roho mbaya kutoka kwa Mungu ikamjia Sauli kwa nguvu, naye akatabiri ndani ya nyumba. Basi Daudi alikuwa akipiga kinubi kwa mkono wake kama siku zote; naye Sauli alikuwa na mkuki mkononi mwake. Mara Sauli akautupa ule mkuki; maana alisema, Nitampiga Daudi hadi ukutani. Daudi akaepa, mara mbili. Sauli akamwogopa Daudi, kwa sababu BWANA alikuwa pamoja naye, ila amemwacha Sauli. Kwa ajili ya hayo Sauli akamwondosha kwake, akamfanya awe kamanda wake juu ya askari elfu moja; naye akatoka na kuingia mbele ya watu. Naye Daudi akatenda kwa busara katika njia zake zote naye BWANA alikuwa pamoja naye. Sauli alipoona ya kwamba alitenda kwa busara sana, yeye alimwogopa. Lakini Israeli wote na Yuda wakampenda Daudi; kwa kuwa aliwaongoza wakienda na kurudi vitani. Kisha Sauli akamwambia Daudi, Tazama, binti yangu mkubwa, Merabu, huyu nitakupa wewe ili umwoe; ila na wewe uniwie hodari wa vita, na kuvipiga vita vya BWANA. Maana Sauli alisema moyoni mwake, Mkono wangu usiwe juu yake, bali mkono wa Wafilisti na uwe juu yake. Naye Daudi akamwambia Sauli, Mimi ni nani, na jamaa zangu ni akina nani, au mbari ya babangu, katika Israeli, hata mimi niwe mkwewe mfalme? Lakini ikawa, wakati ule, ilipopasa Daudi apewe Merabu, binti Sauli, aliolewa na Adrieli, Mmeholathi. Walakini Mikali, binti Sauli, alimpenda Daudi; watu wakamwambia Sauli, na neno hilo likampendeza. Naye Sauli akasema moyoni, Mimi nitamwoza huyu, awe mtego kwake, tena kwamba mkono wa Wafilisti uwe juu yake. Basi Sauli akamwambia Daudi mara ya pili, Leo utakuwa mkwe wangu. Naye Sauli akawaagiza watumishi wake, Zungumzeni na Daudi kwa siri, na kusema, Angalia, mfalme anakuridhia, na watumishi wake wote wanakupenda; haya basi! Na uwe mkwewe mfalme. Nao watumishi wa Sauli wakanena maneno hayo masikioni mwa Daudi. Daudi akasema, Je! Ninyi mnaona kuwa ni shani mimi kuwa mkwewe mfalme, nami ni maskini, tena sina cheo? Na hao watumishi wa Sauli wakampasha habari, wakisema, Ndivyo hivyo alivyosema Daudi. Naye Sauli akasema, Mwambieni Daudi hivi, Mfalme hataki mahari yoyote, ila anataka govi mia moja za Wafilisti, ili ajilipize kisasi adui za mfalme. Basi Sauli alidhani kumwangamiza Daudi kwa mkono wa Wafilisti. Na watumishi wake walipomwambia Daudi; maneno hayo, ilimpendeza Daudi sana kuwa mkwewe mfalme. Na siku zilikuwa hazijaisha bado; basi Daudi akainuka, akaenda yeye na watu wake, akaua katika Wafilisti watu mia mbili; na Daudi akazileta govi zao, wakampa mfalme hesabu kamili, ili awe mkwewe mfalme. Naye Sauli akamwoza Mikali, binti yake. Sauli akaona na kutambua ya kwamba BWANA alikuwa pamoja na Daudi; na huyo Mikali, binti Sauli, akampenda. Naye Sauli akazidi kumwogopa Daudi; tangu wakati huo, Sauli akawa adui yake Daudi daima. Wakati huo wakuu wa Wafilisti wakatokeza; kisha ikawa, kila mara walipotokeza, Daudi alipata ushindi zaidi kuliko watumishi wote wa Sauli hivyo jina lake likawa na sifa kuu.
1 Samueli 18:1-30 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ikawa Daudi alipokwisha kusema na Sauli, roho ya Yonathani, ikaambatana na roho ya Daudi, Yonathani akampenda kama roho yake mwenyewe. Sauli akamtwaa siku ile, wala hakumwacha arudi tena nyumbani kwa baba yake. Nao Yonathani na Daudi wakaahidiana, kwa kuwa alimpenda kama roho yake mwenyewe. Ndipo Yonathani akalivua joho alilokuwa amelivaa, akampa Daudi, na mavazi yake, hata na upanga wake pia, na upinde wake, na mshipi wake. Basi Daudi akatoka kwenda kila mahali alikotumwa na Sauli, akatenda kwa akili; Sauli akamweka juu ya watu wa vita; jambo hili likawa jema machoni pa watu wote, na machoni pa watumishi wa Sauli pia. Hata ikawa, walipokuwa wakienda, hapo Daudi aliporudi baada ya kumwua yule Mfilisti, wanawake wakatoka katika miji yote ya Israeli, kwa kuimba na kucheza, ili kumlaki mfalme Sauli; wakatoka na matari, na shangwe, na vinanda. Nao wale wanawake wakaitikiana wakicheza, wakasema, Sauli amewaua elfu zake, Na Daudi makumi elfu yake. Basi Sauli akaghadhibika sana, na maneno haya yakamchukiza; akasema, Wamempa Daudi makumi elfu, na mimi wamenipa elfu tu; kuna nini tena awezayo kupata, isipokuwa ni ufalme? Sauli akamwonea Daudi wivu tangu siku ile. Ikawa siku ya pili yake, roho mbaya kutoka kwa Mungu ikamjilia Sauli kwa nguvu, naye akatabiri ndani ya nyumba. Basi Daudi alikuwa akipiga kinubi kwa mkono wake kama siku zote; naye Sauli alikuwa na mkuki mkononi mwake. Mara Sauli akautupa ule mkuki; maana alisema, Nitampiga Daudi hata ukutani. Daudi akaepa, akatoka mbele yake, mara mbili. Sauli akamwogopa Daudi, kwa sababu BWANA alikuwa pamoja naye, ila amemwacha Sauli. Kwa ajili ya hayo Sauli akamwondosha kwake, akamfanya awe akida wake juu ya askari elfu; naye akatoka na kuingia mbele ya watu. Naye Daudi akatenda kwa busara katika njia zake zote naye BWANA alikuwa pamoja naye. Sauli alipoona ya kwamba alitenda kwa busara sana, yeye alimwogopa. Lakini Israeli wote na Yuda wakampenda Daudi; kwa kuwa alitoka na kuingia mbele yao. Kisha Sauli akamwambia Daudi, Tazama, binti yangu mkubwa, Merabu, huyu nitakupa wewe ili umwoe; ila na wewe uniwie hodari wa vita, na kuvipiga vita vya BWANA. Maana Sauli alisema moyoni mwake, Mkono wangu usiwe juu yake, bali mkono wa Wafilisti na uwe juu yake. Naye Daudi akamwambia Sauli, Mimi ni nani, na jamaa zangu ni akina nani, au mbari ya babangu, katika Israeli, hata mimi niwe mkwewe mfalme? Lakini ikawa, wakati ule, ilipopasa Daudi apewe Merabu, binti Sauli, aliolewa na Adrieli, Mmeholathi. Walakini Mikali, binti Sauli, alimpenda Daudi; watu wakamwambia Sauli, na neno hilo likampendeza. Naye Sauli akasema moyoni, Mimi nitamwoza huyu, awe mtego kwake, tena kwamba mkono wa Wafilisti uwe juu yake. Basi Sauli akamwambia Daudi mara ya pili, Leo utakuwa mkwe wangu. Naye Sauli akawaagiza watumishi wake, Zungumzeni na Daudi kwa siri, na kusema, Angalia, mfalme anakuridhia, na watumishi wake wote wanakupenda; haya basi! Na uwe mkwewe mfalme. Nao watumishi wa Sauli wakanena maneno hayo masikioni mwa Daudi. Daudi akasema, Je! Ninyi mwaona kuwa ni shani mimi kuwa mkwewe mfalme, nami ni maskini, tena sina cheo? Na hao watumishi wa Sauli wakampasha habari, wakisema, Ndivyo hivyo alivyosema Daudi. Naye Sauli akasema, Mwambieni Daudi hivi, Mfalme hataki mahari yo yote, ila anataka govi mia za Wafilisti, ili ajilipize kisasi adui za mfalme. Basi Sauli alidhani kumwangamiza Daudi kwa mkono wa Wafilisti. Na watumishi wake walipomwambia Daudi; maneno hayo, ilimpendeza Daudi sana kuwa mkwewe mfalme. Na siku zilikuwa hazijaisha bado; basi Daudi akainuka, akaenda yeye na watu wake, akaua katika Wafilisti watu mia mbili; na Daudi akazileta govi zao, wakampa mfalme hesabu kamili, ili awe mkwewe mfalme. Naye Sauli akamwoza Mikali, binti yake. Sauli akaona na kutambua ya kwamba BWANA alikuwa pamoja na Daudi; na huyo Mikali, binti Sauli, akampenda. Naye Sauli akazidi kumwogopa Daudi; Sauli akawa adui yake Daudi sikuzote. Wakati huo wakuu wa Wafilisti wakatoka; kisha ikawa, kila mara walipotoka, Daudi akatenda kwa busara zaidi ya watumishi wote wa Sauli hivyo jina lake likawa na sifa kuu.
1 Samueli 18:1-30 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Baada ya Daudi kumaliza kuongea na Sauli, roho ya Yonathani ikaambatana na roho ya Daudi, naye akampenda kama nafsi yake mwenyewe. Kuanzia siku ile Sauli akamchukua Daudi naye hakumruhusu kurudi nyumbani mwa baba yake. Yonathani akafanya agano na Daudi kwa sababu alimpenda kama nafsi yake mwenyewe. Yonathani akavua joho alilokuwa amevaa na kumpa Daudi, pamoja na koti lake, silaha zake, hata pamoja na upanga wake, upinde wake na mshipi wake. Lolote Sauli alilomtuma Daudi kufanya, alifanikiwa sana, hata Sauli akampa cheo cha juu katika jeshi. Jambo hili likawapendeza watu wote, hata maafisa wa Sauli pia. Watu walipokuwa wanarudi nyumbani baada ya Daudi kumuua yule Mfilisti, wanawake wakaja kutoka pande zote za miji ya Israeli kumlaki Mfalme Sauli kwa kuimba na kucheza, kwa nyimbo za furaha na kwa matari na zeze. Walipokuwa wanacheza, wakaimba: “Sauli amewaua elfu zake, naye Daudi makumi elfu yake.” Sauli akakasirika sana; sehemu hii ya kurudia rudia ya wimbo huu ilimkasirisha sana. Akafikiri kuwa, “Wamempa Daudi makumi elfu, lakini mimi wamenipa elfu tu. Apate nini zaidi isipokuwa ufalme?” Kuanzia wakati ule na kuendelea Sauli akawa na jicho la wivu juu ya Daudi. Kesho yake roho mbaya iliyoachiwa nafasi na Mungu ikaja kwa nguvu juu ya Sauli. Alikuwa akitabiri nyumbani mwake, wakati Daudi alikuwa akipiga kinubi, kama alivyozoea. Sauli alikuwa na mkuki mkononi mwake; akautupa kwa nguvu, akijiambia mwenyewe, “Nitamchoma kwa mkuki abaki hapo ukutani.” Lakini Daudi akamkwepa mara mbili. Sauli akamwogopa Daudi, kwa sababu BWANA alikuwa pamoja na Daudi, lakini alikuwa amemwacha yeye. Kwa hiyo Sauli akamwondoa Daudi mbele yake na kumpa kuwa kiongozi wa watu elfu moja, naye Daudi akatoka na kuingia akiongoza vikosi katika vita. Katika kila kitu alichofanya, Daudi alipata mafanikio makubwa, kwa sababu BWANA alikuwa pamoja naye. Sauli alipoona jinsi alivyokuwa akifanikiwa, akamwogopa. Lakini Israeli wote na Yuda walimpenda Daudi, kwa sababu ndiye alikuwa akiwaongoza katika vita vyao. Sauli akamwambia Daudi, “Huyu hapa binti yangu mkubwa Merabu. Nitakupa umwoe, endapo tu utanitumikia kwa ushujaa na kupigana vita vya BWANA.” Kwa maana Sauli alisema moyoni mwake, “Sitainua mkono wangu dhidi yake. Acha mkono wa Wafilisti uwe juu yake.” Lakini Daudi akamwambia Sauli, “Mimi ni nani, nayo jamaa yangu ni nini au ukoo wa baba yangu katika Israeli, kwamba mimi niwe mkwewe mfalme?” Basi ulipofika wakati wa Daudi kupewa Merabu, binti Sauli, huyo binti aliozwa kwa Adrieli, Mmeholathi. Basi Mikali binti Sauli alimpenda Daudi, nao walipomwambia Sauli kuhusu jambo hili, likampendeza. Sauli akawaza, “Nitampa Daudi binti yangu, ili apate kuwa mtego kwake, ili mkono wa Wafilisti upate kuwa juu yake.” Hivyo Sauli akamwambia Daudi, “Sasa unayo nafasi ya pili ya kuwa mkwe wangu.” Ndipo Sauli akawaagiza watumishi wake, akisema, “Zungumzeni na Daudi kwa siri na kumwambia, ‘Tazama, mfalme amependezwa nawe, nao watumishi wake wote wanakupenda. Basi na uwe mkwewe mfalme.’ ” Watumishi wa Sauli wakarudia hayo maneno kwa Daudi. Lakini Daudi akasema, “Je, mnafikiri ni jambo dogo kuwa mkwewe mfalme? Mimi ni mtu maskini tu, na nisiyejulikana sana.” Watumishi wa Sauli walipomweleza vile Daudi alivyosema, Sauli akajibu, “Mwambieni Daudi, ‘Mfalme hataki zawadi nyingine kuwa mahari, isipokuwa magovi mia moja ya Wafilisti, ili kulipiza kisasi juu ya adui zake.’ ” Mawazo ya Sauli yalikuwa Daudi akaanguke mikononi mwa Wafilisti. Watumishi walipomwambia Daudi mambo haya, ikampendeza kuwa mkwewe mfalme. Basi kabla siku iliyopangwa haijafika, Daudi na watu wake walitoka na kuwaua Wafilisti mia mbili. Akayaleta magovi yao na kupeleka hesabu kamilifu kwa mfalme, ili apate kuwa mkwewe mfalme. Ndipo Sauli akamwoza Daudi Mikali binti yake. Sauli alipotambua kuwa BWANA alikuwa pamoja na Daudi na kwamba Mikali binti yake anampenda Daudi, Sauli akazidi kumwogopa Daudi, naye Sauli akabaki kuwa adui yake siku zote za maisha yake. Majemadari wa jeshi la Wafilisti waliendelea kupigana vita na kadiri walivyoendelea kupigana, Daudi akazidi kutenda kwa hekima kuliko maafisa wengine wa Sauli, nalo jina lake likajulikana sana.