1 Samueli 17:41-47
1 Samueli 17:41-47 Biblia Habari Njema (BHN)
Yule Mfilisti, naye akaanza kumwendea Daudi, na yule aliyemchukulia ngao yake akiwa mbele yake. Yule Mfilisti alipoangalia na kumwona vizuri Daudi, alimdharau, kwani Daudi alikuwa kijana tu, mwenye afya na wa kupendeza. Goliathi akamwuliza Daudi, “Sasa, hiyo fimbo ni ya nini? Unadhani mimi ni mbwa hata unijie kwa fimbo?” Mfilisti huyo akamlaani Daudi kwa miungu yake. Mfilisti akamwambia Daudi, “Njoo kwangu! Mwili wako nitawapa ndege wa angani na wanyama wa porini!” Lakini Daudi akamwambia Goliathi, “Wewe unanijia kwa upanga, mkuki na sime. Lakini mimi ninakujia kwa jina la Mwenyezi-Mungu wa majeshi, Mungu wa askari wa Israeli, ambaye wewe umemtukana. Siku ya leo, Mwenyezi-Mungu atakutia mikononi mwangu. Nitakubwaga chini, nitakukata kichwa chako; na miili ya wanajeshi wa Wafilisti nitawapa ndege wa angani na wanyama wa porini. Ndipo dunia nzima itakapojua kuwa Mungu yuko katika Israeli. Watu wote waliokusanyika hapa leo, watajua kuwa Mwenyezi-Mungu hahitaji mikuki wala sime kuwaokoa watu. Hii ni vita ya Mwenyezi-Mungu, naye atawatia nyinyi nyote mikononi mwetu.”
1 Samueli 17:41-47 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Huyo Mfilisti naye akamsogelea Daudi na kumkaribia; na mtu yule aliyemchukulia ngao yake akamtangulia. Hata Mfilisti alipotazama huku na huku, akamwona Daudi akamdharau; kwa kuwa ni kijana tu mwekundu, tena ana sura nzuri. Mfilisti akamwambia Daudi, Je! Mimi ni mbwa hata umenijia kwa fimbo? Mfilisti akamlaani Daudi kwa miungu yake. Mfilisti akamwambia Daudi, Njoo huku kwangu; nyama yako nitawapa ndege wa angani na wanyama wa mwituni. Ndipo Daudi akamwambia yule Mfilisti, Wewe unanijia mimi na upanga, na fumo, na mkuki, bali mimi ninakujia wewe kwa jina la BWANA wa majeshi, Mungu wa majeshi ya Israeli uliowatukana. Siku hii ya leo BWANA atakuua mkononi mwangu, nami nitakupiga, na kukuondolea kichwa chako, nami leo nitawapa ndege wa angani na wanyama wa nchi mizoga ya majeshi ya Wafilisti, ili kwamba dunia nzima wajue ya kuwa yuko Mungu katika Israeli. Nao jamii ya watu wote pia wajue ya kwamba BWANA haokoi kwa upanga wala kwa mkuki; maana vita ni vya BWANA, naye atawatia ninyi mikononi mwetu.
1 Samueli 17:41-47 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

1 Samueli 17:41-47 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Wakati ule ule, yule Mfilisti, akiwa na mbeba ngao wake mbele yake, akaendelea kujongea karibu na Daudi. Mfilisti akamwangalia Daudi kote na kumwona kuwa ni kijana tu, mwekundu na mzuri wa kupendeza, naye akamdharau. Akamwambia Daudi, “Je, mimi ni mbwa, hata unanijia na fimbo?” Yule Mfilisti akamlaani Daudi kwa miungu yake. Tena Mfilisti akamwambia, “Njoo hapa, nami nitawapa ndege wa angani na wanyama wa mwituni nyama yako.” Daudi akamwambia yule Mfilisti. “Wewe unanijia na upanga, mkuki na fumo, lakini mimi ninakujia kwa jina la BWANA wa majeshi, Mungu wa majeshi ya Israeli, ambaye wewe umemtukana. Siku hii BWANA atakutia mkononi mwangu, nami nitakupiga na kukukata kichwa chako. Leo nitawapa ndege wa angani na wanyama wa nchi mizoga ya jeshi la Wafilisti, nayo dunia yote itajua kuwa yuko Mungu katika Israeli. Wale wote waliokusanyika hapa watajua kuwa BWANA haokoi kwa upanga wala kwa mkuki; kwa kuwa vita ni vya BWANA, naye atawatia ninyi wote mikononi mwetu.”