1 Samueli 17:4-11
1 Samueli 17:4-11 Biblia Habari Njema (BHN)
Kutoka kwenye kambi ya Wafilisti, alijitokeza shujaa mmoja aitwaye Goliathi, mwenyeji wa mji wa Gathi. Urefu wake ulikaribia mita tatu. Kichwani alivaa kofia ya shaba, na deraya ya shaba kifuani yenye uzito wa kilo 57. Miguu yake pia ilikuwa na kinga ya shaba na mabegani pake alibeba mkuki wa shaba. Mpini wa mkuki wake ulikuwa kama mti wa mfumanguo, na chembe cha mkuki huo, kilikuwa na uzito wa kilo saba. Ngao yake ilibebwa na mtu mwingine aliyemtangulia. Goliathi alisimama na kuwapigia kelele wanajeshi wa Israeli, akisema, “Mnafanya nini hapo? Je, mmekuja kupigana vita? Mimi ni Mfilisti, nyinyi ni watumwa wa Shauli. Chagueni mtu mmoja wenu aje kupigana nami. Akinishinda na kuniua, sisi tutakuwa watumwa wenu. Lakini nikimshinda na kumuua basi, nyinyi mtakuwa watumwa wetu na kututumikia.” Kisha Mfilisti huyo aliendelea kusema kwa majivuno, “Nawataka wanajeshi wa Israeli siku hii kumtoa mtu mmoja aje kupigana nami.” Shauli pamoja na wanajeshi wote wa Israeli walipoyasikia maneno hayo ya Mfilisti huyo, walifadhaika na kuogopa sana.
1 Samueli 17:4-11 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ndipo akatoka shujaa katika kambi ya Wafilisti, aliyeitwa Goliathi, wa Gathi, ambaye urefu wake ulikuwa mikono sita na shibiri moja. Alikuwa na chapeo ya shaba kichwani, tena amevaa darii ya shaba; na uzani wake ile darii ya shaba ulikuwa shekeli elfu tano za shaba. Tena amevaa mabamba ya shaba miguuni mwake, naye alikuwa na mkuki wa shaba kati ya mabega yake. Na mpini wa mkuki wake ulikuwa kama mti wa mfumaji; na kichwa cha mkuki wake kilikuwa shekeli mia sita za chuma uzito wake; na mtu aliyemchukulia ngao yake akamtangulia. Naye akasimama, akawapigia kelele majeshi ya Israeli akawaambia, Mbona mmetoka kupanga vita? Je! Mimi si Mfilisti, na ninyi si watumishi wa Sauli? Jichagulieni mtu, akanishukie mimi. Kama akiweza kupigana nami na kuniua, sisi tutakuwa watumwa wenu; nami nikimshinda na kumwua, ninyi mtakuwa watumwa wetu, na kututumikia. Yule Mfilisti akasema, Nayatukana leo majeshi ya Israeli; nipeni mtu tupigane. Basi Sauli na Israeli wote waliposikia maneno hayo ya Mfilisti, wakafadhaika na kuogopa sana.
1 Samueli 17:4-11 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ndipo akatoka shujaa katika kambi ya Wafilisti, aliyeitwa Goliathi, wa Gathi, ambaye urefu wake ulikuwa mikono sita na shibiri moja. Alikuwa na chapeo ya shaba kichwani, tena amevaa darii ya shaba; na uzani wake ile darii ya shaba ulikuwa shekeli elfu tano za shaba. Tena amevaa mabamba ya shaba miguuni mwake, naye alikuwa na mkuki wa shaba kati ya mabega; yake. Na mti wa fumo lake ulikuwa kama mti wa mfumaji; na kichwa cha mkuki wake kilikuwa shekeli mia sita za chuma uzito wake; na mtu aliyemchukulia ngao yake akamtangulia. Naye akasimama, akawapigia kelele majeshi ya Israeli akawaambia, Mbona mmetoka kupanga vita? Je! Mimi si Mfilisti, na ninyi si watumishi wa Sauli? Jichagulieni mtu, akanishukie mimi. Kama akiweza kupigana nami na kuniua, sisi tutakuwa watumwa wenu; nami nikimshinda yeye na kumwua, ninyi mtakuwa watumwa wetu, na kututumikia. Yule Mfilisti akasema, Nayatukana leo majeshi ya Israeli; nipeni mtu tupigane. Basi Sauli na Israeli wote waliposikia maneno hayo ya Mfilisti, wakafadhaika na kuogopa sana.
1 Samueli 17:4-11 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Shujaa aliyeitwa Goliathi, aliyetoka Gathi, akajitokeza kutoka kambi ya Wafilisti. Alikuwa na urefu dhiraa sita na shibiri moja. Alikuwa na chapeo ya shaba kichwani mwake, na alivaa dirii ya shaba kifuani mwake yenye uzito wa shekeli elfu tano. Miguuni mwake alivaa mabamba ya shaba, na alikuwa na mkuki wa shaba mgongoni mwake. Mpini wa huo mkuki ulikuwa kama mti wa mfumaji, na ncha ya chuma yake ilikuwa na uzito wa shekeli mia sita. Mbeba ngao wake alitangulia mbele yake. Goliathi alisimama na kuwaambia majeshi ya Israeli kwa sauti kuu, akisema, “Kwa nini mmetoka kupanga vita? Je, mimi si Mfilisti, na ninyi ni watumishi wa Sauli? Chagueni mtu na anishukie mimi. Kama anaweza kupigana nami na kuniua, tutakuwa chini yenu; lakini nikimshinda na kumuua, ninyi mtakuwa chini yetu, na mtatutumikia.” Kisha yule Mfilisti akasema, “Siku hii ya leo nayatukana majeshi ya Israeli! Nipeni mtu tupigane.” Kwa kusikia maneno ya Wafilisti, Sauli na Waisraeli wote wakafadhaika na kuogopa.