1 Samueli 16:14-23
1 Samueli 16:14-23 Biblia Habari Njema (BHN)
Baadaye roho ya Mwenyezi-Mungu ilimwacha Shauli, na roho mwovu kutoka kwa Mwenyezi-Mungu ikamsumbua. Ndipo watumishi wake Shauli wakamwambia, “Tunajua kwamba roho mwovu kutoka kwa Mungu anakusumbua. Sasa, ee bwana wetu, amuru watumishi wako wanaokutumikia wamtafute mtu mwenye ufundi wa kupiga kinubi, na huyo roho mwovu kutoka kwa Mungu atakapokujia, mtu huyo atapiga kinubi, nawe utapata nafuu.” Shauli akawaambia watumishi wake, “Nitafutieni mtu huyo anayeweza kupiga kinubi vizuri, mniletee.” Kijana mmoja miongoni mwa watumishi akasema, “Nimemwona kijana mmoja wa Yese, wa mji wa Bethlehemu. Kijana huyo ana ujuzi wa kupiga kinubi. Huyo kijana ni shujaa, hodari wa kupigana vitani, ana busara katika kusema na mwenye umbo zuri; Mwenyezi-Mungu yuko pamoja naye.” Hivyo, Shauli alituma ujumbe kwa Yese, na kusema, “Nitumie mwanao Daudi, ambaye anachunga kondoo.” Yese alimtuma Daudi kwa Shauli pamoja na punda aliyebeba mikate, kiriba cha divai na mwanambuzi. Daudi alipofika akaingia kumtumikia Shauli. Shauli alimpenda sana, hata akamfanya awe mwenye kumbebea silaha zake. Halafu Shauli alituma ujumbe kwa Yese na kusema, “Nampenda Daudi; mwache akae hapa anitumikie.” Kila mara, yule roho mwovu kutoka kwa Mungu alipomjia Shauli, Daudi alichukua kinubi chake na kuanza kukipiga, na roho huyo alimwacha Shauli, naye akaburudika na kupata nafuu.
1 Samueli 16:14-23 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi, Roho ya BWANA ilikuwa imemwacha Sauli, na roho mbaya kutoka kwa BWANA ikamsumbua. Nao watumishi wa Sauli wakamwambia, Angalia, sasa roho mbaya kutoka kwa Mungu inakusumbua. Basi bwana wetu na atuamuru sisi watumishi wake waliopo hapa mbele yako watafute mtu aliye stadi wa kupiga kinubi; basi itakuwa, roho ile mbaya kutoka kwa Mungu itakapokujia, yeye atapiga kinubi kwa mkono wake, nawe utapona. Basi Sauli akawaambia, Vema, nitafutieni mtu aliye stadi wa kupiga kinubi, mniletee. Ndipo mmoja wa watumishi wake akasema, Tazama, nimemwona mtoto mmoja wa Yese, Mbethlehemi, aliye stadi wa kupiga kinubi, tena ni mtu shujaa, hodari wa vita, anenaye kwa busara, mtu mzuri, ambaye BWANA yuko pamoja naye. Basi Sauli akawatuma wajumbe kwa Yese akasema, Mtume Daudi mwanao kwangu, aliye pamoja na kondoo. Yese akatwaa punda, wa kuchukua mikate, na kiriba cha divai, na mwana-mbuzi, akampelekea Sauli kwa mkono wa Daudi mwanawe. Basi Daudi akamwendea Sauli, akasimama mbele yake, naye akampenda sana; naye akawa mtu wa kumchukulia silaha zake. Kisha Sauli akatuma ujumbe kwa Yese, akasema, Tafadhali, mwache Daudi asimame mbele yangu; maana ameona kibali machoni pangu. Ikawa, ile roho mbaya kutoka kwa Mungu ilipomjia Sauli, ndipo Daudi alipokishika kinubi na kukipiga kwa mkono wake, naye Sauli akaburudishwa, na ile roho mbaya ikamwacha.
1 Samueli 16:14-23 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi, roho ya BWANA ilikuwa imemwacha Sauli, na roho mbaya kutoka kwa BWANA ikamsumbua. Nao watumishi wa Sauli wakamwambia, Angalia, sasa roho mbaya kutoka kwa Mungu inakusumbua. Basi bwana wetu na atuamuru sisi watumishi wake waliopo hapa mbele yako watafute mtu aliye stadi wa kupiga kinubi; basi itakuwa, roho ile mbaya kutoka kwa Mungu itakapokujilia, yeye atapiga kinubi kwa mkono wake, nawe utapona. Basi Sauli akawaambia, Vema, nitafutieni mtu aliye stadi wa kupiga kinubi, mkaniletee. Ndipo akajibu mmoja wa watumishi wake akasema, Tazama, nimemwona mwana mmoja wa Yese, Mbethlehemi, aliye stadi wa kupiga kinubi, tena ni mtu shujaa, hodari wa vita, anenaye kwa busara, mtu mzuri, ambaye BWANA yu pamoja naye. Basi Sauli akampelekea Yese wajumbe, akasema, Nipelekee Daudi mwanao, aliye pamoja na kondoo. Yese akatwaa punda, wa kuchukua mikate, na kiriba cha divai, na mwana-mbuzi, akampelekea Sauli kwa mkono wa Daudi mwanawe. Basi Daudi akamwendea Sauli, akasimama mbele yake, naye akampenda sana; naye akapata kuwa mtu wa kumchukulia silaha zake. Kisha Sauli akapeleka watu kwa Yese, akasema, Tafadhali, mwache Daudi asimame mbele yangu; maana ameona kibali machoni pangu. Ikawa, ile roho mbaya kutoka kwa Mungu ilipomjilia Sauli, ndipo Daudi akakishika kinubi, akakipiga kwa mkono wake, naye Sauli akaburudishwa, na ile roho mbaya ikamwacha.
1 Samueli 16:14-23 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Basi Roho wa BWANA alikuwa ameondoka kwa Sauli, nayo roho mbaya ikaachiwa nafasi na BWANA ili imtese. Watumishi wa Sauli wakamwambia, “Tazama, roho mbaya imeachiwa nafasi na BWANA nayo inakutesa. Basi bwana wetu na aamuru watumishi wake walio hapa watafute mtu anayeweza kupiga kinubi. Atakipiga kinubi wakati roho mbaya iliyoachiwa nafasi na Mungu ikujiapo, nawe utajisikia vizuri.” Basi Sauli akawaambia watumishi wake, “Mtafuteni mtu apigaye kinubi vizuri mkamlete kwangu.” Mmoja wa watumishi wake akajibu, “Nimemwona mwana wa Yese Mbethlehemu ambaye anajua kupiga kinubi. Yeye ni mtu hodari na shujaa. Ni mwenye busara katika kunena, mtu mzuri wa umbo. BWANA yu pamoja naye.” Ndipo Sauli akatuma wajumbe kwa Yese na kumwambia, “Nitumie mwanao Daudi, ambaye anachunga kondoo.” Kwa hiyo Yese akamchukua punda aliyepakizwa mikate, kiriba cha divai na mwana-mbuzi, na kuvipeleka vitu hivyo kwa Sauli pamoja na Daudi mwanawe. Daudi akafika kwa Sauli na kuingia kwenye kazi yake. Sauli akampenda sana, naye Daudi akawa mmoja wa wabeba silaha wake. Basi Sauli akatuma ujumbe kwa Yese, akisema, “Mruhusu Daudi abaki katika utumishi wangu, kwa kuwa ninapendezwa naye.” Kila mara roho mbaya iliyoachiwa nafasi na Mungu ilipomjia Sauli, Daudi alichukua kinubi chake na kupiga. Ndipo Sauli angetulizwa na kujisikia vizuri, nayo ile roho mbaya ingemwacha.