Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Samueli 16:1-23 - Compare All Versions

1 Samueli 16:1-23 BHN (Biblia Habari Njema)

Mwenyezi-Mungu akamwambia Samueli, “Utamlilia Shauli mpaka lini? Wewe unajua kuwa mimi nimemkataa kuwa mfalme juu ya Israeli. Sasa, jaza upembe wako mafuta, uondoke. Nitakutuma kwa Yese wa mji wa Bethlehemu. Maana nimejipatia mfalme miongoni mwa wanawe.” Samueli akasema, “Nitawezaje kwenda? Kama Shauli akisikia habari hizo, ataniua!” Mwenyezi-Mungu akamwambia, “Chukua ndama pamoja nawe, na ukifika huko useme, ‘Nimekuja kumtolea Mwenyezi-Mungu tambiko’. Mwalike Yese kwenye tambiko hiyo nami nitakuonesha la kufanya. Utampaka mafuta kwa ajili yangu mtu yule nitakayekutajia.” Samueli akafanya kama alivyoambiwa na Mwenyezi-Mungu, akaenda Bethlehemu. Wazee wa mji wakatoka kumlaki wakiwa wanatetemeka, wakamwuliza, “Je, umekuja kwa amani?” Samueli akawaambia, “Nimekuja kwa amani. Nimekuja kumtolea tambiko Mwenyezi-Mungu. Jitakaseni wenyewe halafu twendeni kutoa tambiko.” Samueli akamtakasa Yese pamoja na wanawe, akawakaribisha kwenye tambiko. Walipofika, na Samueli alipomwona Eliabu, alijisemea moyoni mwake, “Hakika, mpakwa mafuta wa Mwenyezi-Mungu ndiye huyu aliye mbele ya Mwenyezi-Mungu!” Lakini Mwenyezi-Mungu alimwambia, “Usiangalie sura yake na urefu wa kimo chake. Mimi nimemkataa kwani siangalii mambo kama wanavyoyaangalia binadamu wenye kufa. Binadamu huangalia uzuri wa nje, lakini mimi naangalia moyoni.” Kisha, Yese akamwita Abinadabu na kumleta mbele ya Samueli. Lakini Samueli akasema, “Wala huyu hakuchaguliwa na Mwenyezi-Mungu.” Yese akamleta Shama. Samueli akasema, “Wala huyu hakuchaguliwa na Mwenyezi-Mungu.” Yese aliwapitisha wanawe wote saba mbele ya Samueli lakini Samueli akamwambia, “Mwenyezi-Mungu hajamchagua yeyote kati ya hawa.” Halafu akamwambia, “Je, wanao wote wako hapa?” Yese akajibu, “Bado yuko mdogo, lakini amekwenda kuchunga kondoo.” Samueli akamwambia, “Mtume mtu amlete; sisi hatutaketi chini, mpaka atakapokuja hapa.” Hivyo, Yese alituma mtu, naye akaletwa. Yule kijana alikuwa mwenye afya, mwenye macho maangavu na wa kupendeza. Mwenyezi-Mungu akamwambia Samueli, “Sasa, huyu ndiye; inuka umpake mafuta.” Samueli akachukua upembe wake wenye mafuta akammiminia Daudi mafuta mbele ya kaka zake. Mara roho ya Mwenyezi-Mungu ikamjia Daudi kwa nguvu, ikakaa tangu siku hiyo na kuendelea. Kisha Samueli akarudi mjini Rama. Baadaye roho ya Mwenyezi-Mungu ilimwacha Shauli, na roho mwovu kutoka kwa Mwenyezi-Mungu ikamsumbua. Ndipo watumishi wake Shauli wakamwambia, “Tunajua kwamba roho mwovu kutoka kwa Mungu anakusumbua. Sasa, ee bwana wetu, amuru watumishi wako wanaokutumikia wamtafute mtu mwenye ufundi wa kupiga kinubi, na huyo roho mwovu kutoka kwa Mungu atakapokujia, mtu huyo atapiga kinubi, nawe utapata nafuu.” Shauli akawaambia watumishi wake, “Nitafutieni mtu huyo anayeweza kupiga kinubi vizuri, mniletee.” Kijana mmoja miongoni mwa watumishi akasema, “Nimemwona kijana mmoja wa Yese, wa mji wa Bethlehemu. Kijana huyo ana ujuzi wa kupiga kinubi. Huyo kijana ni shujaa, hodari wa kupigana vitani, ana busara katika kusema na mwenye umbo zuri; Mwenyezi-Mungu yuko pamoja naye.” Hivyo, Shauli alituma ujumbe kwa Yese, na kusema, “Nitumie mwanao Daudi, ambaye anachunga kondoo.” Yese alimtuma Daudi kwa Shauli pamoja na punda aliyebeba mikate, kiriba cha divai na mwanambuzi. Daudi alipofika akaingia kumtumikia Shauli. Shauli alimpenda sana, hata akamfanya awe mwenye kumbebea silaha zake. Halafu Shauli alituma ujumbe kwa Yese na kusema, “Nampenda Daudi; mwache akae hapa anitumikie.” Kila mara, yule roho mwovu kutoka kwa Mungu alipomjia Shauli, Daudi alichukua kinubi chake na kuanza kukipiga, na roho huyo alimwacha Shauli, naye akaburudika na kupata nafuu.

1 Samueli 16:1-23 SRUV (Swahili Revised Union Version)

BWANA akamwambia Samweli, utamlilia Sauli hadi lini, kwa kuwa mimi nimemkataa asiwatawale Waisraeli? Ijaze pembe yako mafuta, uende, nami nitakutuma kwa Yese, Mbethlehemi; maana nimejipatia mfalme katika wanawe. Samweli akasema, Nawezaje kwenda? Sauli akipata habari, ataniua. Basi BWANA akasema, Chukua ndama pamoja nawe, ukaseme, Nimekuja ili kumtolea BWANA dhabihu. Umwalike Yese aje kwenye dhabihu, nami nitakuonesha utakayotenda; nawe utampaka mafuta yule nitakayemtaja kwako. Samweli akafanya hayo aliyosema BWANA, akaenda Bethlehemu. Wakaja wazee wa mji kumlaki, wakitetemeka, nao wakasema, Je! Umekuja kwa amani? Naye akasema, Naam, kwa amani; nimekuja kumtolea BWANA dhabihu; jitakaseni; njoni pamoja nami kwenye dhabihu. Akawatakasa Yese na wanawe, akawaita kwenye dhabihu. Ikawa walipokuja, alimtazama Eliabu, akasema, Yakini masihi wa BWANA yupo hapa mbele zake. Lakini BWANA akamwambia Samweli, Usimtazame uso wake, wala urefu wa kimo chake; kwa maana mimi nimemkataa. BWANA haangalii kama binadamu aangaliavyo; maana wanadamu huitazama sura ya nje, bali BWANA huutazama moyo. Ndipo Yese akamwita Abinadabu, akampitisha mbele ya Samweli. Naye akasema, BWANA hakumchagua huyu. Ndipo Yese akampitisha Shama. Naye akasema, Wala BWANA hakumchagua huyu. Yese akawapitisha wanawe saba mbele ya Samweli. Samweli akamwambia Yese, BWANA hakuwachagua hawa. Kisha Samweli akamwambia Yese, Watoto wako wote wapo hapa? Naye akasema, Amesalia mdogo wao, na tazama, anawachunga kondoo. Basi Samweli akamwambia Yese, Tuma watu, wamlete; kwa sababu hatutaketi hadi atakapokuja huku. Basi akatuma mtu, naye akamleta kwao. Naye alikuwa mwekundu, mwenye macho mazuri, na umbo lake lilikuwa la kupendeza. BWANA akasema, Ondoka, umtie mafuta; maana huyu ndiye. Ndipo Samweli akaitwaa pembe yenye mafuta, akamtia mafuta kati ya ndugu zake; na Roho ya BWANA ikamjia Daudi kwa nguvu kuanzia siku ile. Basi Samweli akaondoka, akaenda zake Rama. Basi, Roho ya BWANA ilikuwa imemwacha Sauli, na roho mbaya kutoka kwa BWANA ikamsumbua. Nao watumishi wa Sauli wakamwambia, Angalia, sasa roho mbaya kutoka kwa Mungu inakusumbua. Basi bwana wetu na atuamuru sisi watumishi wake waliopo hapa mbele yako watafute mtu aliye stadi wa kupiga kinubi; basi itakuwa, roho ile mbaya kutoka kwa Mungu itakapokujia, yeye atapiga kinubi kwa mkono wake, nawe utapona. Basi Sauli akawaambia, Vema, nitafutieni mtu aliye stadi wa kupiga kinubi, mniletee. Ndipo mmoja wa watumishi wake akasema, Tazama, nimemwona mtoto mmoja wa Yese, Mbethlehemi, aliye stadi wa kupiga kinubi, tena ni mtu shujaa, hodari wa vita, anenaye kwa busara, mtu mzuri, ambaye BWANA yuko pamoja naye. Basi Sauli akawatuma wajumbe kwa Yese akasema, Mtume Daudi mwanao kwangu, aliye pamoja na kondoo. Yese akatwaa punda, wa kuchukua mikate, na kiriba cha divai, na mwana-mbuzi, akampelekea Sauli kwa mkono wa Daudi mwanawe. Basi Daudi akamwendea Sauli, akasimama mbele yake, naye akampenda sana; naye akawa mtu wa kumchukulia silaha zake. Kisha Sauli akatuma ujumbe kwa Yese, akasema, Tafadhali, mwache Daudi asimame mbele yangu; maana ameona kibali machoni pangu. Ikawa, ile roho mbaya kutoka kwa Mungu ilipomjia Sauli, ndipo Daudi alipokishika kinubi na kukipiga kwa mkono wake, naye Sauli akaburudishwa, na ile roho mbaya ikamwacha.

1 Samueli 16:1-23 SUV (Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia)

BWANA akamwambia Samweli, Hata lini utamlilia Sauli, ikiwa mimi nimemkataa asiwamiliki Israeli? Ijaze pembe yako mafuta, uende, nami nitakupeleka kwa Yese, Mbethlehemi; maana nimejipatia mfalme katika wanawe. Samweli akasema, Nawezaje kwenda? Sauli akipata habari, ataniua. Basi BWANA akasema, Chukua ndama pamoja nawe, ukaseme, Nimekuja ili kumtolea BWANA dhabihu. Ukamwite Yese aje kwenye dhabihu, nami nitakuonyesha utakayotenda; nawe utamtia mafuta yule nitakayemtaja kwako. Samweli akafanya hayo aliyosema BWANA, akaenda Bethlehemu. Wakaja wazee wa mji kumlaki, wakitetemeka, nao wakasema, Je! Umekuja kwa amani? Naye akasema, Naam, kwa amani; nimekuja kumtolea BWANA dhabihu; jitakaseni; njoni pamoja nami kwenye dhabihu. Akawatakasa Yese na wanawe, akawaita kwenye dhabihu. Ikawa walipokuja, alimtazama Eliabu, akasema, Yakini masihi wa BWANA yupo hapa mbele zake. Lakini BWANA akamwambia Samweli, Usimtazame uso wake, wala urefu wa kimo chake; kwa maana mimi nimemkataa. BWANA haangalii kama binadamu aangaliavyo; maana wanadamu huitazama sura ya nje, bali BWANA huutazama moyo. Ndipo Yese akamwita Abinadabu, akampitisha mbele ya Samweli. Naye akasema, BWANA hakumchagua huyu. Ndipo Yese akampitisha Shama. Naye akasema, wala BWANA hakumchagua huyu. Yese akawapitisha wanawe saba mbele ya Samweli. Samweli akamwambia Yese, BWANA hakuwachagua hawa. Kisha Samweli akamwambia Yese, Watoto wako wote wapo hapa? Naye akasema, Amesalia mdogo wao, na tazama, anawachunga kondoo. Basi Samweli akamwambia Yese, Tuma watu, wamlete; kwa sababu hatutaketi hata atakapokuja huku. Basi akatuma mtu, naye akamleta kwao. Naye alikuwa mwekundu, mwenye macho mazuri, na umbo lake lilikuwa la kupendeza. BWANA akasema, Ondoka, umtie mafuta; maana huyu ndiye. Ndipo Samweli akaitwaa pembe yenye mafuta, akamtia mafuta kati ya ndugu zake; na roho ya BWANA ikamjilia Daudi kwa nguvu tangu siku ile. Basi Samweli akaondoka, akaenda zake Rama. Basi, roho ya BWANA ilikuwa imemwacha Sauli, na roho mbaya kutoka kwa BWANA ikamsumbua. Nao watumishi wa Sauli wakamwambia, Angalia, sasa roho mbaya kutoka kwa Mungu inakusumbua. Basi bwana wetu na atuamuru sisi watumishi wake waliopo hapa mbele yako watafute mtu aliye stadi wa kupiga kinubi; basi itakuwa, roho ile mbaya kutoka kwa Mungu itakapokujilia, yeye atapiga kinubi kwa mkono wake, nawe utapona. Basi Sauli akawaambia, Vema, nitafutieni mtu aliye stadi wa kupiga kinubi, mkaniletee. Ndipo akajibu mmoja wa watumishi wake akasema, Tazama, nimemwona mwana mmoja wa Yese, Mbethlehemi, aliye stadi wa kupiga kinubi, tena ni mtu shujaa, hodari wa vita, anenaye kwa busara, mtu mzuri, ambaye BWANA yu pamoja naye. Basi Sauli akampelekea Yese wajumbe, akasema, Nipelekee Daudi mwanao, aliye pamoja na kondoo. Yese akatwaa punda, wa kuchukua mikate, na kiriba cha divai, na mwana-mbuzi, akampelekea Sauli kwa mkono wa Daudi mwanawe. Basi Daudi akamwendea Sauli, akasimama mbele yake, naye akampenda sana; naye akapata kuwa mtu wa kumchukulia silaha zake. Kisha Sauli akapeleka watu kwa Yese, akasema, Tafadhali, mwache Daudi asimame mbele yangu; maana ameona kibali machoni pangu. Ikawa, ile roho mbaya kutoka kwa Mungu ilipomjilia Sauli, ndipo Daudi akakishika kinubi, akakipiga kwa mkono wake, naye Sauli akaburudishwa, na ile roho mbaya ikamwacha.

1 Samueli 16:1-23 NEN (Neno)

BWANA akamwambia Samweli, “Utamlilia Sauli hadi lini, maadamu nimemkataa asiendelee kuwa mfalme juu ya Israeli? Jaza pembe yako mafuta, ushike njia uende; ninakutuma kwa Yese huko Bethlehemu. Nimemchagua mmoja wa wanawe kuwa mfalme.” Lakini Samweli akasema, “Nitaendaje? Sauli atasikia kuhusu jambo hili na ataniua.” BWANA akamwambia, “Chukua ndama jike, useme, ‘Nimekuja kumtolea BWANA dhabihu.’ Mwalike Yese aje kwenye dhabihu, nami nitakuonesha utakalofanya. Utanipakia mafuta yule nitakuonesha.” Samweli akafanya kile BWANA alichosema. Alipofika Bethlehemu, wazee wa mji wakatetemeka walipomlaki. Wakauliza, “Je, umekuja kwa amani?” Samweli akajibu, “Ndiyo, kwa amani; nimekuja kumtolea BWANA dhabihu. Jiwekeni wakfu na mje kwenye dhabihu pamoja nami.” Ndipo akamweka Yese wakfu pamoja na wanawe na kuwaalika kwenye dhabihu. Walipofika, Samweli akamwona Eliabu, naye akafikiri, “Hakika mpakwa mafuta wa BWANA anasimama hapa mbele za BWANA.” Lakini BWANA akamwambia Samweli, “Usitazame sura yake wala kimo chake, kwa kuwa nimemkataa. BWANA hatazami katika vile vitu mwanadamu avitazamavyo. Mwanadamu hutazama katika sura ya nje, lakini BWANA hutazama moyoni.” Kisha Yese akamwita Abinadabu na kumpitisha mbele ya Samweli. Lakini Samweli akasema, “Hata huyu BWANA hakumchagua.” Kisha Yese akampitisha Shama, lakini Samweli akasema, “Wala huyu BWANA hakumchagua.” Yese alikuwa na wana saba aliowapitisha mbele ya Samweli, lakini Samweli akamwambia, “BWANA hajawachagua hawa.” Hivyo akamuuliza Yese, “Je, hawa ndio wana pekee ulio nao?” Yese akajibu, “Bado yuko mdogo kuliko wote, lakini anachunga kondoo.” Samweli akasema, “Tuma aitwe; hatutaketi hadi afike.” Basi akatuma aitwe, naye akaletwa. Alingʼaa kwa afya, na mwenye sura nzuri na umbo la kupendeza. Ndipo BWANA akasema, “Inuka na umpake mafuta; huyu ndiye.” Basi Samweli akachukua ile pembe ya mafuta na kumpaka mafuta mbele ya ndugu zake. Kuanzia siku ile na kuendelea Roho wa BWANA akaja juu ya Daudi kwa nguvu. Kisha Samweli akaenda zake Rama. Basi Roho wa BWANA alikuwa ameondoka kwa Sauli, nayo roho mbaya ikaachiwa nafasi na BWANA ili imtese. Watumishi wa Sauli wakamwambia, “Tazama, roho mbaya imeachiwa nafasi na BWANA nayo inakutesa. Basi bwana wetu na aamuru watumishi wake walio hapa watafute mtu anayeweza kupiga kinubi. Atakipiga kinubi wakati roho mbaya iliyoachiwa nafasi na Mungu ikujiapo, nawe utajisikia vizuri.” Basi Sauli akawaambia watumishi wake, “Mtafuteni mtu apigaye kinubi vizuri mkamlete kwangu.” Mmoja wa watumishi wake akajibu, “Nimemwona mwana wa Yese Mbethlehemu ambaye anajua kupiga kinubi. Yeye ni mtu hodari na shujaa. Ni mwenye busara katika kunena, mtu mzuri wa umbo. BWANA yu pamoja naye.” Ndipo Sauli akatuma wajumbe kwa Yese na kumwambia, “Nitumie mwanao Daudi, ambaye anachunga kondoo.” Kwa hiyo Yese akamchukua punda aliyepakizwa mikate, kiriba cha divai na mwana-mbuzi, na kuvipeleka vitu hivyo kwa Sauli pamoja na Daudi mwanawe. Daudi akafika kwa Sauli na kuingia kwenye kazi yake. Sauli akampenda sana, naye Daudi akawa mmoja wa wabeba silaha wake. Basi Sauli akatuma ujumbe kwa Yese, akisema, “Mruhusu Daudi abaki katika utumishi wangu, kwa kuwa ninapendezwa naye.” Kila mara roho mbaya iliyoachiwa nafasi na Mungu ilipomjia Sauli, Daudi alichukua kinubi chake na kupiga. Ndipo Sauli angetulizwa na kujisikia vizuri, nayo ile roho mbaya ingemwacha.