1 Samueli 14:1-6
1 Samueli 14:1-6 Biblia Habari Njema (BHN)
Siku moja, Yonathani mwana wa mfalme Shauli alimwambia kijana aliyembebea silaha, “Njoo, twende ngambo kwenye ngome ya Wafilisti.” Lakini Yonathani hakumwambia baba yake. Shauli alikuwa amepiga kambi chini ya mkomamanga huko Migroni, nje ya mji wa Gibea, akiwa pamoja na watu wapatao 600. Ahiya, mwana wa Ahitubu ndugu yake Ikabodi mwana wa Finehasi, mwana wa Eli, kuhani wa Mwenyezi-Mungu mjini Shilo, alikuwa ndiye aliyevaa kizibao cha kuhani. Watu hawakujua kwamba Yonathani amekwisha ondoka. Kwenye kipito ambako Yonathani alipaswa apitie ili afike kwenye ngome ya Wafilisti, kulikuwa na miamba miwili iliyochongoka, upande huu na upande mwingine. Mwamba mmoja uliitwa Bosesi na mwingine uliitwa Sene. Mwamba mmoja ulikuwa kaskazini mwa mji wa Mikmashi na mwingine ulikuwa kusini mkabala na mji wa Gibea. Yonathani akamwambia yule kijana aliyembebea silaha, “Njoo, twende upande wa pili kwenye ile ngome ya hawa watu wasiotahiriwa. Huenda Mwenyezi-Mungu akatusaidia, maana Mwenyezi-Mungu haokoi kwa kutegemea wingi au uchache wa watu.”
1 Samueli 14:1-6 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi ikatukia siku moja, ya kwamba Yonathani, mwana wa Sauli, akamwambia yule kijana aliyembebea silaha zake, Haya! Na tuvuke twende kwa Wafilisti ngomeni, pale ng'ambo ya pili. Lakini hakumwarifu babaye. Naye Sauli alikuwa akikaa katika Viunga vya Gibea, chini ya mkomamanga uliokuwa kwenye uwanja huko Migroni; na hao watu waliokuwa pamoja naye walikuwa watu mia sita; pamoja na Ahiya, mwana wa Ahitubu nduguye Ikabodi, mwana wa Finehasi, mwana wa Eli, kuhani wa BWANA huko Shilo, aliyevaa naivera. Tena hao watu hawakujua ya kwamba Yonathani ameondoka. Na katikati ya mapito, ambayo Yonathani alitaka kuipitia ili kuifikia hiyo ngome ya Wafilisti, palikuwa na kilima cha mwamba upande huu, na kilima cha mwamba upande huu; kimoja kiliitwa Bosesi, na cha pili Sene. Hicho kilima kimoja kimesimama upande wa kaskazini, mbele ya Mikmashi, na hicho cha pili upande wa kusini, mbele ya Geba. Basi, Yonathani akamwambia yule kijana aliyembebea silaha zake, Haya! Na twende tukavuke ngomeni mwa hao wasiotahiriwa; yamkini BWANA atatutendea kazi; kwa maana hakuna la kumzuia BWANA asiokoe, kama ni kwa wengi au kama ni kwa wachache.
1 Samueli 14:1-6 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi ikatukia siku moja, ya kwamba Yonathani, mwana wa Sauli, akamwambia yule kijana aliyemchukulia silaha zake, Haya! Na tuwavukie Wafilisti ngomeni, pale ng’ambo ya pili. Walakini hakumwarifu babaye. Naye Sauli alikuwa akikaa katika upande wa mwisho wa Giba, chini ya mkomamanga ulioko kwenye uga; na hao watu waliokuwa pamoja naye walipata watu mia sita; na Ahiya, mwana wa Ahitubu nduguye Ikabodi, mwana wa Finehasi, mwana wa Eli, kuhani wa BWANA huko Shilo, mwenye kuvaa naivera. Tena hao watu hawakujua ya kwamba Yonathani ameondoka. Na katikati ya mianya, ambayo Yonathani alitaka kuipitia ili kuifikilia hiyo ngome ya Wafilisti, palikuwa na genge la jabali upande huu, na genge la jabali upande huu; jina la moja liliitwa Bosesi, na jina la pili Sene. Hilo genge moja limesimama upande wa kaskazini, mbele ya Mikmashi, na hilo la pili upande wa kusini, mbele ya Geba. Basi, Yonathani akamwambia yule kijana aliyemchukulia silaha zake, Haya! Na twende tukawavukie ngomeni hao wasiotahiriwa; yamkini BWANA atatutendea kazi; kwa maana hakuna la kumzuia BWANA asiokoe, kwamba ni kwa wengi au kwamba ni kwa wachache.
1 Samueli 14:1-6 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Siku moja Yonathani mwana wa Sauli akamwambia kijana mbeba silaha wake, akasema, “Njoo, tuwavukie Wafilisti kwenye doria upande ule mwingine.” Lakini hakumwambia baba yake. Sauli alikuwa akikaa kwenye viunga vya Gibea chini ya mkomamanga huko Migroni. Alikuwa pamoja na watu wapatao mia sita; miongoni mwao alikuwepo Ahiya, aliyekuwa amevaa kizibau. Alikuwa mwana wa Ikabodi, nduguye Ahitubu mwana wa Finehasi, mwana wa Eli, kuhani wa BWANA huko Shilo. Hakuna yeyote aliyekuwa na habari kwamba Yonathani alikuwa ameondoka. Kila upande wa njia ambayo Yonathani alikusudia kupita ili kuvuka kufikia doria ya Wafilisti kulikuwa na jabali; moja lilikuwa linaitwa Bosesi, na jingine Sene. Jabali moja lilisimama kaskazini kuelekea Mikmashi na jingine upande wa kusini kuelekea Geba. Yonathani akamwambia kijana wake mbeba silaha, “Njoo, tuvukie doria ya wale jamaa wasiotahiriwa. Huenda BWANA atatenda kwa ajili yetu. Hakuna chochote kitakachoweza kumzuia BWANA kuokoa, kwamba ni kwa wingi au kwa uchache.”