Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Samueli 10:2-11

1 Samueli 10:2-11 Biblia Habari Njema (BHN)

Leo tutakapoagana, utakutana na watu wawili karibu na kaburi la Raheli huko Selsa katika nchi ya Benyamini. Hao watakuambia kuwa wale punda uliokuwa unawatafuta wamekwisha patikana. Baba yako ameacha kufikiri juu ya punda, ila ana wasiwasi juu yako, akijiuliza kila mara, ‘Nitafanya nini juu ya mwanangu?’ Kutoka hapo utakwenda kwenye mwaloni wa Tabori, mahali ambapo utakutana na wanaume watatu wakiwa njiani kwenda kumtolea Mungu tambiko, huko Betheli. Mmoja wao atakuwa anawachukua wanambuzi watatu, wa pili atakuwa anachukua mikate mitatu na wa tatu atakuwa amebeba kiriba cha divai. “Watakusalimia na kukupa mikate miwili, nawe utaipokea mikononi mwao. Kisha, utakapofika huko Gibea-elohimu, mahali ambapo pana kambi ya kijeshi ya Wafilisti; hapo, utakapokuwa unakaribia mji, utakutana na kundi la manabii. Manabii hao watakuwa wanatoka mahali pa juu huku wakipiga vinubi, matari, filimbi na zeze, na watakuwa wanatabiri. Roho ya Mwenyezi-Mungu itakujia kwa nguvu, nawe utaanza kutabiri pamoja nao na kugeuka kuwa mtu mwingine. Wakati mambo haya yatakapokutokea, chochote utakachoweza kufanya kifanye, kwani Mungu yu pamoja nawe. Utanitangulia kwenda mjini Gilgali, mahali ambapo nitakukuta na kutoa sadaka ya kuteketezwa na tambiko za amani. Utaningojea hapo kwa muda wa siku saba mpaka nije na kukuonesha la kufanya.” Shauli alipogeuka ili kumwacha Samueli, Mungu akabadili moyo wa Shauli. Yale yote aliyoambiwa na Samueli yakatokea siku hiyo. Shauli na mtumishi wake walipofika huko Gibea, alilakiwa na kundi la manabii. Roho ya Mungu ilimjia kwa nguvu, na Shauli akaanza kutabiri pamoja na manabii hao. Watu waliomfahamu Shauli hapo awali, walipomwona anatabiri, wakaulizana, “Kitu gani kimempata mwana wa Kishi? Je, hata Shauli ni mmoja wa manabii?”

1 Samueli 10:2-11 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Utakapoondoka kwangu leo, utakutana na wanaume wawili karibu na kaburi la Raheli, katika mpaka wa Benyamini huko Selsa; nao watakuambia, Punda hao uliokwenda kuwatafuta wameonekana; na tazama, baba yako ameacha kufikiri habari za punda, anafikiri habari zenu, akisema, Nifanye nini kwa ajili ya mwanangu? Kisha utakwenda mbele kutoka hapo, na kufika kwenye mwaloni wa Tabori, na hapo watu watatu watakutana nawe, wanaokwea kumwendea Mungu huko Betheli, mmoja anachukua wana-mbuzi watatu, na mwingine anachukua mikate mitatu, na mwingine anachukua kiriba cha divai; nao watakusalimu na kukupa mikate miwili; nawe utaipokea mikononi mwao. Baada ya hayo utafika Gibea ya Mungu, hapo palipo na ngome ya Wafilisti; kisha itakuwa, utakapofika mjini, utakutana na kundi la manabii wakishuka kutoka mahali pa juu, wenye kinanda, na tari, na kinubi, na filimbi mbele yao, nao watakuwa wakitabiri; na Roho ya BWANA itakujia kwa nguvu, nawe utatabiri pamoja nao, nawe utageuzwa kuwa mtu mwingine. Basi, hapo ishara hizi zitakapokutukia, fanya kama uonavyo vema; kwa kuwa Mungu yuko pamoja nawe. Nawe utateremka mbele yangu mpaka Gilgali; nami, angalia, nitakuteremkia huko, ili kutoa sadaka za kuteketezwa, na kuchinja sadaka za amani; siku saba utangoja, hata nitakapokujia, na kukuonesha yatakayokupasa kuyafanya. Ikawa, alipogeuka kumwacha Samweli, Mungu akambadilisha moyo; nazo ishara zile zote zikatukia siku ile ile. Basi, walipofika Gibea, tazama, kikosi cha manabii wakakutana naye; kisha Roho ya Mungu ikamjia kwa nguvu, naye akatabiri kati yao. Ikawa, wote waliomjua zamani walipoliona jambo hilo, kwamba, tazama, huyo anatabiri pamoja na manabii, ndipo watu wakasemezana, Ni nini hilo lililompata mwana wa Kishi? Je! Sauli pia yumo miongoni mwa manabii?

1 Samueli 10:2-11 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Utakapoondoka kwangu leo, utakutana na wanaume wawili karibu na kaburi la Raheli, katika mpaka wa Benyamini huko Selsa; nao watakuambia, Punda hao uliokwenda kuwatafuta wameonekana; na tazama, baba yako ameacha kufikiri habari za punda, anafikiri habari zenu, akisema, Nifanye nini kwa ajili ya mwanangu? Kisha utakwenda mbele kutoka hapo, na kufika kwa mwaloni wa Tabori, na hapo watu watatu watakutana nawe, wanaokwea kumwendea Mungu huko Betheli, mmoja anachukua wana-mbuzi watatu, na mwingine anachukua mikate mitatu, na mwingine anachukua kiriba cha divai; nao watakusalimu na kukupa mikate miwili; nawe utaipokea mikononi mwao. Baada ya hayo utafika Gibea ya Mungu, hapo palipo na ngome ya Wafilisti; kisha itakuwa, utakapofika mjini, utakutana na kundi la manabii wakishuka kutoka mahali pa juu, wenye kinanda, na tari, na kinubi, na filimbi mbele yao, nao watakuwa wakitabiri; na roho ya BWANA itakujilia kwa nguvu, nawe utatabiri pamoja nao, nawe utageuzwa kuwa mtu mwingine. Basi, hapo ishara hizi zitakapokutukia, fanya kama uonavyo vema; kwa kuwa Mungu yu pamoja nawe. Nawe utatelemka mbele yangu mpaka Gilgali; nami, angalia, nitakutelemkia huko, ili kutoa sadaka za kuteketezwa, na kuchinja sadaka za amani; siku saba utangoja, hata nitakapokujia, na kukuonyesha yatakayokupasa kuyafanya. Ikawa, alipogeuka kumwacha Samweli, Mungu akambadilisha moyo; nazo ishara zile zote zikatukia siku ile ile. Basi, walipofika Gibea, tazama, kikosi cha manabii wakakutana naye; kisha roho ya Mungu ikamjilia kwa nguvu, naye akatabiri kati yao. Ikawa, wote waliomjua zamani walipoliona jambo hilo, kwamba, tazama, huyo anatabiri pamoja na manabii, ndipo watu wakasemezana, Ni nini hilo lililompata mwana wa Kishi? Je! Sauli pia yumo miongoni mwa manabii?

1 Samueli 10:2-11 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

Utakapoondoka kwangu leo, utakutana na watu wawili karibu na kaburi la Raheli, huko Selsa kwenye mpaka wa Benyamini. Watakuambia, ‘Punda wale uliotoka kwenda kuwatafuta, wamekwisha kupatikana. Sasa baba yako ameacha kufikiri kuhusu punda na sasa ana hofu kukuhusu wewe. Anauliza, “Nitafanyaje kuhusu mwanangu?” ’ “Kisha utaenda mbele kutoka hapa hadi uufikie mwaloni wa Tabori. Watu watatu wanaopanda kwenda kumwabudu Mungu huko Betheli watakutana nawe hapo. Mmoja atakuwa amechukua wana-mbuzi watatu, mwingine mikate mitatu, na mwingine kiriba cha divai. Watakusalimu na kukupa mikate miwili, ambayo utaipokea kutoka kwao. “Baada ya hayo utaenda Gibea ya Mungu, ambapo hapo kuna kambi ya Wafilisti. Unapokaribia mji utakutana na kundi la manabii wakiteremka kutoka mahali pa juu pa kuabudia wakiwa na vinubi, matari, filimbi na zeze vikipigwa mbele yao, nao watakuwa wakitoa unabii. Roho wa BWANA atakuja juu yako kwa nguvu, nawe utatoa unabii pamoja nao; nawe utageuzwa kuwa mtu wa tofauti. Mara ishara hizi zitakapotimizwa, fanya lolote mkono wako upasao kufanya, kwa kuwa Mungu yu pamoja nawe. “Tangulia kushuka mbele yangu hadi Gilgali. Hakika nami nitateremka nikujie ili kutoa dhabihu za sadaka za kuteketezwa na dhabihu za amani, lakini lazima ungoje kwa siku saba hata nitakapokujia na kukuambia likupasalo kufanya.” Ikawa Sauli alipogeuka kumwacha Samweli, Mungu aliubadilisha moyo wa Sauli, na ishara hizi zote zikatimizwa siku ile. Walipofika Gibea, akakutana na kundi la manabii. Roho wa Mungu akaja juu yake kwa nguvu, naye akajiunga nao katika kutoa unabii kwao. Ikawa wale wote waliomfahamu hapo mwanzo walipomwona akitoa unabii pamoja na manabii, wakaulizana, “Ni nini hiki kilichomtokea mwana wa Kishi? Je, Sauli naye pia yumo miongoni mwa manabii?”