1 Samueli 10:1-24
1 Samueli 10:1-24 Biblia Habari Njema (BHN)
Ndipo Samueli akachukua chupa ndogo ya mafuta akammiminia Shauli kichwani, akambusu na kumwambia, “Mwenyezi-Mungu amekutia mafuta uwe mtawala juu ya watu wake. Leo tutakapoagana, utakutana na watu wawili karibu na kaburi la Raheli huko Selsa katika nchi ya Benyamini. Hao watakuambia kuwa wale punda uliokuwa unawatafuta wamekwisha patikana. Baba yako ameacha kufikiri juu ya punda, ila ana wasiwasi juu yako, akijiuliza kila mara, ‘Nitafanya nini juu ya mwanangu?’ Kutoka hapo utakwenda kwenye mwaloni wa Tabori, mahali ambapo utakutana na wanaume watatu wakiwa njiani kwenda kumtolea Mungu tambiko, huko Betheli. Mmoja wao atakuwa anawachukua wanambuzi watatu, wa pili atakuwa anachukua mikate mitatu na wa tatu atakuwa amebeba kiriba cha divai. “Watakusalimia na kukupa mikate miwili, nawe utaipokea mikononi mwao. Kisha, utakapofika huko Gibea-elohimu, mahali ambapo pana kambi ya kijeshi ya Wafilisti; hapo, utakapokuwa unakaribia mji, utakutana na kundi la manabii. Manabii hao watakuwa wanatoka mahali pa juu huku wakipiga vinubi, matari, filimbi na zeze, na watakuwa wanatabiri. Roho ya Mwenyezi-Mungu itakujia kwa nguvu, nawe utaanza kutabiri pamoja nao na kugeuka kuwa mtu mwingine. Wakati mambo haya yatakapokutokea, chochote utakachoweza kufanya kifanye, kwani Mungu yu pamoja nawe. Utanitangulia kwenda mjini Gilgali, mahali ambapo nitakukuta na kutoa sadaka ya kuteketezwa na tambiko za amani. Utaningojea hapo kwa muda wa siku saba mpaka nije na kukuonesha la kufanya.” Shauli alipogeuka ili kumwacha Samueli, Mungu akabadili moyo wa Shauli. Yale yote aliyoambiwa na Samueli yakatokea siku hiyo. Shauli na mtumishi wake walipofika huko Gibea, alilakiwa na kundi la manabii. Roho ya Mungu ilimjia kwa nguvu, na Shauli akaanza kutabiri pamoja na manabii hao. Watu waliomfahamu Shauli hapo awali, walipomwona anatabiri, wakaulizana, “Kitu gani kimempata mwana wa Kishi? Je, hata Shauli ni mmoja wa manabii?” Mtu fulani, mkazi wa mahali hapo, akasema, “Je, baba yao ni nani?” Hivyo kukazuka methali isemayo, “Je, hata Shauli ni mmoja wa manabii?” Shauli alipomaliza kutabiri, alikwenda mahali pa ibada juu. Baba mdogo wa Shauli alipowaona Shauli na mtumishi, akawauliza, “Mlikuwa wapi?” Shauli akajibu, “Tulikwenda kuwatafuta punda, na tulipoona hawapatikani, tulikwenda kumwona Samueli.” Yule baba mdogo wa Shauli akamwambia, “Tafadhali, niambie kile alichokuambia Samueli.” Shauli akajibu, “Alituambia waziwazi kuwa punda wamepatikana.” Lakini Shauli hakumweleza kuwa Samueli alimwambia kuwa atakuwa mfalme. Samueli aliwaita watu wote wakusanyike mbele ya Mwenyezi-Mungu huko Mizpa. Walipowasili aliwaambia, “Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, anasema hivi: Niliwatoa Waisraeli nchini Misri, nikawaokoa nyinyi kutoka kwa Wamisri na falme nyingine zilizowakandamiza. Lakini leo hii mmenikataa mimi Mungu wenu ambaye nawaokoa kutoka maafa na huzuni zenu; nanyi mmesema, ‘La! Tuwekee mfalme juu yetu.’ Sasa, basi, jikusanyeni nyote mbele yangu mkiwa katika makabila yenu na kwa maelfu yenu.” Kisha Samueli akayapanga makabila yote ya Israeli, kabila la Benyamini likachukuliwa kwa kura. Akalileta mbele kabila la Benyamini, kulingana na koo zake, na ukoo wa Matri ukachaguliwa kwa kura. Mwisho akauleta mbele ukoo wa Matri, na Shauli mwana wa Kishi akachaguliwa kwa kura. Lakini walipomtafuta hakupatikana. Wakamwuliza Mungu tena, “Je, kuna mtu zaidi anayekuja?” Mwenyezi-Mungu akawajibu, “Anajificha kwenye mizigo.” Basi, walikwenda mbio, wakamtafuta Shauli na kumleta. Shauli aliposimama miongoni mwa watu alikuwa mrefu kuliko watu wote, kuanzia mabegani. Samueli akawaambia watu wote, “Huyu ndiye mtu aliyeteuliwa na Mwenyezi-Mungu katika watu wote; hakuna yeyote aliye kama yeye.” Watu wote wakapiga kelele: “Aishi mfalme.”
1 Samueli 10:1-24 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ndipo Samweli akatwaa kichupa cha mafuta, akayamimina kichwani pake, akambusu, akasema, Je! BWANA hakukutia mafuta [uwe mkuu juu ya watu wake Israeli? Nawe utamiliki watu wa BWANA, na kuwaokoa kutoka kwa mikono ya adui zao; kisha hii itakuwa ishara kwako ya kuwa BWANA amekutia mafuta] uwe mkuu juu ya urithi wake. Utakapoondoka kwangu leo, utakutana na wanaume wawili karibu na kaburi la Raheli, katika mpaka wa Benyamini huko Selsa; nao watakuambia, Punda hao uliokwenda kuwatafuta wameonekana; na tazama, baba yako ameacha kufikiri habari za punda, anafikiri habari zenu, akisema, Nifanye nini kwa ajili ya mwanangu? Kisha utakwenda mbele kutoka hapo, na kufika kwenye mwaloni wa Tabori, na hapo watu watatu watakutana nawe, wanaokwea kumwendea Mungu huko Betheli, mmoja anachukua wana-mbuzi watatu, na mwingine anachukua mikate mitatu, na mwingine anachukua kiriba cha divai; nao watakusalimu na kukupa mikate miwili; nawe utaipokea mikononi mwao. Baada ya hayo utafika Gibea ya Mungu, hapo palipo na ngome ya Wafilisti; kisha itakuwa, utakapofika mjini, utakutana na kundi la manabii wakishuka kutoka mahali pa juu, wenye kinanda, na tari, na kinubi, na filimbi mbele yao, nao watakuwa wakitabiri; na Roho ya BWANA itakujia kwa nguvu, nawe utatabiri pamoja nao, nawe utageuzwa kuwa mtu mwingine. Basi, hapo ishara hizi zitakapokutukia, fanya kama uonavyo vema; kwa kuwa Mungu yuko pamoja nawe. Nawe utateremka mbele yangu mpaka Gilgali; nami, angalia, nitakuteremkia huko, ili kutoa sadaka za kuteketezwa, na kuchinja sadaka za amani; siku saba utangoja, hata nitakapokujia, na kukuonesha yatakayokupasa kuyafanya. Ikawa, alipogeuka kumwacha Samweli, Mungu akambadilisha moyo; nazo ishara zile zote zikatukia siku ile ile. Basi, walipofika Gibea, tazama, kikosi cha manabii wakakutana naye; kisha Roho ya Mungu ikamjia kwa nguvu, naye akatabiri kati yao. Ikawa, wote waliomjua zamani walipoliona jambo hilo, kwamba, tazama, huyo anatabiri pamoja na manabii, ndipo watu wakasemezana, Ni nini hilo lililompata mwana wa Kishi? Je! Sauli pia yumo miongoni mwa manabii? Naye akajibu mtu mmoja wa mahali hapo, akasema, Na baba yao ni nani? Kwa hiyo ikawa mithali, Je! Sauli pia yumo miongoni mwa manabii? Naye alipokwisha kutabiri, alipafikia mahali pale pa juu. Basi babaye mdogo akamwuliza Sauli na mtumishi wake, Je! Mlikwenda wapi? Naye akajibu, Tulikwenda ili kuwatafuta hao punda; na tulipoona ya kwamba hawakuonekana, tulimwendea Samweli. Babaye mdogo Sauli akasema, Tafadhali niambie, huyo Samweli aliwaambiaje? Lakini Sauli akamjibu babaye mdogo, Alituambia waziwazi ya kuwa hao punda wamekwisha onekana. Lakini habari ya ufalme, ambayo Samweli alimwambia, hakuitaja. Basi Samweli akawakusanya watu mbele za BWANA huko Mispa akawaambia wana wa Israeli, BWANA, Mungu wa Israeli, asema hivi, Niliwatoa Waisraeli kutoka Misri, nami niliwaokoa ninyi kutoka kwa mikono ya Wamisri, na ya falme zote zilizowaonea; lakini leo mmemkataa Mungu wenu, naye ndiye awaponyaye katika misiba yenu yote na shida zenu; nanyi mmemwambia, Sivyo, lakini weka mfalme juu yetu. Basi, sasa, njoni mbele za BWANA, kwa makabila yenu na kwa maelfu yenu. Basi Samweli akayaleta makabila yote ya Israeli karibu; na kabila la Benyamini likachukuliwa kwa kura. Kisha akalileta kabila la Benyamini karibu, kulingana na jamaa zao; jamaa ya Wamatri ikachukuliwa kwa kura. Akaileta jamaa ya Wamatri karibu, mtu baada ya mtu; kisha Sauli, mwana wa Kishi, akachaguliwa kwa kura; lakini walipomtafuta hakuonekana. Basi wakazidi kumwuliza BWANA, Amebaki mtu asiyekuja huku bado? Naye BWANA akajibu, Tazama, amejificha kwenye mizigo. Basi wakaenda mbio wakamleta kutoka huko; naye aliposimama kati ya watu, alikuwa mrefu kuliko watu wote, tangu mabega yake kwenda juu. Samweli akawaambia watu wote, Mnamwona mtu huyu aliyechaguliwa na BWANA, kwamba hakuna mtu mfano wake katika watu wote. Ndipo watu wote wakapiga kelele, wakasema, Mfalme na aishi!
1 Samueli 10:1-24 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ndipo Samweli akatwaa kichupa cha mafuta, akayamimina kichwani pake, akambusu, akasema, Je! BWANA hakukutia mafuta [uwe mkuu juu ya watu wake Israeli? Nawe utamiliki watu wa BWANA, na kuwaokoa na mikono ya adui zao; kisha hii itakuwa ishara kwako ya kuwa BWANA amekutia mafuta] uwe mkuu juu ya urithi wake. Utakapoondoka kwangu leo, utakutana na wanaume wawili karibu na kaburi la Raheli, katika mpaka wa Benyamini huko Selsa; nao watakuambia, Punda hao uliokwenda kuwatafuta wameonekana; na tazama, baba yako ameacha kufikiri habari za punda, anafikiri habari zenu, akisema, Nifanye nini kwa ajili ya mwanangu? Kisha utakwenda mbele kutoka hapo, na kufika kwa mwaloni wa Tabori, na hapo watu watatu watakutana nawe, wanaokwea kumwendea Mungu huko Betheli, mmoja anachukua wana-mbuzi watatu, na mwingine anachukua mikate mitatu, na mwingine anachukua kiriba cha divai; nao watakusalimu na kukupa mikate miwili; nawe utaipokea mikononi mwao. Baada ya hayo utafika Gibea ya Mungu, hapo palipo na ngome ya Wafilisti; kisha itakuwa, utakapofika mjini, utakutana na kundi la manabii wakishuka kutoka mahali pa juu, wenye kinanda, na tari, na kinubi, na filimbi mbele yao, nao watakuwa wakitabiri; na roho ya BWANA itakujilia kwa nguvu, nawe utatabiri pamoja nao, nawe utageuzwa kuwa mtu mwingine. Basi, hapo ishara hizi zitakapokutukia, fanya kama uonavyo vema; kwa kuwa Mungu yu pamoja nawe. Nawe utatelemka mbele yangu mpaka Gilgali; nami, angalia, nitakutelemkia huko, ili kutoa sadaka za kuteketezwa, na kuchinja sadaka za amani; siku saba utangoja, hata nitakapokujia, na kukuonyesha yatakayokupasa kuyafanya. Ikawa, alipogeuka kumwacha Samweli, Mungu akambadilisha moyo; nazo ishara zile zote zikatukia siku ile ile. Basi, walipofika Gibea, tazama, kikosi cha manabii wakakutana naye; kisha roho ya Mungu ikamjilia kwa nguvu, naye akatabiri kati yao. Ikawa, wote waliomjua zamani walipoliona jambo hilo, kwamba, tazama, huyo anatabiri pamoja na manabii, ndipo watu wakasemezana, Ni nini hilo lililompata mwana wa Kishi? Je! Sauli pia yumo miongoni mwa manabii? Naye akajibu mtu mmoja wa mahali hapo, akasema, Na baba yao n’nani? Kwa hiyo ikawa mithali, Je! Sauli pia yumo miongoni mwa manabii? Naye alipokwisha kutabiri, alipafikilia mahali pale pa juu. Basi babaye mdogo akamwuliza Sauli na mtumishi wake, Je! Mlikwenda wapi? Naye akajibu, Tulikwenda ili kuwatafuta hao punda; na tulipoona ya kwamba hawakuonekana, tulimwendea Samweli. Babaye mdogo Sauli akasema, Tafadhali uniambie, huyo Samweli aliwaambiaje? Lakini Sauli akamjibu babaye mdogo, Alituambia waziwazi ya kuwa hao punda wamekwisha onekana. Lakini habari ya ufalme, ambayo Samweli alimwambia, hakuitaja habari hiyo. Basi Samweli akawakusanya watu mbele za BWANA huko Mispa akawaambia wana wa Israeli, BWANA, Mungu wa Israeli, asema hivi, Naliwatoa Israeli kutoka Misri, nami naliwaokoa ninyi na mikono ya Wamisri, na ya falme zote zilizowaonea; lakini leo mmemkataa Mungu wenu, naye ndiye awaponyaye katika misiba yenu yote na shida zenu; nanyi mmemwambia, Sivyo, lakini weka mfalme juu yetu. Basi, sasa, hudhurieni mbele za BWANA, kwa kabila zenu na kwa elfu zenu. Basi Samweli akawaleta kabila zote za Israeli karibu; na kabila ya Benyamini ikatwaliwa. Kisha akaileta kabila ya Benyamini karibu, kwa jamaa zao; jamaa ya Wamatri ikatwaliwa. Akaileta jamaa ya Wamatri karibu, mtu baada ya mtu; kisha Sauli, mwana wa Kishi, akatwaliwa; lakini walipomtafuta hakuonekana. Basi wakazidi kumwuliza BWANA, Amebaki mtu asiyekuja huku bado? Naye BWANA akajibu, Tazama, amejificha penye mizigo. Basi wakaenda mbio wakamleta kutoka huko; naye aliposimama kati ya watu, alikuwa mrefu kuliko watu wote, tangu mabega yake kwenda juu. Samweli akawaambia watu wote, Mnamwona mtu huyu aliyechaguliwa na BWANA, ya kuwa hakuna mtu mfano wake katika watu wote. Ndipo watu wote wakapiga kelele, wakasema, Mfalme na aishi!
1 Samueli 10:1-24 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Ndipo Samweli akachukua chupa ndogo ya mafuta na kuyamimina juu ya kichwa cha Sauli, akambusu, akisema, “Je, BWANA hakukupaka mafuta uwe kiongozi juu ya urithi wake? Utakapoondoka kwangu leo, utakutana na watu wawili karibu na kaburi la Raheli, huko Selsa kwenye mpaka wa Benyamini. Watakuambia, ‘Punda wale uliotoka kwenda kuwatafuta, wamekwisha kupatikana. Sasa baba yako ameacha kufikiri kuhusu punda na sasa ana hofu kukuhusu wewe. Anauliza, “Nitafanyaje kuhusu mwanangu?” ’ “Kisha utaenda mbele kutoka hapa hadi uufikie mwaloni wa Tabori. Watu watatu wanaopanda kwenda kumwabudu Mungu huko Betheli watakutana nawe hapo. Mmoja atakuwa amechukua wana-mbuzi watatu, mwingine mikate mitatu, na mwingine kiriba cha divai. Watakusalimu na kukupa mikate miwili, ambayo utaipokea kutoka kwao. “Baada ya hayo utaenda Gibea ya Mungu, ambapo hapo kuna kambi ya Wafilisti. Unapokaribia mji utakutana na kundi la manabii wakiteremka kutoka mahali pa juu pa kuabudia wakiwa na vinubi, matari, filimbi na zeze vikipigwa mbele yao, nao watakuwa wakitoa unabii. Roho wa BWANA atakuja juu yako kwa nguvu, nawe utatoa unabii pamoja nao; nawe utageuzwa kuwa mtu wa tofauti. Mara ishara hizi zitakapotimizwa, fanya lolote mkono wako upasao kufanya, kwa kuwa Mungu yu pamoja nawe. “Tangulia kushuka mbele yangu hadi Gilgali. Hakika nami nitateremka nikujie ili kutoa dhabihu za sadaka za kuteketezwa na dhabihu za amani, lakini lazima ungoje kwa siku saba hata nitakapokujia na kukuambia likupasalo kufanya.” Ikawa Sauli alipogeuka kumwacha Samweli, Mungu aliubadilisha moyo wa Sauli, na ishara hizi zote zikatimizwa siku ile. Walipofika Gibea, akakutana na kundi la manabii. Roho wa Mungu akaja juu yake kwa nguvu, naye akajiunga nao katika kutoa unabii kwao. Ikawa wale wote waliomfahamu hapo mwanzo walipomwona akitoa unabii pamoja na manabii, wakaulizana, “Ni nini hiki kilichomtokea mwana wa Kishi? Je, Sauli naye pia yumo miongoni mwa manabii?” Mtu mmoja ambaye aliishi huko akajibu, “Je, naye baba yao ni nani?” Basi ikawa mithali, kusema, “Je, Sauli pia yumo miongoni mwa manabii?” Baada ya Sauli kumaliza kutoa unabii, alienda mahali pa juu pa kuabudia. Basi babaye mdogo akamuuliza Sauli na mtumishi wake, “Je, mlikuwa wapi?” Akajibu, “Tulikuwa tukiwatafuta punda. Lakini tulipoona hawapatikani, tulienda kwa Samweli.” Babaye mdogo Sauli akasema, “Niambie Samweli amekuambia nini.” Sauli akajibu, “Alituhakikishia kwamba punda wamepatikana.” Lakini hakumwambia babaye mdogo kila kitu Samweli alichomwambia kuhusu ufalme. Samweli akawaita watu wa Israeli kuja kwa BWANA huko Mispa, naye akawaambia, “Hili ndilo asemalo BWANA, Mungu wa Israeli: ‘Niliwatoa Israeli kutoka Misri, nami niliwaokoa toka nguvu za Misri na falme zote zilizowadhulumu.’ Lakini sasa mmemkataa Mungu wenu, ambaye anawaokoa toka katika maafa yenu yote na taabu zenu zote. Nanyi mmesema, ‘Hapana, tuteulie mfalme atutawale.’ Sasa basi, jihudhurisheni wenyewe mbele za BWANA kwa makabila yenu na kwa koo zenu.” Samweli alipoyasogeza makabila yote ya Israeli, kabila la Benyamini likachaguliwa. Kisha akalisogeza mbele kabila la Benyamini, kufuatana na koo zao, nao ukoo wa Matri ukachaguliwa. Mwishoni Sauli mwana wa Kishi akachaguliwa. Lakini walipomtafuta, hakuonekana. Wakazidi kuuliza kwa BWANA, “Je, huyo mtu amekwisha kufika hapa?” Naye BWANA akasema, “Ndiyo, amejificha kwenye mizigo.” Wakakimbia na kumleta kutoka huko, naye aliposimama kati ya watu, alikuwa mrefu kuliko watu wengine wote. Samweli akawaambia watu wote, “Je, mnamwona mtu ambaye BWANA amemchagua? Hayupo aliye kama yeye miongoni mwa watu wote.” Ndipo watu wakasema kwa sauti kuu, “Mfalme aishi maisha marefu.”