1 Samueli 1:6-11
1 Samueli 1:6-11 Biblia Habari Njema (BHN)
Lakini Penina, mchokozi wa Hana, daima alikuwa akimkasirisha vikali na kumuudhi Hana kwa kuwa Mwenyezi-Mungu hakumjalia watoto. Mambo haya yaliendelea mwaka baada ya mwaka. Kila mara Hana alipokwenda kwenye nyumba ya Mwenyezi-Mungu, Penina alimkasirisha Hana hata ikawa Hana analia na kukataa kula chochote. Elkana, mumewe, kila mara alimwuliza, “Kwa nini unalia? Kwa nini hutaki kula? Kwa nini una huzuni moyoni mwako? Je, mimi si bora kwako kuliko watoto kumi wa kiume?” Siku moja, walipokuwa wamemaliza kula na kunywa katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu huko Shilo, Hana akasimama. Wakati huo, kuhani Eli alikuwa amekaa kwenye kiti karibu na mwimo wa nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Hana alikuwa na huzuni sana. Na alipokuwa anamwomba Mwenyezi-Mungu akawa analia kwa uchungu. Akaweka nadhiri akisema, “Ee Mwenyezi-Mungu wa majeshi, kama tu utayaangalia mateso yangu mimi mtumishi wako ukanikumbuka mimi, bila kunisahau, mimi mtumishi wako, ukanijalia mimi mtumishi wako, mtoto wa kiume, nitakupa wewe Mwenyezi-Mungu mtoto huyo awe wako maisha yake yote; wembe hautapita kichwani pake kamwe.”
1 Samueli 1:6-11 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ila mwenzake humchokoza sana, ili kumwuudhi, kwa sababu BWANA alikuwa amemfunga tumbo. Tena mumewe akafanya hivyo mwaka kwa mwaka, hapo yule mwanamke alipokwea kwenda nyumbani kwa BWANA, ndivyo yule alivyomchokoza; basi, kwa hiyo, yeye akalia, asile chakula. Elkana mumewe akamwambia, Hana, unalilia nini? Kwa nini huli? Kwa nini moyo wako una huzuni? Je! Mimi si bora kwako kuliko watoto kumi? Ndipo Hana akainuka, walipokula na kunywa huko Shilo. Naye Eli, kuhani, alikuwa akiketi kitini pake penye mwimo wa hekalu la BWANA. Naye huyo mwanamke alikuwa na uchungu rohoni mwake, akamwomba BWANA akalia sana. Akaweka nadhiri, akasema, Ee BWANA wa majeshi, ikiwa wewe utayaangalia mateso la mjakazi wako, na kunikumbuka, wala usinisahau mimi mjakazi wako, na kunipa mimi mjakazi wako mtoto wa kiume, ndipo mimi nitakapompa BWANA huyo mtoto siku zote za maisha yake, wala wembe hautamfikia kichwani kamwe.
1 Samueli 1:6-11 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ila mwenzake humchokoza sana, hata kumsikitisha, kwa sababu BWANA alikuwa amemfunga tumbo. Tena mumewe akafanya hivyo mwaka kwa mwaka, hapo yule mwanamke alipokwea kwenda nyumbani kwa BWANA, ndivyo yule alivyomchokoza; basi, kwa hiyo, yeye akalia, asile chakula. Elkana mumewe akamwambia, Hana, unalilia nini? Kwani huli chakula? Kwa nini moyo wako una huzuni? Je! Mimi si bora kwako kuliko watoto kumi? Ndipo Hana akainuka, walipokwisha kula na kunywa huko Shilo. Naye Eli, kuhani, alikuwa akiketi kitini pake penye mwimo wa hekalu la BWANA. Naye huyo mwanamke alikuwa na uchungu rohoni mwake, akamwomba BWANA akalia sana. Akaweka nadhiri, akasema, Ee BWANA wa majeshi, ikiwa wewe utaliangalia teso la mjakazi wako, na kunikumbuka, wala usinisahau mimi mjakazi wako, na kunipa mimi mjakazi wako mtoto mume, ndipo mimi nitakapompa BWANA huyo mtoto siku zote za maisha yake, wala wembe hautamfikilia kichwani kamwe.
1 Samueli 1:6-11 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Kwa sababu BWANA alikuwa amemfunga tumbo, mke mwenzake alikuwa anamchokoza ili kumuudhi. Hili liliendelea mwaka baada ya mwaka. Kila mara Hana alipoenda katika nyumba ya BWANA, mke mwenzake alikuwa akimkasirisha hadi analia na kushindwa kula. Elkana mumewe akawa anamwambia, “Hana, kwa nini unalia? Kwa nini huli? Kwa nini kuvunjika moyo? Je, mimi si bora zaidi kwako kuliko watoto kumi?” Siku moja walipokuwa wamemaliza kula na kunywa huko Shilo, Hana alisimama. Wakati huo kuhani Eli alikuwa ameketi kwenye kiti pembeni mwa mwimo wa mlango wa Hekalu la BWANA. Kwa uchungu wake mwingi Hana alimwomba BWANA, akilia kwa uchungu. Naye akaweka nadhiri, akisema, “Ee BWANA wa majeshi, laiti ungeangalia huzuni kuu ya mtumishi wako na kunikumbuka mimi, wala usimsahau mtumishi wako nawe ukampa mwana, basi huyo mwana nitamtoa kwa BWANA kwa siku zote za maisha yake, wala wembe hautapita kichwani mwake.”