1 Petro 2:9-12
1 Petro 2:9-12 Biblia Habari Njema (BHN)
Lakini nyinyi ni ukoo mteule, makuhani wa Mfalme, taifa takatifu; watu wake Mungu mwenyewe, mlioteuliwa kutangaza matendo makuu ya Mungu aliyewaiteni kutoka gizani, akawaingizeni katika mwanga wake mkuu. Wakati mmoja nyinyi hamkuwa watu wa Mungu, lakini sasa nyinyi ni watu wake; wakati mmoja hamkupewa huruma ya Mungu, lakini sasa mmepokea huruma. Wapenzi wangu, nawasihi nyinyi kama wageni na wakimbizi hapa duniani! Achaneni na tamaa za mwili ambazo hupingana na roho. Mwenendo wenu kati ya watu wasiomjua Mungu unapaswa kuwa mwema kabisa, ili hata watakapowasingizieni kwamba mnatenda mabaya, waweze kutambua matendo yenu mema na hivyo wamtukuze Mungu siku ya kuja kwake.
1 Petro 2:9-12 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Bali ninyi ni uzao mteule, ukuhani wa kifalme, taifa takatifu, watu wa milki ya Mungu, mpate kuzitangaza fadhili zake yeye aliyewaita mtoke gizani mkaingie katika nuru yake ya ajabu; ninyi mliokuwa kwanza si taifa, bali sasa ni taifa la Mungu; mliokuwa hamkupata rehema, bali sasa mmepata rehema. Wapenzi, nawasihi kama wapitaji na wasafiri, ziepukeni tamaa za mwili zipiganazo na roho. Muwe na mwenendo mzuri kati ya Mataifa, ili, iwapo huwasingizia kuwa watenda mabaya, wayatazamapo matendo yenu mazuri, wamtukuze Mungu siku ya kujiliwa.
1 Petro 2:9-12 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Bali ninyi ni mzao mteule, ukuhani wa kifalme, taifa takatifu, watu wa milki ya Mungu, mpate kuzitangaza fadhili zake yeye aliyewaita mtoke gizani mkaingie katika nuru yake ya ajabu; ninyi mliokuwa kwanza si taifa, bali sasa ni taifa la Mungu; mliokuwa hamkupata rehema, bali sasa mmepata rehema. Wapenzi, nawasihi kama wapitaji na wasafiri, ziepukeni tamaa za mwili zipiganazo na roho. Mwe na mwenendo mzuri kati ya Mataifa, ili, iwapo huwasingizia kuwa watenda mabaya, wayatazamapo matendo yenu mazuri, wamtukuze Mungu siku ya kujiliwa.
1 Petro 2:9-12 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Lakini ninyi ni taifa teule, ukuhani wa kifalme, taifa takatifu, watu walio milki ya Mungu, mlioitwa ili kutangaza sifa zake yeye aliyewaita kutoka gizani mkaingie katika nuru yake ya ajabu. Mwanzo ninyi mlikuwa si taifa, lakini sasa ninyi ni taifa la Mungu. Mwanzo mlikuwa hamjapata rehema, lakini sasa mmepata rehema. Wapendwa, ninawasihi, mkiwa kama wageni na wapitaji hapa ulimwenguni, epukeni tamaa mbaya za mwili ambazo hupigana vita na roho zenu. Kuweni na mwenendo mzuri mbele ya watu wasiomjua Mungu, ili kama wanawasingizia kuwa watenda mabaya, wayaone matendo yenu mema nao wamtukuze Mungu siku atakapokuja kwetu.