Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Wafalme 9:1-28

1 Wafalme 9:1-28 Biblia Habari Njema (BHN)

Mfalme Solomoni alipomaliza kujenga nyumba ya Mwenyezi-Mungu na ikulu na majengo mengine yote aliyokusudia kujenga, Mwenyezi-Mungu alimtokea tena kama alivyomtokea kule Gibeoni. Mwenyezi-Mungu alimwambia, “Nimesikia sala yako na ombi lako. Nimeitakasa nyumba hii ambayo umenijengea ili watu waliabudu jina langu hapa milele. Nitaichunga na kuipenda wakati wote. Nawe kama ukinitumikia kwa unyofu wa moyo na uadilifu kama baba yako Daudi alivyofanya, ukitii amri zangu na kutimiza yale yote niliyokuamuru, ukifuata masharti yangu na maagizo yangu; basi, mimi nitakiimarisha kiti chako cha kifalme juu ya Israeli milele, kama nilivyomwahidi Daudi baba yako, nikisema, Hutakosa mtu wa kukaa juu ya kiti cha enzi cha Israeli. Lakini wewe au watoto wako mkigeuka na kuacha kunifuata, msiposhika amri zangu na maongozi niliyowapani, mkienda kutumikia miungu mingine na kuiabudu, basi, nitawahamisha watu wangu, Israeli, kutoka nchi hii ambayo nimewapa; kadhalika na nyumba hii ambayo nimeiweka wakfu kwa ajili ya jina langu, nitaitupilia mbali nami, na kuifanya kitu cha kupuuzwa na kudharauliwa miongoni mwa mataifa yote. Na nyumba hii itabomoka na kuwa magofu; kila apitaye karibu atashtuka na kutikisa kichwa, na kuuliza, ‘Kwa nini Mwenyezi-Mungu amefanya hivyo kwa nchi hii na kwa nyumba hii?’ Watu wengine watajibu, ‘Ni kwa sababu walimwacha Mwenyezi-Mungu, Mungu wao, aliyewatoa babu zao katika nchi ya Misri, wakashikamana na miungu mingine, wakaiabudu na kuitumikia; kwa hiyo, Mwenyezi-Mungu amewaletea maafa haya yote.’” Kisha miaka ishirini ilipokwisha pita, ambayo Solomoni alizijenga zile nyumba mbili: Nyumba ya Mwenyezi-Mungu na ikulu, mfalme Solomoni alimpa Hiramu mfalme wa Tiro, miji ishirini katika mkoa wa Galilaya (kwa sababu huyo Hiramu alikuwa amempelekea Solomoni mbao za mierezi na miberoshi, na dhahabu pia, kadiri alivyohitaji kwa ujenzi). Lakini Hiramu alipowasili kutoka Tiro na kuiona miji hiyo aliyokuwa amepewa na Solomoni hakupendezwa nayo. Basi, akamwuliza Solomoni, “Ndugu yangu, ni miji gani hii ambayo umenipa?” Ndio sababu miji hiyo inaitwa nchi ya Kabuli hata leo. Hiramu alikuwa amempelekea mfalme Solomoni dhahabu kilo 3,600. Yafuatayo ni maelezo juu ya jinsi mfalme Solomoni alivyotumia kazi za kulazimishwa kujenga nyumba ya Mwenyezi-Mungu, ikulu yake, ngome ya Milo na ukuta wa Yerusalemu, na pia katika kujenga upya miji ya Hazori, Megido na Gezeri; (Gezeri ndio mji ambao Farao, mfalme wa Misri, alikuwa ameuteka, akauchoma moto na kuwaua Wakanaani, wakazi wake. Baadaye, binti Farao alipoolewa na Solomoni, mfalme wa Misri alimpa binti yake mji huo wa Gezeri uwe zawadi ya harusi. Basi, Solomoni aliujenga upya mji wa Gezeri); hali kadhalika alijenga Beth-horoni ya chini; kadhalika miji ifuatayo: Baalathi, na Tamari, mji ulio nyikani katika nchi ya Yuda na miji yake yote ya ghala, magari yake ya kukokotwa, na wapandafarasi wake; pia chochote alichotaka kujenga katika Yerusalemu, Lebanoni au kwingineko katika ufalme wake. Watu wengine wote waliobaki miongoni mwa Waamori, Wahiti, Waperizi, Wahivi na Wayebusi, yaani wote hao ambao hawakuwa wa taifa la Israeli, pamoja na wazawa wao ambao Waisraeli hawakuweza kuwaangamiza kabisa, Solomoni aliwafanyiza kazi za kulazimishwa hata leo. Lakini kati ya Waisraeli, Solomoni hakumfanya mtu yeyote kuwa mtumwa; wao ndio waliokuwa askari, watumishi wake, makamanda wake, maofisa wake, makamanda wa magari yake ya kukokotwa, na wapandafarasi wake. Ifuatayo ndiyo jumla ya maofisa wakuu waliohusika na uangalizi wa kazi ya Solomoni: Watu 550, hao ndio waliosimamia watu waliofanya kazi. Baadaye binti Farao aliuhama mji wa Daudi, akaenda kukaa katika nyumba yake mwenyewe ambayo Solomoni alimjengea; kisha Solomoni akajenga ngome ya Milo. Mara tatu kila mwaka, Solomoni alitoa tambiko za kuteketezwa na tambiko za amani juu ya madhabahu aliyokuwa amemjengea Mwenyezi-Mungu, akamfukizia Mwenyezi-Mungu ubani; pia alifanya marekebisho ya nyumba. Mfalme Solomoni aliunda merikebu nyingi huko Esion-geberi, karibu na Elothi iliyo pwani ya Bahari ya Shamu, katika nchi ya Edomu. Naye mfalme Hiramu akawatuma maofisa wake na mabaharia pamoja na watumishi wa Solomoni. Walisafiri kwenda nchi ya Ofiri, na kuchukua toka huko dhahabu, wakamletea mfalme Solomoni kadiri ya kilo 14,000.

1 Wafalme 9:1-28 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Ikawa Sulemani alipokwisha kuijenga nyumba ya BWANA, na nyumba ya mfalme, na mambo yote yaliyoingia moyoni mwake Sulemani, naye akataka kuyafanya, basi, BWANA akamtokea Sulemani mara ya pili kama alivyomtokea huko Gibeoni. BWANA akamwambia, Nimeyasikia maombi yako na dua zako, ulizotoa mbele zangu. Nimeitakasa nyumba hii uliyoijenga ili niweke jina langu humo milele; tena macho yangu na moyo wangu utakuwapo hapo siku zote; na wewe, ukienda mbele zangu kama alivyokwenda Daudi, baba yako, kwa ukamilifu wa moyo, na kwa adili, kufanya hayo yote niliyokuamuru, na kuzishika sheria zangu na hukumu zangu, ndipo nitakapokifanya imara kiti cha ufalme wako juu ya Israeli milele; kama nilivyomwahidia Daudi, baba yako, nikisema, Hutakosa kuwa na mtu wa kukaa katika kiti cha enzi cha Israeli. Bali mkighairi, mkaacha kunifuata, ninyi na watoto wenu, msizishike sheria zangu na amri zangu, nilizoziweka mbele yenu, tena mkienda na kuitumikia miungu mingine na kuiabudu, basi nitawakatilia Israeli mbali na nchi hii niliyowapa; na nyumba hii niliyoitakasa kwa jina langu, nitaitupilia mbali na macho yangu, na Israeli watakuwa mithali na neno la tusi katika mataifa yote. Na ijapokuwa nyumba hii imetukuka namna hii, lakini kila apitaye atashtuka na kuizomea; nao watasema, Kwa nini BWANA ameitenda nchi hii na nyumba hii mambo haya? Na watu watajibu, Kwa sababu walimwacha BWANA, Mungu wao, aliyewatoa baba zao katika nchi ya Misri, wakashikamana na miungu mingine na kuiabudu na kuitumikia, basi ndiyo sababu BWANA ameleta mabaya haya yote juu yao. Ikawa miaka ishirini ilipopita, ambayo katika hiyo Sulemani alizijenga zile nyumba mbili, nyumba ya BWANA na nyumba yake mfalme, (basi Hiramu, mfalme wa Tiro, alikuwa amemletea Sulemani mierezi na miberoshi, na dhahabu, sawasawa na haja zake zote), ndipo mfalme Sulemani akampa Hiramu miji ishirini ya nchi ya Galilaya. Naye Hiramu akatoka Tiro kuitazama hiyo miji Sulemani aliyompa; wala hakupendezwa. Akasema, Miji gani hii uliyonipa, ndugu yangu? Akaiita nchi ya Kabuli, hata leo. Hiramu alikuwa amemletea mfalme talanta mia moja na ishirini za dhahabu. Na hii ndiyo sababu ya shokoa aliyoitoza mfalme Sulemani; ili kuijenga nyumba ya BWANA, na nyumba yake mwenyewe, na Milo, na ukuta wa Yerusalemu, na Hasori, na Megido, na Gezeri. Farao, mfalme wa Misri, alikuwa amepanda akautwaa Gezeri, na kuuteketeza kwa moto, akawaua Wakanaani waliokaa mjini, akampa zawadi binti yake, mkewe Sulemani. Naye Sulemani akaujenga Gezeri, na Beth-horoni wa chini, na Baalathi, na Tamari ulio nyikani, katika nchi; na miji yote ya hazina iliyokuwa yake Sulemani; na miji ya magari yake, na miji ya watu wake wapandao farasi, na kila alichopenda kujenga Sulemani huko Yerusalemu, na katika Lebanoni, na katika nchi yote ya mamlaka yake. Kwa habari ya watu wote waliosalia, Waamori, Wahiti, Waperizi, Wahivi, na Wayebusi, wasiokuwa wa wana wa Israeli; watoto wao waliosalia baada yao katika nchi, ambao wana wa Israeli hawakuweza kuwaharibu kabisa, katika hao Sulemani akawatumikisha shokoa hata leo. Lakini kwa wana wa Israeli Sulemani hakumtumikisha mtu yeyote shokoa; ila wao walikuwa askari, watumishi wake, makamanda wake, maafisa wake, makamanda wa magari yake na wapanda farasi wake. Hao maofisa wakuu, waliokuwa juu ya kazi yake Sulemani, walikuwa mia tano na hamsini, waliowasimamia watu watendao kazi. Lakini binti Farao akapanda toka mji wa Daudi, mpaka hiyo nyumba yake Sulemani, aliyomjengea; kisha, aliijenga Milo. Na mara tatu kila mwaka Sulemani alikuwa akitoa sadaka za kuteketezwa na sadaka za amani juu ya madhabahu aliyomjengea BWANA akafukiza uvumba pamoja nazo juu ya madhabahu iliyokuwako mbele za BWANA. Hivyo akaimaliza nyumba. Tena, mfalme Sulemani akaunda merikebu huko Ezion-geberi, ulioko karibu na Elothi, pwani ya Bahari ya Shamu, katika nchi ya Edomu. Naye Hiramu akatuma merikebuni watumishi wake, wanamaji wenye kuijua bahari, pamoja na watumishi wake Sulemani. Wakafika Ofiri, wakachukua toka huko dhahabu, talanta mia nne na ishirini, wakamletea mfalme Sulemani.

1 Wafalme 9:1-28 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Ikawa Sulemani alipokwisha kuijenga nyumba ya BWANA, na nyumba ya mfalme, na mambo yote yaliyoingia moyoni mwake Sulemani, naye akataka kuyafanya, basi, BWANA akamtokea Sulemani mara ya pili kama alivyomtokea huko Gibeoni. BWANA akamwambia, Nimeyasikia maombi yako na dua zako, ulizotoa mbele zangu. Nimeitakasa nyumba hii uliyoijenga ili niweke jina langu humo milele; tena macho yangu na moyo wangu utakuwapo hapo siku zote; na wewe, ukienda mbele zangu kama alivyokwenda Daudi, baba yako, kwa ukamilifu wa moyo, na kwa adili, kufanya hayo yote niliyokuamuru, na kuzishika sheria zangu na hukumu zangu, ndipo nitakapokifanya imara kiti cha ufalme wako juu ya Israeli milele; kama nilivyomwahidia Daudi, baba yako, nikisema, Hutakosa kuwa na mtu wa kukaa katika kiti cha enzi cha Israeli. Bali mkighairi, mkaacha kunifuata, ninyi na watoto wenu, msizishike sheria zangu na amri zangu, nilizoziweka mbele yenu, tena mkienda na kuitumikia miungu mingine na kuiabudu, basi nitawakatilia Israeli mbali na nchi hii niliyowapa; na nyumba hii niliyoitakasa kwa jina langu, nitaitupilia mbali na macho yangu, na Israeli watakuwa mithali na neno la tusi katika mataifa yote. Na ijapokuwa nyumba hii imetukuka namna hii, lakini kila apitaye atasituka na kuizomea; nao watasema, Kwa nini BWANA ameitenda nchi hii na nyumba hii mambo haya? Na watu watajibu, Kwa sababu walimwacha BWANA, Mungu wao, aliyewatoa baba zao katika nchi ya Misri, wakashikamana na miungu mingine na kuiabudu na kuitumikia, basi ndiyo sababu BWANA ameleta mabaya haya yote juu yao. Ikawa miaka ishirini ilipopita, ambayo katika hiyo Sulemani alizijenga zile nyumba mbili, nyumba ya BWANA na nyumba yake mfalme, (basi Hiramu, mfalme wa Tiro, alikuwa amemletea Sulemani mierezi na miberoshi, na dhahabu, sawasawa na haja zake zote), ndipo mfalme Sulemani akampa Hiramu miji ishirini ya nchi ya Galilaya. Naye Hiramu akatoka Tiro kuitazama hiyo miji Sulemani aliyompa; wala haikumpendcza. Akasema, Miji gani hii uliyonipa, ndugu yangu? Akaiita nchi ya Kabuli, hata leo. Hiramu akamletea mfalme talanta sitini za dhahabu. Na hii ndiyo sababu ya shokoa aliyoitoza mfalme Sulemani; ili kuijenga nyumba ya BWANA, na nyumba yake mwenyewe, na Milo, na ukuta wa Yerusalemu, na Hazori, na Megido, na Gezeri. Farao, mfalme wa Misri, alikuwa amepanda akautwaa Gezeri, na kuuteketeza kwa moto, akawaua Wakanaani waliokaa mjini, akampa zawadi binti yake, mkewe Sulemani. Naye Sulemani akaujenga Gezeri, na Beth-horoni wa chini, na Baalathi, na Tamari ulio nyikani, katika nchi; na miji yote ya hazina iliyokuwa yake Sulemani; na miji ya magari yake, na miji ya watu wake wapandao farasi, na kila alichopenda kujenga Sulemani huko Yerusalemu, na katika Lebanoni, na katika nchi yote ya mamlaka yake. Kwa habari ya watu wote waliosalia, Waamori, Wahiti, Waperizi, Wahivi, na Wayebusi, wasiokuwa wa wana wa Israeli; watoto wao waliosalia baada yao katika nchi, ambao wana wa Israeli hawakuweza kuwaharibu kabisa, katika hao Sulemani akawatumikisha shokoa hata leo. Lakini wa wana wa Israeli Sulemani hakumtumikisha mtu shokoa; ila ndio watu wa vita, na wangoje wake, na wakuu wake, na akida zake, na wakuu, wa magari yake, na wa wapanda farasi wake. Hao maakida wakuu, waliokuwa juu ya kazi yake Sulemani, walikuwa mia tano na hamsini, waliowaamuru watu watendao kazi. Lakini binti Farao akapanda toka mji wa Daudi, mpaka hiyo nyumba yake Sulemani, aliyomjengea; kisha, aliijenga Milo. Na mara tatu kila mwaka Sulemani alikuwa akitoa sadaka za kuteketezwa na sadaka za amani juu ya madhabahu aliyomjengea BWANA akafukiza uvumba pamoja nazo juu ya madhabahu iliyokuwako mbele za BWANA. Hivyo akaimaliza nyumba. Tena, mfalme Sulemani akaunda merikebu huko Ezion-geberi, ulioko karibu na Elothi, pwani ya Bahari ya Shamu, katika nchi ya Edomu. Naye Hiramu akatuma merikebuni watumishi wake, wanamaji wenye kuijua bahari, pamoja na watumishi wake Sulemani. Wakafika Ofiri, wakachukua toka huko dhahabu, talanta mia nne na ishirini, wakamletea mfalme Sulemani.

1 Wafalme 9:1-28 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

Sulemani alipomaliza kujenga Hekalu la BWANA na jumba la kifalme, na alipokwisha kufanya yote aliyotaka kufanya, BWANA akamtokea mara ya pili, vile alivyomtokea huko Gibeoni. BWANA akamwambia: “Nimesikia dua na maombi uliyofanya mbele zangu, nimeliweka wakfu Hekalu hili ambalo umelijenga, kwa kuweka Jina langu humo milele. Macho yangu na moyo wangu utakuwa humo siku zote. “Kwako wewe, kama ukienenda kwa unyofu wa moyo na uadilifu, kama baba yako Daudi alivyofanya na kutenda yote ninayoyaagiza kwa kutunza maagizo yangu na sheria, nitakiimarisha kiti chako cha utawala juu ya Israeli milele kama nilivyomwahidi Daudi baba yako niliposema, ‘Hutakosa kamwe kuwa na mtu kwenye kiti cha utawala cha Israeli.’ “Lakini ninyi au wana wenu mkinigeukia mbali na kuziacha amri na maagizo yangu niliyowapa na kwenda kuitumikia miungu mingine na kuiabudu, basi nitakatilia mbali Israeli kutoka nchi niliyowapa, nami nitalikataa Hekalu hili nililolitakasa kwa ajili ya Jina langu. Ndipo Israeli itakuwa kitu cha kudharauliwa na watu na kuwa kitu cha kudhihakiwa miongoni mwa watu wote. Ingawa hekalu hili linavutia sasa, wote watakaolipita watashangaa na kudhihaki wakisema, ‘Kwa nini BWANA amefanya kitu kama hiki katika nchi hii na kwa Hekalu hili?’ Watu watajibu, ‘Kwa sababu wamemwacha BWANA Mungu wao, aliyewatoa baba zao Misri, nao wamekumbatia miungu mingine, wakaiabudu na kuitumikia, ndiyo sababu BWANA ameyaleta maafa haya yote juu yao.’ ” Miaka ishirini ilipopita, muda ambao Sulemani alijenga majengo haya mawili, yaani Hekalu la BWANA na jumba la kifalme, Mfalme Sulemani akampa Hiramu mfalme wa Tiro miji ishirini katika Galilaya, kwa sababu Hiramu alikuwa amempatia mierezi na misunobari yote na dhahabu yote kama alivyohitaji. Lakini Hiramu alipotoka Tiro kwenda kuiona ile miji ambayo Sulemani alikuwa amempa, hakupendezwa nayo. Hiramu akauliza, “Hii ni miji ya namna gani uliyonipa, ndugu yangu?” Naye akaiita nchi ya Kabul, jina lililoko hadi leo. Basi Hiramu alikuwa amempelekea mfalme talanta mia moja na ishirini za dhahabu. Haya ni maelezo kuhusu kazi za kulazimishwa ambazo Mfalme Sulemani aliwafanyiza watu ili kulijenga Hekalu la BWANA, na jumba lake la kifalme, na Milo, ukuta wa Yerusalemu, Hazori, Megido na Gezeri. (Farao mfalme wa Misri alikuwa ameushambulia na kuuteka mji wa Gezeri. Alikuwa ameuchoma moto. Akawaua Wakanaani waliokuwa wakikaa humo na kisha kuutoa kwa binti yake, yaani mkewe Sulemani, kama zawadi ya arusi. Sulemani akaujenga tena Gezeri.) Akajenga Beth-Horoni ya Chini, akajenga Baalathi na Tamari kwenye jangwa katika eneo la nchi yake. Vilevile, alijenga miji ya ghala na ya magari yake ya vita na kwa ajili ya farasi wake na wapanda farasi: alijenga kila alichotaka katika Yerusalemu, katika Lebanoni, na katika eneo lote alilotawala. Watu wote waliosalia miongoni mwa Waamori, Wahiti, Waperizi, Wahivi, na Wayebusi (watu wasiokuwa Waisraeli), yaani, wazao wao waliobakia katika nchi, ambao Waisraeli hawakuwaangamiza kabisa, Sulemani akawalazimisha kuwa shokoa, kama ilivyo hadi leo. Lakini Sulemani hakumfanya Mwisraeli yeyote kuwa mtumwa; hao ndio walikuwa wapiganaji wake, viongozi wa serikali yake, maafisa wake, wakuu wake wa jeshi, majemadari wa magari yake ya vita, na wapanda farasi wake. Pia walikuwa maafisa wakuu wasimamizi wa miradi ya Sulemani: maafisa mia tano na hamsini waliwasimamia watu waliofanya kazi. Baada ya binti Farao kuja kutoka Mji wa Daudi na kuingia jumba la kifalme ambalo Sulemani alikuwa amemjengea, Sulemani akajenga Milo. Sulemani akatoa dhabihu za kuteketezwa na sadaka za amani mara tatu kwa mwaka juu ya madhabahu aliyokuwa amemjengea BWANA. Pamoja na hizo dhabihu, akafukiza uvumba mbele za BWANA, hivyo kutimiza kanuni za Hekalu. Mfalme Sulemani pia akatengeneza meli huko Esion-Geberi, iliyo karibu na Elathi katika Edomu, kwenye ukingo wa Bahari ya Shamu. Naye Hiramu akawatuma watu wake; mabaharia walioijua bahari, kuhudumu katika hizo meli pamoja na watu wa Sulemani. Wakasafiri kwa bahari hadi Ofiri na kurudi na talanta mia nne na ishirini (420) za dhahabu, ambazo walimkabidhi Mfalme Sulemani.