Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Wafalme 7:13-51

1 Wafalme 7:13-51 Biblia Habari Njema (BHN)

Kisha mfalme Solomoni alimwita Hiramu kutoka Tiro. Huyo, alikuwa mwana wa mjane wa kabila la Naftali, na baba yake alikuwa mkazi wa Tiro, mfua shaba. Hiramu alikuwa na hekima nyingi na akili, na fundi stadi wa kazi yoyote ya shaba. Basi, alikuja kwa mfalme Solomoni, akamfanyia kazi yake yote. Hiramu alitengeneza nguzo mbili za shaba, kila moja ikiwa na urefu wa mita 54, na mzingo wa mita 5.5. Ndani zilikuwa na tundu ambalo unene wa pande zake ulikuwa sentimita 2. Akatengeneza pia taji mbili za shaba, kila moja ikiwa na kimo cha mita 2.25; akaziweka juu ya nguzo hizo. Halafu, alifuma nyavu mbili zenye mapambo ya mrabamraba, akatengeneza na taji kwa kusokota mkufu: Vyote hivyo kwa ajili ya kupamba taji za shaba zilizowekwa juu ya zile nguzo. Hali kadhalika, alitengeneza matunda aina ya makomamanga, akayapanga safu mbili kuzunguka zile taji juu ya kila nguzo. Na taji hizo zilizokuwa juu ya nguzo mbele ya sebule, zilipambwa kwa mifano ya maua ya yungiyungi, kimo chake mita 1.75. Taji hizo zilikuwa juu ya hizo nguzo mbili, na pia zilikuwa juu ya sehemu ya mviringo iliyojitokeza karibu na zile nyavu. Palikuwa na mifano 400 ya matunda ya mkomamanga, imepangwa safu mbili kuzunguka kila taji. Hiramu aliziweka nguzo hizo kwenye sebule ya hekalu; nguzo aliyoisimika upande wa kusini iliitwa Yakini, na ile aliyoisimika upande wa kaskazini iliitwa Boazi. Vichwa vya nguzo hizo vilipambwa kwa mfano wa maua ya yungiyungi. Na hivyo kazi ya kutengeneza nguzo ikamalizika. Hiramu alitengeneza Birika liitwalo Bahari. Lilikuwa la mviringo lenye upana wa mita 4.5 kutoka ukingo hadi ukingo, na urefu wa mita 2.25 na mzingo wa mita 13.5. Chini ya ukingo wake, kulizunguka tangi hilo, kulikuwa na safu mbili za vibuyu, kila kimoja mita 13.5. Vibuyu hivyo vilikuwa vimetengenezwa wakati huohuo tangi hilo lilipofanywa. Nalo tangi lilikuwa limewekwa juu ya sanamu za mafahali kumi na wawili; tatu zikielekea upande wa kaskazini, tatu zikielekea magharibi, tatu kusini, na nyingine tatu mashariki. Tangi liliwekwa juu ya mafahali hao, sehemu zao za nyuma zikiwa ndani. Unene wa ukingo wake ulikuwa sentimita 7.5; nao ulikuwa ukifanana na ukingo wa kikombe na kama ua la yungiyungi. Tangi liliweza kujaa maji kiasi cha lita 40,000. Hiramu pia alitengeneza magari kumi ya shaba, kila gari likiwa na urefu wa mita 1.75, upana wa mita 1.75, na kimo cha mita 1.25. Magari hayo yalikuwa yameundwa hivi: Kulikuwa na mabamba ya chuma ambayo yalikuwa yameshikiliwa na mitalimbo. Juu ya mabamba hayo yaliyoshikiliwa na mitalimbo, kulikuwa na sanamu za simba, mafahali na viumbe wenye mabawa. Sanamu hizo za simba na mafahali, zilikuwa zimefunikwa na kutandikwa mapambo yaliyosokotwa vizuri. Isitoshe, kila gari lilikuwa na magurudumu manne ya shaba, na vyuma vya katikati vya kuyazungukia magurudumu hayo, vilikuwa vya shaba. Kwenye pembe nne za gari kulikuwa na vishikizo vya shaba kwa ajili ya birika kubwa. Karibu ya kila kishikio kuliwekwa mapambo ya maua ya kusokotwa. Mlango wa gari ulikuwa katika sehemu iliyotokeza juu kwa kiasi cha nusu mita. Kwa nje, mlango ulikuwa umetiwa michoro; na mabamba yake yalikuwa ya mraba, si ya mviringo. Na hayo magurudumu manne yalikuwa chini ya yale mabamba; vyuma vya katikati kuzunguka magurudumu hayo vilikuwa vimeunganishwa na mfumo wa gari lenyewe; na kimo cha magurudumu hayo kilikuwa sentimita 66. Hayo magurudumu yalikuwa kama magurudumu ya magari ya kukokotwa; na vyuma vyake vya katikati, duara zake, mataruma yake na vikombe vyake: Hivyo vyote vilikuwa vya kusubu. Chini ya kila gari kulikuwa na mihimili minne kwenye pembe zake, nayo ilishikamanishwa na gari. Na juu ya kila gari palikuwa na utepe uliofanyiza duara ya kimo cha sentimita 22; na vishikio na mabamba yaliyokuwa upande wa juu yalishikamana na gari lenyewe. Kwenye nafasi wazi iliyopatikana katika vishikio na mabamba ya kila gari, Hiramu alichonga michoro ya viumbe wenye mabawa, simba na miti ya mitende, akazungushia na mashada ya mapambo. Mifano hiyo yote kumi ya magari ilifanana, ikiwa na kimo kimoja na muundo uleule. Hiramu, pia alitengeneza mabirika kumi ya shaba, moja kwa kila gari. Kila birika ilikuwa na upana wa mita 1.75, na iliweza kuchukua maji kadiri ya lita 880. Akaweka magari matano upande wa kusini wa nyumba, na matano upande wa kaskazini; na lile tangi akaliweka kwenye pembe ya kusini-mashariki ya nyumba. Hiramu alitengeneza pia vyungu, sepetu na mabirika. Basi, Hiramu akamaliza kazi aliyoamriwa na mfalme Solomoni kuhusu nyumba ya Mwenyezi-Mungu: Nguzo mbili, mabakuli mawili ya taji zilizowekwa juu ya nguzo, na nyavu mbili kwa ajili ya kufunika hizo taji mbili, mifano ya makomamanga 400 kwa ajili ya nyavu hizo mbili, safu mbili za makomamanga kwa kila wavu ili kupamba zile taji mbili zilizokuwa juu ya nguzo. Hali kadhalika, alitengeneza magari kumi, na vishikio kumi katika magari hayo; na tangi lile moja na sanamu za mafahali kumi na wawili, chini ya hilo tangi. Halafu vile vyungu, sepetu na mabirika, vyombo hivyo vyote vilivyokuwa katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu ambavyo Hiramu alimtengenezea mfalme Solomoni, vilikuwa vya shaba iliyongarishwa. Vitu hivyo vyote mfalme alivitengeneza katika uwanda wa Yordani, sehemu ya udongo wa mfinyanzi iliyokuwa kati ya Sukothi na Sarethani. Solomoni hakupima uzani wa vifaa hivi vyote kwa kuwa vilikuwa vingi sana, na kwa sababu uzani wa shaba haukujulikana. Solomoni alitengeneza vifaa vyote vilivyokuwa katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu: Madhabahu ya dhahabu, meza ya dhahabu kwa ajili ya mikate ya kuwekwa mbele ya Mungu, vinara vya taa vya dhahabu safi vilivyowekwa mbele ya mahali patakatifu sana, vitano upande wa kusini na vitano upande wa kaskazini; maua, taa, koleo, vyote vikiwa vya dhahabu; vikombe, makasi ya kukatia tambi za mishumaa, mabakuli, vyetezo vya kuwekea ubani, miiko ya kuchukulia moto, vyote vya dhahabu safi; bawaba za milango ya sehemu ya ndani kabisa ya nyumba – pale mahali patakatifu sana – na bawaba za milango ya ukumbi wa ibada wa hekalu bawaba zote za dhahabu. Basi, mfalme Solomoni akamaliza kazi zote zilizohusu nyumba ya Mwenyezi-Mungu. Kisha Solomoni akaleta mali yote ambayo baba yake Daudi, alikuwa ameiweka wakfu, yaani: Fedha, dhahabu na vyombo; akaiweka katika hazina za nyumba ya Mwenyezi-Mungu.

1 Wafalme 7:13-51 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Mfalme Sulemani akatuma watu kumleta Hiramu kutoka Tiro. Naye alikuwa mwana wa mwanamke mjane wa kabila la Naftali, na babaye alikuwa mtu wa Tiro, mfua shaba; naye alikuwa mwingi wa hekima na akili, stadi wa kufanya kazi zote za shaba. Akamfikia mfalme Sulemani, akamfanyia kazi yake yote. Kwa maana alizifanyiza zile nguzo mbili za shaba, mikono kumi na minane kwenda juu kwake kila moja; na uzi wa mikono kumi na miwili kuizunguka nguzo hii au hii. Akatengeneza mataji mawili ya shaba iliyoyeyushwa ya kuwekwa juu ya vichwa vya nguzo; kwenda juu kwake taji moja mikono mitano, na mikono mitano kwenda juu kwake taji la pili. Kulikuwa na nyavu kama kazi ya kusuka, na masongo ya mikufu, kwa mataji yaliyokuwako juu ya vichwa vya nguzo; saba kwa taji moja, na saba kwa taji la pili. Hivyo akazitengeneza nguzo; na kulikuwa na safu mbili za kuzunguka juu ya wavu mmoja, zifunike mataji yaliyokuwako juu ya vichwa vya nguzo; akafanya vivyo hivyo kwa taji la pili. Na mataji yaliyokuwa juu ya nguzo ukumbini yalikuwa ya kazi ya mayungi, mikono minne. Kulikuwako tena taji juu ya nguzo mbili, karibu na uvimbe uliokuwako kando ya wavu; na makomamanga yalikuwa mia mbili, safu safu pande zote juu ya taji la pili. Akazisimamisha nguzo ukumbini pa hekalu; akaisimamisha nguzo ya kulia, akaiita jina lake Yakini; akaisimamisha nguzo ya kushoto, akaiita jina lake Boazi. Na juu ya nguzo kulikuwa na kazi ya mayungi; hivyo mambo ya nguzo yakatimia. Tena akatengeneza bahari ya kusubu, mikono kumi toka ukingo hata ukingo, ikaviringana, na mikono mitano ilikuwa kwenda juu kwake; na uzi wa mikono thelathini kuizunguka kabisa. Na chini ya ukingo wake kulikuwa na maboga yaliyoizunguka, kwa mikono kumi, yakiizunguka bahari; kulikuwa na safu mbili za hayo maboga, yakafanywa katika kalibu hapo bahari ilipofanywa. Ikakaa juu ya ng'ombe kumi na wawili, watatu wakitazama kaskazini, na watatu wakitazama magharibi, na watatu wakitazama kusini, na watatu wakitazama mashariki; na bahari iliwekwa juu yao, na pande zao za nyuma zote zilikuwa ndani. Na unene wake ulikuwa nyanda nne; na ukingo wake ukafanywa kama ukingo wa kikombe, kama ua la yungi; huingia bathi elfu mbili. Akavifanya vile vitako kumi vya shaba; mikono minne urefu wa kitako kimoja, na mikono minne upana wake, na mikono mitatu kwenda juu kwake. Na kazi ya vitako ndiyo hii; vilikuwa na papi; na papi zilikuwa katikati ya vipandio; na juu ya papi zilizokuwa katikati ya vipandio kulikuwa na simba, na ng'ombe, na makerubi; na juu ya vipandio kulikuwa na kitako; na chini ya simba na ng'ombe kulikuwa na masongo ya kazi ya kupembeza. Kila kitako kilikuwa na magurudumu manne ya shaba, na vipini vya shaba; na miguu yake minne ilikuwa na mataruma; chini ya birika yalikuwako mataruma ya kusubu, yenye masongo kila moja mbavuni. Na kinywa chake ndani ya taji na juu yake kilikuwa mkono mmoja; na kinywa chake kikaviringana kama kazi ya vitako, mkono mmoja na nusu; tena juu ya kinywa chake kulikuwa na nakshi, na papi zao zilikuwa za mraba, wala hazikuviringana. Na magurudumu manne yalikuwa chini ya papi; na mikono ya magurudumu ndani ya vitako; na kwenda juu kwake gurudumu moja mkono mmoja na nusu. Na kazi ya magurudumu ilikuwa kama kazi ya gurudumu la gari; mikono yake, na maduara, na matindi, na vipande vya ndani, vyote vilikuwa vya kusubu. Kulikuwa na mataruma manne katika pembe nne za kitako kimoja; mataruma hayo ni kitu kimoja na kitako chenyewe. Na juu ya kitako kulikuwa na duara nusu mkono kwenda juu kwake; na juu ya kitako mashikio yake na papi zake vilikuwa vya namna iyo hiyo. Akachora juu ya mabamba ya mashikio yake, na juu ya papi zake, makerubi, na simba, na mitende, moja moja kama ilivyokuwa nafasi, na masongo pande zote. Hivyo akavifanya vile vitako kumi; vyote vilikuwa vya kalibu moja, na cheo kimoja, na namna moja. Akafanya birika kumi za shaba; birika moja huingia bathi arubaini; na kila birika ilikuwa mikono minne; birika moja juu ya kitako kimoja, katika vile vitako kumi. Akaviweka vile vitako, vitano upande wa kulia wa nyumba, na vitano upande wa kushoto wa nyumba; akaiweka ile bahari upande wa kulia wa nyumba upande wa mashariki, kuelekea kusini. Tena Huramu akazifanya birika, na majembe, na mabakuli. Hivyo Huramu akazimaliza kazi zote alizomfanyia mfalme Sulemani katika nyumba ya BWANA; zile nguzo mbili, na mabakuli mawili ya mataji yalikuwa juu ya nguzo; na nyavu mbili za kuvifunika hivyo viumbe viwili vya mataji yaliyokuwa juu ya nguzo; na makomamanga mia nne ya zile nyavu mbili; safu mbili za makomamanga kwa kila wavu, kuyafunika nayo mabakuli mawili ya mataji yaliyokuwa juu ya nguzo; na vile vitako kumi, na birika kumi juu ya vitako; na ile bahari moja, na ng'ombe kumi na wawili chini ya ile bahari; na masufuria, na majembe, na mabeseni; hata vyombo hivyo vyote, Huramu alivyomfanyia mfalme Sulemani, katika nyumba ya BWANA, vyote vilikuwa vya shaba iliyosuguliwa. Katika uwanda wa Yordani ndipo mfalme alipovisubu, katika udongo mzito kati ya Sukothi na Sarethani. Sulemani akaviacha vyombo vyote visipimwe kwa kuwa vilikuwa vingi mno; wala uzito wa shaba haukujulikana. Sulemani akavitengeneza vyombo vyote vilivyokuwamo nyumbani mwa BWANA; madhabahu ya dhahabu, na ile meza iliyokuwa na mikate ya wonyesho juu yake ilikuwa ya dhahabu; na vinara vya taa, vitano upande wa kulia, na vitano upande wa kushoto, mbele ya chumba cha ndani, vya dhahabu safi; na maua, na taa, na koleo ya dhahabu; na vikombe, na makasi, na mabakuli, na miiko, na vyetezo, vya dhahabu safi; na bawaba za dhahabu, za milango ya nyumba ya ndani, yaani, patakatifu pa patakatifu, na za milango ya nyumba, ndiyo hekalu. Hivyo kazi yote aliyoifanya mfalme Sulemani katika nyumba ya BWANA ikamalizika. Sulemani akaviingiza vile vitu alivyovitakasa Daudi baba yake, yaani, fedha, na dhahabu, na vyombo; akavitia ndani ya hazina za nyumba ya BWANA.

1 Wafalme 7:13-51 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Mfalme Sulemani akatuma watu kumleta Huramu kutoka Tiro. Naye alikuwa mwana wa mwanamke mjane wa kabila ya Naftali, na babaye alikuwa mtu wa Tiro, mfua shaba; naye alikuwa mwingi wa hekima na akili, mstadi wa kufanya kazi zote za shaba. Akamfikilia mfalme Sulemani, akamfanyia kazi yake yote. Kwa maana alizifanyiza zile nguzo mbili za shaba, mikono kumi na minane kwenda juu kwake kila moja; na uzi wa mikono kumi na miwili kuizunguka nguzo hii au hii. Akafanya taji mbili za shaba iliyoyeyushwa za kuwekwa juu ya vichwa vya nguzo; kwenda juu kwake taji moja mikono mitano, na mikono mitano kwenda juu kwake taji ya pili. Kulikuwa na nyavu kama kazi ya kusuka, na masongo ya mikufu, kwa taji zilizokuwako juu ya vichwa vya nguzo; saba kwa taji moja, na saba kwa taji ya pili Hivyo akazifanya nguzo; na kulikuwa na safu mbili za kuzunguka juu ya wavu mmoja, zifunike taji zilizokuwako juu ya vichwa vya nguzo; akafanya vivyo hivyo kwa taji ya pili. Na taji zilizokuwa juu ya nguzo ukumbini zilikuwa za kazi ya mayungi, mikono minne. Kulikuwako tena taji juu ya nguzo mbili, karibu na uvimbe uliokuwako kando ya wavu; na makomamanga yalikuwa mia mbili, safu safu pande zote juu ya taji ya pili. Akazisimamisha nguzo ukumbini pa hekalu; akaisimamisha nguzo ya kuume, akaiita jina lake Yakini; akaisimamisha nguzo ya kushoto, akaiita jina lake Boazi. Na juu ya nguzo kulikuwa na kazi ya mayungi; hivyo mambo ya nguzo yakatimia. Tena akaifanya bahari ya kusubu, mikono kumi toka ukingo hata ukingo, ikaviringana, na mikono mitano ilikuwa kwenda juu kwake; na uzi wa mikono thelathini kuizunguka kabisa. Na chini ya ukingo wake kulikuwa na maboga yaliyoizunguka, kwa mikono kumi, yakiizunguka bahari; kulikuwa na safu mbili za hayo maboga, yakafanywa kalibuni hapo bahari ilipofanywa. Ikakaa juu ya ng’ombe kumi na wawili, watatu wakitazama kaskazini, na watatu wakitazama magharibi, na watatu wakitazama kusini, na watatu wakitazama mashariki; na bahari iliwekwa juu yao, na pande zao za nyuma zote zilikuwa ndani. Na unene wake ulikuwa nyanda nne; na ukingo wake ukafanywa kama ukingo wa kikombe, kama ua la yungi; huingia bathi elfu mbili. Akayafanya yale matako kumi ya shaba; mikono minne urefu wa tako moja, na mikono minne upana wake, na mikono mitatu kwenda juu kwake. Na kazi ya matako ndiyo hii; yalikuwa na papi; na papi zilikuwa katikati ya vipandio; na juu ya papi zilizokuwa katikati ya vipandio kulikuwa na simba, na ng’ombe, na makerubi; na juu ya vipandio kulikuwa na tako; na chini ya simba na ng’ombe kulikuwa na masongo ya kazi ya kupembeza. Kila tako lilikuwa na magurudumu manne ya shaba, na vipini vya shaba; na miguu yake minne ilikuwa na mataruma; chini ya birika yalikuwako mataruma ya kusubu, yenye masongo kila moja mbavuni. Na kinywa chake ndani ya taji na juu yake kilikuwa mkono mmoja; na kinywa chake kikaviringana kama kazi ya tako, mkono mmoja na nusu; tena juu ya kinywa chake kulikuwa na nakshi, na papi zao zilikuwa za mraba, wala hazikuviringana. Na magurudumu manne yalikuwa chini ya papi; na mikono ya magurudumu ndani ya tako; na kwenda juu kwake gurudumu moja mkono mmoja na nusu. Na kazi ya magurudumu ilikuwa kama kazi ya gurudumu la gari; mikono yake, na maduara, na matindi, na vipande vya ndani, vyote vilikuwa vya kusubu. Kulikuwa na mataruma manne katika pembe nne za tako moja; mataruma hayo ni kitu kimoja na tako lenyewe. Na juu ya tako kulikuwa na duara nusu mkono kwenda juu kwake; na juu ya tako mashikio yake na papi zake vilikuwa vya namna iyo hiyo. Akachora juu ya mabamba ya mashikio yake, na juu ya papi zake, makerubi, na simba, na mitende, moja moja kama ilivyokuwa nafasi, na masongo pande zote. Hivyo akayafanya yale matako kumi; yote yalikuwa ya kalibu moja, na cheo kimoja, na namna moja. Akafanya birika kumi za shaba; birika moja huingia bathi arobaini; na kila birika ilikuwa mikono minne; birika moja juu ya tako moja, katika yale matako kumi. Akayaweka yale matako, matano upande wa kuume wa nyumba, na matano upande wa kushoto wa nyumba; akaiweka ile bahari upande wa kuume wa nyumba upande wa mashariki, kuelekea kusini. Tena Huramu akazifanya birika, na majembe, na mabakuli. Hivyo Huramu akazimaliza kazi zote alizomfanyia mfalme Sulemani katika nyumba ya BWANA; zile nguzo mbili, na vimbe mbili za taji zilikuwa juu ya nguzo; na nyavu mbili za kuzifunika hizo vimbe mbili za taji zilizokuwa juu ya nguzo; na makomamanga mia nne ya zile nyavu mbili; safu mbili za makomamanga kwa kila wavu, kuzifunika hizo vimbe mbili za taji zilizokuwa juu ya nguzo; na yale matako kumi, na birika kumi juu ya matako; na ile bahari moja, na ng’ombe kumi na wawili chini ya ile bahari; na masufuria, na majembe, na mabakuli; hata vyombo hivyo vyote, Huramu alivyomfanyia mfalme Sulemani, katika nyumba ya BWANA, vyote vilikuwa vya shaba iliyosuguliwa. Katika uwanda wa Yordani ndipo mfalme alipovisubu, katika udongo mzito kati ya Sukothi na Sarethani. Sulemani akaviacha vyombo vyote visipimwe kwa kuwa vilikuwa vingi mno; wala uzito wa shaba haukujulikana. Sulemani akavifanya vyombo vyote vilivyokuwamo nyumbani mwa BWANA; madhabahu ya dhahabu, na ile meza iliyokuwa na mikate ya wonyesho juu yake ilikuwa ya dhahabu; na vinara vya taa, vitano upande wa kuume, na vitano upande wa kushoto, mbele ya chumba cha ndani, vya dhahabu safi; na maua, na taa, na koleo ya dhahabu; na vikombe, na makasi, na mabakuli, na miiko, na vyetezo, vya dhahabu safi; na bawaba za dhahabu, za milango ya nyumba ya ndani, yaani, patakatifu pa patakatifu, na za milango ya nyumba, ndiyo hekalu. Hivyo ikamalizika kazi yote Sulemani mfalme aliyoifanya katika nyumba ya BWANA. Sulemani akaviingiza vile vitu alivyovitakasa Daudi baba yake, yaani, fedha, na dhahabu, na vyombo; akavitia ndani ya hazina za nyumba ya BWANA.

1 Wafalme 7:13-51 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

Mfalme Sulemani akatuma watu Tiro kumleta Hiramu, ambaye mama yake alikuwa mjane kutoka kabila la Naftali na baba yake alikuwa mtu wa Tiro tena fundi wa shaba. Hiramu alikuwa na ustadi wa hali ya juu na mzoefu katika aina zote za kazi ya shaba. Alikuja kwa Mfalme Sulemani na kufanya kazi zake zote alizopangiwa. Hiramu akasubu nguzo mbili za shaba, kila moja ikiwa na urefu wa dhiraa kumi na nane, na mzingo wa dhiraa kumi na mbili kwa mstari. Pia alitengeneza mataji mawili ya shaba ya kusubu ili kuyaweka juu ya hizo nguzo; kila taji lilikuwa na kimo cha dhiraa tano kwenda juu. Wavu wa mikufu iliyosokotewa kwenye zile taji juu ya zile nguzo, saba kwa kila taji. Akatengeneza makomamanga katika safu mbili kuzunguka kila wavu kuremba mataji yaliyo juu ya nguzo. Alifanya hivyo kwa kila nguzo. Mataji yaliyokuwa juu ya nguzo kwenye baraza, yalikuwa katika umbo la yungiyungi, kimo chake ni dhiraa nne. Juu ya mataji ya zile nguzo mbili, juu ya ile sehemu yenye umbo kama bakuli, karibu na ule wavu, kulikuwa na yale makomamanga mia mbili katika safu kuzunguka pande zote. Hiramu akazisimamisha zile nguzo barazani pa Hekalu. Nguzo iliyokuwa upande wa kusini akaiita Yakini, na ile ya upande wa kaskazini akaiita Boazi. Mataji yaliyokuwa juu yalikuwa na umbo la yungiyungi. Hivyo kazi ya nguzo ikakamilika. Hiramu akasubu Bahari ya chuma, yenye umbo la mviringo, ya dhiraa kumi kutoka ukingo hadi ukingo, na kimo cha dhiraa tano. Mzunguko wake ulikuwa dhiraa thelathini. Chini ya ukingo, ilizungukwa na mapambo ya maboga kumi kwa kila dhiraa. Maboga hayo yalikuwa yamesubiwa katika safu mbili ili kuwa kitu kimoja na hiyo Bahari. Ile Bahari iliwekwa juu ya mafahali kumi na wawili, watatu wakielekea kaskazini, watatu wakielekea magharibi, watatu wakielekea kusini, na watatu wakielekea mashariki. Hiyo Bahari iliwekwa juu yao, na sehemu zao za nyuma zilielekeana. Bahari hiyo ilikuwa na unene wa nyanda moja, na ukingo wake ulifanana na ukingo wa kikombe, kama ua la yungiyungi lililochanua; nayo ingejazwa na bathi elfu mbili. Pia akatengeneza vitako kumi vya shaba vinavyoweza kuhamishika, kila kimoja kilikuwa na urefu wa dhiraa nne, upana dhiraa nne na kimo chake dhiraa tatu. Hivi ndivyo vile vitako vilivyotengenezwa: Vilikuwa na mbao za pembeni zilizounganishwa na mihimili. Juu ya mbao kati ya hiyo mihimili kulikuwa na simba, mafahali na makerubi, pia kwenye mihimili yake. Juu na chini ya simba na mafahali kulikuwa na shada za maua yaliyofuliwa. Kila kitako kilikuwa na magurudumu manne ya shaba, na vyuma vya kuyazungusha. Kila kitako kilikuwa na sinia iliyowekwa juu ya vishikizo vinne viliyosubiwa shada za maua kila upande. Ndani ya kitako kulikuwa na nafasi ya wazi iliyokuwa na umbile la mviringo lenye kina cha dhiraa moja. Nafasi hii ya wazi ilikuwa ya mviringo, pamoja na kitako chake ilikuwa dhiraa moja na nusu. Kuzunguka huo mdomo wake kulitiwa nakshi. Papi za vitako zilikuwa mraba na si za mviringo. Yale magurudumu manne yalikuwa chini ya papi, na vyuma vya kuyazungushia viliunganishwa kwenye kitako. Kipenyo cha kila gurudumu kilikuwa dhiraa moja na nusu. Magurudumu hayo yalitengenezwa kama ya magari ya kukokotwa na farasi; vyuma vya kuzungushia magurudumu, duara zake, matindi yake na vitovu vyake, vyote vilikuwa vya kusubu. Kila kitako kilikuwa na mikono minne, moja kwenye kila pembe, ukichomoza kutoka kile kitako. Juu ya kitako kulikuwa na utepe wa mviringo wenye kina cha nusu dhiraa. Vishikio na papi vilishikamana upande wa juu wa kitako. Aliweka nakshi za makerubi, simba na mitende juu ya vishikio na juu ya papi, katika kila nafasi, na shada za maua kuzunguka. Hivi ndivyo Hiramu alivyotengeneza vile vitako kumi. Vyote vilisubiwa kwenye kalibu moja na vilifanana kwa vipimo na kwa umbo. Kisha akatengeneza masinia kumi ya shaba, kila moja likiwa na ujazo wa bathi arobaini, yakiwa na kipenyo cha dhiraa nne kila sinia moja kwa kila kimoja cha vile vitako kumi. Aliweka vitako vitano upande wa kusini wa Hekalu na vingine vitano upande wa kaskazini. Akaweka ile Bahari upande wa kusini, katika pembe ya kusini-mashariki ya Hekalu. Pia akatengeneza masinia, masepetu na mabakuli ya kunyunyizia. Kwa hiyo Huramu akakamilisha kazi zote katika Hekalu la BWANA kama vile Mfalme Sulemani alikuwa amemwagiza: nguzo mbili; mataji mawili yenye umbo la bakuli juu ya hizo nguzo; nyavu mbili za kupamba hayo mataji mawili yenye umbo la bakuli juu ya hizo nguzo; makomamanga mia nne kwa ajili ya hizo nyavu mbili (safu mbili za makomamanga kwa kila wavu, yakipamba hayo mataji mawili yenye umbo la bakuli juu ya hizo nguzo); vitako kumi pamoja na masinia yake kumi; ile Bahari ya chuma na wale mafahali kumi na wawili chini yake; masufuria, masepetu na mabakuli ya kunyunyizia. Vyombo hivi vyote ambavyo Huramu alimtengenezea Mfalme Sulemani kwa ajili ya Hekalu la BWANA vilikuwa vya shaba iliyongʼarishwa. Mfalme akaamuru wavisubu katika kalibu ya udongo wa mfinyanzi katika uwanda wa Yordani ulio kati ya Sukothi na Sarethani. Sulemani hakupima vitu hivi vyote kwa sababu vilikuwa vingi sana; hivyo, uzani wa shaba haukukadiriwa. Sulemani pia akatengeneza samani zote zilizokuwa ndani ya Hekalu la BWANA: madhabahu ya dhahabu; meza ya dhahabu za kuweka mikate ya Wonesho; vinara vya taa vya dhahabu safi (vitano upande wa kuume na vitano upande wa kushoto, mbele ya mahali patakatifu); shada za maua, na taa, na makoleo, vyote vikiwa vya dhahabu; vyombo vya dhahabu safi: masinia, mikasi ya kusawazishia tambi, mabakuli ya kunyunyizia, vyano na vyetezo; na bawaba za dhahabu kwa ajili ya milango ya chumba cha ndani sana, yaani Patakatifu pa Patakatifu, na pia kwa ajili ya milango ya ukumbi mkuu wa Hekalu. Hivyo, Mfalme Sulemani alipomaliza kazi zote za Hekalu la BWANA, akaviingiza ndani vile vitu ambavyo Daudi baba yake alikuwa ameviweka wakfu: fedha, dhahabu na samani; kisha akaviweka katika hazina za Hekalu la BWANA.