1 Wafalme 6:1-38
1 Wafalme 6:1-38 Biblia Habari Njema (BHN)
Solomoni alianza kujenga nyumba ya Mwenyezi-Mungu katika mwaka wa 480 baada ya Waisraeli kutoka Misri. Huo ulikuwa mwaka wa nne wa utawala wa Solomoni juu ya Israeli, katika mwezi wa Zifu, yaani mwezi wa pili. Nyumba hiyo ambayo mfalme Solomoni alimjengea Mwenyezi-Mungu ilikuwa na urefu wa mita 27, upana wa mita 9, na kimo cha mita 13.5. Ukumbi wa sebule ya nyumba ulikuwa na upana wa mita 4.5 toka upande mmoja wa nyumba mpaka upande mwingine. Na kina chake mbele ya hiyo nyumba kilikuwa mita 9. Aliiwekea nyumba hiyo madirisha mapana kwa ndani na membamba kwa nje. Pia alijenga nguzo kuzunguka, ili kutegemeza ukuta wa nje; akatengeneza na vyumba vya pembeni kila upande. Vyumba vya chini, katika hivyo vyumba vya nyongeza, vilikuwa na upana wa mita 2.25, na ghorofa iliyofuata ilikuwa na upana wa mita 2.75, na ghorofa ya juu kabisa ilikuwa na upana wa mita 3. Ghorofa hizo zilikuwa zimetofautiana kwa upana, kwa sababu Solomoni alikuwa amepunguza kiasi ukuta wa nje kuzunguka nyumba, ili boriti za kutegemeza jengo zisishikamane na kuta. Wakati nyumba ilipokuwa inajengwa, hapakusikika ndani ya nyumba mlio wa nyundo, wala wa chombo chochote cha chuma, maana ilijengwa kwa mawe yaliyokuwa yamechongwa na kutayarishwa kabisa huko yalikochukuliwa. Mlango wa kuingilia sehemu ya chini ya jengo lililoongezwa ubavuni mwa nyumba, ulikuwa upande wa kusini. Ndani, mlikuwa na ngazi ambayo watu waliweza kupanda ili kwenda ghorofa ya katikati na ya mwisho. Hivyo, Solomoni aliijenga nyumba, ikamalizika. Dari ya nyumba alikuwa ameitengeneza kwa boriti na mbao za mierezi. Kuuzunguka ukuta wa nje wa nyumba hiyo, alijenga vyumba vya ghorofa vyenye kimo cha mita 2.25; navyo vilikuwa vimeunganishwa na nyumba kwa boriti za mierezi. Wakati huo, ujumbe huu wa Mwenyezi-Mungu ukamjia Solomoni, “Kuhusu nyumba hii unayoijenga, kama ukifuata maongozi yangu, ukayatii maagizo yangu na amri zangu, nitakutimizia mambo yote niliyomwahidi baba yako Daudi. Mimi nitakaa miongoni mwa wazawa wa Israeli, na sitawaacha kamwe watu wangu, Israeli.” Hivyo, Solomoni akaijenga nyumba na kuimaliza. Upande wa ndani wa kuta za nyumba aliufunika kwa mbao za mierezi, kutoka sakafuni mpaka kwenye boriti za dari; na sakafu akaitandika mbao za miberoshi. Chumba cha ndani, kilichoitwa mahali patakatifu sana, kilijengwa katika sehemu ya nyuma ya nyumba. Kilikuwa kimejengwa kwa mbao za mierezi kutoka sakafuni hadi darini, na urefu wake ulikuwa mita 9. Nyumba ile iliyokuwa mbele ya mahali patakatifu sana, ilikuwa na urefu wa mita 18. Mbao za mierezi zilizotanda ukuta wa nyumba kwa ndani zilikuwa zimepambwa kwa michoro ya mibuyu na maua yaliyochanua. Kila sehemu ilikuwa imefunikwa kwa mbao za mierezi, wala hapana jiwe lililoonekana. Katika sehemu ya ndani kabisa ya jengo hilo, Solomoni alitayarisha chumba cha pekee ambamo sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu liliwekwa. Chumba hicho kilikuwa na urefu wa mita 9, upana wa mita 9, na kimo cha mita 9; nacho kilipambwa kwa dhahabu safi. Pia, alitengeneza madhabahu kwa mbao za mierezi. Solomoni aliipamba kwa dhahabu safi sehemu ya ndani ya nyumba, na mbele ya hicho chumba cha ndani akaweka minyororo ya dhahabu kutoka upande mmoja mpaka upande wa pili, aliipamba kwa dhahabu. Nyumba yote aliipamba kwa dhahabu, na madhabahu iliyokuwa katika chumba cha ndani kabisa. Alitengeneza kwa mbao za mizeituni sanamu za viumbe wawili wenye mabawa, kila sanamu ikiwa na kimo cha mita 4.5, akaziweka katika chumba cha ndani kabisa. Kila bawa lilikuwa na urefu wa mita 2.5; kwa hiyo urefu kutoka ncha ya bawa moja mpaka ncha ya bawa lingine ulikuwa mita 4.5. Kiumbe mwingine alikuwa na urefu wa mita 4.5; viumbe wote wawili walikuwa na vipimo vilevile na umbo lilelile. Urefu wa kiumbe mmoja ulikuwa mita 4.5; pia urefu wa kiumbe mwingine ulikuwa uleule. Sanamu hizo zilikuwa sambamba, zikiwa na mabawa yaliyokunjuliwa: Bawa la mmoja likigusa ukuta mmoja, na bawa la mwingine likigusa ukuta wa pili, huku yale mengine yaligusana katikati ya chumba. Nazo sanamu hizo alizipamba kwa dhahabu. Kuta za kila chumba alizipamba kwa kuchongwa michoro ya viumbe wenye mabawa, mitende na michoro ya maua yaliyochanua. Aliipaka dhahabu sakafu ya vyumba vya ndani na vya nje. Kwa kuingia chumba cha ndani kabisa alitengeneza milango kwa mbao za mizeituni. Vizingiti na miimo ya milango vilifanya umbo la pembe tano. Katika milango hiyo miwili ya mizeituni, alichora viumbe wenye mabawa, mitende na maua yaliyochanua; akaipamba michoro hiyo kwa dhahabu. Hali kadhalika, alitengeneza mlango wa mraba wa kuingia sebuleni. Miimo ya mlango huo ilikuwa ya mizeituni, na mabamba yake mawili yalikuwa ya miberoshi; kila bamba liliweza kukunjwa mara moja. Juu ya mabamba hayo ya mlango, kulichorwa viumbe wenye mabawa, mitende na maua yaliyochanua; akaipamba vizuri michoro hiyo kwa dhahabu. Alijenga ukumbi wa ndani ambao kuta zake zilikuwa za tabaka tatu za mawe yaliyochongwa, na tabaka moja la boriti za mwerezi. Msingi wa nyumba ya Mwenyezi-Mungu ulijengwa mnamo mwezi wa Zifu katika mwaka wa nne. Na katika mwezi wa Buli, yaani mwezi wa nane, katika mwaka wa kumi na mmoja, ujenzi wa nyumba ulimalizika, na kazi ilikuwa imekamilika kama ilivyopangwa. Ujenzi huo ulimchukua Solomoni miaka saba.
1 Wafalme 6:1-38 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ikawa katika mwaka wa mia nne na themanini baada ya wana wa Israeli kutoka nchini Misri, katika mwaka wa nne wa kutawala kwake Sulemani juu ya Israeli, katika mwezi wa Zivu, ndio mwezi wa pili, akaanza kuijenga nyumba ya BWANA. Nayo nyumba hiyo mfalme Sulemani aliyomjengea BWANA, urefu wake ulikuwa mikono sitini, na upana wake ishirini, na kwenda juu kwake mikono thelathini. Na ukumbi mbele ya hekalu la nyumba, urefu wake ulikuwa mikono ishirini, kadiri ya upana wa nyumba; na upana wake mikono kumi mbele ya nyumba. Akaifanyia nyumba madirisha ya miangaza yenye kimia. Nao ukuta wa nyumba akauzungushia vyumba, kushikamana na kuta za nyumba kotekote, za hekalu na za chumba cha ndani; akafanya vyumba vya mbavuni pande zote. Chumba cha chini kilikuwa mikono mitano upana wake, na chumba cha katikati kilikuwa mikono sita upana wake, na chumba cha tatu kilikuwa mikono saba upana wake; kwa kuwa upande wa nje akaupunguza ukuta wa nyumba pande zote, ili boriti zisishikamane kutani mwa nyumba. Na nyumba ilipokuwa ikijengwa, ikajengwa kwa mawe yaliyokwisha kuchongwa machimboni; wala nyundo, wala shoka, wala chombo cha chuma chochote, sauti yake haikusikiwa ilipokuwa ikijengwa nyumba. Mlango wa vyumba vya chini ulikuwapo upande wa kulia wa nyumba; mtu hupanda ngazi za kuzunguka mpaka vyumba vya katikati, na kutoka vile vya katikati mpaka vile vya tatu. Basi ndivyo alivyoijenga nyumba, akaimaliza; akaifunika nyumba kwa boriti na mbao za mwerezi. Akavijenga vyumba mbavuni mwa nyumba yote, kwenda juu kwake kila kimoja kilikuwa mikono mitano; vikaitegemea nyumba kwa boriti za mwerezi. Neno la BWANA likamjia Sulemani, kusema, Katika habari ya nyumba hii unayoijenga, kama ukienda katika sheria zangu, na kuzifanya hukumu zangu, na kuzishika amri zangu zote na kwenda katika hizo; ndipo nitakapolithibitisha neno langu kwako, nililomwambia Daudi baba yako. Nami nitakaa katikati ya wana wa Israeli, wala sitawaacha watu wangu Israeli. Basi Sulemani akaijenga hiyo nyumba akaimaliza. Akazijenga kuta za nyumba ndani kwa mbao za mwerezi; toka sakafu ya nyumba hata boriti za juu, akazifunika ndani kwa mti; akafunika sakafu ya nyumba kwa mbao za mberoshi. Akajenga mikono ishirini pande za nyuma za nyumba toka chini hata juu kwa mbao za mwerezi; naam, ndani akaijengea chumba cha ndani, yaani, patakatifu pa patakatifu. Nayo nyumba, ndiyo hekalu la mbele, ilikuwa mikono arubaini. Na ndani ya nyumba, mlikuwa na mwerezi ulionakishiwa maboga na maua yaliyofunuka wazi; mlikuwa na mwerezi mahali pote; wala mawe hayakuonekana. Akaweka tayari chumba cha ndani katikati ya nyumba ndani, ili atie humo sanduku la Agano la BWANA. Na ndani yake chumba hicho cha ndani mlikuwa na nafasi, mikono ishirini urefu, na mikono ishirini upana, na mikono ishirini kwenda juu kwake; akaifunika na dhahabu safi. Akaifunika madhabahu nayo kwa mwerezi. Hivyo Sulemani akaifunika nyumba ndani kwa dhahabu safi. Akaitenga kwa mikufu ya dhahabu mbele ya chumba cha ndani; akapafunika na dhahabu. Akaifunika nyumba yote kwa dhahabu, hata ilipokwisha nyumba yote; tena madhabahu yote iliyokuwa ya chumba cha ndani akaifunika kwa dhahabu. Akafanya ndani ya chumba cha ndani makerubi mawili ya mzeituni, kwenda juu mikono kumi. Na bawa moja la kerubi lilikuwa mikono mitano urefu wake, na bawa la pili la kerubi mikono mitano; mikono kumi toka mwisho wa bawa moja hata mwisho wa bawa la pili. Na kerubi la pili lilikuwa mikono kumi; makerubi yote mawili walikuwa ya cheo kimoja na namna moja. Kwenda juu kwake kerubi moja kulikuwa mikono kumi, na kerubi la pili vivyo hivyo. Akayaweka hayo makerubi katika nyumba ya ndani; na mabawa ya makerubi yakanyoshwa, bawa la moja likafika ukutani huko, na bawa la kerubi la pili likafika ukutani huko; mabawa yao yakagusana katikati ya nyumba. Akayafunika makerubi kwa dhahabu. Akazinakshi kuta zote za nyumba kwa nakshi za makerubi, na mitende, na maua yaliyofunuka wazi, pande za ndani na nje. Na sakafu ya nyumba akaifunika na dhahabu ndani na nje. Akayafanyia maingilio ya chumba cha ndani milango ya mzeituni; kizingiti na miimo ilikuwa ya pande tano. Hivyo akafanya milango miwili ya mzeituni; akanakshi juu yake nakshi za makerubi, na mitende, na maua yaliyofunuka wazi, akaifunika kwa dhahabu; akatia dhahabu juu ya makerubi, na juu ya mitende. Ndivyo alivyoyafanyia maingilio ya hekalu miimo ya mzeituni, yenye pande nne; na milango miwili ya mberoshi; mbao mbili za mlango mmoja zilikuwa za kukunjana, na mbao mbili za mlango wa pili za kukunjana. Akanakshi juu yake makerubi, na mitende, na maua yaliyofunuka wazi; akazifunika kwa dhahabu iliyonyoshwa juu ya machoro. Akaijengea behewa ya ndani safu tatu za mawe ya kuchongwa, na safu moja ya mihimili ya mierezi. Katika mwaka wa nne nyumba ya BWANA ilitiwa msingi, katika mwezi wa Zivu. Na katika mwaka wa kumi na mmoja, katika mwezi wa Buli, ndio mwezi wa nane, nyumba ikaisha, mambo yake yote, kulingana na kanuni zote. Basi muda wa miaka saba alikuwa katika kuijenga.
1 Wafalme 6:1-38 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ikawa katika mwaka wa mia nne na themanini baada ya kutoka wana wa Israeli katika nchi ya Misri, katika mwaka wa nne wa kutawala kwake Sulemani juu ya Israeli, katika mwezi wa Zivu, ndio mwezi wa pili, akaanza kuijenga nyumba ya BWANA. Nayo nyumba hiyo mfalme Sulemani aliyomjengea BWANA, urefu wake ulikuwa mikono sitini, na upana wake ishirini, na kwenda juu kwake mikono thelathini. Na ukumbi mbele ya hekalu la nyumba, urefu wake ulikuwa mikono ishirini, kadiri ya upana wa nyumba; na upana wake mikono kumi mbele ya nyumba. Akaifanyia nyumba madirisha ya miangaza yenye kimia. Nao ukuta wa nyumba akauzungushia vyumba, kushikamana na kuta za nyumba kote kote, za hekalu na za chumba cha ndani; akafanya vyumba vya mbavuni pande zote. Chumba cha chini kilikuwa mikono mitano upana wake, na chumba cha katikati kilikuwa mikono sita upana wake, na chumba cha tatu kilikuwa mikono saba upana wake; kwa kuwa upande wa nje akaupunguza ukuta wa nyumba pande zote, ili boriti zisishikamane kutani mwa nyumba. Na nyumba ilipokuwa ikijengwa, ikajengwa kwa mawe yaliokwisha kuchongwa chimboni; wala nyundo, wala shoka, wala chombo cha chuma cho chote, sauti yake haikusikiwa ilipokuwa ikijengwa nyumba. Mlango wa vyumba vya chini ulikuwapo upande wa kuume wa nyumba; mtu hupanda madaraja ya kuzunguka mpaka vyumba vya katikati, na kutoka vile vya katikati mpaka vile vya tatu. Basi ndivyo alivyoijenga nyumba, akaimaliza; akaifunika nyumba kwa boriti na mbao za mwerezi. Akavijenga vyumba mbavuni mwa nyumba yote, kwenda juu kwake kila kimoja kilikuwa mikono mitano; vikaitegemea nyumba kwa boriti za mwerezi. Neno la BWANA likamjia Sulemani, kusema, Katika habari ya nyumba hii unayoijenga, kama ukienda katika sheria zangu, na kuzifanya hukumu zangu, na kuzishika amri zangu zote na kwenda katika hizo; ndipo nitakapolithibitisha neno langu kwako, nililomwambia Daudi baba yako. Nami nitakaa katikati ya wana wa Israeli, wala sitawaacha watu wangu Israeli. Basi Sulemani akaijenga hiyo nyumba akaimaliza. Akazijenga kuta za nyumba ndani kwa mbao za mwerezi; toka sakafu ya nyumba hata boriti za juu, akazifunika ndani kwa mti; akafunika sakafu ya nyumba kwa mbao za mberoshi. Akajenga mikono ishirini pande za nyuma za nyumba toka chini hata juu kwa mbao za mwerezi; naam, ndani akaijengea chumba cha ndani, yaani, patakatifu pa patakatifu. Nayo nyumba, ndiyo hekalu la mbele, ilikuwa mikono arobaini. Na ndani ya nyumba, mlikuwa na mwerezi ulionakishiwa maboga na maua yaliyofunuka wazi; mlikuwa na mwerezi mahali pote; wala mawe hayakuonekana. Akaweka tayari chumba cha ndani katikati ya nyumba ndani, ili atie humo sanduku la agano la BWANA. Na ndani yake chumba hicho cha ndani mlikuwa na nafasi, mikono ishirini urefu, na mikono ishirini upana, na mikono ishirini kwenda juu kwake; akaifunika na dhahabu safi. Akaifunika madhabahu nayo kwa mwerezi. Hivyo Sulemani akaifunika nyumba ndani kwa dhahabu safi. Akaitenga kwa mikufu ya dhahabu mbele ya chumba cha ndani; akapafunika na dhahabu. Akaifunika nyumba yote kwa dhahabu, hata ilipokwisha nyumba yote; tena madhabahu yote iliyokuwa ya chumba cha ndani akaifunika kwa dhahabu. Akafanya ndani ya chumba cha ndani makerubi mawili ya mzeituni, kwenda juu mikono kumi. Na bawa moja la kerubi lilikuwa mikono mitano urefu wake, na bawa la pili la kerubi mikono mitano; mikono kumi toka mwisho wa bawa moja hata mwisho wa bawa la pili. Na kerubi la pili lilikuwa mikono kumi; makerubi yote mawili walikuwa ya cheo kimoja na namna moja. Kwenda juu kwake kerubi moja kulikuwa mikono kumi, na kerubi la pili vivyo. Akayaweka hayo makerubi katika nyumba ya ndani; na mabawa ya makerubi yakanyoshwa, bawa la moja likafika ukutani huko, na bawa la kerubi la pili likafika ukutani huko; mabawa yao yakagusana katikati ya nyumba. Akayafunika makerubi kwa dhahabu. Akazinakshi kuta zote za nyumba kwa nakshi za makerubi, na mitende, na maua yaliyofunuka wazi, pande za ndani na nje. Na sakafu ya nyumba akaifunika na dhahabu ndani na nje. Akayafanyia maingilio ya chumba cha ndani milango ya mzeituni; kizingiti na miimo ilikuwa ya pande tano. Hivyo akafanya milango miwili ya mzeituni; akanakshi juu yake nakshi za makerubi, na mitende, na maua yaliyofunuka wazi, akaifunika kwa dhahabu; akatia dhahabu juu ya makerubi, na juu ya mitende. Ndivyo alivyoyafanyia maingilio ya hekalu miimo ya mzeituni, yenye pande nne; na milango miwili ya mberoshi; mbao mbili za mlango mmoja zilikuwa za kukunjana, na mbao mbili za mlango wa pili za kukunjana. Akanakshi juu yake makerubi, na mitende, na maua yaliyofunuka wazi; akazifunika kwa dhahabu iliyonyoshwa juu ya machoro. Akaijengea behewa ya ndani safu tatu za mawe ya kuchongwa, na safu moja ya mihimili ya mierezi. Katika mwaka wa nne nyumba ya BWANA ilitiwa msingi, katika mwezi wa Zivu. Hata katika mwaka wa kumi na mmoja, katika mwezi wa Buli, ndio mwezi wa nane, nyumba ikaisha, mambo yake yote, na sharti zake zote. Basi muda wa miaka saba alikuwa katika kuijenga.
1 Wafalme 6:1-38 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Katika mwaka wa mia nne na themanini baada ya Waisraeli kutoka nchi ya Misri, katika mwaka wa nne wa utawala wa Sulemani katika Israeli, katika mwezi wa Zivu, uliokuwa mwezi wa pili, alianza kujenga Hekalu la BWANA. Hekalu ambalo Mfalme Sulemani alilijenga kwa ajili ya BWANA lilikuwa na urefu wa dhiraa sitini, upana wa dhiraa ishirini, na kimo cha dhiraa thelathini kwenda juu. Baraza iliyokuwa mbele ya ukumbi mkuu wa Hekalu iliongeza upana wa Hekalu kwa dhiraa ishirini, na kuchomoza dhiraa kumi mbele ya Hekalu. Akatengeneza madirisha membamba katika Hekalu. Akajenga vyumba vya pembeni kulizunguka Hekalu lote, vikishikamana na kuta za ukumbi wa Hekalu na za Patakatifu pa Patakatifu. Ghorofa ya chini kabisa ilikuwa na upana wa dhiraa tano, ya kati ilikuwa dhiraa sita, na ya tatu ilikuwa dhiraa saba. Kuzunguka ukuta wa nje wa Hekalu akapunguza ukuta pande zote ili boriti zisishikane kwenye kuta za Hekalu. Katika kujenga Hekalu, yalitumika tu mawe yaliyochongwa huko machimboni, wala hakuna nyundo, patasi au chombo kingine chochote cha chuma kilichosikika katika eneo la ujenzi wa Hekalu wakati lilipokuwa likijengwa. Ingilio la ghorofa ya chini kabisa lilikuwa upande wa kusini wa Hekalu; ngazi ilielekea ghorofa ya kati na kutoka hapo ilielekea hadi ghorofa ya tatu. Basi Sulemani akajenga Hekalu na kulikamilisha, akiliweka paa za boriti na mbao za mwerezi. Mfalme Sulemani akajenga vyumba vya pembeni kuzunguka Hekalu lote. Kimo cha kila kimoja kilikuwa dhiraa tano. Navyo vilikuwa vimeunganishwa na Hekalu kwa boriti za mwerezi. Neno la BWANA likamjia Sulemani kusema: “Kuhusu Hekalu hili unalojenga, kama ukifuata amri zangu, ukatunza masharti yangu na kushika maagizo yangu yote na kuyatii, nitatimiza kupitia kwako ahadi niliyomwahidi Daudi baba yako. Nami nitakaa miongoni mwa Waisraeli, nami sitawaacha watu wangu Israeli.” Basi Sulemani akajenga Hekalu na kulikamilisha. Akazifunika kuta zake za ndani kwa mbao za mwerezi, akizipigilia ukutani kuanzia sakafuni mwa Hekalu hadi kwenye dari, na kufunika sakafu ya Hekalu kwa mbao za misunobari. Akagawa dhiraa ishirini sehemu ya nyuma ya Hekalu kwa mbao za mwerezi kuanzia kwenye sakafu hadi darini ili kufanya sehemu takatifu ya ndani, yaani Patakatifu pa Patakatifu. Ukumbi mkuu uliokuwa mbele ya chumba hiki ulikuwa na urefu wa dhiraa arobaini. Ndani, Hekalu lilipambwa na mbao za mwerezi zilizonakshiwa mifano ya maboga na maua yaliyochanua. Kila kitu kilikuwa cha mwerezi; hakuna jiwe ambalo lilionekana. Ndani ya Hekalu akatengeneza mahali patakatifu pa kuliweka Sanduku la Agano la BWANA. Mahali patakatifu palikuwa na urefu wa dhiraa ishirini, upana wa dhiraa ishirini, na kimo cha dhiraa ishirini. Akapafunika upande wa ndani, na madhabahu ya mwerezi pia, kwa dhahabu safi. Sulemani akalifunika Hekalu upande wa ndani kwa dhahabu safi, na akaitandaza mikufu ya dhahabu kutoka upande mmoja hadi ule mwingine mbele ya mahali patakatifu, palipofunikwa kwa dhahabu. Basi akafunika upande wote wa ndani kwa dhahabu. Pia akafunika kwa dhahabu yale madhabahu yaliyokuwa ndani ya mahali patakatifu. Katika mahali patakatifu, akatengeneza makerubi wawili kwa mzeituni, kila moja likiwa na dhiraa kumi kwenda juu. Bawa moja la kerubi wa kwanza lilikuwa na urefu wa dhiraa tano na bawa jingine dhiraa tano, hivyo urefu kutoka ncha ya bawa moja hadi ncha ya bawa jingine ulikuwa dhiraa kumi. Kerubi wa pili alikuwa na urefu wa dhiraa kumi pia, kwa kuwa makerubi hao wawili walifanana kwa vipimo na kwa umbo. Kimo cha kila kerubi kilikuwa dhiraa kumi. Aliwaweka makerubi hao katika chumba cha ndani kabisa cha Hekalu, mabawa yao yakiwa yamekunjuliwa. Bawa la kerubi mmoja liligusa ukuta mmoja, wakati bawa la yule mwingine liligusa ukuta wa upande mwingine, nayo mabawa yao mengine yaligusana katikati ya chumba. Akafunika wale makerubi kwa dhahabu. Kuta zote za Hekalu, za vyumba vya ndani na vya nje, zilipambwa kwa nakshi za makerubi, mitende na maua yaliyochanua. Pia alifunika sakafu zote za vyumba vya ndani na vya nje vya Hekalu kwa dhahabu. Katika ingilio la mahali patakatifu sana, alitengeneza milango ya mbao za mzeituni, yenye miimo ya sehemu moja ya tano ya upana wa madhabahu. Kwenye milango hiyo miwili ya mbao za mzeituni, alinakshi makerubi, mitende, pamoja na maua yaliyochanua, na kufunika makerubi na mitende kwa dhahabu iliyofuliwa. Kwa namna hiyo hiyo, alitengeneza miimo kwa mbao za mzeituni yenye upana wa robo ya upana wa ukumbi mkuu kwa ajili ya ingilio la ukumbi huo. Pia akatengeneza milango miwili kwa mbao za msunobari, kila mmoja ukiwa na vipande viwili ambavyo vilikunjwa kwa bawaba. Akanakshi makerubi, mitende na maua yaliyochanua juu yake, na kufunika kwa dhahabu iliyonyoshwa vizuri juu ya michoro. Tena akajenga ua wa ndani safu tatu za mawe yaliyochongwa, na safu moja ya boriti za mwerezi zilizosawazishwa. Msingi wa Hekalu la BWANA uliwekwa katika mwaka wa nne, katika mwezi wa Zivu. Katika mwaka wa kumi na moja, mwezi wa Buli, ndio mwezi wa nane, Hekalu lilikamilika katika hatua zake zote kwa kufuatana na maelekezo yake Sulemani. Alilijenga kwa miaka saba.