1 Wafalme 5:1-5
1 Wafalme 5:1-5 Biblia Habari Njema (BHN)
Naye mfalme Hiramu wa Tiro, aliyekuwa rafiki ya Daudi, alipopata habari kwamba Solomoni amekuwa mfalme mahali pa baba yake, alituma watumishi kwake. Ndipo Solomoni akampelekea Hiramu ujumbe huu: “Wajua kwamba baba yangu Daudi hakuweza kumjengea Mwenyezi-Mungu, Mungu wake, hekalu la kumwabudia, kwa sababu ya kukumbana na vita vingi dhidi ya maadui wa nchi jirani mpaka hapo Mwenyezi-Mungu alipompatia ushindi. Lakini sasa, Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu, amenijalia amani pande zote. Sina adui wala taabu. Basi, nimeamua kumjengea Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu, nyumba ya kumwabudia. Na hii ni sawa kabisa kama Mwenyezi-Mungu alivyomwahidi baba yangu akisema: ‘Mwanao ambaye nitamfanya aketi katika kiti chako cha enzi, atanijengea nyumba!’
1 Wafalme 5:1-5 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ndipo Hiramu, mfalme wa Tiro, akawatuma watumishi wake kwa Sulemani; kwani alikuwa amesikia ya kwamba wamemtia mafuta awe mfalme mahali pa baba yake. Kwa maana Hiramu alikuwa akimpenda Daudi siku zote. Basi Sulemani akatuma watu kwa Hiramu, akasema, Wajua kuwa Daudi baba yangu hakuweza kujenga nyumba kwa jina la BWANA, Mungu wake, kwa sababu ya vita vilivyomzunguka pande zote, hata BWANA alipowatia watu chini ya nyayo zake. Ila leo BWANA, Mungu wangu, amenipa amani kila upande; hakuna adui, wala tukio baya. Nami, tazama, nakusudia kujenga nyumba kwa jina la BWANA, Mungu wangu, kama BWANA alivyomwambia Daudi baba yangu, akisema, Mwana wako, nitakayemweka katika kiti chake cha enzi mahali pako, ndiye atakayeijenga nyumba kwa jina langu.
1 Wafalme 5:1-5 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ndipo Hiramu, mfalme wa Tiro, akawatuma watumishi wake kwa Sulemani; kwani alikuwa amesikia ya kwamba wamemtia mafuta awe mfalme mahali pa baba yake. Kwa maana Hiramu alikuwa akimpenda Daudi siku zote. Basi Sulemani akatuma watu kwa Hiramu, akasema, Umemjua Daudi baba yangu jinsi asivyoweza kujenga nyumba kwa jina la BWANA, Mungu wake, kwa sababu ya vita vilivyomzunguka pande zote, hata BWANA alipowatia watu chini ya nyayo zake. Ila leo BWANA, Mungu wangu, amenipa amani kila upande; hakuna adui, wala tukio baya. Nami, tazama, nakusudia kujenga nyumba kwa jina la BWANA, Mungu wangu, kama BWANA alivyomwambia Daudi baba yangu, akisema, Mwana wako, nitakayemweka katika kiti chake cha enzi mahali pako, ndiye atakayeijenga nyumba kwa jina langu.
1 Wafalme 5:1-5 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Hiramu mfalme wa Tiro aliposikia kuwa Sulemani amepakwa mafuta awe mfalme mahali pa Daudi baba yake, akatuma wajumbe kwa Sulemani, kwa sababu Hiramu siku zote alikuwa na uhusiano mzuri wa kirafiki na Daudi. Sulemani akapeleka ujumbe huu kwa Hiramu: “Unajua kwamba baba yangu Daudi hakuweza kujenga Hekalu kwa ajili ya Jina la BWANA Mungu wake kwa sababu ya vita vilivyopiganwa dhidi yake kutoka pande zote, hadi BWANA alipowaweka adui zake chini ya miguu yake. Lakini sasa BWANA Mungu wangu amenipa utulivu kila upande hakuna adui wala maafa. Kwa hiyo, ninakusudia kujenga Hekalu kwa ajili ya Jina la BWANA, Mungu wangu, kama BWANA alivyomwambia baba yangu Daudi, aliposema, ‘Mwanao nitakayemweka kwenye kiti cha ufalme mahali pako, ndiye atajenga Hekalu kwa ajili ya Jina langu.’