Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Wafalme 4:1-34

1 Wafalme 4:1-34 Biblia Habari Njema (BHN)

Solomoni alikuwa mfalme wa nchi yote ya Israeli, na wafuatao walikuwa baadhi ya maofisa wake wa vyeo vya juu: Azaria, mwana wa Sadoki, alikuwa kuhani. Elihorefu na Ahiya wana wa Shausha, walikuwa makatibu; Yehoshafati mwana wa Ahiludi, alikuwa mweka kumbukumbu za habari. Benaya mwana wa Yehoyada, alikuwa jemadari wa jeshi; nao Sadoki na Abiathari, walikuwa makuhani. Azaria mwana wa Nathani, alikuwa ofisa mkuu tawala; kuhani Zabudi mwana wa Nathani, alikuwa rafiki wa mfalme. Ahishari alikuwa mkuu wa ikulu na Adoniramu mwana wa Abda, alikuwa msimamizi wa kazi za kulazimishwa. Solomoni aliteua maofisa tawala kumi na wawili kwa nchi nzima ya Israeli. Hao walipewa jukumu la kutafuta chakula kwa ajili ya mfalme na nyumba yake; kila mmoja wao alileta chakula kutoka mkoani kwake kwa mwezi mmoja kila mwaka. Haya ndiyo majina ya hao maofisa tawala: Ben-huri alisimamia sehemu ya milima ya Efraimu; Ben-dekeri alisimamia miji ya Makai, Shaalbimu, Beth-shemeshi na Elon-beth-hanani. Ben-hesedi alisimamia mji wa Arubothi, alisimamia pia Soko na nchi yote ya Heferi. Ben-abinadabu, mume wa Tafathi, binti Solomoni, alisimamia kanda yote ya Nafath-dori. Baana, mwana wa Ahiludi, alisimamia miji ya Taanaki, Megido, na sehemu yote ya Beth-sheani iliyo karibu na mji wa Zarethi, kusini ya mji wa Yezreeli, na kutoka Beth-sheani mpaka miji ya Abel-mehola, na hata kupita mji wa Yokmeamu. Ben-geberi, alisimamia mji wa Ramoth-gileadi pamoja na vijiji vya Gileadi vilivyokuwa chini ya Yairi, mwana wa Manase; pia alisimamia mkoa wa Argobu ulioko Bashani; yote jumla ilikuwa miji mikubwa sitini iliyozungushiwa kuta na kuwekwa fito za shaba malangoni. Ahinadabu, mwana wa Ido, alisimamia jimbo la Mahanaimu. Ahimaasi, mumewe Basemathi, binti Solomoni, alisimamia wilaya ya Naftali. Baana mwana wa Hushai, alisimamia wilaya ya Asheri na Bealothi. Yehoshafati mwana wa Parua, alisimamia wilaya ya Isakari. Shimei, mwana wa Ela, alisimamia wilaya ya Benyamini. Geberi, mwana wa Uri, alisimamia wilaya ya Gileadi, ambayo hapo awali ilitwaliwa na Sihoni mfalme wa Waamori, na Ogu mfalme wa Bashani. Licha ya hawa kumi na wawili, palikuwa na mkuu mmoja aliyesimamia nchi nzima ya Yuda. Watu wa Yuda na wa Israeli walikuwa wengi kama mchanga wa pwani, nao walikuwa wakila, wakinywa, na kufurahi. Solomoni alitawala falme zote kuanzia mto Eufrate mpaka nchi ya Wafilisti, hadi mpakani na Misri. Mataifa yote yalimtumikia na kulipa kodi kwake wakati wote wa maisha yake. Chakula alichohitaji Solomoni kwa siku moja, kilikuwa unga laini madebe 360, na unga wa kawaida madebe 720, ng'ombe wanono kumi, na ng'ombe wa kundini ishirini, kondoo 100 pamoja na kulungu, paa, swala na kuku wanono. Naam, nchi yote magharibi ya mto Eufrate: Kutoka Tifsa mpaka mji wa Gaza, ilikuwa chini ya utawala wake. Wafalme wote magharibi ya mto Eufrate walikuwa chini yake, na alikuwa na amani na nchi zote jirani. Siku zote za utawala wake Solomoni, watu wa Yuda na watu wa Israeli, toka Dani mpaka Beer-sheba, walikaa salama, kila mtu kwenye miti yake ya mizabibu na mitini. Solomoni alikuwa na vibanda 40,000 kwa ajili ya farasi wa magari yake ya kukokotwa, na askari wapandafarasi 12,000. Wale maofisa wake kumi na wawili, kila mmoja kwa mwezi aliopangiwa, walipeleka chakula cha kutosha kwa ajili ya mfalme na wale wote waliokula nyumbani mwake. Mahitaji yao yote yalitoshelezwa. Zamu ya kila mmoja ilipofika, alipeleka pia shayiri na majani ya kulisha farasi na wanyama waendao kasi. Mungu alimpa Solomoni hekima zaidi na akili kwa wingi; maarifa yake yalikuwa kama mchanga wa pwani, hayakuwa na kipimo. Hekima ya Solomoni iliipita hekima ya watu wa mashariki na iliishinda hekima ya watu wa Misri. Aliwashinda watu wote kwa hekima; aliwashinda Ethani, yule Mwezrahi, Hemani na Kalkoli na Darda, wana wa Maholi; na sifa zake zilienea katika mataifa yote jirani. Alitunga methali 3,000 na nyimbo 1,500. Alizungumza habari za miti, kuanzia mwerezi ulioko Lebanoni, hata husopo, mmea uotao ukutani. Alizungumza pia juu ya wanyama, ndege, jamii ya wanyama wenye damu baridi watagao mayai, na juu ya samaki. Watu kutoka mataifa yote, na wafalme wote waliopata kusikia habari kuhusu hekima yake, walikuja kumsikiliza.

1 Wafalme 4:1-34 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Basi mfalme Sulemani akawa mfalme juu ya Israeli wote. Na hawa ndio wakuu aliokuwa nao; Azaria mwana wa Sadoki, kuhani, Elihorefu na Ahiya, wana wa Shausha, waandishi; Yehoshafati mwana wa Ahiludi mwenye kuandika tarehe; na Benaya mwana wa Yehoyada alikuwa jemadari wa jeshi; na Sadoki na Abiathari walikuwa makuhani; na Azaria mwana wa Nathani alikuwa afisa mkuu tawala; na Zabudi mwana wa Nathani alikuwa kuhani, rafiki yake mfalme. Na Ahishari alikuwa mkuu wa kasri; na Adoramu mwana wa Abda alikuwa msimamizi wa shokoa. Sulemani alikuwa na maafisa tawala kumi na wawili juu ya Israeli wote, walioleta chakula cha mfalme na nyumba yake; kila mtu alikuwa na mwezi mmoja katika mwaka kuleta chakula. Na haya ndiyo majina yao. Mwana wa Huri, mlimani mwa Efraimu. Mwana wa Dekari, kutoka Makasi, na Shaalbimu na Beth-shemeshi na Elon-beth-hanani. Mwana wa Hesedi, katika Arubothi; na Soko ilikuwa kwake na nchi yote ya Heferi. Mwana wa Abinadabu katika Nafath-dori yote; ndiye aliyekuwa naye Tafathi binti Sulemani kuwa mke wake. Baana mwana wa Ahiludi, katika Taanaki na Megido, na Beth-sheani yote, iliyo kando ya Sarethani, chini ya Yezreeli, tangu Beth-sheani mpaka Abel-mehola, hata kupita Yokmeamu. Mwana wa Geberi katika Ramoth-gileadi; na kwake ilikuwa miji ya Yairi mwana wa Manase iliyomo Gileadi; na kwake ilikuwa wilaya ya Argobu, iliyomo Bashani, miji mikubwa sitini yenye kuta na makomeo ya shaba. Ahinadabu mwana wa Ido, katika Mahanaimu. Ahimaasi, katika Naftali; naye ndiye aliyemwoa Basemathi binti Sulemani. Baana mwana wa Hushai, katika Asheri na Bealothi. Yehoshafati mwana wa Parua, katika Isakari. Shimei mwana wa Ela, katika Benyamini. Geberi mwana wa Uri, katika nchi ya Gileadi, nchi ya Sihoni mfalme wa Waamori, na Ogu mfalme wa Bashani; naye alikuwa mkuu pekee katika nchi hiyo. Yuda na Israeli walikuwa wengi kama mchanga wa pwani kwa wingi, wakila, na kunywa, na kufurahi. Sulemani akatawala juu ya falme zote, toka Mto mpaka nchi ya Wafilisti, na hata mpaka wa Misri; walimletea tunu, na kumtumikia Sulemani siku zote za maisha yake. Na vyakula vya Sulemani vya siku moja vilikuwa kori thelathini za unga mzuri, na kori sitini za ngano, na ng'ombe kumi walionona, na ng'ombe ishirini za malisho, na kondoo mia moja, pamoja na ayala, na paa, na kulungu, na kuku walionona. Kwani alikuwa akitawala nchi yote upande huu wa Mto, toka Tifsa mpaka Gaza, juu ya wafalme wote wa upande huu wa Mto; naye alikuwa na amani pande zake zote. Yuda na Israeli wakakaa salama, kila mtu chini ya mzabibu wake na chini ya mtini wake, tokea Dani mpaka Beer-sheba, siku zote za Sulemani. Tena Sulemani alikuwa na mabanda ya farasi elfu arubaini kwa magari yake, na wapandao farasi elfu kumi na mbili. Na maofisa wale wakaleta chakula kwa mfalme Sulemani na kwa wote walioijia meza ya mfalme Sulemani, kila mtu katika mwezi wake, kisipunguke kitu. Shayiri pia na majani kwa farasi, na kwa wanyama wenye mbio, wakaleta mahali walipokuwapo, kila mtu kwa kadiri ya kazi yake. Mungu akampa Sulemani hekima, na akili nyingi sana, na moyo mkuu, kama mchanga ulioko pwani. Hekima ya Sulemani ikapita hekima ya watu wote wa mashariki, na hekima zote za Misri. Kwa kuwa alikuwa na hekima kuliko watu wote; kuliko Ethani Mwezrahi, na Hemani, na Kalkoli, na Darda, wana wa Maholi; zikaenea sifa zake kati ya mataifa yote yaliyozunguka. Naye akanena mifano elfu tatu, na nyimbo zake zilikuwa elfu moja na tano. Akanena habari za miti tangu mwerezi ulioko Lebanoni hata hisopo umeao ukutani; pia akanena habari za wanyama, na za ndege, na vitambaavyo, na samaki. Watu wakaja kutoka mataifa yote, toka wafalme wote wa ulimwengu, waliokuwa wamepata habari za hekima yake, ili waisikie hekima ya Sulemani.

1 Wafalme 4:1-34 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Basi mfalme Sulemani akawa mfalme juu ya Israeli wote. Na hawa ndio wakuu aliokuwa nao; Azaria mwana wa Sadoki, kuhani, Elihorefu na Ahiya, wana wa Shausha, waandishi; Yehoshafati mwana wa Ahiludi mwenye kuandika tarehe; na Benaya mwana wa Yehoyada alikuwa juu ya jeshi; na Sadoki na Abiathari walikuwa makuhani; na Azaria mwana wa Nathani alikuwa juu ya maakida; na Zabudi mwana wa Nathani alikuwa kuhani, rafiki wake mfalme. Na Ahishari alikuwa juu ya nyumba; na Adoramu mwana wa Abda alikuwa juu ya shokoa. Sulemani alikuwa na maakida kumi na wawili juu ya Israeli wote, walioleta chakula cha mfalme na nyumba yake; kila mtu alikuwa na mwezi mmoja katika mwaka kuleta chakula. Na haya ndiyo majina yao. Mwana wa Huri, mlimani mwa Efraimu. Mwana wa Dekari, kutoka Makasi, na Shaalbimu na Bethshemeshi na Elon-beth-hanani. Mwana wa Hesedi, katika Arubothi; na Soko ilikuwa kwake na nchi yote ya Heferi. Mwana wa Abinadabu katika Nafath-dori yote; ndiye aliyekuwa naye Tafathi binti Sulemani kuwa mke wake. Baana mwana wa Ahiludi, katika Taanaki na Megido, na Beth-sheani yote, iliyo kando ya Sarethani, chini ya Yezreeli, tangu Beth-sheani mpaka Abel-mehola, hata kupita Yokmeamu. Mwana wa Geberi katika Ramoth-gileadi; na kwake ilikuwa miji ya Yairi mwana wa Manase iliyomo Gileadi; na kwake ilikuwa wilaya ya Argobu, iliyomo Bashani, miji mikubwa sitini yenye kuta na makomeo ya shaba. Ahinadabu mwana wa Ido, katika Mahanaimu. Ahimaasi, katika Naftali; naye ndiye aliyemwoa Basemathi binti Sulemani. Baana mwana wa Hushai, katika Asheri na Bealothi. Yehoshafati mwana wa Parua, katika Isakari. Shimei mwana wa Ela, katika Benyamini. Geberi mwana wa Uri, katika nchi ya Gileadi, nchi ya Sihoni mfalme wa Waamori, na Ogu mfalme wa Bashani; naye alikuwa akida wa pekee katika nchi hiyo. Yuda na Israeli walikuwa wengi kama mchanga wa pwani kwa wingi, wakila, na kunywa, na kufurahi. Sulemani akatawala juu ya falme zote, toka Mto mpaka nchi ya Wafilisti, na hata mpaka wa Misri; walimletea tunu, na kumtumikia Sulemani siku zote za maisha yake. Na vyakula vya Sulemani vya siku moja vilikuwa kori thelathini za unga mzuri, na kori sitini za ngano, na ng’ombe kumi walionona, na ng’ombe ishirini za malisho, na kondoo mia, pamoja na ayala, na paa, na kulungu, na kuku walionona. Kwani alikuwa akitawala nchi yote upande huu wa Mto, toka Tifsa mpaka Gaza, juu ya wafalme wote wa upande huu wa Mto; naye alikuwa na amani pande zake zote. Yuda na Israeli wakakaa salama, kila mtu chini ya mzabibu wake na chini ya mtini wake, tokea Dani mpaka Beer-sheba, siku zote za Sulemani. Tena Sulemani alikuwa na mabanda ya farasi arobaini elfu kwa magari yake, na wapandao farasi kumi na mbili elfu. Na maakida wale wakaleta chakula kwa mfalme Sulemani na kwa wote walioijia meza ya mfalme Sulemani, kila mtu katika mwezi wake, kisipunguke kitu. Shayiri pia na majani kwa farasi, na kwa wanyama wenye mbio, wakaleta mahali walipokuwapo, kila mtu kwa kadiri ya kazi yake. Mungu akampa Sulemani hekima, na akili nyingi sana, na moyo mkuu, kama mchanga ulioko pwani. Hekima ya Sulemani ikapita hekima ya wana wote wa mashariki, na hekima zote za Misri. Kwa kuwa alikuwa na hekima kuliko watu wote; kuliko Ethani Mwezrahi, na Hemani, na Kalkoli, na Darda, wana wa Maholi; zikaenea sifa zake kati ya mataifa yote yaliyozunguka. Naye akanena mifano elfu tatu, na nyimbo zake zilikuwa elfu moja na tano. Akanena habari za miti tangu mwerezi ulioko Lebanoni hata hisopo umeao ukutani; pia akanena habari za wanyama, na za ndege, na vitambaavyo, na samaki. Wakaja wa mataifa yote ili waisikie hekima ya Sulemani, toka wafalme wote wa ulimwengu, waliokuwa wamepata habari za hekima yake.

1 Wafalme 4:1-34 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

Basi Mfalme Sulemani akatawala Israeli yote. Hawa walikuwa maafisa wake wakuu: Kuhani: Azaria mwana wa Sadoki; Elihorefu na Ahiya, wana wa Shisha: waandishi; Yehoshafati mwana wa Ahiludi: karani; Benaya mwana wa Yehoyada: jemadari mkuu wa jeshi; Sadoki na Abiathari: makuhani; Azaria mwana wa Nathani: kiongozi wa maafisa wa wilaya; Zabudi mwana wa Nathani: kuhani na mshauri binafsi wa mfalme; Ahishari: msimamizi wa jumba la kifalme; Adoniramu mwana wa Abda: msimamizi wa kazi za kulazimisha. Pia Sulemani alikuwa na watawala kumi na wawili wa wilaya katika Israeli yote, walioshughulikia mahitaji ya mfalme na ya watu wa nyumbani kwa mfalme. Kila mmoja alitoa chakula kwa mwezi mmoja katika mwaka. Majina yao ni haya: Ben-Huri: katika nchi ya vilima ya Efraimu; Ben-Dekari: katika Makasi, Shaalbimu, Beth-Shemeshi na Elon-Beth-Hanani; Ben-Hesedi: katika Arubothi (Soko na nchi yote ya Heferi zilikuwa zake); Ben-Abinadabu: katika Nafoth-Dori (alimwoa Tafathi binti Sulemani); Baana mwana wa Ahiludi: katika Taanaki na Megido, na katika Beth-Shani yote karibu na Sarethani chini ya Yezreeli, kuanzia Beth-Shani hadi Abel-Mehola kupita hadi Yokmeamu; Ben-Geberi: katika Ramoth-Gileadi (makazi ya Yairi mwana wa Manase katika Gileadi ilikuwa yake, kadhalika wilaya ya Argobu katika Bashani na miji yake mikubwa sitini iliyozungukwa na kuta zenye makomeo ya shaba); Ahinadabu mwana wa Ido: katika Mahanaimu; Ahimaasi: katika Naftali (alikuwa amemwoa Basemathi binti Sulemani); Baana mwana wa Hushai: katika Asheri na katika Bealothi; Yehoshafati mwana wa Parua: katika Isakari; Shimei mwana wa Ela: katika Benyamini; Geberi mwana wa Uri: katika Gileadi (nchi ya Sihoni mfalme wa Waamori na nchi ya Ogu mfalme wa Bashani). Naye alikuwa mtawala pekee katika eneo hilo. Watu wa Yuda na Israeli walikuwa wengi kama mchanga wa pwani; walikula, wakanywa na kufurahi. Mfalme Sulemani akatawala katika falme zote kuanzia Mto hadi nchi ya Wafilisti, hadi kwenye mpaka wa Misri. Nchi hizi zilileta ushuru na zilikuwa chini ya Sulemani, siku zote za maisha yake. Mahitaji ya Sulemani ya kila siku yalikuwa kori thelathini za unga laini, kori sitini za unga wa kawaida. Ngʼombe kumi wa zizini, ngʼombe ishirini wa malisho, kondoo na mbuzi mia moja, pamoja na ayala, paa, kulungu na kuku wazuri sana. Kwa kuwa Sulemani alitawala falme zote magharibi ya Mto, kuanzia Tifsa hadi Gaza, naye akawa na amani pande zote. Wakati wa maisha ya Sulemani, watu wa Yuda na Israeli, kuanzia Dani hadi Beer-Sheba, waliishi salama, kila mtu chini ya mzabibu wake na chini ya mtini wake. Sulemani alikuwa na mabanda elfu nne ya magari ya vita, na farasi elfu kumi na mbili. Maafisa wa eneo hilo, kila mmoja katika mwezi wake, walileta mahitaji kwa ajili ya Mfalme Sulemani na wote waliokula mezani mwa mfalme. Walihakikisha kuwa hakuna chochote kilichopungua. Pia walileta kiasi walichopangiwa cha shayiri na majani kwa ajili ya farasi wa magari ya vita na farasi wengine mahali palipostahili. Mungu akampa Sulemani hekima na akili kubwa, pia ufahamu mpana usiopimika kama mchanga ulioko pwani ya bahari. Hekima ya Sulemani ilikuwa kubwa kuliko hekima ya watu wote wa Mashariki na kubwa kuliko hekima yote ya Misri. Alikuwa na hekima kuliko kila mwandishi, akiwemo Ethani Mwezrahi; kuliko Hemani, Kalkoli na Darda, wana wa Maholi. Umaarufu wake ukaenea kwa mataifa yote yaliyomzunguka. Akanena mithali elfu tatu, na nyimbo zake zilikuwa elfu moja na tano (1,005). Akaelezea maisha ya mimea kuanzia mwerezi wa Lebanoni hadi hisopo iotayo ukutani. Pia akafundisha kuhusu wanyama na ndege, wanyama wanaotambaa na samaki. Watu wa mataifa yote wakaja kusikiliza hekima ya Sulemani, wakiwa wametumwa na wafalme wote wa ulimwengu, waliokuwa wamesikia kuhusu hekima yake.