1 Wafalme 22:1-18
1 Wafalme 22:1-18 Biblia Habari Njema (BHN)
Kwa muda wa miaka mitatu hivi, kulikuwa na amani kati ya Israeli na Aramu. Lakini mnamo mwaka wa tatu, Yehoshafati, mfalme wa Yuda, alifika kumtembelea Ahabu, mfalme wa Israeli. Ahabu akawaambia watumishi wake, “Je, hamjui kwamba Ramoth-gileadi ni mali yetu? Mbona basi tunajikalia tu bila kuunyakua kutoka kwa mfalme wa Aramu?” Kisha akamwambia Yehoshafati, “Je, utaandamana nami kupigana huko Ramoth-gileadi?” Naye Yehoshafati akamjibu mfalme wa Israeli, “Naam; mimi na wewe ni kitu kimoja, na pia watu wangu ni watu wako, farasi wangu ni farasi wako.” Kisha Yehoshafati aliendelea kumwambia mfalme wa Israeli: “Lakini, kwanza mwulize Mwenyezi-Mungu ushauri.” Basi, Ahabu akaitisha kikao cha manabii wapatao 400, akawauliza, “Je, niende nikaushambulie mji wa Ramoth-gileadi au nisiende?” Wao wakamjibu: “Nenda! Mwenyezi-Mungu atakupatia ushindi.” Lakini, Yehoshafati akasema, “Je, hapa hakuna nabii mwingine wa Mwenyezi-Mungu ambaye twaweza kumwuliza shauri?” Naye mfalme wa Israeli akamjibu Yehoshafati, “Yupo, bado mmoja, Mikaya mwana wa Imla. Yeye twaweza kumwuliza shauri la Mwenyezi-Mungu. Lakini namchukia sana kwa sababu yeye, kamwe hatabiri jambo jema juu yangu, ila mabaya tu.” Yehoshafati akamwambia, “Si vizuri mfalme kusema hivyo.” Basi, Ahabu, mfalme wa Israeli, akamwita mtumishi mmoja, akamwamuru, “Haraka! Nenda ukamlete Mikaya mwana wa Imla.” Wakati huo, mfalme wa Israeli pamoja na Yehoshafati mfalme wa Yuda, walikuwa wameketi katika viti vyao vya enzi wakikaa kwenye kiwanja cha kupuria nafaka kwenye lango la kuingilia mjini Samaria nao walikuwa wamevalia mavazi yao ya kifalme; wakati huo manabii wote wakawa wanatabiri mbele yao. Kisha mmoja wa manabii hao, Sedekia mwana wa Kenaana, akajitengenezea pembe za chuma akasema, “Mwenyezi-Mungu asema hivi: ‘Kwa pembe hizi, utawarudisha nyuma Waaramu na kuwaangamiza.’” Hata wale manabii wengine wote wakatabiri vivyo hivyo, wakasema, “Nenda uushambulie Ramoth-gileadi, utashinda! Mwenyezi-Mungu atautia mikononi mwako.” Wakati huo, yule mtumishi aliyetumwa kwenda kwa Mikaya, alimwambia, “Manabii wengine wote kwa pamoja, wamemtabiria mfalme ushindi; tafadhali, nawe pia ufanye kama wao, umtabirie mema.” Lakini Mikaya akamjibu, “Ninaapa kwa Mwenyezi-Mungu aliye hai, mimi nitasema tu yale atakayoniambia Mwenyezi-Mungu.” Basi, Mikaya alipofika mbele ya mfalme, mfalme alimwuliza, “Je, twende kupigana vita huko Ramoth-gileadi ama tusiende?” Naye alimjibu, “Nenda na ufanikiwe, naye Mwenyezi-Mungu atautia mikononi mwako.” Lakini mfalme akamwambia, “Nitakuapisha mara ngapi kwamba unaposema nami kwa jina la Mwenyezi-Mungu, ni lazima uniambie ukweli mtupu?” Ndipo, Mikaya akasema, “Niliona watu wote wa Israeli wametawanyika milimani kama kondoo wasio na mchungaji. Naye Mwenyezi-Mungu akasema, ‘Watu hawa hawana kiongozi; basi warudi kila mtu nyumbani kwake kwa amani.’” Hapo, mfalme wa Israeli akamwambia Yehoshafati, “Sikukuambia kamwe hatatabiri jema juu yangu ila mabaya tu?”
1 Wafalme 22:1-18 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Wakakaa miaka mitatu pasipo vita kati ya Shamu na Israeli. Ikawa, mwaka wa tatu Yehoshafati mfalme Wa Yuda akamshukia mfalme wa Israeli. Mfalme wa Israeli akawaambia watumishi wake, Je! Hamjui ya kuwa Ramoth-Gileadi ni yetu? Nasi tumenyamaza tusiitwae mkononi mwa mfalme wa Shamu? Akamwambia Yehoshafati, Je! Utakwenda nami tupigane na Ramoth-gileadi? Yehoshafati akamwambia mfalme wa Israeli, Mimi ni kama wewe, na watu wangu ni kama watu wako na farasi wangu ni kama farasi wako. Yehoshafati akamwambia mfalme wa Israeli, Uulize leo, nakusihi, kwa neno la BWANA. Ndipo mfalme wa Israeli akawakusanya pamoja manabii, kama watu mia nne. Akawaambia Je! Niende juu ya Ramoth-Gileadi kuupiga vita, au ninyamaze? Wakasema Kwea; kwa kuwa BWANA atautia mkononi mwa mfalme. Lakini Yehoshafati akasema, Je! Hayupo hapa nabii mwingine wa BWANA, ili tumwulize yeye? Mfalme wa Israeli akamwambia Yehoshafati, Yupo mtu mmoja, ambaye tungeweza kumwuliza BWANA kwa yeye, yaani Mikaya mwana wa Imla; lakini namchukia; kwa sababu hanibashirii mema, ila mabaya. Yehoshafati akasema, La! Mfalme asiseme hivi. Ndipo mfalme wa Israeli akamwita ofisa, akamwambia, mlete hima Mikaya mwana wa Imla. Basi mfalme wa Israeli na Yehoshafati mfalme wa Yuda walikuwa wakikaa kila mtu katika kiti chake cha enzi, wamevaa mavazi yao, katika sakafu langoni pa Samaria; na manabii wote wakafanya unabii mbele yao. Na Sedekia mwana wa Kenaana akajifanyia pembe za chuma, akasema, BWANA asema hivi, Kwa hizo utawasukuma Washami, hata waharibike. Na manabii wote wakasema hivyo kwa unabii, wakisema, Kwea Ramoth-Gileadi, ukafanikiwe; kwa kuwa BWANA atautia mkononi mwa mfalme. Na yule mjumbe, aliyekwenda kumwita Mikaya, akamwambia, akasema, Angalia sasa, maneno ya manabii kwa kinywa kimoja husema mema kwa mfalme; neno lako na liwe, nakusihi, kama neno la mmojawapo wao, ukaseme mema. Mikaya akasema, Kama BWANA aishivyo, neno lile BWANA aniambialo, ndilo nitakalolinena. Na alipokuja kwa mfalme, mfalme alimwambia, Je! Mikaya, tuende Ramoth-Gileadi kupiga vita, au tunyamaze? Akamwambia, Kwea, ufanikiwe; kwa kuwa BWANA atautia mkononi mwa mfalme. Mfalme akamwambia, Mara ngapi nikuapishe usiniambie neno ila yaliyo kweli, kwa jina la BWANA? Akasema, Niliwaona Waisraeli wote wametawanyika milimani, kama kondoo wasio na mchungaji. BWANA akasema, Hawa hawana bwana; na warudi kila mtu nyumbani kwake kwa amani. Mfalme wa Israeli akamwambia Yehoshafati, Je! Sikukuambia, hatanibashiria mema, ila mabaya?
1 Wafalme 22:1-18 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Wakakaa miaka mitatu pasipo vita kati ya Shamu na Israeli. Ikawa, mwaka wa tatu Yehoshafati mfalme Wa Yuda akamshukia mfalme wa Israeli. Mfalme wa Israeli akawaambia watumishi wake, Je! Hamjui ya kuwa Ramoth-Gileadi ni yetu? Nasi tumenyamaza tusiitwae mkononi mwa mfalme wa Shamu? Akamwambia Yehoshafati, Je! Utakwenda nami tupigane na Ramoth-gileadi? Yehoshafati akamwambia mfalme wa Israeli, Mimi ni kama wewe, na watu wangu ni kama watu wako na farasi zangu ni kama farasi zako. Yehoshafati akamwambia mfalme wa Israeli, Uulize leo, nakusihi, kwa neno la BWANA. Ndipo mfalme wa Israeli akawakusanya pamoja manabii, kama watu mia nne. Akawaambia Je! Niende juu ya Ramoth-Gileadi kuupiga vita, au ninyamaze? Wakasema Kwea; kwa kuwa BWANA atautia mkononi mwa mfalme. Lakini Yehoshafati akasema, Je! Hayupo hapa nabii wa BWANA tena, ili tumwulize yeye? Mfalme wa Israeli akamwambia Yehoshafati, Yupo mtu mmoja, ambaye tungeweza kumwuliza BWANA kwa yeye, yaani Mikaya mwana wa Imla; lakini namchukia; kwa sababu hanibashirii mema, ila mabaya. Yehoshafati akasema, La! Mfalme asiseme hivi. Ndipo mfalme wa Israeli akamwita akida, akamwambia, mlete hima Mikaya mwana wa Imla. Basi mfalme wa Israeli na Yehoshafati mfalme wa Yuda walikuwa wakikaa kila mtu katika kiti chake cha enzi, wamevaa mavazi yao, katika sakafu langoni pa Samaria; na manabii wote wakafanya unabii mbele yao. Na Zedekia mwana wa Kenaana akajifanyia pembe za chuma, akasema, BWANA asema hivi, Kwa hizo utawasukuma Washami, hata waharibike. Na manabii wote wakasema hivyo kwa unabii, wakisema, Kwea Ramoth-Gileadi, ukafanikiwe; kwa kuwa BWANA atautia mkononi mwa mfalme. Na yule mjumbe, aliyekwenda kumwita Mikaya, akamwambia, akasema, Angalia sasa, maneno ya manabii kwa kinywa kimoja husema mema kwa mfalme; neno lako na liwe, nakusihi, kama neno la mmojawapo wao, ukaseme mema. Mikaya akasema, Kama BWANA aishivyo, neno lile BWANA aniambialo, ndilo nitakalolinena. Na alipokuja kwa mfalme, mfalme alimwambia, Je! Mikaya, tuende Ramoth-Gileadi kupiga vita, au tunyamaze? Akamwambia, Kwea, ufanikiwe; kwa kuwa BWANA atautia mkononi mwa mfalme. Mfalme akamwambia, Mara ngapi nikuapishe usiniambie neno ila yaliyo kweli, kwa jina la BWANA? Akasema, Naliwaona Waisraeli wote wametawanyika milimani, kama kondoo wasio na mchungaji. BWANA akasema, Hawa hawana bwana; na warudi kila mtu nyumbani kwake kwa amani. Mfalme wa Israeli akamwambia Yehoshafati, Je! Sikukuambia, hatanibashiria mema, ila mabaya?
1 Wafalme 22:1-18 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Kwa miaka mitatu hapakuwa na vita kati ya Aramu na Israeli. Lakini katika mwaka wa tatu, Yehoshafati mfalme wa Yuda akateremka kwenda kumwona mfalme wa Israeli. Mfalme wa Israeli alikuwa amewaambia maafisa wake, “Je, hamjui Ramoth-Gileadi ni mali yetu, na bado hatufanyi chochote kuirudisha kwetu kutoka kwa mfalme wa Aramu?” Kwa hiyo akamuuliza Yehoshafati, “Je, utaenda pamoja nami kupigana dhidi ya Ramoth-Gileadi?” Yehoshafati akamjibu mfalme wa Israeli, “Mimi ni kama wewe, watu wangu ni kama watu wako, farasi wangu ni kama farasi wako.” Lakini Yehoshafati pia akamwambia mfalme wa Israeli, “Kwanza tafuta ushauri wa BWANA.” Kwa hiyo mfalme wa Israeli akawaleta pamoja manabii, wanaume wapatao mia nne, akawauliza, “Je, niende vitani dhidi ya Ramoth-Gileadi, au niache?” Wakajibu, “Naam, nenda, kwa kuwa Bwana ataiweka Ramoth-Gileadi mkononi mwa mfalme.” Lakini Yehoshafati akauliza, “Je, hayuko nabii wa BWANA hapa ambaye tunaweza kumuuliza?” Mfalme wa Israeli akamjibu Yehoshafati, “Bado yupo mtu mmoja ambaye kupitia kwake twaweza kuuliza ushauri wa BWANA, lakini namchukia kwa sababu hatabiri jambo lolote jema kunihusu, ila hunitabiria mabaya kila mara. Yeye ni Mikaya mwana wa Imla.” Yehoshafati akajibu, “Mfalme hapaswi kusema hivyo.” Kwa hiyo mfalme wa Israeli akamwita mmoja wa maafisa wake na kusema, “Mlete Mikaya mwana wa Imla mara moja.” Wakiwa wamevalia majoho yao ya kifalme, mfalme wa Israeli na Yehoshafati mfalme wa Yuda walikuwa wameketi juu ya viti vyao vya kifalme katika sakafu ya kupuria, kwenye ingilio la lango la Samaria, huku manabii wote wakitabiri mbele yao. Wakati huu Sedekia mwana wa Kenaana alikuwa ametengeneza pembe za chuma. Naye akatangaza, “Hivi ndivyo asemavyo BWANA, ‘Kwa hizi pembe utawapiga Waaramu hadi waangamizwe.’ ” Manabii wengine wote walikuwa wanatabiri kitu hicho hicho wakisema, “Ishambulie Ramoth-Gileadi na uwe mshindi. Kwa kuwa BWANA ataitia mkononi mwa mfalme.” Mjumbe aliyekuwa ameenda kumwita Mikaya akamwambia, “Tazama, manabii wote kama mtu mmoja wanatabiri ushindi kwa mfalme. Neno lako na likubaliane na lao, nawe unene mema kuhusu mfalme.” Lakini Mikaya akasema, “Hakika kama BWANA aishivyo, nitamwambia kile tu BWANA atakachoniambia.” Alipofika, mfalme akamuuliza, “Mikaya, je, twende vitani dhidi ya Ramoth-Gileadi au niache?” Akamjibu, “Shambulia na ushinde, kwa kuwa BWANA atawatia mkononi mwa mfalme.” Mfalme akamwambia, “Je, ni mara ngapi nitakuapisha ili usiniambie kitu chochote ila kweli tu kwa jina la BWANA?” Ndipo Mikaya akajibu, “Niliona Israeli wote wametawanyika vilimani kama kondoo wasio na mchungaji, naye BWANA akasema, ‘Watu hawa hawana kiongozi. Mwache kila mmoja aende nyumbani kwa amani.’ ” Mfalme wa Israeli akamwambia Yehoshafati, “Sikukuambia kwamba huwa hatabiri jambo lolote jema kunihusu, ila mabaya tu?”