Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Wafalme 21:1-29

1 Wafalme 21:1-29 Biblia Habari Njema (BHN)

Nabothi, mwenyeji wa Yezreeli, alikuwa na shamba lake la mizabibu huko Yezreeli, karibu na ikulu ya Ahabu, mfalme wa Samaria. Basi, siku moja, Ahabu akamwambia Nabothi, “Nipe shamba lako la mizabibu nilifanye shamba la mboga, kwa sababu liko karibu na nyumba yangu. Nitakupa shamba lingine zuri zaidi, au ukitaka, nitakulipa thamani yake, fedha taslimu.” Lakini, Nabothi akamjibu, “Jambo la kukupa wewe urithi nilioupata kwa wazee wangu, Mwenyezi-Mungu na apishe mbali.” Hapo, Ahabu akaenda zake nyumbani amejaa chuki na huzuni nyingi, kwa sababu Nabothi, mwenyeji wa Yezreeli, alimwambia kwamba hatampa kile alichorithi kutoka kwa wazee wake. Basi, akajilaza kitandani, akauficha uso wake na kususia chakula. Yezebeli, mkewe, akamwendea na kumwuliza, “Mbona umejaa huzuni moyoni hata kula huli?” Naye akamwambia, “Kwa sababu nilizungumza na Nabothi, mwenyeji wa Yezreeli, nikamtaka aniuzie shamba lake la mizabibu, ama akipenda nimpe shamba lingine badala ya hilo. Lakini yeye akaniambia, ‘Sitakupa shamba langu la mizabibu.’” Hapo, Yezebeli, mkewe, akamwambia, “Anayetawala Israeli ni nani? Si ni wewe? Amka, ule na uchangamke; mimi binafsi nitakupa shamba la mizabibu la Nabothi, Myezreeli.” Basi, Yezebeli akaandika barua kadha kwa jina la Ahabu na kuzipiga mhuri wa mfalme. Kisha akapeleka barua hizo kwa wazee na watu mashuhuri walioishi na Nabothi huko mjini. Barua zenyewe ziliandikwa hivi: “Pigeni mbiu ya mfungo, mkutane na kumpa Nabothi mahali pa heshima kati ya watu. Kisha, tafuteni walaghai wawili wamkabili na kumshtaki wakisema: ‘Wewe umemwapiza Mungu na mfalme.’ Kisha mtoeni nje, mkamuue kwa kumpiga mawe!” Basi, wakazi wenzake Nabothi, wazee na watu mashuhuri wa mji wa Yezreeli, wakafanya kama Yezebeli alivyowaagiza. Kwa mujibu wa barua aliyowapelekea, wakapiga mbiu ya mfungo, wakakutana na kumweka Nabothi mahali pa heshima kati ya watu. Wale walaghai wawili wakaketi kumkabili Nabothi, kisha wakamshtaki hadharani wakisema, “Nabothi amemwapiza Mungu na mfalme.” Basi, Nabothi akatolewa nje ya mji, akauawa kwa kupigwa mawe. Kisha, Yezebeli akapelekewa habari kwamba Nabothi amekwisha uawa kwa kupigwa mawe. Mara tu Yezebeli alipopata habari kwamba Nabothi amekwisha uawa kwa kupigwa mawe, akamwambia Ahabu, “Inuka! Nenda ukamiliki lile shamba la mizabibu la Nabothi, Myezreeli, ambalo alikataa kukuuzia. Nabothi hayuko hai tena; amekwisha fariki.” Mara tu Ahabu aliposikia Nabothi amekwisha fariki, aliinuka kwenda kulimiliki shamba la mizabibu la Nabothi. Basi, neno la Mwenyezi-Mungu likamjia nabii Elia wa Tishbe: “Inuka uende kukutana na Ahabu mfalme wa Israeli, ambaye yuko Samaria. Utamkuta katika shamba la mizabibu la Nabothi, akilimiliki. Mwambie, Mwenyezi-Mungu asema hivi: ‘Umeua na kumiliki pia?’ Mwambie Mwenyezi-Mungu asema hivi: ‘Mahali pale mbwa walipoiramba damu ya Nabothi, ndipo watakapoilamba damu yako.’” Basi, Ahabu alipomwona Elia, akasema, “Ewe adui yangu, umenifuma?” Elia akamjibu, “Naam! Nimekufuma, kwa sababu wewe umenuia kabisa kutenda maovu mbele ya Mwenyezi-Mungu. Haya! Mwenyezi-Mungu asema hivi: ‘Hakika, nitakuletea maangamizi. Nitakuzoa wewe na kufutilia mbali kila mwanamume wa ukoo wako katika Israeli, awe mtumwa au huru. Jamaa yako nitaifanya kama jamaa ya Yeroboamu, mwana wa Nebati, na kama jamaa ya Baasha mwana wa Ahiya, kwa sababu umeiwasha hasira yangu na kuwafanya watu wa Israeli watende dhambi.’ Tena, Mwenyezi-Mungu asema hivi juu ya Yezebeli: ‘Mbwa wataula mwili wa Yezebeli humuhumu mjini Yezreeli. Naam, yeyote wa jamaa yake atakayefia mjini, mbwa watamla; na yeyote atakayefia shambani, ndege wa angani watamla.’” (Hakuna mtu aliyenuia kutenda maovu mbele ya Mwenyezi-Mungu kama Ahabu, ambaye alishawishiwa na Yezebeli, mkewe. Alitenda machukizo kwa kuabudu sanamu za miungu kama walivyofanya Waamori ambao hapo awali Mwenyezi-Mungu aliwafukuza mbele ya watu wa Israeli). Lakini, Ahabu aliposikia maneno hayo, alirarua nguo zake, akajivalia gunia peke yake, akafunga, akawa analala na gunia, na kwenda huko na huko kwa huzuni. Basi, ujumbe huu wa Mwenyezi-Mungu ukamjia Elia wa Tishbe: “Umeona jinsi Ahabu alivyojinyenyekesha mbele yangu? Basi, kwa kuwa amejinyenyekesha, sitaleta yale maangamizi akiwa hai, lakini nyakati za utawala wa mwanawe nitaiangamiza jamaa yake Ahabu.”

1 Wafalme 21:1-29 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Ikawa baada ya hayo, Nabothi Myezreeli alikuwa na shamba la mizabibu katika Yezreeli, karibu na nyumba ya kifalme ya Ahabu mfalme wa Samaria. Ahabu akasema na Nabothi, akamwambia, Nipe shamba lako la mizabibu nilifanye shamba la mboga, maana ni karibu na nyumba yangu; nami nitakupa badala yake shamba la mizabibu lililo zuri zaidi; au ukipenda, nitakupa fedha sawasawa na thamani yake. Nabothi akamwambia Ahabu, BWANA apishe mbali nikupe wewe urithi wa baba zangu. Basi Ahabu akaenda nyumbani kwake, ana moyo mzito, tena amekasirika, kwa sababu ya neno lile aliloambiwa na Nabothi Myezreeli, akisema, Sitakupa urithi wa baba zangu. Akajilaza kitandani pake, akageuza uso wake, akakataa kula. Lakini Yezebeli mkewe akamwendea, akamwambia, Kwa nini roho yako ina huzuni hata usile chakula? Akamwambia, Kwa sababu nimesema na Nabothi Myezreeli, nikamwambia, Unipe shamba lako la mizabibu kwa fedha, au, ukipenda, nitakupa shamba la mizabibu lingine badala yake. Akajibu, Sitakupa shamba langu la mizabibu. Yezebeli mkewe akamwambia, Je! Sasa wewe unaumiliki ufalme wa Israeli? Ondoka, ule chakula, moyo wako ufurahi; mimi nitakupa shamba la mizabibu la Nabothi Myezreeli. Basi, akaandika nyaraka kwa jina la Ahabu, akazitia mhuri wake, akazipeleka zile nyaraka kwa wazee, na kwa watu wenye nguvu waliokuwa katika mji wake, waliokaa pamoja na Nabothi. Akaandika katika zile nyaraka, akasema, Pigeni mbiu ya watu kufunga, mkamketishe Nabothi juu mbele ya watu, mkawaketishe watu wawili, watu walaghai, ili wamshitaki, na kumshuhudia, kunena, Umemtukana Mungu na mfalme. Kisha mchukueni nje, mkampige kwa mawe, ili afe. Wale wazee wa mji wake, na walio wenye nguvu waliokaa mjini mwake, wakafanya kama Yezebeli alivyowaagiza, kama ilivyoandikwa katika nyaraka alizowapelekea. Wakapiga mbiu ya watu kufunga, wakamweka Nabothi juu mbele ya watu. Na hao watu wawili, watu wasiofaa, wakaingia, wakaketi mbele yake; wale watu wasiofaa wakamshuhudia Nabothi mbele ya watu, wakasema, Nabothi amemtukana Mungu na mfalme. Ndipo wakamchukua nje ya mji, wakampiga kwa mawe hata akafa. Wakampelekea Yezebeli habari, wakasema, Nabothi amepigwa kwa mawe, amekufa. Ikawa Yezebeli aliposikia ya kwamba Nabothi amepigwa kwa mawe na kufa, Yezebeli akamwambia Ahabu, Inuka, ulitamalaki shamba la mizabibu la Nabothi Myezreeli, alilokataa kukupa kwa fedha, maana Nabothi hayuko hai, lakini amekufa. Ikawa Ahabu aliposikia ya kwamba Nabothi amekufa, akaondoka, aliteremkie shamba la mizabibu la Nabothi Myezreeli, ili alitamalaki. Neno la BWANA likamjia Eliya Mtishbi, kusema, Ondoka, ushuke, ukutane na Ahabu mfalme wa Israeli, akaaye katika Samaria; yuko katika shamba la mizabibu la Nabothi, ndiko alikoshukia ili alitamalaki. Ukamwambie, ukisema, BWANA asema hivi, Je! Umeua, ukatamalaki? Nawe utamwambia, kusema, BWANA asema hivi, Mahali pale mbwa walipoiramba damu ya Nabothi, mbwa watairamba na damu yako, naam, damu yako. Ahabu akamwambia Eliya, Je! Umenipata, ewe adui yangu? Akamwambia, Nimekupata, kwa sababu umejiuza utende yaliyo mabaya machoni pa BWANA. Angalia, nitaleta mabaya juu yako; nami nitakuangamiza kabisa, nitamkatia Ahabu kila mwanamume, aliyefungwa na aliyeachwa katika Israeli. Kisha nitaifanya nyumba yako iwe kama nyumba ya Yeroboamu mwana wa Nebati, na kama nyumba ya Baasha mwana wa Ahiya, kwa ajili ya chukizo ulilonichukiza, hata kunighadhibisha, ukawakosesha Israeli. Tena BWANA alinena habari za Yezebeli, akisema, Mbwa watamla Yezebeli katika kiwanja cha Yezreeli. Mtu wa nyumba ya Ahabu afaye mjini, mbwa watamla, na yeye afaye mashambani ndege wa angani watamla. (Lakini hapakuwa na mtu kama Ahabu, aliyejiuza atende maovu machoni pa BWANA ambaye Yezebeli mkewe alimchochea. Akachukiza mno, kwa kuzifuata sanamu sawasawa na yote waliyoyafanya Waamori, BWANA aliowafukuza mbele ya wana wa Israeli.) Ikawa, Ahabu alipoyasikia maneno hayo, akayararua mavazi yake, akavaa magunia mwilini mwake, akafunga, akajilaza juu ya magunia, akaenda kwa upole. Neno la BWANA likaja kwa Eliya Mtishbi, kusema, Huoni jinsi Ahabu alivyojidhili mbele yangu? Basi kwa sababu amejidhili mbele yangu, sitayaleta yale mabaya katika siku zake; ila katika siku za mwanawe nitayaleta mabaya hayo juu ya nyumba yake.

1 Wafalme 21:1-29 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Ikawa baada ya hayo, Nabothi Myezreeli alikuwa na shamba la mizabibu katika Yezreeli, karibu na nyumba ya kifalme ya Ahabu mfalme wa Samaria. Ahabu akasema na Nabothi, akamwambia, Nipe shamba lako la mizabibu nilifanye shamba la mboga, maana ni karibu na nyumba yangu; nami nitakupa badala yake shamba la mizabibu lililo zuri zaidi; au ukipenda, nitakupa fedha sawasawa na thamani yake. Nabothi akamwambia Ahabu, BWANA apishe mbali nikupe wewe urithi wa baba zangu. Basi Ahabu akaenda nyumbani kwake, ana moyo mzito, tena amekasirika, kwa sababu ya neno lile aliloambiwa na Nabothi Myezreeli, akisema, Sitakupa urithi wa baba zangu. Akajilaza kitandani pake, akageuza uso wake, akakataa kula. Lakini Yezebeli mkewe akamwendea, akamwambia, Kwa nini roho yako ina huzuni hata usile chakula? Akamwambia, Kwa sababu nimesema na Nabothi Myezreeli, nikamwambia, Unipe shamba lako la mizabibu kwa fedha, au, ukipenda, nitakupa shamba la mizabibu lingine badala yake. Akajibu, Sitakupa shamba langu la mizabibu. Yezebeli mkewe akamwambia, Je! Sasa wewe unaumiliki ufalme wa Israeli? Ondoka, ule chakula, moyo wako ufurahi; mimi nitakupa shamba la mizabibu la Nabothi Myezreeli. Basi, akaandika nyaraka kwa jina la Ahabu, akazitia muhuri yake, akazipeleka zile nyaraka kwa wazee, na kwa watu wenye nguvu waliokuwa katika mji wake, waliokaa pamoja na Nabothi. Akaandika katika zile nyaraka, akasema, Pigeni mbiu ya watu kufunga, mkamweke Nabothi juu mbele ya watu, mkainue watu wawili, watu wasiofaa, ili wamshitaki, na kumshuhudia, kunena, Umemtukana Mungu na mfalme. Kisha mchukueni nje, mkampige kwa mawe, ili afe. Wale wazee wa mji wake, na walio wenye nguvu waliokaa mjini mwake, wakafanya kama Yezebeli alivyowaagiza, kama ilivyoandikwa katika nyaraka alizowapelekea. Wakapiga mbiu ya watu kufunga, wakamweka Nabothi juu mbele ya watu. Na hao watu wawili, watu wasiofaa, wakaingia, wakaketi mbele yake; wale watu wasiofaa wakamshuhudia Nabothi mbele ya watu, wakasema, Nabothi amemtukana Mungu na mfalme. Ndipo wakamchukua nje ya mji, wakampiga kwa mawe hata akafa. Wakampelekea Yezebeli habari, wakasema, Nabothi amepigwa kwa mawe, amekufa. Ikawa Yezebeli aliposikia ya kwamba Nabothi amepigwa kwa mawe na kufa, Yezebeli akamwambia Ahabu, Inuka, ulitamalaki shamba la mizabibu la Nabothi Myezreeli, alilokataa kukupa kwa fedha, maana Nabothi hako hai, lakini amekufa. Ikawa Ahabu aliposikia ya kwamba Nabothi amekufa, akaondoka, alitelemkie shamba la mizabibu la Nabothi Myezreeli, ili alitamalaki. Neno la BWANA likamjia Eliya Mtishbi, kusema, Ondoka, ushuke, ukutane na Ahabu mfalme wa Israeli, akaaye katika Samaria; yuko katika shamba la mizabibu la Nabothi, ndiko alikoshukia ili alitamalaki. Ukamwambie, ukisema, BWANA asema hivi, Je! Umeua, ukatamalaki? Nawe utamwambia, kusema, BWANA asema hivi, Mahali pale mbwa walipoiramba damu ya Nabothi, mbwa watairamba na damu yako, naam, damu yako. Ahabu akamwambia Eliya, Je! Umenipata, ewe adui yangu? Akamwambia, Nimekupata, kwa sababu umejiuza utende yaliyo mabaya machoni pa BWANA. Angalia, nitaleta mabaya juu yako; nami nitakuangamiza kabisa, nitamkatia Ahabu kila mume, aliyefungwa na aliyeachwa katika Israeli. Kisha nitaifanya nyumba yako iwe kama nyumba ya Yeroboamu mwana wa Nebati, na kama nyumba ya Baasha mwana wa Ahiya, kwa ajili ya chukizo ulilonichukiza, hata kunighadhibisha, ukawakosesha Israeli. Tena BWANA alinena habari za Yezebeli, akisema, Mbwa watamla Yezebeli katika kiwanja cha Yezreeli. Mtu wa nyumba ya Ahabu afaye mjini, mbwa watamla, na yeye afaye mashambani ndege wa angani watamla. (Lakini hapakuwa na mtu kama Ahabu, aliyejiuza atende maovu machoni pa BWANA ambaye Yezebeli mkewe alimchochea. Akachukiza mno, kwa kuzifuata sanamu sawasawa na yote waliyoyafanya Waamori, BWANA aliowafukuza mbele ya wana wa Israeli.) Ikawa, Ahabu alipoyasikia maneno hayo, akayararua mavazi yake, akavaa magunia mwilini mwake, akafunga, akajilaza juu ya magunia, akaenda kwa upole. Neno la BWANA likaja kwa Eliya Mtishbi, kusema, Huoni jinsi Ahabu alivyojidhili mbele yangu? Basi kwa sababu amejidhili mbele yangu, sitayaleta yale mabaya katika siku zake; ila katika siku za mwanawe nitayaleta mabaya hayo juu ya nyumba yake.

1 Wafalme 21:1-29 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

Baada ya hayo, pakawa na tukio lililohusisha shamba la mizabibu la Nabothi Myezreeli. Shamba hilo lilikuwa Yezreeli, karibu na jumba la kifalme la Ahabu, mfalme wa Samaria. Ahabu akamwambia Nabothi, “Nipe shamba lako la mizabibu liwe langu, nilime bustani ya mboga kwa kuwa liko karibu na jumba langu. Nitakupa shamba jingine la mizabibu lililo zuri zaidi, au kama utapenda, nitakulipa kulingana na thamani ya shamba lako.” Lakini Nabothi akamjibu, “BWANA na apishe mbali kukupa wewe urithi wa baba zangu.” Basi Ahabu akaenda nyumbani kwa uchungu na hasira kwa sababu Nabothi Myezreeli alikuwa amemwambia, “Sitakupa urithi wa baba zangu.” Akajinyoosha juu ya kitanda akisononeka, na akakataa kula. Yezebeli mke wake akaingia na akamuuliza, “Kwa nini unahuzunika hivi? Kwa nini huli chakula?” Akamjibu, “Kwa sababu nilimwambia Nabothi Myezreeli, ‘Niuzie shamba lako la mizabibu, au ukipenda, nitakupa shamba jingine la mizabibu badala yake.’ Lakini akasema, ‘Sitakupa shamba langu la mizabibu.’ ” Yezebeli mke wake akamuuliza, “Hivi ndivyo unavyofanya, nawe ni mfalme wa Israeli yote? Inuka na ule! Changamka. Nitakupa shamba la mizabibu la Nabothi Myezreeli.” Kwa hiyo akaandika barua kwa jina la Ahabu, akaweka muhuri wa Ahabu juu ya hizo barua; kisha akazituma kwa wazee na kwa watu wenye vyeo walioishi na Nabothi katika mji wake. Katika barua hizo aliandika: “Tangazeni siku ya watu kufunga, na mkamketishe Nabothi mbele ya watu. Waketisheni walaghai wawili mkabala naye, nao washuhudie dhidi yake kuwa amemlaani Mungu na mfalme pia. Kisha mtoeni nje na kumpiga kwa mawe hadi afe.” Hivyo wazee na watu wenye vyeo walioishi katika mji wa Nabothi wakafanya kama Yezebeli alivyoelekeza katika barua alizowaandikia. Wakatangaza mfungo na kumketisha Nabothi mbele ya watu. Kisha walaghai wawili wakaja wakaketi mkabala naye; nao wakaleta mashtaka dhidi ya Nabothi mbele ya watu, wakisema, “Nabothi amemlaani Mungu na mfalme pia.” Kwa hiyo wakamtoa nje na kumpiga kwa mawe hadi akafa. Kisha wakatuma ujumbe kwa Yezebeli, kusema, “Nabothi amepigwa mawe na amekufa.” Mara tu Yezebeli aliposikia kwamba Nabothi amepigwa mawe na amekufa, akamwambia Ahabu, “Amka na umiliki lile shamba la mizabibu la Nabothi Myezreeli, ambalo alikataa kukuuzia. Hayuko hai tena, bali amekufa.” Ahabu aliposikia Nabothi amekufa, akainuka, kisha akashuka kwenda kulimiliki shamba la mizabibu la Nabothi. Kisha neno la BWANA likamjia Eliya Mtishbi, kusema: “Shuka ukakutane na Ahabu mfalme wa Israeli, anayetawala Samaria. Sasa yuko katika shamba la mizabibu la Nabothi, ambalo ameenda kulimiliki. Umwambie, ‘Hivi ndivyo asemavyo BWANA: Je, hujamuua mtu na kuitwaa mali yake?’ Kisha umwambie, ‘Hivi ndivyo asemavyo BWANA: Mahali mbwa walipoiramba damu ya Nabothi, mbwa watairamba damu yako pia; naam, yako wewe!’ ” Ahabu akamwambia Eliya, “Kwa hiyo umenipata, wewe adui yangu!” Akajibu, “Ndiyo, nimekupata. Kwa sababu umejiuza mwenyewe kwa kufanya uovu mbele za macho ya BWANA. ‘Nitaleta maafa juu yako. Nitaangamiza uzao wako na kukatilia mbali kila mwanaume wa jamaa ya Ahabu katika Israeli, awe mtumwa au mtu huru. Nitaifanya nyumba yako kuwa kama ile ya Yeroboamu mwana wa Nebati, na kama ya Baasha mwana wa Ahiya, kwa sababu umenighadhibisha kwa kusababisha Israeli kutenda dhambi.’ “Pia BWANA anasema kumhusu Yezebeli: ‘Mbwa watamla Yezebeli karibu na ukuta wa Yezreeli.’ “Mbwa watawala wale wa nyumba ya Ahabu watakaofia mjini, nao wale watakaofia mashambani wataliwa na ndege wa angani.” (Hapajapata kamwe kuwa na mtu kama Ahabu, aliyejiuza mwenyewe kutenda uovu machoni pa BWANA, akiwa anachochewa na Yezebeli mkewe. Alitenda uovu sana kwa kuzifuata sanamu, kama Waamori ambao BWANA aliowafukuza mbele ya Israeli.) Ahabu aliposikia maneno haya, akararua nguo zake, akavaa gunia na kufunga. Akalala na kujifunika gunia na kwenda kwa unyenyekevu. Ndipo neno la BWANA lilipomjia Eliya Mtishbi kusema, “Umeona jinsi Ahabu alivyojinyenyekeza mbele zangu? Kwa kuwa amejishusha mwenyewe, sitaleta maafa haya wakati akiwa hai, lakini nitayaleta juu ya nyumba yake katika siku za mwanawe.”