1 Wafalme 16:1-34
1 Wafalme 16:1-34 Biblia Habari Njema (BHN)
Neno la Mwenyezi-Mungu lilimjia Yehu mwana wa Hanani, dhidi ya Baasha: “Wewe Baasha, mimi nilikuinua kutoka mavumbini, nikakufanya kiongozi wa watu wangu Israeli. Wewe umemwiga Yeroboamu, ukawafanya watu wangu Israeli watende dhambi na kunikasirisha kwa dhambi zao. Haya! Sasa, nitakufutilia mbali wewe na jamaa yako; nitaitendea jamaa yako kama nilivyoitendea jamaa ya Yeroboamu mwana wa Nebati. Yeyote wa jamaa yako atakayefia mjini, mbwa watamla; na yeyote atakayefia shambani, ndege wa angani watamla.” Matendo mengine ya Baasha na ushujaa wake, yote yameandikwa katika Kitabu cha Mambo ya Nyakati ya Wafalme wa Israeli. Hatimaye, Baasha alifariki, akazikwa huko Tirza; mwanawe Ela akatawala mahali pake. Tena neno la Mwenyezi-Mungu dhidi ya Baasha na jamaa yake, lilimjia Yehu mwanawe Hanani kwa sababu ya maovu aliyotenda mbele ya Mwenyezi-Mungu. Baasha alimkasirisha Mwenyezi-Mungu kwa matendo yake; alimwiga Yeroboamu na jamaa yake na kuiletea jamaa yake maangamizi. Mnamo mwaka wa ishirini na sita wa utawala wa Asa mfalme wa Yuda, Ela mwana wa Baasha, alianza kutawala huko Israeli kutoka Tirza. Alitawala kwa muda wa miaka miwili. Mtumishi wake Zimri ambaye alisimamia nusu ya kikosi cha magari yake ya kukokotwa, alikula njama juu yake. Siku moja, mfalme Ela alipokuwa huko Tirza nyumbani kwa Arsa aliyekuwa msimamizi wa ikulu, alikunywa, akalewa. Basi, Zimri akaingia ndani, akamuua. Kisha akatawala mahali pake. Huu ulikuwa mwaka wa ishirini na saba wa utawala wa Asa mfalme wa Yuda. Mara tu alipoanza kutawala, Zimri aliwaua watu wote wa jamaa ya Baasha; hakumwachia hata mwanamume mmoja wa jamaa yake wala wa rafiki zake; ikawa kama alivyosema Mwenyezi-Mungu dhidi ya Baasha, kwa njia ya nabii Yehu. Mambo haya yalifanyika kwa sababu ya dhambi alizotenda Baasha na mwanawe Ela. Walimkasirisha Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, kwa kutenda dhambi na kuwafanya watu wa Israeli watende dhambi kwa sanamu za miungu yao. Matendo mengine ya Ela, yote yameandikwa katika Kitabu cha Mambo ya Nyakati ya Wafalme wa Israeli. Zimri alitawala huko Israeli kutoka Tirza kwa muda wa siku saba. Huo ulikuwa mwaka wa ishirini na saba wa utawala wa Asa mfalme wa Yuda. Basi, watu wa Israeli walikuwa wamepiga kambi kuuzingira mji wa Gibethoni wa Wafilisti, na majeshi ya watu wa Israeli waliposikia kwamba Zimri alikuwa amekula njama, akamuua mfalme, wote wakamtawaza Omri, amiri jeshi wao, kuwa mfalme wa Israeli siku hiyohiyo. Omri na majeshi yake akaondoka Gibethoni, akaenda na kuuzingira mji wa Tirza. Zimri alipoona kwamba mji umezingirwa, aliingia ngomeni, ndani ya ikulu, akaichoma moto, naye akafia humo. Jambo hilo lilifanyika kwa sababu ya dhambi alizotenda alifanya maovu mbele ya Mwenyezi-Mungu, akamwiga Yeroboamu na kuwafanya watu wa Israeli watende dhambi. Matendo mengine ya Zimri na njama aliyokula, yote yameandikwa katika Kitabu cha Mambo ya Nyakati ya Wafalme wa Israeli. Watu wa Israeli, sasa, waligawanyika makundi mawili: Kundi moja lilimtambua Tibni mwana wa Ginathi kuwa mfalme, na kundi la pili lilimtambua Omri. Hatimaye watu wa kundi lililomtambua Omri, wakawazidi nguvu wale waliomtambua Tibni mwanawe Ginathi; Tibni akafa na Omri akawa mfalme. Omri alianza kutawala mnamo mwaka wa thelathini na mmoja wa utawala wa Asa mfalme wa Yuda. Alitawala kwa muda wa miaka kumi na miwili; miaka sita alikuwa anatawala kutoka mjini Tirza. Alinunua mlima wa Samaria kwa vipande 6,000 vya fedha kutoka kwa mtu mmoja aitwaye Shemeri, akajenga ngome juu yake, na mji. Mji wenyewe akauita Samaria, kwa heshima ya Shemeri aliyeumiliki mlima huo hapo awali. Omri alitenda maovu mbele ya Mwenyezi-Mungu; alifanya maovu zaidi ya wale wote waliomtangulia. Kwa sababu alimwiga Yeroboamu mwana wa Nebati, akamkasirisha Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, kwa kuwafanya watu wa Israeli watende dhambi kwa kuabudu sanamu za miungu. Matendo mengine ya Omri na ushujaa wake, yote yameandikwa katika Kitabu cha Mambo ya Nyakati ya Wafalme wa Israeli. Hatimaye, Omri alifariki, akazikwa huko Samaria; mwanawe Ahabu akatawala mahali pake. Mnamo mwaka wa thelathini na nane wa utawala wa Asa mfalme wa Yuda, Ahabu mwana wa Omri, alianza kutawala Israeli. Alitawala huko Samaria kwa muda wa miaka ishirini na miwili. Ahabu alitenda maovu mbele ya Mwenyezi-Mungu kuliko wafalme wote waliomtangulia. Tena, licha ya kuiga mwenendo mbaya wa Yeroboamu mwana wa Nebati, Ahabu alimwoa Yezebeli binti Ethbaali, mfalme wa Wasidoni; akamtumikia na kumwabudu Baali. Alimjengea Baali hekalu huko Samaria, na ndani yake akatengeneza madhabahu ya kumtambikia. Hali kadhalika, alitengeneza sanamu ya Ashera mungu wa kike. Ahabu alitenda maovu mengi, akamkasirisha Mwenyezi-Mungu Mungu wa Israeli zaidi ya wafalme wote wa Israeli waliomtangulia. Wakati wa utawala wake, Hieli kutoka Betheli, aliujenga upya mji wa Yeriko. Na sawa kabisa na neno la Mwenyezi-Mungu alilonena kwa njia ya Yoshua mwana wa Nuni, Hieli alifiwa na mzaliwa wake wa kwanza Abiramu, wakati wa kuiweka misingi ya Yeriko, akafiwa pia na mwanawe mdogo Segubu, wakati wa kuyaweka malango yake.
1 Wafalme 16:1-34 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ndipo neno la BWANA likamjia Yehu mwana wa Hanani juu ya Baasha, kusema, Kwa kuwa mimi nilikuinua kutoka katika mavumbi, na kukufanya uwe mkuu juu ya watu wangu Israeli; nawe umeiendea njia ya Yeroboamu, na kuwakosesha watu wangu Israeli, hata wanighadhibishe kwa makosa yao; angalia, kuondoa nitawaondoa Baasha na jamaa yake; tena nitaifanya nyumba yako iwe kama nyumba ya Yeroboamu mwana wa Nebati. Mtu amfiaye Baasha mjini mbwa watamla; naye amfiaye mashambani ndege wa angani watamla. Basi, mambo yote ya Baasha yaliyosalia, na aliyoyafanya, na nguvu zake, je! Hayakuandikwa katika Kitabu cha Kumbukumbu za Wafalme wa Israeli? Baasha akalala na babaze, akazikwa katika Tirza; naye Ela mwanawe akatawala mahali pake. Tena neno la BWANA likaja kwa mkono wa nabii Yehu mwana wa Hanani juu ya Baasha, na juu ya nyumba yake, kwa sababu ya mabaya yote aliyoyatenda machoni pa BWANA, akimghadhibisha kwa kazi ya mikono yake, kwa kufanana na nyumba ya Yeroboamu, na kwa sababu aliiharibu. Katika mwaka wa ishirini na sita wa Asa mfalme wa Yuda, Ela mwana wa Baasha alianza kutawala juu ya Israeli huko Tirza, akatawala miaka miwili. Na mtumwa wake Zimri, jemadari wa nusu ya magari yake, akamlia njama; alipokuwako Tirza akinywa hata kulewa nyumbani mwa Arsa, aliyekuwa juu ya nyumba huko Tirza; Zimri akaingia akampiga, akamwua, katika mwaka wa ishirini na saba wa Asa mfalme wa Yuda, akatawala mahali pake. Ikawa, alipoanza kutawala, mara alipoketi juu ya kiti chake cha enzi, akawaua nyumba yote ya Baasha; hakumwachia mwanamume yeyote, wa jamaa zake, wala wa rafiki zake. Hivyo Zimri akaiharibu nyumba yote ya Baasha, sawasawa na neno la BWANA, alilolinena juu ya Baasha kwa Yehu nabii, kwa sababu ya makosa yake Baasha, na makosa yote ya Ela mwanawe, waliyoyakosa, na kuwakosesha Israeli, wakimghadhibisha BWANA, Mungu wa Israeli, kwa matendo yao ya ubatili. Na mambo yote ya Ela yaliyosalia, na yote aliyoyafanya, je! Hayakuandikwa katika Kitabu cha Kumbukumbu za Wafalme wa Israeli? Katika mwaka wa ishirini na saba wa Asa mfalme wa Yuda, Zimri akatawala muda wa siku saba huko Tirza. Basi, watu walikuwa wametua kambini kupigana na Gibethoni, ulio wa Wafilisti. Na hao watu waliokuwako kambini wakasikia habari ya kwamba Zimri amekula njama, tena amemwua mfalme; kwa hiyo Israeli wote wakamfanya Omri, jemadari wa jeshi, awe mfalme juu ya Israeli siku ile kambini. Omri akapanda kutoka Gibethoni, na Israeli wote pamoja naye, wakauhusuru Tirza. Ikawa Zimri alipoona ya kuwa mji umetwaliwa, akaingia ngomeni mwa nyumba ya mfalme, akaiteketeza nyumba ya mfalme juu yake kwa moto, akafa; kwa sababu ya makosa aliyoyakosa, akifanya mabaya machoni pa BWANA, kwa kuiendea njia ya Yeroboamu na makosa yake aliyoyafanya akiwakosesha Israeli. Na mambo yote ya Zimri yaliyosalia na fitina yake aliyoifanya, je! Hayakuandikwa katika Kitabu cha Kumbukumbu za Wafalme wa Israeli? Ndipo watu wa Israeli wakagawanywa sehemu mbili; nusu ya watu wakamfuata Tibni mwana wa Ginathi, ili wamfanye mfalme; nusu wakamfuata Omri. Lakini hao watu waliomfuata Omri wakawashinda watu waliomfuata Tibni mwana wa Ginathi; basi akafa Tibni, akatawala Omri. Katika mwaka wa thelathini na moja wa Asa, mfalme wa Yuda, Omri alianza kutawala juu ya Israeli, akatawala miaka kumi na miwili. Akatawala huko Tirza miaka sita. Kisha akanunua kilima cha Samaria kwa Shemeri kwa talanta mbili za fedha; akajenga juu ya kilima kile, akauita mji alioujenga Samaria, kwa kufuata jina lake Shemeri, aliyekuwa mwenye kilima. Omri akafanya yaliyo mabaya machoni pa BWANA, akatenda maovu kuliko wote waliomtangulia; kwa kuwa aliiendea njia yote ya Yeroboamu mwana wa Nebati, na makosa yake, aliyowakosesha Israeli, ili kumghadhibisha BWANA, Mungu wa Israeli, kwa matendo yao ya ubatili. Nayo mambo yote ya Omri yaliyosalia aliyoyatenda, na uthabiti alioufanya, je! Hayakuandikwa katika Kitabu cha Kumbukumbu za Wafalme wa Israeli? Omri akalala na babaze, akazikwa huko Samaria; na Ahabu mwanawe akatawala mahali pake. Ahabu mwana wa Omri alianza kutawala juu ya Israeli katika mwaka wa thelathini na nane wa Asa mfalme wa Yuda; akatawala Ahabu mwana wa Omri juu ya Israeli katika Samaria miaka ishirini na miwili. Ahabu mwana wa Omri akafanya yaliyo mabaya machoni pa BWANA kuliko wote waliomtangulia. Ikawa, kama ingalikuwa neno dogo tu kuyaendea makosa ya Yeroboamu mwana wa Nebati, akamwoa Yezebeli binti Ethbaali, mfalme wa Wasidoni, akaenda akamtumikia Baali, akamsujudia. Akamjengea Baali madhabahu katika nyumba ya Baali, aliyoijenga huko Samaria. Ahabu akaifanya Ashera; Ahabu akazidi kumghadhibisha BWANA, Mungu wa Israeli, kuliko wafalme wote wa Israeli waliomtangulia. Katika siku zake, Hieli Mbetheli akajenga Yeriko; akatia misingi yake kwa kufiwa na Abiramu mzaliwa wake wa kwanza, na kuyaweka malango yake kwa kufiwa na mwana wake mdogo Segubu; sawasawa na neno la BWANA alilolinena kwa Yoshua mwana wa Nuni.
1 Wafalme 16:1-34 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ndipo neno la BWANA likamjia Yehu mwana wa Hanani juu ya Baasha, kusema, Kwa kuwa mimi nilikuinua kutoka katika mavumbi, na kukufanya uwe mkuu juu ya watu wangu Israeli; nawe umeiendea njia ya Yeroboamu, na kuwakosesha watu wangu Israeli, hata wanighadhibishe kwa makosa yao; angalia, kuondoa nitawaondoa Baasha na jamaa yake; tena nitaifanya nyumba yako iwe kama nyumba ya Yeroboamu mwana wa Nebati. Mtu amfiaye Baasha mjini mbwa watamla; naye amfiaye mashambani ndege wa angani watamla. Basi, mambo yote ya Baasha yaliyosalia, na aliyoyafanya, na nguvu zake, je! Hayakuandikwa katika kitabu-cha-tarehe cha wafalme wa Israeli? Baasha akalala na babaze, akazikwa katika Tirza; naye Ela mwanawe akatawala mahali pake. Tena neno la BWANA likaja kwa mkono wa nabii Yehu mwana wa Hanani juu ya Baasha, na juu ya nyumba yake, kwa sababu ya mabaya yote aliyoyatenda machoni pa BWANA, akimghadhibisha kwa kazi ya mikono yake, kwa kufanana na nyumba ya Yeroboamu, na kwa sababu aliiharibu. Katika mwaka wa ishirini na sita wa Asa mfalme wa Yuda, Ela mwana wa Baasha alianza kutawala juu ya Israeli huko Tirza, akatawala miaka miwili. Na mtumwa wake Zimri, jemadari wa nusu ya magari yake, akamfanyia fitina; alipokuwako Tirza akinywa hata kulewa nyumbani mwa Arsa, aliyekuwa juu ya nyumba huko Tirza; Zimri akaingia akampiga, akamwua, katika mwaka wa ishirini na saba wa Asa mfalme wa Yuda, akatawala mahali pake. Ikawa, alipoanza kutawala, mara alipoketi juu ya kiti chake cha enzi, akawaua nyumba yote ya Baasha; hakumwachia mwanamume ye yote, wa jamaa zake, wala wa rafiki zake. Hivyo Zimri akaiharibu nyumba yote ya Baasha, sawasawa na neno la BWANA, alilolinena juu ya Baasha kwa Yehu nabii, kwa sababu ya makosa yake Baasha, na makosa yote ya Ela mwanawe, waliyoyakosa, na kuwakosesha Israeli, wakimghadhibisha BWANA, Mungu wa Israeli, kwa matendo yao ya ubatili. Na mambo yote ya Ela yaliyosalia, na yote aliyoyafanya, je! Hayakuandikwa katika kitabu-cha-tarehe cha wafalme wa Israeli? Katika mwaka wa ishirini na saba wa Asa mfalme wa Yuda, Zimri akatawala muda wa siku saba huko Tirza. Basi, watu walikuwa wametua maragoni kupigana na Gibethoni, ulio wa Wafilisti. Na hao watu waliokuwako maragoni wakasikia habari ya kwamba Zimri amefanya fitina, tena amempiga mfalme; kwa hiyo Israeli wote wakamfanya Omri, jemadari wa jeshi, awe mfalme juu ya Israeli siku ile maragoni. Omri akapanda kutoka Gibethoni, na Israeli wote pamoja naye, wakauhusuru Tirza. Ikawa Zimri alipoona ya kuwa mji umetwaliwa, akaingia ngomeni mwa nyumba ya mfalme, akaiteketeza nyumba ya mfalme juu yake kwa moto, akafa; kwa sababu ya makosa aliyoyakosa, akifanya mabaya machoni pa BWANA, kwa kuiendea njia ya Yeroboamu na makosa yake aliyoyafanya akiwakosesha Israeli. Na mambo yote ya Zimri yaliyosalia na fitina yake aliyoifanya, je! Hayakuandikwa katika kitabu-cha-tarehe cha wafalme wa Israeli? Ndipo watu wa Israeli wakatengwa sehemu mbili; nusu ya watu wakamfuata Tibni mwana wa Ginathi, ili wamfanye mfalme; nusu wakamfuata Omri. Lakini hao watu waliomfuata Omri wakawashinda watu waliomfuata Tibni mwana wa Ginathi; basi akafa Tibni, akatawala Omri. Katika mwaka wa thelathini na moja wa Asa, mfalme wa Yuda, Omri alianza kutawala juu ya Israeli, akatawala miaka kumi na miwili. Akatawala huko Tirza miaka sita. Kisha akanunua kilima cha Samaria kwa Shemeri kwa talanta mbili za fedha; akajenga juu ya kilima kile, akauita mji alioujenga Samaria, kwa kuliandama jina lake Shemeri, aliyekuwa mwenye kilima. Omri akafanya yaliyo mabaya machoni pa BWANA, akatenda maovu kuliko wote waliomtangulia; kwa kuwa aliiendea njia yote ya Yeroboamu mwana wa Nebati, na makosa yake, aliyowakosesha Israeli, ili kumghadhibisha BWANA, Mungu wa Israeli, kwa matendo yao ya ubatili. Nayo mambo yote ya Omri yaliyosalia aliyoyatenda, na uthabiti alioufanya, je! Hayakuandikwa katika kitabu-cha-tarehe cha wafalme wa Israeli? Omri akalala na babaze, akazikwa huko Samaria; na Ahabu mwanawe akatawala mahali pake. Ahabu mwana wa Omri alianza kutawala juu ya Israeli katika mwaka wa thelathini na nane wa Asa mfalme wa Yuda; akatawala Ahabu mwana wa Omri juu ya Israeli katika Samaria miaka ishirini na miwili. Ahabu mwana wa Omri akafanya yaliyo mabaya machoni pa BWANA kuliko wote waliomtangulia. Ikawa, kama ingalikuwa neno dogo tu kuyaendea makosa ya Yeroboamu mwana wa Nebati, akamwoa Yezebeli binti Ethbaali, mfalme wa Wasidoni, akaenda akamtumikia Baali, akamsujudia. Akamjengea Baali madhabahu katika nyumba ya Baali, aliyoijenga huko Samaria. Ahabu akaifanya Ashera; Ahabu akazidi kumghadhibisha BWANA, Mungu wa Israeli, kuliko wafalme wote wa Israeli waliomtangulia. Katika siku zake, Hieli Mbetheli akajenga Yeriko; akatia misingi yake kwa kufiwa na Abiramu mzaliwa wake wa kwanza, na kuyaweka malango yake kwa kufiwa na mwana wake mdogo Segubu; sawasawa na neno la BWANA alilolinena kwa Yoshua mwana wa Nuni.
1 Wafalme 16:1-34 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
21 Ndipo neno la BWANA likamjia Yehu mwana wa Hanani dhidi ya Baasha, kusema: “Nilikuinua kutoka mavumbini na kukufanya mtawala wa watu wangu Israeli, lakini ukaenenda katika njia za Yeroboamu na kusababisha watu wangu Israeli kutenda dhambi na kunikasirisha kwa dhambi zao. Basi nitamwangamiza Baasha pamoja na nyumba yake, nami nitaifanya nyumba yako kama ile ya Yeroboamu mwanawe Nebati. Mbwa watawala walio wa nyumba ya Baasha watakaofia ndani ya mji, na ndege wa angani watawala wale watakaofia mashambani.” Kuhusu matukio mengine ya utawala wa Baasha, aliyoyafanya na mafanikio yake, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Israeli? Baasha akalala na baba zake naye akazikwa huko Tirsa. Naye Ela mwanawe akawa mfalme baada yake. Zaidi ya hayo, neno la BWANA likamjia Baasha pamoja na nyumba yake kupitia kwa nabii Yehu mwana wa Hanani, kwa sababu ya maovu yote aliyokuwa ametenda machoni pa BWANA, akimkasirisha kwa mambo aliyotenda, na kuwa kama nyumba ya Yeroboamu aliyoiangamiza. Katika mwaka wa ishirini na sita wa utawala wa Asa mfalme wa Yuda, Ela mwana wa Baasha akawa mfalme wa Israeli, naye akatawala huko Tirsa kwa miaka miwili. Zimri, mmoja wa maafisa wake, aliyekuwa na amri juu ya nusu ya magari yake ya vita, akapanga njama dhidi ya Ela. Wakati huo Ela alikuwa Tirsa, akilewa katika nyumba ya Arsa, aliyekuwa msimamizi wa jumba la kifalme huko Tirsa. Zimri akaingia, akampiga na kumuua katika mwaka wa ishirini na saba wa utawala wa Asa mfalme wa Yuda. Kisha Zimri akawa mfalme baada yake. Mara tu alipoanza kutawala na kukalia kiti chake cha kifalme, aliua jamaa yote ya Baasha. Hakumwacha mwanaume hata mmoja, akiwa ni ndugu au rafiki. Hivyo, Zimri akawaangamiza jamaa yote ya Baasha, kama BWANA alivyonena dhidi ya Baasha kupitia kwa nabii Yehu: kwa sababu ya dhambi zote Baasha na mwanawe Ela walizokuwa wametenda na wakasababisha Israeli kuzitenda, basi wakamkasirisha BWANA, Mungu wa Israeli, kwa sanamu zao batili. Kuhusu matukio mengine ya utawala wa Ela, na yote aliyoyafanya, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Israeli? Katika mwaka wa ishirini na saba wa utawala wa Asa mfalme wa Yuda, Zimri akatawala huko Tirsa siku saba. Jeshi lilikuwa limepiga kambi karibu na Gibethoni, mji wa Wafilisti. Waisraeli waliokuwa kambini waliposikia kuwa Zimri amepanga njama ya kumuua mfalme, wakamtangaza Omri, jemadari wa jeshi, kuwa mfalme wa Israeli yote siku hiyo hiyo huko kambini. Ndipo Omri na Waisraeli wote pamoja naye wakaondoka Gibethoni na kuizingira Tirsa. Zimri alipoona kuwa mji umechukuliwa, alienda ndani ya ngome ya jumba la kifalme na kulichoma moto hilo jumba na kujiteketeza ndani yake. Kwa hiyo akafa, kwa sababu ya dhambi alizotenda, akifanya maovu machoni pa BWANA na kuenenda katika njia za Yeroboamu na katika dhambi alizotenda na kusababisha Israeli kuzifanya. Kuhusu matukio mengine ya utawala wa Zimri, na uasi alioutenda, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Israeli? Kisha, watu wa Israeli wakagawanyika katika makundi mawili, nusu wakamuunga mkono Tibni mwana wa Ginathi ili awe mfalme, na nusu nyingine wakamuunga mkono Omri. Lakini wafuasi wa Omri wakajionesha kuwa wenye nguvu kuliko wale wa Tibni, mwana wa Ginathi. Hivyo Tibni akafa, na Omri akawa mfalme. Katika mwaka wa thelathini na moja wa utawala wa Asa mfalme wa Yuda, Omri akawa mfalme wa Israeli, naye akatawala kwa miaka kumi na mbili, sita kati ya hiyo katika Tirsa. Alinunua kilima cha Samaria kutoka kwa Shemeri kwa talanta mbili za fedha na akajenga mji juu ya hicho kilima, akiuita Samaria, kutokana na Shemeri, jina la mmiliki wa kwanza wa kilima hicho. Lakini Omri akatenda maovu machoni pa BWANA na kutenda dhambi kuliko wote waliomtangulia. Akaenenda katika njia zote za Yeroboamu mwana wa Nebati na katika dhambi zake, ambazo alisababisha Israeli kutenda, hivyo basi wakamkasirisha BWANA, Mungu wa Israeli, kwa sanamu zao batili. Kuhusu matukio mengine ya utawala wa Omri, yale aliyofanya na mafanikio aliyokuwa nayo, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Israeli? Omri akalala na baba zake, akazikwa huko Samaria. Naye Ahabu mwanawe akawa mfalme baada yake. Katika mwaka wa thelathini na nane wa utawala wa Asa mfalme wa Yuda, Ahabu mwana wa Omri akawa mfalme wa Israeli, naye akatawala Israeli akiwa Samaria kwa miaka ishirini na mbili. Ahabu mwana wa Omri akafanya maovu zaidi machoni pa BWANA kuliko yeyote aliyemtangulia. Kama vile haikutosha kuishi kama Yeroboamu mwana wa Nebati, akamwoa Yezebeli binti Ethbaali, mfalme wa Wasidoni, naye akaanza kumtumikia Baali na kumwabudu. Akatengeneza madhabahu kwa ajili ya Baali katika hekalu la Baali alilolijenga huko Samaria. Pia Ahabu alitengeneza nguzo ya Ashera na kufanya mengi ili kumkasirisha BWANA, Mungu wa Israeli, kuliko walivyofanya wafalme wote wa Israeli waliomtangulia. Wakati wa Ahabu, Hieli ule Mbetheli, akaijenga Yeriko upya. Aliweka misingi yake kwa gharama ya mzaliwa wake wa kwanza Abiramu, na kuweka malango yake kwa gharama ya mwanawe mdogo Segubu, kama BWANA alivyonena kupitia kwa Yoshua, mwana wa Nuni.