Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Wafalme 1:1-27

1 Wafalme 1:1-27 Biblia Habari Njema (BHN)

Mfalme Daudi, wakati alipokuwa mzee sana, watumishi wake walimfunika kwa mablanketi, lakini hata hivyo, hakuweza kupata joto. Kwa hivyo wakamwambia, “Bwana wetu mfalme, afadhali tukutafutie msichana akutumikie na kukutunza; alale pamoja nawe kusudi akupatie joto.” Basi, wakatafutatafuta msichana mzuri kote nchini Israeli. Akapatikana msichana mmoja mzuri aitwaye Abishagi, Mshunami; wakamleta kwa mfalme. Msichana huyo, alikuwa mzuri sana. Basi, akaanza kumtumikia na kumtunza mfalme; lakini mfalme hakulala naye. Wakati huo, Adoniya, mwana wa Daudi na Hagithi, akaanza kujigamba kwamba yeye ndiye atakayekuwa mfalme. Basi, akajitayarishia magari ya kukokotwa, wapandafarasi na wapiga mbio hamsini wa kumtangulia na kumshangilia. Lakini baba yake, Daudi, hakuwa amemkemea mwanawe hata mara moja na kumwuliza kwa nini alikuwa amefanya hivyo. Adoniya, ama kwa hakika, alikuwa mwenye sura ya kupendeza sana; na alikuwa amemfuata Absalomu kwa kuzaliwa. Adoniya akashauriana na Yoabu mwana wa Seruya, na kuhani Abiathari; nao wakamfuata na kumuunga mkono. Lakini kuhani Sadoki, na Benaya, mwana wa Yehoyada, na nabii Nathani na Shimei, Rei pamoja na walinzi wa Daudi, hawakumuunga mkono Adoniya. Siku moja, Adoniya alitoa sadaka ya kondoo, ng'ombe na ndama wanono kwenye Jiwe la Nyoka, karibu na chemchemi iitwayo Enrogeli. Akawaalika kwenye karamu ya sadaka hiyo ndugu zake wote, yaani wana wengine wa mfalme, na watumishi wote wa mfalme waliokuwa wa kabila la Yuda. Lakini, nabii Nathani, Benaya, walinzi wa mfalme na Solomoni ndugu yake hakuwaalika. Hapo, Nathani akamwendea Bathsheba mama yake Solomoni, akamwuliza, “Je, hujasikia kwamba Adoniya, mwanawe Hagithi, amejinyakulia mamlaka ya ufalme na bwana wetu Daudi hana habari? Basi, kama ukitaka kuyaokoa maisha yako na ya mwanao Solomoni, nakushauri hivi: Mwendee mfalme Daudi, umwulize, ‘Je, bwana wangu mfalme, hukuniapia mimi mtumishi wako ukisema, “Mwana wako Solomoni atatawala mahali pangu na atakaa juu ya kiti changu cha enzi?” Imekuwaje basi, sasa Adoniya anatawala?’ Na utakapokuwa bado unaongea na mfalme, mimi nitaingia na kuyathibitisha maneno yako.” Basi, Bathsheba alimwendea mfalme chumbani mwake (wakati huo mfalme alikuwa mzee sana, naye Abishagi, Mshunami alikuwa akimhudumia). Bathsheba aliinama, akamsujudia mfalme, naye mfalme akamwuliza, “Unataka nini?” Bathsheba akamjibu, “Bwana wangu, uliniapia mimi mtumishi wako mbele ya Bwana Mungu wako, ukisema: ‘Mwana wako Solomoni atatawala baada yangu, na ataketi juu ya kiti changu cha enzi.’ Sasa, tazama, Adoniya anatawala ingawa wewe bwana wangu mfalme hujui kuhusu hayo. Ametoa sadaka ya ng'ombe, ya vinono, na kondoo wengi, na kuwaita wana wote wa mfalme, kuhani Abiathari, na Yoabu jemadari wa jeshi, lakini mtumishi wako Solomoni hakumkaribisha. Na sasa, bwana wangu mfalme, Waisraeli wote wanakungojea, ili uwaambie yule atakayeketi juu ya kiti chako baada yako, bwana wangu mfalme. La sivyo, itatokea ya kwamba, wakati ambapo wewe bwana wangu, mfalme, utakapofariki mimi pamoja na mwanangu Solomoni tutahesabika kama wenye hatia.” Wakati Bathsheba alipokuwa akizungumza na mfalme, nabii Nathani aliingia ikulu. Nao watu wakamwambia mfalme, “Nabii Nathani yuko hapa.” Naye alipomfikia mfalme, alimwinamia mfalme mpaka uso ukafika chini udongoni. Ndipo Nathani aliposema, “Bwana wangu, je, ulisema, ‘Adoniya atatawala baada yangu na atakaa juu ya kiti changu cha enzi?’ Kwa maana leo ameteremka, akatoa sadaka ya ng'ombe, vinono na kondoo wengi na amewakaribisha wana wa mfalme, Yoabu jemadari wa jeshi, na kuhani Abiathari, na, tazama, wanakula na kunywa mbele yake, na kusema, ‘Uishi mfalme Adoniya!’ Lakini hakunialika mimi, mtumishi wako wala kuhani Sadoki, wala Benaya mwana wa Yehoyada na mtumishi wako Solomoni. Je, yote haya umeyafanya wewe bwana wangu, mfalme, bila kuwaambia watumishi wako mtu atakayekaa juu ya kiti chako cha enzi baada yako?”

1 Wafalme 1:1-27 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Mfalme Daudi alikuwa mzee, mkongwe katika siku zake, nao wakamfunika nguo, lakini asipate joto. Kwa hiyo watumishi wake wakamwambia, Bwana wangu mfalme na atafutiwe kijana mwanamwali; naye asimame mbele ya mfalme, amtunze; alale kifuani mwako, ili bwana wangu mfalme apate joto Basi wakatafuta msichana mzuri katika nchi yote ya Israeli, wakamwona Abishagi, Mshunami, wakamleta kwa mfalme. Naye msichana huyo alikuwa mzuri sana; akamtunza mfalme, akamtumikia; lakini mfalme hakumjua. Ndipo Adonia mwana wa Hagithi akatakabari, akasema, Mimi nitakuwa mfalme. Akajiwekea tayari magari na wapanda farasi, na watu hamsini wapige mbio mbele yake. Tena baba yake hakumchukiza wakati wowote kwa kusema, Mbona umefanya hivi? Kisha, alikuwa mtu mzuri sana; naye alizaliwa baada ya Absalomu. Akashauriana na Yoabu, mwana wa Seruya, na Abiathari, kuhani; nao wakamsaidia Adonia, wakamfuata. Ila Sadoki, kuhani, na Benaya, mwana wa Yehoyada, na Nathani, nabii, na Shimei, na Rei, na mashujaa wa Daudi, hao hawakuwa pamoja na Adonia. Adonia akatoa sadaka ya kondoo, ng'ombe na ndama wanono, karibu na jiwe la Zohelethi, lililo karibu na chemchemi Enrogeli; akawaita ndugu zake wote, wana wa mfalme, na watu wote wa Yuda, watumishi wa mfalme; ila nabii Nathani, Benaya, walinzi wa mfalme na Sulemani ndugu yake hakuwaalika. Ndipo Nathani akamwambia Bathsheba, mamaye Sulemani, akasema, Je! Hukusikia ya kuwa Adonia, mwana wa Hagithi, amekuwa mfalme, na bwana wetu Daudi hana habari? Haya basi, nikupe shauri, tafadhali, upate kuiokoa roho yako, na roho ya mwanao Sulemani. Nenda uingie ndani kwa mfalme Daudi, ukamwambie, Je! Hukuniapia mimi mjakazi wako, Ee mfalme, bwana wangu, kusema, Hakika yake Sulemani mwana wako atamiliki baada yangu, na kuketi katika kiti changu cha enzi? Mbona basi anamiliki Adonia? Tazama, wakati ule utakapokuwa katika kusema na mfalme, mimi nami nitaingia nyuma yako, na kuyahakikisha maneno yako. Basi Bathsheba akaingia ndani kwa mfalme, ndani ya chumba chake; naye mfalme alikuwa mzee sana; na Abishagi, Mshunami, alikuwa akimtumikia mfalme. Bathsheba akainama, akamsujudia mfalme. Naye mfalme akamwuliza, Wataka nini? Akamwambia, Bwana wangu, uliniapia mimi mjakazi wako kwa BWANA, Mungu wako, ya kwamba, bila shaka Sulemani mwanao atamiliki baada yangu, yeye ndiye atakayeketi katika kiti changu cha enzi. Na sasa, angalia, Adonia anamiliki; na wewe, bwana wangu mfalme, huna habari. Tena amechinja ng'ombe, na vinono, na kondoo tele, na kuwaita wana wa mfalme wote pia, na Abiathari, kuhani, na Yoabu, jemadari wa jeshi. Ila Sulemani, mtumishi wako, huyu hakumwita. Ee mfalme, bwana wangu, macho ya Israeli wote yanakuelekea wewe, kwamba uwaambie ni nani atakayeketi katika kiti chako cha enzi baada yako, Ee mfalme, bwana wangu. Ama sivyo itakuwa, bwana wangu mfalme atakapolala pamoja na baba zake, mimi na mwanangu Sulemani tutahesabiwa kuwa wahalifu. Basi tazama, alipokuwa katika kusema na mfalme, Nathani, nabii, aliingia. Wakamwambia mfalme wakasema, Tazama, Nathani, nabii. Naye alipoingia ndani mbele ya mfalme, akamsujudia kifudifudi. Nathani akasema, Ee mfalme, bwana wangu, je! Wewe umesema ya kwamba, Adonia atamiliki baada yangu, ndiye atakayeketi katika kiti changu cha enzi? Maana leo ameshuka, na kuchinja ng'ombe, na vinono, na kondoo tele, naye amewaita wana wote wa mfalme, na majemadari wa jeshi, na Abiathari, kuhani; na tazama, wanakula na kunywa mbele yake, wakisema, Na aishi mfalme Adonia! Lakini mimi, mtumishi wako, na Sadoki, kuhani, na Benaya, mwana wa Yehoyada, na Sulemani, mtumishi wako, hakutuita sisi. Je! Bwana wangu mfalme ndiye aliyelitenda jambo hili, bila kutujulisha sisi watumishi wako ni nani atakayeketi katika kiti cha enzi cha bwana wangu mfalme baada yake?

1 Wafalme 1:1-27 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Mfalme Daudi alikuwa mzee, mkongwe katika siku zake, nao wakamfunika nguo, lakini asipate moto. Kwa hiyo watumishi wake wakamwambia, Bwana wangu mfalme na atafutiwe kijana mwanamwali; naye asimame mbele ya mfalme, amtunze; alale kifuani mwako, ili bwana wangu mfalme apate moto. Basi wakatafuta kijana mzuri mipakani mwote mwa Israeli, wakamwona Abishagi, Mshunami, wakamleta kwa mfalme. Naye kijana huyo alikuwa mzuri sana; akamtunza mfalme, akamtumikia; walakini mfalme hakumjua. Ndipo Adonia mwana wa Hagithi akatakabari, akasema, Mimi nitakuwa mfalme. Akajiwekea tayari magari na wapanda farasi, na watu hamsini wapige mbio mbele yake. Tena baba yake hakumchukiza wakati wo wote kwa kusema, Mbona umefanya hivi? Kisha, alikuwa mtu mzuri sana; naye alizaliwa baada ya Absalomu. Akashauriana na Yoabu, mwana wa Seruya, na Abiathari, kuhani; nao wakamsaidia Adonia, wakamfuata. Ila Sadoki, kuhani, na Benaya, mwana wa Yehoyada, na Nathani, nabii, na Shimei, na Rei, na mashujaa wa Daudi, hao hawakuwa pamoja na Adonia. Adonia akachinja kondoo, na ng’ombe, na vinono, karibu na jiwe la Zohelethi, lililo karibu na chemchemi Rogeli; akawaita ndugu zake wote, wana wa mfalme, na watu wote wa Yuda, watumishi wa mfalme; ila Nathani, nabii, na Benaya, na mashujaa, na Sulemani nduguye, hakuwaita hao. Ndipo Nathani akamwambia Bath-sheba, mamaye Sulemani, akasema, Je! Hukusikia ya kuwa Adonia, mwana wa Hagithi, anamiliki, na bwana wetu Daudi hana habari? Haya basi, nikupe shauri, tafadhali, upate kuiokoa roho yako, na roho ya mwanao Sulemani. Enenda uingie ndani kwa mfalme Daudi, ukamwambie, Je! Hukuniapia mimi mjakazi wako, Ee mfalme, bwana wangu, kusema, Hakika yake Sulemani mwana wako atamiliki baada yangu, na kuketi katika kiti changu cha enzi? Mbona basi anamiliki Adonia? Tazama, wakati ule utakapokuwa katika kusema na mfalme, mimi nami nitaingia nyuma yako, na kuyahakikisha maneno yako. Basi Bath-sheba akaingia ndani kwa mfalme, ndani ya chumba chake; naye mfalme alikuwa mzee sana; na Abishagi, Mshunami, alikuwa akimtumikia mfalme. Bath-sheba akainama, akamsujudia mfalme. Naye mfalme akamwuliza, Wataka nini? Akamwambia, Bwana wangu, uliniapia mimi mjakazi wako kwa BWANA, Mungu wako, ya kwamba, bila shaka Sulemani mwanao atamiliki baada yangu, yeye ndiye atakayeketi katika kiti changu cha enzi. Na sasa, angalia, Adonia anamiliki; na wewe, bwana wangu mfalme, huna habari. Tena amechinja ng’ombe, na vinono, na kondoo tele, na kuwaita wana wa mfalme wote pia, na Abiathari, kuhani, na Yoabu, jemadari wa jeshi. Ila Sulemani, mtumishi wako, huyu hakumwita. Ee mfalme, bwana wangu, macho ya Israeli wote yanakuelekea wewe, kwamba uwaambie ni nani atakayeketi katika kiti chako cha enzi baada yako, Ee mfalme, bwana wangu. Ama sivyo itakuwa, bwana wangu mfalme atakapolala pamoja na baba zake, mimi na mwanangu Sulemani tutahesabiwa kuwa wahalifu. Basi tazama, alipokuwa katika kusema na mfalme, Nathani, nabii, aliingia. Wakamwambia mfalme wakasema, Tazama, Nathani, nabii. Naye alipoingia ndani mbele ya mfalme, akamsujudia kifudifudi. Nathani akasema, Ee mfalme, bwana wangu, je! Wewe umesema ya kwamba, Adonia atamiliki baada yangu, ndiye atakayeketi katika kiti changu cha enzi? Maana leo ameshuka, na kuchinja ng’ombe, na vinono, na kondoo tele, naye amewaita wana wote wa mfalme, na majemadari wa jeshi, na Abiathari, kuhani; na tazama, wanakula na kunywa mbele yake, wakisema, Na aishi mfalme Adonia! Walakini mimi, mimi mtumishi wako, na Sadoki, kuhani, na Benaya, mwana wa Yehoyada, na Sulemani, mtumishi wako, hakutuita sisi. Je! Bwana wangu mfalme ndiye aliyelitenda jambo hili, bila kutujulisha sisi watumishi wako ni nani atakayeketi katika kiti cha enzi cha bwana wangu mfalme baada yake?

1 Wafalme 1:1-27 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

Mfalme Daudi alipokuwa mzee umri ukiwa umesogea, hakuweza kupata joto hata walipomfunika kwa nguo. Kwa hiyo watumishi wake wakamwambia, “Turuhusu tumtafute mwanamwali bikira amhudumie mfalme na kumtunza. Anaweza kulala pembeni mwake ili bwana wetu mfalme apate joto.” Kisha wakatafuta katika Israeli yote ili kumpata msichana mzuri wa sura na wakampata Abishagi Mshunami, wakamleta kwa mfalme. Msichana huyo alikuwa mzuri sana wa sura. Akamtunza mfalme na kumhudumia, lakini mfalme hakufanya naye tendo la ndoa. Basi Adoniya mwana wa Hagithi akajigamba na kusema, “Mimi nitakuwa mfalme.” Hivyo akaweka tayari magari ya vita na wapanda farasi, pamoja na watu hamsini wa kumtangulia wakikimbia. (Baba yake hakuwa ameingilia na kumuuliza, “Kwa nini unafanya hivyo?” Alikuwa pia kijana mzuri sana wa sura, na alizaliwa baada ya Absalomu.) Adoniya akashauriana na Yoabu mwana wa Seruya, na kuhani Abiathari, nao wakamsaidia. Lakini kuhani Sadoki, Benaya mwana wa Yehoyada, nabii Nathani, Shimei, Rei na walinzi maalum wa Daudi hawakujiunga na Adoniya. Ndipo Adoniya akatoa dhabihu ya kondoo, ngʼombe na ndama walionona kwenye Jiwe la Zohelethi karibu na En-Rogeli. Akawaalika ndugu zake wote wana wa mfalme, na wanaume wote wa Yuda waliokuwa maafisa wa mfalme, lakini hakumwalika nabii Nathani, wala Benaya, wala walinzi maalum wa mfalme, wala ndugu yake Sulemani. Ndipo Nathani akamuuliza Bathsheba, mama yake Sulemani, “Je, hujasikia kwamba Adoniya mwana wa Hagithi, amekuwa mfalme pasipo bwana wetu Daudi kujua jambo hili? Sasa basi, acha nikushauri jinsi utakavyookoa uhai wako mwenyewe na uhai wa mwanao Sulemani. Ingia kwa Mfalme Daudi na umwambie, ‘Bwana wangu mfalme, je hukuniapia mimi mtumishi wako: “Hakika mwanao Sulemani atakuwa mfalme baada yangu na ndiye atakayeketi kwenye kiti changu cha ufalme”? Kwa nini basi Adoniya amekuwa mfalme?’ Utakapokuwa ukizungumza na mfalme, nitaingia na kuthibitisha hayo uliyoyasema.” Hivyo Bathsheba akaenda kumwona mfalme chumbani mwake, ambapo Abishagi Mshunami alikuwa akimhudumia; naye mfalme alikuwa mzee sana. Bathsheba akainama na kusujudu, uso wake ukagusa chini mbele ya mfalme. Mfalme akauliza, “Ni nini unachokitaka?” Akamwambia, “Bwana wangu, wewe mwenyewe uliniapia mimi mtumishi wako kwa BWANA Mungu wako kwamba: ‘Sulemani Mwanao atakuwa mfalme baada yangu na ndiye atakayeketi kwenye kiti changu cha ufalme.’ Lakini sasa Adoniya amekuwa mfalme, nawe, bwana wangu mfalme huna habari kuhusu jambo hilo. Ametoa dhabihu idadi kubwa ya ngʼombe, ndama walionona na kondoo, naye amewaalika wana wa mfalme wote, kuhani Abiathari, na Yoabu jemadari wa jeshi, lakini hakumwalika Sulemani mtumishi wako. Bwana wangu mfalme, macho ya Israeli yote yanakutazama wewe wajue kutoka kwako kuwa ni nani atakayeketi kwenye kiti cha ufalme cha bwana wangu mfalme baada yake. Kama sivyo, mara tu bwana wangu mfalme atakapopumzishwa pamoja na baba zake, mimi na mwanangu Sulemani tutatendewa kama wahalifu.” Alipokuwa angali anazungumza na mfalme, nabii Nathani akafika. Wakamwambia mfalme, “Nabii Nathani yuko hapa.” Kisha akaenda mbele ya mfalme na kumsujudia hadi uso wake ukagusa chini. Nathani akasema, “Je, bwana wangu mfalme, umetangaza kuwa Adoniya atakuwa mfalme baada yako na kwamba ataketi kwenye kiti chako cha ufalme? Leo ameshuka na kutoa dhabihu idadi kubwa ya ngʼombe, ndama walionona na kondoo. Amewaalika wana wote wa mfalme, jemadari wa jeshi, na kuhani Abiathari. Sasa hivi, wanakula na kunywa pamoja naye wakisema, ‘Aishi maisha marefu, Mfalme Adoniya!’ Lakini mimi mtumishi wako, na kuhani Sadoki, Benaya mwana wa Yehoyada, na mtumishi wako Sulemani hakutualika. Je, hili ni jambo ambalo bwana wangu mfalme amelifanya pasipo kuwajulisha watumishi wake ili wapate kujua ni nani atakayeketi kwenye kiti cha ufalme cha bwana wangu mfalme baada yake?”