1 Wakorintho 15:35-41
1 Wakorintho 15:35-41 Biblia Habari Njema (BHN)
Lakini mtu anaweza kuuliza: “Wafu watafufuliwaje? Watakuwa na mwili wa namna gani?” Hayo ni maswali ya kijinga! Ukipanda mbegu, isipokufa kwanza haitaota. Unachopanda ni mbegu tu, labda ya ngano au nafaka nyingine, na si mmea mzima ambao hutokea baadaye. Mungu huipa hiyo mbegu mwili anaoutaka mwenyewe; kila mbegu hupata mwili wake wa pekee. Miili ya viumbe vyote si sawa. Miili ya binadamu ni ya namna moja, ya wanyama ni ya namna nyingine, ya ndege ni ya namna nyingine na miili ya samaki pia ni ya namna nyingine. Iko miili ya mbinguni na miili ya duniani; uzuri wa miili ya mbinguni ni mwingine, na uzuri wa miili ya duniani ni mwingine. Uko uzuri wa jua, wa mwezi na wa nyota; hata nyota nazo huhitilafiana kwa uzuri.
1 Wakorintho 15:35-41 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Lakini labda mtu atasema, Wafu wafufuliwaje? Nao huja kwa mwili gani? Ewe mpumbavu! Uipandayo haihuiki, isipokufa; nayo uipandayo, huupandi mwili ule utakaokuwa, ila chembe tupu, ikiwa ni ya ngano au nyingineyo; lakini Mungu huipa mwili kama apendavyo, na kila mbegu mwili wake. Nyama zote hazifanani; nyingine ni ya wanadamu, nyingine ya hayawani, nyingine ya ndege, nyingine ya samaki. Tena kuna miili ya mbinguni, na miili ya duniani; lakini fahari yake ile ya mbinguni ni mbali, na fahari yake ile ya duniani ni mbali. Kuna fahari moja ya jua, na fahari nyingine ya mwezi, na fahari nyingine ya nyota; maana iko tofauti ya fahari hata kati ya nyota na nyota.
1 Wakorintho 15:35-41 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Lakini labda mtu atasema, Wafufuliwaje wafu? Nao huja kwa mwili gani? Ewe mpumbavu! Uipandayo haihuiki, isipokufa; nayo uipandayo, huupandi mwili ule utakaokuwa, ila chembe tupu, ikiwa ni ya ngano au nyingineyo; lakini Mungu huipa mwili kama apendavyo, na kila mbegu mwili wake. Nyama yote si nyama moja; ila nyingine ni ya wanadamu, nyingine ya hayawani, nyingine ya ndege, nyingine ya samaki. Tena kuna miili ya mbinguni, na miili ya duniani; lakini fahari yake ile ya mbinguni ni mbali, na fahari yake ile ya duniani ni mbali. Kuna fahari moja ya jua, na fahari nyingine ya mwezi, na fahari nyingine ya nyota; maana iko tofauti ya fahari hata kati ya nyota na nyota.
1 Wakorintho 15:35-41 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Lakini mtu anaweza kuuliza, “Wafu wafufuliwaje? Watakuwa na mwili wa namna gani?” Ninyi wapumbavu kiasi gani? Mpandacho hakiwi hai kama hakikufa. Mpandapo, hampandi mwili ule utakao kuwa, bali mwapanda mbegu tu, pengine ya ngano au ya kitu kingine. Lakini Mungu huipa mbegu umbo kama alivyokusudia mwenyewe na kila aina ya mbegu huipa umbo lake. Kwa maana nyama zote si za aina moja. Binadamu wana nyama ya aina moja, wanyama wana aina nyingine, kadhalika ndege na samaki wana nyama tofauti. Pia kuna miili ya mbinguni na miili ya duniani, lakini fahari wa ile miili ya mbinguni ni wa aina moja na fahari wa ile miili ya duniani ni wa aina nyingine. Jua lina fahari ya aina moja, mwezi nao una fahari yake na nyota pia, nazo nyota hutofautiana katika fahari.