Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Wakorintho 14:26-40

1 Wakorintho 14:26-40 Biblia Habari Njema (BHN)

Ndugu, tuseme nini, basi? Mnapokutana pamoja, mmoja aimbe wimbo, mwingine atoe mafundisho, mwingine awe na ufunuo kutoka kwa Mungu, mwingine atumie kipaji cha kusema kwa lugha ngeni na mwingine afafanue yanayosemwa. Yote yawe kwa ajili ya kulijenga kanisa. Wakiwapo watu wenye vipaji vya kusema kwa lugha ngeni, waseme wawili au watatu, si zaidi, tena mmojammoja; na aweko mtu wa kufafanua yanayosemwa. Lakini kama hakuna awezaye kufafanua, basi, mwenye kusema lugha ngeni anyamaze mkutanoni, aseme na nafsi yake mwenyewe na Mungu. Kuhusu wale wenye kipaji cha kutangaza ujumbe wa Mungu, waseme wawili au watatu, na wengine wayapime maneno yao. Ikiwa mmoja anaposema na mwingine wa wasikilizaji amepata ufunuo kutoka kwa Mungu, basi, yule anayesema anyamaze. Maana nyote mwaweza kutangaza ujumbe wa Mungu, mmoja baada ya mwingine, ili nyote mpate kujifunza na kutiwa moyo. Kipaji cha kutangaza ujumbe wa Mungu ni lazima kitawaliwe na huyo mwenye hicho kipaji. Maana Mungu si Mungu wa fujo, ila wa amani. Kama ilivyo desturi katika makanisa yote ya watu wa Mungu, wanawake wakae kimya katika mikutano ya waumini. Hawana ruhusa kusema; ila wawe watii kama isemavyo sheria. Ikiwa wanayo maswali ya kuuliza, wawaulize waume zao nyumbani, maana ni aibu kwa mwanamke kusema katika mikutano ya waumini. Je, mnadhani neno la Mungu limetoka kwenu nyinyi au kwamba limewajieni nyinyi peke yenu? Kama mtu yeyote anadhani kwamba yeye ni mjumbe wa Mungu au kwamba anacho kipaji cha Roho, na ajue kwamba haya ninayowaandikia nyinyi ni amri ya Bwana. Lakini mtu asiyetambua hayo, basi, mtu asimjali mtu huyo. Hivyo basi, ndugu zangu, mnapaswa kuwa na hamu ya kutangaza ujumbe wa Mungu; lakini msimkataze mtu kusema kwa lugha ngeni. Lakini yote yafanyike kwa heshima na kwa utaratibu.

1 Wakorintho 14:26-40 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Basi tuseme nini ndugu zangu? Mnapokutana pamoja, kila mmoja ana wimbo, au neno la mafundisho, au ufunuo, lugha mpya au atatafsiri. Mambo yote yatendeke kwa ajili ya kulijenga kanisa. Kama mtu yeyote akinena kwa lugha, basi waseme watu wawili au watatu si zaidi, mmoja baada ya mwingine na lazima awepo mtu wa kutafsiri. Lakini kama hakuna mtu wa kutafsiri, hao watu na wanyamaze kimya kanisani na wanene na nafsi zao wenyewe na Mungu. Manabii wawili au watatu wanene na wengine wapime yale yasemwayo. Kama mtu yeyote aliyeketi karibu, akipata ufunuo, basi yule wa kwanza na anyamaze. Kwa maana wote mnaweza kutoa unabii, mmoja baada ya mwingine, ili kila mtu apate kufundishwa na kutiwa moyo. Roho za manabii huwatii manabii. Kwa maana Mungu si Mungu wa machafuko bali ni Mungu wa amani. Kama ilivyo katika makusanyiko yote ya watakatifu, wanawake wanapaswa kuwa kimya kanisani. Hawaruhusiwi kusema, bali wanyenyekee kama sheria isemavyo. Kama wakitaka kuuliza kuhusu jambo lolote, wawaulize waume zao nyumbani. Kwa maana ni aibu kwa mwanamke kuzungumza kanisani. Je, neno la Mungu lilianzia kwenu? Au ni ninyi tu ambao neno la Mungu limewafikia? Kama mtu yeyote akidhani kwamba yeye ni nabii, au ana karama za rohoni, basi na akubali kwamba haya ninayoandika ni maagizo kutoka kwa Bwana. Kama mtu akipuuza jambo hili yeye mwenyewe atapuuzwa. Kwa hiyo ndugu zangu, takeni sana kutoa unabii na msikataze watu kusema kwa lugha. Lakini kila kitu kitendeke kwa heshima na kwa utaratibu.

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha