1 Mambo ya Nyakati 29:10-16
1 Mambo ya Nyakati 29:10-16 Biblia Habari Njema (BHN)
Ndipo Daudi akamtukuza Mwenyezi-Mungu mbele ya mkutano wote, akisema: “Utukuzwe milele na milele, ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wa baba yetu Israeli. Ukuu ni wako, ee Mwenyezi-Mungu, una nguvu, utukufu, ushindi na enzi. Vyote vilivyoko mbinguni na duniani ni vyako. Ee Mwenyezi-Mungu, ufalme ni wako, nawe umetukuzwa, u mkuu juu ya vitu vyote. Utajiri na heshima hutoka kwako, vyote wavitawala. Uwezo na nguvu vimo mkononi mwako, nawe wawakuza uwapendao, na huwaimarisha wote. Sasa ee Mungu wetu, tunakushukuru na kulisifu jina lako tukufu. “Lakini, mimi ni nani, na watu wangu ni nani, hata tuweze kukupa kitu? Kwa maana vitu vyote vyatoka kwako, tumekutolea vilivyo vyako wewe mwenyewe. Sisi tu wageni mbele yako, na wasafiri kama walivyokuwa babu zetu wote. Siku zetu duniani ni kama kivuli kipitacho, hapa hakuna tumaini la kukaa. Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, wingi wote huu tuliotoa ili kukujengea nyumba kwa ajili ya utukufu wa jina lako takatifu, watoka mkononi mwako na yote ni yako.
1 Mambo ya Nyakati 29:10-16 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Kwa hiyo Daudi akamhimidi BWANA, mbele ya mkutano wote; naye Daudi akasema, Uhimidiwe, Ee BWANA, Mungu wa Israeli baba yetu, milele na milele. Ee BWANA, ukuu ni wako, na uweza, na utukufu, na ushindi, na enzi; maana vitu vyote vilivyo mbinguni na duniani ni vyako; ufalme ni wako, Ee BWANA, nawe umetukuzwa, u mkuu juu ya vitu vyote. Utajiri na heshima hutoka kwako wewe, nawe watawala juu ya vyote; na mkononi mwako mna uweza na nguvu; tena mkononi mwako mna kuwatukuza na kuwawezesha wote. Basi sasa, Mungu wetu, tunakushukuru na kulisifu jina lako tukufu. Lakini mimi ni nani, na watu wangu ni nani, hata tuweze kutoa kwa hiari hivi? Kwani vitu vyote vyatoka kwako na katika vitu vyako mwenyewe tumekutolea. Kwani sisi tu wageni na wapitaji mbele zako, kama walivyokuwa baba zetu wote; siku zetu duniani ni kama kivuli, na hakuna tumaini la kuishi. Ee BWANA, Mungu wetu, akiba hii yote tuliyoiweka, ili tukujengee nyumba kwa ajili ya jina lako takatifu, yote inatoka mkononi mwako, na yote ni yako wewe.
1 Mambo ya Nyakati 29:10-16 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Kwa hiyo Daudi akamhimidi BWANA, mbele ya mkutano wote; naye Daudi akasema, Uhimidiwe, Ee BWANA, Mungu wa Israeli baba yetu, milele na milele. Ee BWANA, ukuu ni wako, na uweza, na utukufu, na kushinda, na enzi; maana vitu vyote vilivyo mbinguni na duniani ni vyako; ufalme ni wako, Ee BWANA, nawe umetukuzwa, u mkuu juu ya vitu vyote. Utajiri na heshima hutoka kwako wewe, nawe watawala juu ya vyote; na mkononi mwako mna uweza na nguvu; tena mkononi mwako mna kuwatukuza na kuwawezesha wote. Basi sasa, Mungu wetu, twakushukuru na kulisifu jina lako tukufu. Lakini mimi ni nani, na watu wangu ni nani, hata tuweze kutoa kwa hiari hivi? Kwani vitu vyote vyatoka kwako na katika vitu vyako mwenyewe tumekutolea. Kwani sisi tu wageni mbele zako, na wasafiri, kama walivyokuwa baba zetu wote; ni kama kivuli siku zetu duniani, wala taraji ya kukaa hapana. Ee BWANA, Mungu wetu, akiba hii yote tuliyoiweka, ili tukujengee nyumba kwa ajili ya jina lako takatifu, yatoka yote mkononi mwako, na yote ni yako wewe.
1 Mambo ya Nyakati 29:10-16 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Daudi akamhimidi BWANA mbele ya kusanyiko lote, akisema: “Uhimidiwe wewe, Ee BWANA, Mungu wa Israeli baba yetu, tangu milele hata milele. Ukuu na uweza, ni vyako, Ee BWANA, na utukufu na enzi na uzuri, kwa kuwa kila kilichoko mbinguni na duniani ni chako wewe. Ee BWANA, ufalme ni wako; umetukuzwa kuwa mkuu juu ya yote. Utajiri na heshima vyatoka kwako; wewe ndiwe unayetawala vitu vyote. Mikononi mwako kuna nguvu na uweza ili kuinua na kuwapa wote nguvu, Sasa, Mungu wetu, tunakushukuru na kulisifu Jina lako tukufu. “Lakini mimi ni nani, nao watu wangu ni nani, hata tuweze kukutolea kwa ukarimu namna hii? Vitu vyote vyatoka kwako, nasi tumekutolea tu vile vinavyotoka mkononi mwako. Sisi ni wageni na wapitaji machoni pako, kama walivyokuwa baba zetu wote. Siku zetu duniani ni kama kivuli, bila tumaini. Ee BWANA Mungu wetu, kwa wingi wote huu ambao tumekutolea kwa kujenga Hekalu kwa ajili ya Jina lako Takatifu, vimetoka mkononi mwako, navyo vyote ni mali yako.