1 Mambo ya Nyakati 29:1-22
1 Mambo ya Nyakati 29:1-22 Biblia Habari Njema (BHN)
Mfalme Daudi akaumbia ule mkutano wote uliojumuika, “Solomoni, mwanangu, ambaye peke yake amechaguliwa na Mungu, bado yungali mdogo, na hana uzoefu mwingi, na kazi hii ni kubwa. Nyumba atakayoijenga si ya mwanadamu, bali ni ya Mungu, Mwenyezi-Mungu. Basi, nimejitahidi kwa kadiri ya uwezo wangu wote kuiwekea nyumba ya Mungu wangu, akiba ya dhahabu ya kutengenezea vitu vya dhahabu, fedha ya kutengenezea vitu vya fedha, shaba ya kutengenezea vitu vya shaba, chuma cha kutengenezea vitu vya chuma, na miti ya kutengenezea vitu vya miti. Zaidi ya hayo, nimevitayarisha kwa wingi vito vya rangi na mawe ya kujazia vito vya njumu, mawe ya rangi, mawe ya thamani ya kila namna na marumaru. Tena, zaidi ya vyote nilivyotoa kwa ajili ya nyumba takatifu, ninayo hazina yangu binafsi ya dhahabu na fedha, na kwa sababu naipenda nyumba ya Mungu wangu, naitoa kwa ajili ya nyumba ya Mungu wangu: Tani 3,000 za dhahabu kutoka Ofiri, talanta 700 za fedha safi ya kuzifunikia kuta za nyumba, na kwa ajili ya kutengenezea vitu vya kila aina vitakavyotengenezwa na mafundi kwa mikono. Nimeweka dhahabu kwa ajili ya vyombo vya dhahabu, na fedha kwa ajili ya vyombo vya fedha. Ni nani basi atakayemtolea Mwenyezi-Mungu kwa hiari ili ajiweke wakfu hivi leo kwa Mwenyezi-Mungu?” Ndipo wakuu wa koo, viongozi wa makabila ya Israeli, makamanda wa maelfu na wa mamia; pia na maofisa wasimamizi wa kazi za mfalme walipotoa kwa hiari yao. Walitoa kwa ajili ya huduma za nyumba ya Mungu: Tani 170 za dhahabu, tani 340 za fedha, tani 620 za shaba na tani 3,400 za chuma. Wale ambao walikuwa na vito vya thamani walivitoa vitiwe katika hazina ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu, chini ya uangalizi wa Yehieli, Mgershoni. Ndipo watu wakafurahi kwa sababu walitoa kwa hiari, maana kwa moyo wao wote walimtolea Mwenyezi-Mungu kwa hiari, naye mfalme Daudi alifurahi sana. Ndipo Daudi akamtukuza Mwenyezi-Mungu mbele ya mkutano wote, akisema: “Utukuzwe milele na milele, ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wa baba yetu Israeli. Ukuu ni wako, ee Mwenyezi-Mungu, una nguvu, utukufu, ushindi na enzi. Vyote vilivyoko mbinguni na duniani ni vyako. Ee Mwenyezi-Mungu, ufalme ni wako, nawe umetukuzwa, u mkuu juu ya vitu vyote. Utajiri na heshima hutoka kwako, vyote wavitawala. Uwezo na nguvu vimo mkononi mwako, nawe wawakuza uwapendao, na huwaimarisha wote. Sasa ee Mungu wetu, tunakushukuru na kulisifu jina lako tukufu. “Lakini, mimi ni nani, na watu wangu ni nani, hata tuweze kukupa kitu? Kwa maana vitu vyote vyatoka kwako, tumekutolea vilivyo vyako wewe mwenyewe. Sisi tu wageni mbele yako, na wasafiri kama walivyokuwa babu zetu wote. Siku zetu duniani ni kama kivuli kipitacho, hapa hakuna tumaini la kukaa. Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, wingi wote huu tuliotoa ili kukujengea nyumba kwa ajili ya utukufu wa jina lako takatifu, watoka mkononi mwako na yote ni yako. Ninajua Mungu wangu, kwamba wewe waujaribu moyo, nawe unapendezwa na unyofu. Nami, katika unyofu wa moyo wangu nimetoa vitu hivi vyote kwa hiari yangu, na sasa ninaona watu wako walioko hapa, wakikutolea kwa hiari na furaha. Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Abrahamu, Isaka na Israeli, babu zetu, dumisha maazimio ya namna hiyo na fikira za namna hiyo mioyoni mwa watu wako, na ielekeze mioyo ya watu wako kwako. Mjalie Solomoni mwanangu ili kwa moyo wote ashike amri zako, maamuzi na maagizo yako, atekeleze yote ili aweze kuijenga nyumba hii ya enzi niliyoifanyia matayarisho.” Kisha, mfalme Daudi aliwaambia wote waliokusanyika, “Msifuni Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu.” Na wote waliokusanyika wakamtukuza Mwenyezi-Mungu, Mungu wa babu zao, wakamsujudia na kumwabudu Mwenyezi-Mungu na kumtolea mfalme Daudi heshima. Wakamtolea tambiko Mwenyezi-Mungu. Siku ya pili yake wakamtolea sadaka za kuteketezwa: Mafahali 1,000, wanakondoo 1,000, pamoja na sadaka zao za vinywaji na tambiko nyingi kwa ajili ya Waisraeli wote. Basi siku hiyo walikula na kunywa kwa furaha kuu mbele ya Mwenyezi-Mungu. Wakamtawaza Solomoni mwana wa Daudi, mara ya pili. Wakampaka mafuta awe mtawala kwa jina la Mwenyezi-Mungu, na Sadoki awe kuhani.
1 Mambo ya Nyakati 29:1-22 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Kisha mfalme Daudi akawaambia kusanyiko lote, Sulemani mwanangu, ambaye Mungu amemchagua peke yake, angali ni mchanga bado na hana uzoefu, nayo kazi hii ni kubwa; kwani nyumba hii ya enzi si kwa mwanadamu, ila kwa BWANA, Mungu. Basi kwa uwezo wangu wote nimeiwekea akiba nyumba ya Mungu wangu, dhahabu kwa vitu vya dhahabu, na fedha kwa vitu vya fedha, na shaba kwa vitu vya shaba, na chuma kwa vitu vya chuma, na miti kwa vitu vya miti; vito vya shohamu, na vya kujazia, vito vya njumu, na vya rangi mbalimbali, na mawe ya thamani ya kila namna, na marumaru tele. Nami tena kwa kuwa nimeiwekea nyumba ya Mungu wangu shauku yangu, nami ninayo hazina yangu mwenyewe ya dhahabu na fedha, ninaitoa kwa ajili ya nyumba ya Mungu wangu, zaidi ya hiyo akiba niliyoiwekea tayari nyumba takatifu; yaani, talanta elfu tatu za dhahabu, za dhahabu ya Ofiri, na talanta elfu saba za fedha iliyosafika, ya kuzifunikiza kuta za nyumba; ya dhahabu, kwa vitu vya dhahabu, na ya fedha kwa vitu vya fedha, na kwa kazi za kila namna zitakazofanywa kwa mikono ya mafundi. Ni nani basi ajitoaye kwa moyo ili ajiweke wakfu leo kwa BWANA? Ndipo wakuu wa koo za mababa, na wakuu wa makabila ya Israeli, na makamanda wa maelfu na wa mamia, pamoja na wasimamizi wa kazi ya mfalme, wakajitoa kwa hiari yao; nao wakatoa, kwa ajili ya utumishi wa nyumba ya Mungu, dhahabu talanta elfu tano, na darkoni elfu kumi, na fedha talanta elfu kumi, na shaba talanta elfu kumi na nane, na chuma talanta elfu mia moja. Na wale walioonekana kuwa na vito vya thamani wakavitoa vitiwe katika hazina ya nyumba ya BWANA, chini ya mkono wa Yehieli, Mgershoni. Ndipo hao watu wakafurahi, kwa sababu wametoa kwa hiari yao wenyewe, kwa moyo wao wote, kwa hiari yao wenyewe, wamemtolea BWANA; mfalme Daudi naye akafurahi sana. Kwa hiyo Daudi akamhimidi BWANA, mbele ya mkutano wote; naye Daudi akasema, Uhimidiwe, Ee BWANA, Mungu wa Israeli baba yetu, milele na milele. Ee BWANA, ukuu ni wako, na uweza, na utukufu, na ushindi, na enzi; maana vitu vyote vilivyo mbinguni na duniani ni vyako; ufalme ni wako, Ee BWANA, nawe umetukuzwa, u mkuu juu ya vitu vyote. Utajiri na heshima hutoka kwako wewe, nawe watawala juu ya vyote; na mkononi mwako mna uweza na nguvu; tena mkononi mwako mna kuwatukuza na kuwawezesha wote. Basi sasa, Mungu wetu, tunakushukuru na kulisifu jina lako tukufu. Lakini mimi ni nani, na watu wangu ni nani, hata tuweze kutoa kwa hiari hivi? Kwani vitu vyote vyatoka kwako na katika vitu vyako mwenyewe tumekutolea. Kwani sisi tu wageni na wapitaji mbele zako, kama walivyokuwa baba zetu wote; siku zetu duniani ni kama kivuli, na hakuna tumaini la kuishi. Ee BWANA, Mungu wetu, akiba hii yote tuliyoiweka, ili tukujengee nyumba kwa ajili ya jina lako takatifu, yote inatoka mkononi mwako, na yote ni yako wewe. Nami ninajua, Mungu wangu, ya kuwa wewe wajaribu moyo, nawe wapendezwa na unyofu. Nami katika unyofu wa moyo wangu nimeyatoa haya yote kwa hiari yangu mwenyewe; nami sasa nimeona kwa furaha watu wako, waliopo hapa, wakikutolea kwa hiari yao. Ee BWANA, Mungu wa Abrahamu, na wa Isaka, na wa Israeli, baba zetu, ulidumishe jambo hili milele katika fikira za mawazo ya mioyo ya watu wako, ukaiongoze mioyo yao kwako; naye Sulemani mwanangu, umjalie ili kwa moyo wote, azishike amri zako, na shuhuda zako, na maagizo yako, akayatende hayo yote na kuijenga nyumba hii ya enzi, niliyoiwekea akiba. Ndipo Daudi akawaambia kusanyiko lote, Haya, mhimidini BWANA, Mungu wenu. Basi kusanyiko lote wakamhimidi BWANA, Mungu wa baba zao, wakainamisha vichwa vyao, wakamsujudia BWANA, na mfalme naye. Siku ya pili yake, wakamtolea BWANA dhabihu, wakamchinjia BWANA sadaka ya kuteketezwa, yaani, ng'ombe elfu moja, na kondoo dume elfu moja, na wana-kondoo elfu moja, pamoja na sadaka zao za vinywaji, na dhabihu nyingi kwa ajili ya Israeli wote; wakala na kunywa mbele za BWANA siku ile, kwa furaha kuu. Wakamtawaza Sulemani, mwana wa Daudi, mara ya pili, wakamtia mafuta mbele za BWANA, awe mkuu, na Sadoki awe kuhani.
1 Mambo ya Nyakati 29:1-22 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Kisha mfalme Daudi akawaambia kusanyiko lote, Sulemani mwanangu, ambaye Mungu amemchagua peke yake, akali ni mchanga bado na mwororo, nayo kazi hii ni kubwa; kwani nyumba hii ya enzi si kwa mwanadamu, ila kwa BWANA, Mungu. Basi kwa uwezo wangu wote nimeiwekea akiba nyumba ya Mungu wangu, dhahabu kwa vitu vya dhahabu, na fedha kwa vitu vya fedha, na shaba kwa vitu vya shaba, na chuma kwa vitu vya chuma, na miti kwa vitu vya miti; vito vya shohamu, na vya kujazia, vito vya njumu, na vya rangi mbalimbali, na mawe ya thamani ya kila namna, na marimari tele. Nami tena kwa kuwa nimeiwekea nyumba ya Mungu wangu shauku yangu, nami ninayo hazina yangu mwenyewe ya dhahabu na fedha, naitoa kwa ajili ya nyumba ya Mungu wangu, zaidi ya hiyo akiba niliyoiwekea tayari nyumba takatifu; yaani, talanta elfu tatu za dhahabu, za dhahabu ya Ofiri, na talanta elfu saba za fedha iliyosafika, ya kuzifunikiza kuta za nyumba; ya dhahabu, kwa vitu vya dhahabu, na ya fedha kwa vitu vya fedha, na kwa kazi za kila namna zitakazofanywa kwa mikono ya mafundi. Ni nani basi ajitoaye kwa moyo ili ajiweke wakfu leo kwa BWANA? Ndipo wakuu wa mbari za mababa, na wakuu wa kabila za Israeli, na maakida wa maelfu na wa mamia, pamoja na wasimamizi wa kazi ya mfalme, wakajitoa kwa hiari yao; nao wakatoa, kwa ajili ya utumishi wa nyumba ya Mungu, dhahabu talanta elfu tano, na darkoni elfu kumi, na fedha talanta elfu kumi, na shaba talanta elfu kumi na nane, na chuma talanta elfu mia. Na wale walioonekana kuwa na vito vya thamani wakavitoa vitiwe katika hazina ya nyumba ya BWANA, chini ya mkono wa Yehieli, Mgershoni. Ndipo hao watu wakafurahi, kwa sababu wametoa kwa hiari yao wenyewe, kwa sababu kwa ukamilifu wa moyo, kwa hiari yao wenyewe, wamemtolea BWANA; mfalme Daudi naye akafurahi kwa furaha kuu. Kwa hiyo Daudi akamhimidi BWANA, mbele ya mkutano wote; naye Daudi akasema, Uhimidiwe, Ee BWANA, Mungu wa Israeli baba yetu, milele na milele. Ee BWANA, ukuu ni wako, na uweza, na utukufu, na kushinda, na enzi; maana vitu vyote vilivyo mbinguni na duniani ni vyako; ufalme ni wako, Ee BWANA, nawe umetukuzwa, u mkuu juu ya vitu vyote. Utajiri na heshima hutoka kwako wewe, nawe watawala juu ya vyote; na mkononi mwako mna uweza na nguvu; tena mkononi mwako mna kuwatukuza na kuwawezesha wote. Basi sasa, Mungu wetu, twakushukuru na kulisifu jina lako tukufu. Lakini mimi ni nani, na watu wangu ni nani, hata tuweze kutoa kwa hiari hivi? Kwani vitu vyote vyatoka kwako na katika vitu vyako mwenyewe tumekutolea. Kwani sisi tu wageni mbele zako, na wasafiri, kama walivyokuwa baba zetu wote; ni kama kivuli siku zetu duniani, wala taraji ya kukaa hapana. Ee BWANA, Mungu wetu, akiba hii yote tuliyoiweka, ili tukujengee nyumba kwa ajili ya jina lako takatifu, yatoka yote mkononi mwako, na yote ni yako wewe. Nami najua, Mungu wangu, ya kuwa wewe wajaribu moyo, nawe wapendezwa na unyofu. Nami katika unyofu wa moyo wangu nimeyatoa haya yote kwa hiari yangu mwenyewe; nami sasa nimeona kwa furaha watu wako, waliopo hapa, wakikutolea kwa hiari yao. Ee BWANA, Mungu wa Ibrahimu, na wa Isaka, na wa Israeli, baba zetu, ulilinde jambo hili milele katika fikira za mawazo ya mioyo ya watu wako, ukaiongoze mioyo yao kwako; naye Sulemani mwanangu, umpe moyo mkamilifu, ili azishike amri zako, na shuhuda zako, na maagizo yako, akayatende hayo yote na kuijenga nyumba hii ya enzi, niliyoiwekea akiba. Ndipo Daudi akawaambia kusanyiko lote, Haya, mhimidini BWANA, Mungu wenu. Basi kusanyiko lote wakamhimidi BWANA, Mungu wa baba zao, wakainama vichwa vyao, wakamsujudia BWANA, na mfalme naye. Wakamtolea BWANA dhabihu, wakamchinjia BWANA sadaka za kuteketezwa, siku ya pili yake, yaani, ng’ombe elfu, na kondoo waume elfu, na wana-kondoo elfu, pamoja na sadaka zao za vinywaji, na dhabihu nyingi kwa ajili ya Israeli wote; wakala na kunywa mbele za BWANA siku ile, kwa furaha kuu. Wakamtawaza Sulemani, mwana wa Daudi, mara ya pili, wakamtia mafuta mbele za BWANA, awe mkuu, na Sadoki awe kuhani.
1 Mambo ya Nyakati 29:1-22 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Ndipo Mfalme Daudi akawaambia kusanyiko lote: “Mwanangu Sulemani, yeye ambaye Mungu amemchagua, ni kijana mdogo na asiye na uzoefu. Kazi hii ni kubwa, kwa sababu Hekalu hili la fahari si kwa ajili ya mwanadamu bali ni kwa ajili ya BWANA Mungu. Kwa uwezo wangu wote nimetenga mali kwa ajili ya Hekalu la Mungu wangu: dhahabu kwa kazi za dhahabu, fedha kwa ajili ya fedha, shaba kwa kazi za shaba, chuma kwa kazi za chuma na miti kwa kazi za miti, vivyo hivyo vito vya shohamu kwa ajili ya kutia kwenye vijalizo, almasi, mawe ya rangi mbalimbali, aina zote za vito vya thamani na marumaru; haya yote kwa wingi mno. Zaidi ya hayo, kwa kujitolea kwangu kwa ajili ya Hekalu la Mungu wangu, sasa ninatoa hazina zangu mwenyewe za dhahabu na fedha kwa ajili ya Hekalu la Mungu wangu, zaidi ya mali niliyotoa kwa ajili ya Hekalu hili takatifu: talanta elfu tatu za dhahabu (dhahabu ya Ofiri), na talanta elfu saba za fedha safi iliyosafishwa, kwa ajili ya kufunika kuta za Hekalu, kwa kazi ya dhahabu na kazi ya fedha na kwa kazi yote itakayofanywa na mafundi. Basi, ni nani anayependa kujitoa kwa BWANA leo?” Ndipo viongozi wa jamaa, maafisa wa makabila ya Israeli, majemadari wa maelfu na majemadari wa mamia, pamoja na maafisa waliokuwa wasimamizi wa kazi za mfalme wakatoa kwa hiari. Wakatoa kwa ajili ya kazi ya Hekalu la Mungu talanta elfu tano na darkoni elfu kumi za dhahabu, talanta elfu kumi za fedha, talanta elfu kumi na nane za shaba, na talanta elfu mia moja za chuma. Kila mmoja aliyekuwa na vito vya thamani akavitoa katika hazina ya Hekalu la BWANA, chini ya uangalizi wa Yehieli Mgershoni. Watu wakafurahi kwa sababu ya itikio la hiari la viongozi wao, kwa kuwa walikuwa wametoa kwa hiari na kwa moyo wote kwa BWANA. Mfalme Daudi pia akafurahi sana. Daudi akamhimidi BWANA mbele ya kusanyiko lote, akisema: “Uhimidiwe wewe, Ee BWANA, Mungu wa Israeli baba yetu, tangu milele hata milele. Ukuu na uweza, ni vyako, Ee BWANA, na utukufu na enzi na uzuri, kwa kuwa kila kilichoko mbinguni na duniani ni chako wewe. Ee BWANA, ufalme ni wako; umetukuzwa kuwa mkuu juu ya yote. Utajiri na heshima vyatoka kwako; wewe ndiwe unayetawala vitu vyote. Mikononi mwako kuna nguvu na uweza ili kuinua na kuwapa wote nguvu, Sasa, Mungu wetu, tunakushukuru na kulisifu Jina lako tukufu. “Lakini mimi ni nani, nao watu wangu ni nani, hata tuweze kukutolea kwa ukarimu namna hii? Vitu vyote vyatoka kwako, nasi tumekutolea tu vile vinavyotoka mkononi mwako. Sisi ni wageni na wapitaji machoni pako, kama walivyokuwa baba zetu wote. Siku zetu duniani ni kama kivuli, bila tumaini. Ee BWANA Mungu wetu, kwa wingi wote huu ambao tumekutolea kwa kujenga Hekalu kwa ajili ya Jina lako Takatifu, vimetoka mkononi mwako, navyo vyote ni mali yako. Ninajua, Mungu wangu, kwamba wewe huujaribu moyo na unapendezwa na unyofu. Vitu hivi vyote nimetoa kwa hiari na kwa moyo mnyofu. Nami sasa nimeona kwa furaha jinsi watu wako walio hapa kwa hiari yao walivyokutolea wewe. Ee BWANA, Mungu wa baba zetu Abrahamu, Isaka na Israeli, weka shauku hii ndani ya mioyo ya watu wako daima na uifanye mioyo yao iwe na uaminifu kwako. Nawe umpe mwanangu Sulemani kujitolea kwako kwa moyo wote ili kuzishika amri zako, masharti yako, maagizo yako na kufanya kila kitu ili kujenga Hekalu hili la fahari ambalo kwa ajili yake nimetoa.” Ndipo Daudi akawaambia kusanyiko lote, “Mhimidini BWANA Mungu wenu.” Hivyo wote wakamhimidi BWANA, Mungu wa baba zao. Wakasujudu, na nyuso zao zikagusa chini mbele za BWANA na mfalme. Siku ya pili yake, wakamtolea BWANA dhabihu na sadaka za kuteketezwa: mafahali elfu moja, kondoo dume elfu moja, na wana-kondoo dume elfu moja, pamoja na sadaka za vinywaji, na sadaka nyingine nyingi sana kwa ajili ya Israeli yote. Wakala na kunywa kwa furaha kubwa mbele za BWANA siku ile. Wakamtawaza Sulemani mwana wa Daudi mara ya pili kuwa mfalme, wakampaka mafuta mbele za BWANA ili awe mfalme na Sadoki kuwa kuhani.