1 Mambo ya Nyakati 27:1-34
1 Mambo ya Nyakati 27:1-34 Biblia Habari Njema (BHN)
Hii ndiyo orodha ya wakuu wa wazawa wa Israeli waliokuwa viongozi wa jamaa, na makamanda wa maelfu na mamia na maofisa wao waliomtumikia mfalme Daudi kuhusu zamu za kuingia na kutoka. Kila mwezi kila mwaka, kundi tofauti la watu 24,000 walilishika zamu ya kufanya kazi. Yashobeamu mwana wa Zabdieli alikuwa kiongozi wa kikosi cha kwanza mnamo mwezi wa kwanza; kikosi chake kilikuwa na watu 24,000. Yeye alikuwa mzawa wa Peresi, naye akawa mkuu wa makamanda wote wa jeshi katika mwezi wa kwanza. Dodai alikuwa kiongozi wa kundi la pili katika mwezi wa pili. Kikosi chake kikiwa na wanajeshi 24,000. Kamanda wa kundi la tatu likiwa na wanajeshi 24,000 alikuwa Benaya mwana wa Yehoyada, aliyekuwa kuhani mkuu. Huyu ndiye Benaya aliyekuwa mtu shujaa katika kundi la watu 30, na kiongozi wa kundi hilo. Naye Amizabadi mwanawe, alikuwa kamanda. Asaheli, nduguye Yoabu, alikuwa wa nne akiongoza kundi la nne lenye wanajeshi 24,000, na baada yake alimfuata Zebadia mwanawe. Mwezi wa tano: Shamhuthi, Mwizrahi; alikuwa na kundi la wanajeshi 24,000. Mwezi wa sita: Ira, mwana wa Ikeshi, Mtekoa; alikuwa na kundi la wanajeshi 24,000. Mwezi wa saba: Helesi, Mpeloni, wa wana wa Efraimu; alikuwa na kundi la wanajeshi 24,000. Mwezi wa nane: Sibekai, Mhushathi, wa Wazera; alikuwa na kundi la wanajeshi 24,000. Mwezi wa tisa: Abiezeri Mwanathothi, wa Wabenyamini; naye alikuwa na kundi la wanajeshi 24,000. Mwezi wa kumi: Maharai, Mnetofathi wa Wazera; naye alikuwa na kundi la wanajeshi 24,000. Mwezi wa kumi na moja: Benaya, Mpirathoni; wa wana wa Efraimu, naye alikuwa na kundi la wanajeshi 24,000. Mwezi wa kumi na mbili: Heldai, Mnetofathi, wa Othnieli; pia naye alikuwa na kundi la wanajeshi 24,000. Hii ndiyo orodha ya wakuu wa makabila ya Israeli: Wa Wareubeni, Eliezeri mwana wa Zikri; Eliezeri ndiye aliyekuwa ofisa mkuu; wa Wasimeoni, Shefatia mwana wa Maaka; wa Lawi, Hashabia mwana wa Kemueli; wa Aroni, Sadoki; wa Yuda, Elihu, mmoja wa ndugu za mfalme Daudi; wa Isakari, Omri mwana wa Mikaeli; wa Zebuluni, Ishmaya mwana wa Obadia; wa Naftali, Yeremothi mwana wa Azrieli; wa wana wa Efraimu, Hoshea mwana wa Azazia; wa nusu ya kabila la Manase, Yoeli mwana wa Pedaya; wa nusu ya kabila la Manase katika Gileadi, Ido mwana wa Zekaria; na wa Benyamini, Yaasieli mwana wa Abneri; wa Dani, Azareli mwana wa Yerohamu. Hao ndio wakuu wa makabila ya Israeli. Mfalme Daudi hakuwahesabu wale waliokuwa chini ya umri wa miaka ishirini kwa maana Mwenyezi-Mungu aliahidi kuwaongeza Waisraeli wawe wengi kama nyota za mbinguni. Yoabu mwana wa Seruya alianza kuwahesabu lakini hakumaliza; tena ghadhabu iliwapata Waisraeli kwa ajili ya tendo hili, nayo hesabu hiyo haikuingizwa katika kumbukumbu za mfalme Daudi. Aliyesimamia hazina za mfalme Daudi alikuwa Azmawethi mwana wa Adieli. Yonathani mwana wa Uzia alisimamia hazina zilizokuwa mashambani, mijini, vijijini na ngomeni. Aliyewasimamia wakulima alikuwa Ezri mwana wa Kelubu. Aliyesimamia kazi ya mashamba ya mizabibu alikuwa Shimei, Mramathi. Aliyesimamia uzalishaji wa divai alikuwa Zabdi, Mshifmi. Aliyesimamia mizabibu na mikuyu ya Shefela alikuwa Baal-hanani, Mgederi. Aliyesimamia ghala za mafuta alikuwa Yoashi. Aliyesimamia mifugo iliyokuwa Sharoni alikuwa Shitrai, Msharoni; aliyesimamia mifugo iliyokuwa mabondeni alikuwa Shafati mwana wa Adlai. Aliyesimamia ngamia alikuwa Obili Mwishmaeli. Aliyesimamia punda alikuwa Yedeya, Mmeronothi. Aliyesimamia makundi ya kondoo alikuwa Yazizi, Mhagri. Hao wote walikuwa watunzaji wa mali ya mfalme Daudi. Yonathani, mjomba wa mfalme Daudi, alikuwa mshauri na mtu mwenye ufahamu na mwandishi. Yeye na Yehieli mwana wa Hakmoni waliwafunza wana wa mfalme. Ahithofeli, alikuwa mshauri wake mfalme; Hushai Mwarki, alikuwa rafiki yake mfalme. Ahithofeli alipofariki, mahali pake palichukuliwa na Yehoyada mwana wa Benaya na Abiathari. Yoabu alikuwa kamanda wa jeshi la mfalme.
1 Mambo ya Nyakati 27:1-34 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi wana wa Israeli kwa hesabu yao, wakuu wa koo za mababa, na makamanda wa maelfu na wa mamia, na wasimamizi wao waliomtumikia mfalme, kwa neno lolote la zamu za kuingia na za kutoka mwezi kwa mwezi, miezi yote ya mwaka, wa kila zamu, walikuwa watu elfu ishirini na nne. Juu ya zamu ya kwanza ya mwezi wa kwanza alikuwa Yashobeamu, mwana wa Zabdieli; na katika zamu yake walikuwa watu elfu ishirini na nne. Yeye alikuwa wa wana wa Peresi, mkuu wa makamanda wote wa jeshi mwezi wa kwanza. Na juu ya zamu ya mwezi wa pili alikuwa Dodai, Mwahohi, na zamu yake; na Miklothi alikuwa afisa mkuu; na katika zamu yake walikuwa watu elfu ishirini na nne. Kamanda wa tatu wa jeshi mwezi wa tatu alikuwa Benaya, mwana wa Yehoyada, kuhani; alikuwa mkuu, na katika zamu yake walikuwa watu elfu ishirini na nne. Huyo Benaya ndiye yule aliyekuwa shujaa wa wale thelathini, na juu ya wale thelathini; na katika zamu yake alikuwa Amizabadi mwanawe. Kamanda wa nne wa mwezi wa nne alikuwa Asaheli, nduguye Yoabu, na Zebadia mwanawe baada yake; na katika zamu yake walikuwa watu elfu ishirini na nne. Kamanda wa tano wa mwezi wa tano alikuwa Shamhuthi, Mwizrahi; na katika zamu yake walikuwa watu elfu ishirini na nne. Kamanda wa sita wa mwezi wa sita alikuwa Ira, mwana wa Ikeshi, Mtekoi; na katika zamu yake walikuwa watu ishirini na nne elfu. Kamanda wa saba wa mwezi wa saba alikuwa Heksi, Mpeloni, wa wana wa Efraimu; na katika zamu yake walikuwa watu elfu ishirini na nne. Kamanda wa nane wa mwezi wa nane alikuwa Sibekai, Mhushathi, wa Wazera; na katika zamu yake walikuwa watu elfu ishirini na nne. Kamanda wa tisa wa mwezi wa tisa alikuwa Abiezeri, Mwanathothi, wa Wabenyamini; na katika zamu yake walikuwa watu elfu ishirini na nne. Kamanda wa kumi wa mwezi wa kumi alikuwa Maharai, Mnetofathi, wa Wazera; na katika zamu yake walikuwa watu elfu ishirini na nne. Kamanda wa kumi na moja wa mwezi wa kumi na moja alikuwa Benaya, Mpirathoni, wa wana wa Efraimu; na katika zamu yake walikuwa watu elfu ishirini na nne. Kamanda wa kumi na mbili wa mwezi wa kumi na mbili alikuwa Heledi, Mnetofathi, wa Othnieli; na katika zamu yake walikuwa watu elfu ishirini na nne. Wakuu wa makabila ya Israeli walikuwa hawa; wa Wareubeni, Eliezeri mwana wa Zikri; wa Wasimeoni, Shefatia mwana wa Maaka; wa Lawi, Hashabia mwana wa Kemueli; wa Haruni, Sadoki; wa Yuda, Elihu, mmojawapo wa nduguze Daudi; wa Isakari, Omri mwana wa Mikaeli; wa Zabuloni, Ishmaya mwana wa Obadia; wa Naftali, Yeremothi mwana wa Azrieli; wa wana wa Efraimu, Hoshea mwana wa Azazia, wa nusu kabila la Manase, Yoeli mwana wa Pedaya; wa nusu kabila la Manase katika Gileadi, Ido mwana wa Zekaria; wa Benyamini, Yaasieli mwana wa Abneri; wa Dani, Azareli mwana wa Yerohamu. Hao walikuwa viongozi wa makabila ya Israeli. Lakini Daudi hakufanya hesabu ya waliokuwa na umri wa chini ya miaka ishirini; kwa kuwa BWANA alikuwa amesema, ya kwamba atawaongeza Israeli mfano wa nyota za mbinguni. Yoabu, mwana wa Seruya, alianza kuwahesabu, lakini hakumaliza; na ghadhabu ikawapata Israeli kwa hayo; wala hesabu hiyo haikuingizwa katika kumbukumbu za mfalme Daudi. Na juu ya hazina za mfalme alikuwa Azmawethi mwana wa Adieli; na juu ya hazina za mashambani, za mijini, na vijijini, na ngomeni, alikuwa Yonathani mwana wa Uzia; na juu ya hao wenye kazi ya kulima shamba alikuwa Ezri mwana wa Kelubu; na juu ya mashamba ya mizabibu alikuwa Shimei, Mramathi; na juu ya mazao ya mizabibu kwa ghala za mvinyo alikuwa Zabdi, Mshifmi; na juu ya mizeituni na mikuyu iliyokuwamo katika Shefela alikuwa Baal-hanani, Mgederi; na juu ya ghala za mafuta alikuwa Yoashi; na juu ya mifugo iliyolishwa katika Sharoni alikuwa Shitrai, Msharoni; na juu ya mifugo iliyokuwamo mabondeni alikuwa Shafati mwana wa Adlai; na juu ya ngamia alikuwa Obili, Mwishmaeli; na juu ya punda alikuwa Yedeya, Mmeronothi; na juu ya makundi ya kondoo alikuwa Yazizi, Mhagri. Hao wote walikuwa watumishi wa akiba alizokuwa nazo mfalme Daudi. Naye Yonathani, mjombawe Daudi, alikuwa mshauri, na mtu wa akili, na mwandishi; Yehieli mwana wa Hakmoni alikuwa pamoja na wana wa mfalme; na Ahithofeli alikuwa mshauri wake mfalme; na Hushai, Mwarki, alikuwa rafiki yake mfalme; na, baada ya Ahithofeli, walikuwa Yehoyada mwana wa Benaya, na Abiathari; na jemadari wa jeshi la mfalme alikuwa Yoabu.
1 Mambo ya Nyakati 27:1-34 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi wana wa Israeli kwa hesabu yao, wakuu wa mbari za mababa, na maakida wa maelfu na wa mamia, na wasimamizi wao waliomtumikia mfalme, kwa neno lo lote la zamu za kuingia na za kutoka mwezi kwa mwezi, miezi yote ya mwaka, wa kila zamu, walikuwa watu ishirini na nne elfu. Juu ya zamu ya kwanza ya mwezi wa kwanza alikuwa Yashobeamu, mwana wa Zabdieli; na katika zamu yake walikuwa watu ishirini na nne elfu. Yeye alikuwa wa wana wa Peresi, mkuu wa maakida wote wa jeshi mwezi wa kwanza. Na juu ya zamu ya mwezi wa pili alikuwa Dodai, Mwahohi, na zamu yake; na Miklothi alikuwa amiri; na katika zamu yake walikuwa watu ishirini na nne elfu. Akida wa tatu wa jeshi mwezi wa tatu alikuwa Benaya, mwana wa Yehoyada, kuhani; alikuwa mkuu, na katika zamu yake walikuwa watu ishirini na nne elfu. Huyo Benaya ndiye yule aliyekuwa shujaa wa wale thelathini, na juu ya wale thelathini; na katika zamu yake alikuwa Amizabadi mwanawe. Akida wa nne wa mwezi wa nne alikuwa Asaheli, nduguye Yoabu, na Zebadia mwanawe baada yake; na katika zamu yake walikuwa watu ishirini na nne elfu. Akida wa tano wa mwezi wa tano alikuwa Shamhuthi, Mwizrahi; na katika zamu yake walikuwa watu ishirini na nne elfu. Akida wa sita wa mwezi wa sita alikuwa Ira, mwana wa Ikeshi, Mtekoi; na katika zamu yake walikuwa watu ishirini na nne elfu. Akida wa saba wa mwezi wa saba alikuwa Heksi, Mpeloni, wa wana wa Efraimu; na katika zamu yake walikuwa watu ishirini na nne elfu. Akida wa nane wa mwezi wa nane alikuwa Sibekai, Mhushathi, wa Wazera; na katika zamu yake walikuwa watu ishirini na nne elfu. Akida wa kenda wa mwezi wa kenda alikuwa Abiezeri, Mwanathothi, wa Wabenyamini; na katika zamu yake walikuwa watu ishirini na nne elfu. Akida wa kumi wa mwezi wa kumi alikuwa Maharai, Mnetofathi, wa Wazera; na katika zamu yake walikuwa watu ishirini na nne elfu. Akida wa kumi na moja wa mwezi wa kumi na moja alikuwa Benaya, Mpirathoni, wa wana wa Efraimu; na katika zamu yake walikuwa watu ishirini na nne elfu. Akida wa kumi na mbili wa mwezi wa kumi na mbili alikuwa Heledi, Mnetofathi, wa Othnieli; na katika zamu yake walikuwa watu ishirini na nne elfu. Tena wakuu wa kabila za Israeli walikuwa hawa; wa Wareubeni, Eliezeri mwana wa Zikri; wa Wasimeoni, Shefatia mwana wa Maaka; wa Lawi, Hashabia mwana wa Kemueli; wa Haruni, Sadoki; wa Yuda, Elihu, mmojawapo wa nduguze Daudi; wa Isakari, Omri mwana wa Mikaeli; wa Zabuloni, Ishmaya mwana wa Obadia; wa Naftali, Yeromothi mwana wa Azrieli; wa wana wa Efraimu, Hoshea mwana wa Azazia, wa nusu kabila ya Manase, Yoeli mwana wa Pedaya; wa nusu kabila ya Manase katika Gileadi, Ido mwana wa Zekaria; wa Benyamini, Yaasieli mwana wa Abneri; wa Dani, Azareli mwana wa Yerohamu. Hao walikuwa maakida wa kabila za Israeli. Lakini Daudi hakufanya hesabu yao wenye miaka ishirini na waliopungua; kwa kuwa BWANA alikuwa amesema, ya kwamba atawaongeza Israeli mfano wa nyota za mbinguni. Yoabu, mwana wa Seruya, akaanza kuhesabu, lakini hakumaliza; na ghadhabu ikawapata Israeli kwa hayo; wala haikuhesabiwa hesabu hiyo ndani ya taarifa za mfalme Daudi. Na juu ya hazina za mfalme alikuwa Azmawethi mwana wa Adieli; na juu ya hazina za mashambani, za mijini, na vijijini, na ngomeni, alikuwa Yonathani mwana wa Uzia; na juu ya hao wenye kazi ya shamba kuilima ardhi alikuwa Ezri mwana wa Kelubu; na juu ya mashamba ya mizabibu alikuwa Shimei, Mramathi; na juu ya mazao ya mizabibu kwa ghala za mvinyo alikuwa Zabdi, Mshifmi; na juu ya mizeituni na mikuyu iliyokuwamo katika Shefela alikuwa Baal-hanani, Mgederi; na juu ya ghala za mafuta alikuwa Yoashi; na juu ya makundi ya ng’ombe waliolishwa katika Sharoni alikuwa Shitrai, Msharoni; na juu ya makundi waliokuwamo mabondeni alikuwa Shafati mwana wa Adlai; na juu ya ngamia alikuwa Obili, Mwishmaeli; na juu ya punda alikuwa Yedeya, Mmeronothi; na juu ya makundi ya kondoo alikuwa Yazizi, Mhagri. Hao wote walikuwa maakida wa akiba alizokuwa nazo mfalme Daudi. Naye Yonathani, mjombawe Daudi, alikuwa mshauri, na mtu wa akili, na mwandishi; Yehieli mwana wa Hakmoni alikuwa pamoja na wana wa mfalme; na Ahithofeli alikuwa mshauri wake mfalme; na Hushai, Mwarki, alikuwa rafiki yake mfalme; na, baada ya Ahithofeli, walikuwa Yehoyada mwana wa Benaya, na Abiathari; na jemadari wa jeshi la mfalme alikuwa Yoabu.
1 Mambo ya Nyakati 27:1-34 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Hii ndiyo orodha ya Waisraeli: viongozi wa jamaa, majemadari wa maelfu, majemadari wa mamia na maafisa wao, waliomtumikia mfalme kwa lolote lililohusu vikosi vya jeshi vilivyokuwa zamu mwezi baada ya mwezi katika mwaka mzima. Kila kikosi kimoja kilikuwa na watu elfu ishirini na nne. Msimamizi wa kikosi cha kwanza kwa mwezi wa kwanza alikuwa Yashobeamu mwana wa Zabdieli. Kulikuwa na watu elfu ishirini na nne katika kikosi chake. Yeye alikuwa mzao wa Peresi, na mkuu wa maafisa wote wa jeshi kwa mwezi wa kwanza. Msimamizi wa kikosi kwa mwezi wa pili alikuwa Dodai Mwahohi. Miklothi ndiye alikuwa kiongozi wa kikosi chake. Kikosi chake kilikuwa na watu elfu ishirini na nne. Jemadari wa kikosi cha tatu kwa mwezi wa tatu alikuwa Benaya mwana wa kuhani Yehoyada. Ndiye alikuwa mkuu wa kikosi chake kilichokuwa na watu elfu ishirini na nne. Huyu ndiye yule Benaya aliyekuwa shujaa miongoni mwa wale Thelathini, na ndiye alikuwa juu ya wale Thelathini. Mwanawe Amizabadi ndiye alikuwa mkuu katika kikosi chake. Jemadari wa nne kwa mwezi wa nne alikuwa Asaheli nduguye Yoabu, mwanawe Zebadia ndiye aliingia mahali pake kwenye uongozi. Kikosi chake kilikuwa na watu elfu ishirini na nne. Jemadari wa kikosi cha tano kwa mwezi wa tano alikuwa Shamhuthi Mwizrahi. Kikosi chake kilikuwa na watu elfu ishirini na nne. Jemadari wa kikosi cha sita kwa mwezi wa sita alikuwa Ira, mwana wa Ikeshi Mtekoa. Kikosi chake kilikuwa na watu elfu ishirini na nne. Jemadari wa kikosi cha saba kwa mwezi wa saba alikuwa Helesi Mpeloni wa Waefraimu. Kikosi chake kilikuwa na watu elfu ishirini na nne. Jemadari wa nane kwa mwezi wa nane, alikuwa Sibekai Mhushathi wa Wazera. Kikosi chake kilikuwa na watu elfu ishirini na nne. Jemadari wa tisa kwa mwezi wa tisa alikuwa Abiezeri Mwanathothi wa Wabenyamini. Kikosi chake kilikuwa na watu elfu ishirini na nne. Jemadari wa kumi kwa mwezi wa kumi alikuwa Maharai Mnetofathi wa Wazera. Kikosi chake kilikuwa na watu elfu ishirini na nne. Jemadari wa kumi na moja kwa mwezi wa kumi na moja alikuwa Benaya Mpirathoni wa Waefraimu. Kikosi chake kilikuwa na watu elfu ishirini na nne. Jemadari wa kumi na mbili kwa mwezi wa kumi na mbili alikuwa Heldai Mnetofathi kutoka jamaa ya Othnieli. Kikosi chake kilikuwa na watu elfu ishirini na nne. Viongozi wa makabila ya Israeli walikuwa: Kwa Wareubeni: Eliezeri mwana wa Zikri; kwa Wasimeoni: Shefatia mwana wa Maaka; kwa Walawi: Hashabia mwana wa Kemueli; kwa Haruni: Sadoki; kwa Yuda: Elihu, nduguye Daudi; kwa Waisakari: Omri mwana wa Mikaeli; kwa Wazabuloni: Ishmaya mwana wa Obadia; kwa Wanaftali: Yeremothi mwana wa Azrieli; kwa Waefraimu: Hoshea mwana wa Azazia; kwa nusu ya kabila la Manase: Yoeli mwana wa Pedaya; kwa nusu nyingine ya kabila la Manase huko Gileadi: Ido mwana wa Zekaria; kwa Wabenyamini: Yaasieli mwana wa Abneri; kwa Wadani: Azareli mwana wa Yerohamu. Hao ndio walikuwa maafisa wa makabila ya Israeli. Daudi hakuwahesabu watu waliokuwa chini ya miaka ishirini, kwa sababu BWANA alikuwa ameahidi kuwafanya Israeli kuwa wengi kama nyota za angani. Yoabu mwana wa Seruya alianza kuwahesabu watu lakini hakumaliza. Kwa sababu ya kuwahesabu watu, hasira ya Mungu iliwaka juu ya Israeli, nayo hiyo hesabu yao haikuingizwa katika kitabu cha kumbukumbu za Mfalme Daudi. Azmawethi mwana wa Adieli ndiye alikuwa msimamizi wa hazina za mfalme. Msimamizi wa hazina katika mashamba, miji, vijiji na kwenye ngome alikuwa Yonathani mwana wa Uzia. Ezri mwana wa Kelubu alikuwa msimamizi wa wafanyakazi waliolima katika mashamba. Shimei Mramathi alikuwa msimamizi wa mashamba ya mizabibu. Zabdi Mshifmi alikuwa msimamizi wa zabibu, utengenezaji na uhifadhi wa divai katika mapipa makubwa. Baal-Hanani Mgederi ndiye alikuwa mwangalizi wa mashamba ya mfalme ya mizeituni na mikuyu katika tambarare za vilima vya magharibi. Yoashi alikuwa msimamizi wa maghala ya mafuta ya zeituni. Shitrai Msharoni alikuwa msimamizi wa mifugo waliolishwa huko Sharoni. Shafati mwana wa Adlai alikuwa msimamizi wa mifugo iliyokuwa makondeni. Obili Mwishmaeli alikuwa msimamizi wa ngamia. Yedeya Mmeronothi alikuwa msimamizi wa punda. Yazizi Mhagri alikuwa msimamizi wa makundi ya kondoo na mbuzi. Hawa wote ndio walikuwa maafisa wasimamizi wa mali alizokuwa nazo Mfalme Daudi. Yonathani mjomba wa Daudi alikuwa mshauri, mtu mwenye ufahamu mkubwa na mwandishi. Yehieli mwana wa Hakmoni alikuwa akiwahudumia wana wa mfalme. Ahithofeli alikuwa mshauri wa mfalme. Hushai Mwarki alikuwa rafiki wa mfalme. Baada ya Ahithofeli, Yehoyada mwana wa Benaya aliingia mahali pake kama mshauri wa mfalme, pamoja na Abiathari. Yoabu alikuwa jemadari wa majeshi ya mfalme.