1 Mambo ya Nyakati 22:2-5
1 Mambo ya Nyakati 22:2-5 Biblia Habari Njema (BHN)
Daudi akatoa amri wageni waliokuwa wanaishi katika nchi ya Israeli wakusanyike, naye akawapangia kazi. Akaweka waashi wachonge vizuri mawe ya kujenga nyumba ya Mungu. Daudi pia akaweka akiba tele ya chuma cha kutengenezea misumari na mafungo ya malango ya nyumba, na akiba tele ya shaba isiyopimika. Mbao za mierezi ambazo Daudi aliletewa na Wasidoni na Watiro zilikuwa hazihesabiki. Daudi akajisemea, “Nyumba ambayo mwanangu Solomoni atamjengea Mwenyezi-Mungu itakuwa ya fahari sana, ya kusifika na tukufu duniani kote. Lakini kwa vile yeye bado angali kijana na bado hana uzoefu mwingi, afadhali nimfanyie matayarisho.” Hivyo basi, Daudi akaweka akiba kubwa sana ya vitu vya ujenzi kabla hajafariki.
1 Mambo ya Nyakati 22:2-5 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi Daudi akaamuru wakusanyike wageni waliokuwa katika nchi ya Israeli; akaweka waashi wachonge mawe ili kujenga nyumba ya Mungu. Daudi akaweka akiba tele ya chuma kwa misumari ya tarabe za malango, na kwa mafungo; na ya shaba akiba tele isiyoweza kupimika; na mierezi isiyo na idadi; kwa kuwa Wasidoni na watu wa Tiro walimletea Daudi mierezi tele. Daudi akasema, Sulemani mwanangu angali ni mchanga bado, na hana uzoefu, nayo nyumba atakayojengewa BWANA haina budi kuwa nzuri mno, yenye sifa na yenye fahari katika nchi zote; kwa hiyo mimi nitaiwekea akiba. Basi Daudi akaweka akiba tele kabla hajafa.
1 Mambo ya Nyakati 22:2-5 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi Daudi akaamuru wakusanyike wageni waliokuwa katika nchi ya Israeli; akaweka waashi wachonge mawe ili kujenga nyumba ya Mungu. Daudi akaweka akiba tele ya chuma kwa misumari ya tarabe za malango, na kwa mafungo; na ya shaba akiba tele isiyo na uzani; na mierezi isiyo na idadi; kwa kuwa Wasidoni na watu wa Tiro wakamletea Daudi mierezi tele. Daudi akasema, Sulemani mwanangu akali ni mchanga bado, na mwororo, nayo nyumba atakayojengewa BWANA haina budi kuwa nzuri mno, yenye sifa na yenye fahari katika nchi zote; kwa hiyo mimi nitaiwekea akiba. Basi Daudi akaweka akiba tele kabla hajafa.
1 Mambo ya Nyakati 22:2-5 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Kwa hiyo Daudi akatoa amri wakusanyike wageni wote walioishi Israeli, na kutoka miongoni mwao, akaweka waashi ili kuchonga mawe kwa ajili ya kujenga nyumba ya Mungu. Daudi akatoa chuma tele ili kutengenezea misumari kwa ajili ya mafungo ya malango ya nyumba na shaba tele isiyopimika. Pia akatoa magogo ya mwerezi yasiyohesabika, kwa kuwa Wasidoni na Watiro walikuwa wamemletea Daudi idadi kubwa ya mierezi. Daudi akasema, “Mwanangu Sulemani bado ni mdogo wa umri na hana uzoefu. Nyumba itakayojengwa kwa ajili ya BWANA inatakiwa iwe yenye uzuri mwingi na sifa na fahari mbele ya mataifa yote. Kwa hiyo nitaifanyia matayarisho.” Daudi akafanya matayarisho makubwa kabla ya kifo chake.