1 Mambo ya Nyakati 21:1-8
1 Mambo ya Nyakati 21:1-8 Biblia Habari Njema (BHN)
Shetani akajitokeza kuwataabisha Waisraeli, akamshawishi Daudii awahesabu watu. Hivyo, Daudi akamwambia Yoabu na wale makamanda wengine, “Nendeni mkawahesabu Waisraeli, kutoka Beer-sheba mpaka Dani. Nileteeni ripoti ili nijue idadi yao.” Lakini Yoabu akasema, “Mwenyezi-Mungu na awaongeze Waisraeli mara mia kuliko walivyo sasa! Bwana wangu mfalme, kwani hawa wote si watumishi wako? Kwa nini basi unataka kufanya jambo ambalo litawatia Waisraeli katika hatia?” Lakini tamko la mfalme lilikuwa na nguvu zaidi dhidi ya Yoabu. Hivyo, Yoabu akaenda katika nchi yote ya Israeli, kisha akarejea Yerusalemu. Yoabu akampelekea mfalme Daudi idadi ya watu: Katika Israeli yote, kulikuwamo wanaume 1,100,000, wenye ujuzi wa kutumia upanga; na katika Yuda kulikuwamo watu 470,000, wenye ujuzi wa kutumia upanga. Lakini Yoabu hakuwahesabu Walawi na Wabenyamini, kwa sababu alichukizwa sana na amri ya mfalme. Mungu hakupendezwa na jambo hilo kwa hiyo akaiadhibu Israeli. Daudi akamwambia Mungu, “Nimetenda dhambi kubwa kwa tendo hili nililolifanya! Lakini nakuomba unisamehe mimi mtumishi wako, kwani nimefanya jambo la kipumbavu kabisa.”
1 Mambo ya Nyakati 21:1-8 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Tena shetani akasimama juu ya Israeli, akamshawishi Daudi kuwahesabu Waisraeli. Basi Daudi akamwambia Yoabu, na wakuu wa watu, Nendeni kawahesabu Israeli toka Beer-sheba mpaka Dani; mkanipashe habari, nipate kujua jumla yao. Naye Yoabu akasema, BWANA na awaongeze watu wake mara mia hesabu yao ilivyo; lakini, bwana wangu mfalme, si wote watumishi wa bwana wangu? Mbona basi bwana wangu analitaka neno hili? Mbona alete hatia kwa Israeli? Lakini neno la mfalme likawa na nguvu juu ya Yoabu. Kwa hiyo Yoabu akaenda zake, akapita kati ya Israeli wote, akafika Yerusalemu. Naye Yoabu akamtolea Daudi jumla ya hesabu ya watu. Na hao wote wa Israeli walikuwa watu milioni moja na laki moja, wenye kufuta panga; na wa Yuda watu elfu mia nne sabini (470,000), wenye kufuta panga. Lakini Lawi na Benyamini hakuwahesabu miongoni mwao; kwa sababu neno la mfalme limemchukiza Yoabu. Neno hilo likawa baya machoni pa Mungu; kwa hiyo akawapiga Israeli. Naye Daudi akamwambia Mungu, Nimekosa sana, kwa kuwa nimelifanya jambo hili; lakini sasa uuondolee mbali, nakusihi, uovu wa mtumishi wako; kwani nimefanya upumbavu kabisa.
1 Mambo ya Nyakati 21:1-8 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Tena shetani akasimama juu ya Israeli, akamshawishi Daudi kuwahesabu Israeli. Basi Daudi akamwambia Yoabu, na wakuu wa watu, Nendeni kawahesabu Israeli toka Beer-sheba mpaka Dani; mkanipashe habari, nipate kujua jumla yao. Naye Yoabu akasema, BWANA na awaongeze watu wake mara mia hesabu yao ilivyo; lakini, bwana wangu mfalme, si wote watumishi wa bwana wangu? Mbona basi bwana wangu analitaka neno hili? Mbona awe sababu ya hatia kwa Israeli? Lakini neno la mfalme likawa na nguvu juu ya Yoabu. Kwa hiyo Yoabu akaenda zake, akapita kati ya Israeli wote, akafika Yerusalemu. Naye Yoabu akamtolea Daudi jumla ya hesabu ya watu. Na hao wote wa Israeli walikuwa watu elfu mara elfu, na mia elfu, wenye kufuta panga; na wa Yuda watu mia nne na sabini elfu, wenye kufuta panga. Lakini Lawi na Benyamini hakuwahesabu miongoni mwao; kwa sababu neno la mfalme limemchukiza Yoabu. Neno hilo likawa baya machoni pa Mungu; kwa hiyo akawapiga Israeli. Naye Daudi akamwambia Mungu, Nimekosa sana, kwa kuwa nimelifanya jambo hili; lakini sasa uuondolee mbali, nakusihi, uovu wa mtumwa wako; kwani nimefanya upumbavu kabisa.
1 Mambo ya Nyakati 21:1-8 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Shetani akainuka dhidi ya Israeli na kumshawishi Daudi ahesabu Waisraeli. Kwa hiyo, Daudi akamwambia Yoabu na majemadari wa jeshi, “Nendeni mkawahesabu Waisraeli kuanzia Beer-Sheba hadi Dani. Kisha mniletee taarifa niweze kufahamu wako wangapi.” Yoabu akajibu, “BWANA na aongeze jeshi lake mara mia na zaidi. Mfalme bwana wangu, kwani hawa wote si raia wa bwana wangu? Kwa nini bwana wangu unataka kufanya hivi? Kwa nini kuleta hatia juu ya Israeli?” Hata hivyo, neno la mfalme likawa na nguvu juu ya Yoabu; kwa hiyo Yoabu akaondoka na kuzunguka Israeli yote, kisha akarudi Yerusalemu. Yoabu akamtolea Daudi idadi ya wapiganaji: Katika Israeli yote kulikuwa na watu milioni moja na elfu mia moja ambao wangeweza kutumia upanga, wakiwemo watu elfu mia nne sabini wa Yuda. Lakini Yoabu hakuwahesabu Walawi na Wabenyamini, kwa sababu alichukizwa sana na amri ya mfalme. Amri hii ilikuwa mbaya machoni pa Mungu pia; hivyo akaiadhibu Israeli. Kisha Daudi akamwambia Mungu, “Nimetenda dhambi kubwa kwa kufanya jambo hili. Sasa, ninakusihi, ondoa hatia ya mtumishi wako. Nimefanya jambo la kipumbavu sana.”