1 Mambo ya Nyakati 13:9-14
1 Mambo ya Nyakati 13:9-14 Biblia Habari Njema (BHN)
Walipofika kwenye uwanja wa kupuria nafaka wa Kidoni, Uza aliunyosha mkono wake kulishikilia sanduku la agano kwa sababu ng'ombe walijikwaa. Mara Mwenyezi-Mungu akamkasirikia Uza kwa kulishika sanduku, akamuua. Uza akafa papo hapo mbele ya Mungu. Daudi alikasirika kwa sababu Mwenyezi-Mungu alimuua Uza akiwa na hasira. Kwa sababu hiyo, mahali hapo huitwa Peres-uza hadi leo. Siku hiyo Daudi akamwogopa Mungu, akasema, “Sasa, nitawezaje kulichukua sanduku la Mungu nyumbani mwangu?” Basi, Daudi hakulichukua sanduku mpaka mji wa Daudi, bali alilipeleka nyumbani kwa Obed-edomu, Mgiti. Sanduku hilo la Mungu lilikaa huko kwa Obed-edomu kwa muda wa miezi mitatu, naye Mwenyezi-Mungu akaibariki nyumba ya Obed-edomu na mali yake yote.
1 Mambo ya Nyakati 13:9-14 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Hata walipofika penye uga wa Nakoni, Uza akaunyosha mkono wake alishike sanduku; kwa maana wale ng'ombe walijikwaa. Ndipo hasira ya BWANA ikawaka juu ya Uza, naye akampiga, kwa sababu alilinyoshea sanduku mkono wake, hadi akafa pale pale mbele za Mungu. Naye Daudi akaona uchungu, kwa kuwa BWANA amemfurikia Uza; akapaita mahali pale Peres-uza hata leo. Naye Daudi akamwogopa Mungu siku ile, akasema, Nitajileteaje sanduku la Mungu kwangu? Basi Daudi hakujichukulia sanduku mjini mwa Daudi, ila akalihamisha kando na kulitia nyumbani kwa Obed-edomu, Mgiti. Sanduku la Mungu likakaa na jamaa ya Obed-edomu, nyumbani mwake, muda wa miezi mitatu; naye BWANA akaibariki nyumba ya Obed-edomu, na yote aliyokuwa nayo.
1 Mambo ya Nyakati 13:9-14 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Hata walipofika penye uga wa Nakoni, Uza akaunyosha mkono wake alishike sanduku; kwa maana wale ng’ombe walikunguwaa. Ndipo hasira ya BWANA ikawaka juu ya Uza, naye akampiga, kwa sababu alilinyoshea sanduku mkono wake, hata akafa pale pale mbele za Mungu. Naye Daudi akaona uchungu, kwa kuwa BWANA amemfurikia Uza; akapaita mahali pale Peres-uza hata leo. Naye Daudi akamwogopa Mungu siku ile, akasema, Nitajileteaje sanduku la Mungu kwangu? Basi Daudi hakujichukulia sanduku mjini mwa Daudi, ila akalihamisha kando na kulitia nyumbani kwa Obed-edomu Mgiti. Sanduku la Mungu likakaa na jamaa ya Obed-edomu, nyumbani mwake, muda wa miezi mitatu; naye BWANA akaibariki nyumba ya Obed-edomu, na yote aliyokuwa nayo.
1 Mambo ya Nyakati 13:9-14 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Walipofika kwenye uwanja wa kupuria nafaka wa Kidoni, Uza akaunyoosha mkono wake ili kulizuia Sanduku, kwa sababu maksai walijikwaa. Hasira ya BWANA ikawaka dhidi ya Uza, akampiga kwa sababu aliuweka mkono wake kwenye Sanduku. Kwa hiyo akafa pale mbele za Mungu. Ndipo Daudi akakasirika kwa sababu ghadhabu ya BWANA ilifurika dhidi ya Uza, mahali pale pakaitwa Peres-Uza hadi leo. Siku ile Daudi akamwogopa Mungu naye akauliza. “Nitawezaje kulichukua Sanduku la Mungu kwangu?” Hakulichukua hilo Sanduku akae nalo katika Mji wa Daudi. Badala yake, akalipeleka nyumbani mwa Obed-Edomu, Mgiti. Sanduku la Mungu likakaa kwa jamaa ya Obed-Edomu, nyumbani mwake kwa miezi mitatu, naye BWANA akaibariki nyumba yake pamoja na kila kitu alichokuwa nacho.