Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Mambo ya Nyakati 13:1-14

1 Mambo ya Nyakati 13:1-14 Biblia Habari Njema (BHN)

Daudi alishauriana na makamanda wa vikosi vya maelfu na vikosi vya mamia, pamoja na viongozi wote. Kisha akawaambia Waisraeli wote waliokusanyika, “Ikiwa mtakubaliana nami, na ikiwa ni mapenzi yake Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, na tufanye hivi: Tutume wajumbe waende wakawaite ndugu zetu waliobaki nchini Israeli, pamoja na makuhani na Walawi walioko katika miji yao na malisho yao, waje wajumuike pamoja nasi. Kisha twende tukalichukue sanduku la agano la Mungu wetu, maana hatukulijali wakati wa utawala wa mfalme Shauli.” Watu wote walikubaliana na pendekezo hilo kwani waliliona kuwa jambo jema. Hivyo, Daudi aliwakusanya Waisraeli wote nchini; toka kijito cha Shihori kilichoko Misri, hadi maingilio ya Hamathi ili kulileta sanduku la Mungu toka Kiriath-yearimu. Daudi, akiandamana na Waisraeli wote, akaenda hadi mjini Baala, yaani Kiriath-yearimu, nchini Yudea, ili kulichukua toka huko sanduku la Mungu linaloitwa kwa jina lake Mwenyezi-Mungu akaaye kwenye kiti chake cha enzi juu ya viumbe vyenye mabawa. Basi, wakalichukua sanduku la Mungu kutoka katika nyumba ya Abinadabu kwa gari jipya. Uza na Ahio waliliendesha gari hilo. Daudi na Waisraeli wote wakawa wanacheza kwa nguvu zao zote, mbele ya Mungu. Waliimba huku wanapiga ala za muziki zilizotengenezwa kwa mvinje: Vinubi, vinanda, matari, matoazi na tarumbeta. Walipofika kwenye uwanja wa kupuria nafaka wa Kidoni, Uza aliunyosha mkono wake kulishikilia sanduku la agano kwa sababu ng'ombe walijikwaa. Mara Mwenyezi-Mungu akamkasirikia Uza kwa kulishika sanduku, akamuua. Uza akafa papo hapo mbele ya Mungu. Daudi alikasirika kwa sababu Mwenyezi-Mungu alimuua Uza akiwa na hasira. Kwa sababu hiyo, mahali hapo huitwa Peres-uza hadi leo. Siku hiyo Daudi akamwogopa Mungu, akasema, “Sasa, nitawezaje kulichukua sanduku la Mungu nyumbani mwangu?” Basi, Daudi hakulichukua sanduku mpaka mji wa Daudi, bali alilipeleka nyumbani kwa Obed-edomu, Mgiti. Sanduku hilo la Mungu lilikaa huko kwa Obed-edomu kwa muda wa miezi mitatu, naye Mwenyezi-Mungu akaibariki nyumba ya Obed-edomu na mali yake yote.

1 Mambo ya Nyakati 13:1-14 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Kisha Daudi akafanya shauri na makamanda wa maelfu, na makamanda wa mamia, naam, na kila kiongozi. Daudi akawaambia jamii yote ya Israeli, Likiwa jema kwenu, tena likiwa limetoka kwa BWANA, Mungu wetu, na tutume watu huku na huku mahali pote kwa ndugu zetu waliosalia katika nchi yote ya Israeli, ambao pamoja nao makuhani na Walawi wamo ndani ya miji yao yenye viunga, ili wakusanyike kwetu; nasi tujirudishie tena sanduku la Mungu wetu; maana hatukulitilia maanani katika siku za Sauli. Nao jamii nzima wakasema ya kwamba watafanya hivyo; kwa kuwa neno hilo lilikuwa jema machoni pa watu wote. Basi Daudi akawakusanya Israeli wote, toka Shihori, kijito cha Misri, hadi pa kuingilia Hamathi, ili walilete sanduku la Mungu kutoka Kiriath-yearimu. Basi Daudi akapanda, yeye na Israeli wote, mpaka Baala, ndio Kiriath-yearimu, ulio wa Yuda, ili kulileta toka huko sanduku la Mungu, BWANA akaaye juu ya makerubi, lililoitwa kwa Jina lake. Wakalipandisha sanduku la Mungu juu ya gari jipya kutoka nyumba ya Abinadabu; na Uza na Ahio wakaliendesha lile gari. Wakacheza Daudi na Israeli wote, mbele za Mungu, kwa nguvu zao zote; na kwa nyimbo na kwa vinubi, na kwa vinanda, na kwa matari, na kwa matoazi, na kwa tarumbeta. Hata walipofika penye uga wa Nakoni, Uza akaunyosha mkono wake alishike sanduku; kwa maana wale ng'ombe walijikwaa. Ndipo hasira ya BWANA ikawaka juu ya Uza, naye akampiga, kwa sababu alilinyoshea sanduku mkono wake, hadi akafa pale pale mbele za Mungu. Naye Daudi akaona uchungu, kwa kuwa BWANA amemfurikia Uza; akapaita mahali pale Peres-uza hata leo. Naye Daudi akamwogopa Mungu siku ile, akasema, Nitajileteaje sanduku la Mungu kwangu? Basi Daudi hakujichukulia sanduku mjini mwa Daudi, ila akalihamisha kando na kulitia nyumbani kwa Obed-edomu, Mgiti. Sanduku la Mungu likakaa na jamaa ya Obed-edomu, nyumbani mwake, muda wa miezi mitatu; naye BWANA akaibariki nyumba ya Obed-edomu, na yote aliyokuwa nayo.

1 Mambo ya Nyakati 13:1-14 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Kisha Daudi akafanya shauri na maakida wa maelfu, na maakida wa mamia, naam, na kila kiongozi. Daudi akawaambia jamii yote ya Israeli, Likiwa jema kwenu, tena likiwa limetoka kwa BWANA, Mungu wetu, na tutume watu huku na huku mahali pote kwa ndugu zetu waliosalia katika nchi yote ya Israeli, ambao pamoja nao makuhani na Walawi wamo ndani ya miji yao yenye viunga, ili wakusanyike kwetu; nasi tujirudishie tena sanduku la Mungu wetu; maana hamkuuliza neno kwa hilo katika siku za Sauli. Nao jamii nzima wakasema ya kwamba watafanya hivyo; kwa kuwa neno hilo lilikuwa jema machoni pa watu wote. Basi Daudi akawakusanya Israeli wote, toka Shihori, kijito cha Misri, hata pa kuingilia Hamathi, ili kwamba walilete sanduku la Mungu kutoka Kiriath-yearimu. Basi Daudi akapanda, yeye na Israeli wote, mpaka Baala, ndio Kiriath-yearimu, ulio wa Yuda, ili kulileta toka huko sanduku la Mungu, BWANA akaaye juu ya makerubi, lililoitwa kwa Jina lake. Wakalipandisha sanduku la Mungu juu ya gari jipya kutoka nyumba ya Abinadabu; na Uza na Ahio wakaliendesha lile gari. Wakacheza Daudi na Israeli wote, mbele za Mungu, kwa nguvu zao zote; na kwa nyimbo na kwa vinubi, na kwa vinanda, na kwa matari, na kwa matoazi, na kwa tarumbeta. Hata walipofika penye uga wa Nakoni, Uza akaunyosha mkono wake alishike sanduku; kwa maana wale ng’ombe walikunguwaa. Ndipo hasira ya BWANA ikawaka juu ya Uza, naye akampiga, kwa sababu alilinyoshea sanduku mkono wake, hata akafa pale pale mbele za Mungu. Naye Daudi akaona uchungu, kwa kuwa BWANA amemfurikia Uza; akapaita mahali pale Peres-uza hata leo. Naye Daudi akamwogopa Mungu siku ile, akasema, Nitajileteaje sanduku la Mungu kwangu? Basi Daudi hakujichukulia sanduku mjini mwa Daudi, ila akalihamisha kando na kulitia nyumbani kwa Obed-edomu Mgiti. Sanduku la Mungu likakaa na jamaa ya Obed-edomu, nyumbani mwake, muda wa miezi mitatu; naye BWANA akaibariki nyumba ya Obed-edomu, na yote aliyokuwa nayo.

1 Mambo ya Nyakati 13:1-14 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

Daudi alishauriana na kila kiongozi wake, majemadari wa maelfu na majemadari wa mamia. Ndipo Daudi akawaambia kusanyiko lote la Israeli, “Mkiona ni vyema, na kama ni mapenzi ya BWANA Mungu wetu, tupeleke ujumbe kwa ndugu zetu wengine walio mbali na walio karibu katika nchi yote ya Israeli, pia kwa makuhani na Walawi walio pamoja nao katika miji yao na maeneo ya malisho ya miji hiyo, waje waungane na sisi. Sisi na tulirudishe Sanduku la Mungu wetu kwetu kwa maana hatukujali wakati wa utawala wa Sauli.” Kusanyiko lote wakakubaliana kufanya hivyo, kwa sababu ilionekana vyema kwa watu wote. Basi Daudi akawakusanya Waisraeli wote, kuanzia Mto Shihori ulioko Misri hadi Lebo-Hamathi, ili kulileta Sanduku la Mungu kutoka Kiriath-Yearimu. Daudi akiwa pamoja na Waisraeli wote wakaenda Baala ya Yuda (yaani Kiriath-Yearimu) kulipandisha Sanduku la Mungu BWANA, yeye anayeketi kwenye kiti cha enzi kati ya makerubi: Sanduku linaloitwa kwa Jina lake. Wakalisafirisha Sanduku la Mungu kwa gari jipya la kukokotwa kutoka nyumba ya Abinadabu; nao Uza na Ahio waliliongoza gari hilo. Daudi pamoja na Waisraeli wote walikuwa wanasifu kwa nguvu zao zote mbele za Mungu, kwa nyimbo na kwa vinubi, zeze, matari, matoazi na tarumbeta. Walipofika kwenye uwanja wa kupuria nafaka wa Kidoni, Uza akaunyoosha mkono wake ili kulizuia Sanduku, kwa sababu maksai walijikwaa. Hasira ya BWANA ikawaka dhidi ya Uza, akampiga kwa sababu aliuweka mkono wake kwenye Sanduku. Kwa hiyo akafa pale mbele za Mungu. Ndipo Daudi akakasirika kwa sababu ghadhabu ya BWANA ilifurika dhidi ya Uza, mahali pale pakaitwa Peres-Uza hadi leo. Siku ile Daudi akamwogopa Mungu naye akauliza. “Nitawezaje kulichukua Sanduku la Mungu kwangu?” Hakulichukua hilo Sanduku akae nalo katika Mji wa Daudi. Badala yake, akalipeleka nyumbani mwa Obed-Edomu, Mgiti. Sanduku la Mungu likakaa kwa jamaa ya Obed-Edomu, nyumbani mwake kwa miezi mitatu, naye BWANA akaibariki nyumba yake pamoja na kila kitu alichokuwa nacho.