1 Mambo ya Nyakati 10:1-10
1 Mambo ya Nyakati 10:1-10 Biblia Habari Njema (BHN)
Basi, Wafilisti walipigana vita dhidi ya Waisraeli; nao Waisraeli walikimbia mbele ya Wafilisti na kuuawa katika mlima wa Gilboa. Lakini Wafilisti wakamzingira Shauli na wanawe, kisha wakawaua Yonathani, Abinadabu na Malki-shua wana wa Shauli. Vita vilikuwa vikali sana dhidi ya Shauli. Wapiga mishale walipomwona walimjeruhi. Ndipo Shauli alipomwambia mtu aliyembebea silaha, “Chomoa upanga wako unichome nife, ili watu hawa wasiotahiriwa wasije wakanidhihaki.” Lakini huyo aliyembebea silaha hakuthubutu; kwa sababu aliogopa sana. Hivyo, Shauli alichukua upanga wake mwenyewe akauangukia. Halafu yule aliyembebea silaha alipoona kuwa Shauli amekufa, naye pia akauangukia upanga wake, akafa. Hivyo ndivyo Shauli alivyokufa, yeye na wanawe watatu, na jamaa yake yote. Nao watu wa Israeli walioishi bondeni walipoona jeshi limewakimbia maadui, na ya kuwa Shauli na wanawe wamekufa, waliihama miji yao wakakimbia. Wafilisti wakaenda na kukaa katika miji hiyo. Kesho yake, Wafilisti walipokwenda kuwateka nyara hao waliouawa, waliikuta maiti ya Shauli na wanawe mlimani Gilboa. Walimvua mavazi, wakachukua kichwa chake pamoja na silaha zake, halafu walituma wajumbe katika nchi yote ya Filistia kutangaza habari njema kwa sanamu zao na watu. Waliziweka silaha za Shauli katika hekalu la miungu yao; kisha wakakitundika kichwa chake katika hekalu la Dagoni.
1 Mambo ya Nyakati 10:1-10 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi Wafilisti wakapigana juu ya Israeli; nao watu wa Israeli wakakimbia mbele ya Wafilisti, wakaanguka wameuawa katika mlima Gilboa. Nao Wafilisti wakamfuatia sana Sauli na wanawe; Wafilisti wakawaua Yonathani, na Abinadabu, na Malkishua, wana wa Sauli. Tena vita vilikuwa vikali sana juu ya Sauli, na wapiga upinde wakampata; hadi akafadhaika sana kwa sababu ya wapiga upinde. Ndipo Sauli akamwambia yule mchukua silaha zake, Futa upanga wako, unichome nao, ili watu hawa wasiotahiriwa wasije wakanisimanga. Lakini huyo mchukua silaha zake akakataa; kwa sababu aliogopa sana. Basi Sauli akautwaa upanga wake, akauangukia. Na mchukua silaha zake alipoona ya kuwa Sauli amekufa, yeye naye akauangukia upanga wake, akafa. Hivyo Sauli akafa, na wanawe watatu; na nyumba yake yote wakafa pamoja. Kisha watu wote wa Israeli, waliokuwa huko bondeni, walipoona ya kuwa wamekimbia, na ya kuwa Sauli na wanawe wamekufa, wakaiacha miji yao, wakakimbia; nao Wafilisti wakaenda wakakaa humo. Hata ikawa siku ya pili yake Wafilisti walipokwenda kuwateka nyara hao waliouawa, walimwona Sauli na wanawe wameanguka juu ya mlima Gilboa. Wakamvua mavazi, wakatwaa kichwa chake, na silaha zake, kisha wakatuma wajumbe kwenda nchi ya Wafilisti pande zote, ili kutangaza habari kwa sanamu zao, na kwa watu. Wakaziweka silaha zake nyumbani mwa miungu yao, wakakitundika kichwa chake nyumbani mwa Dagoni.
1 Mambo ya Nyakati 10:1-10 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi Wafilisti wakapigana juu ya Israeli; nao watu wa Israeli wakakimbia mbele ya Wafilisti, wakaanguka wameuawa katika mlima Gilboa. Nao Wafilisti wakamfuatia sana Sauli na wanawe; Wafilisti wakawaua Yonathani, na Abinadabu, na Malkishua, wana wa Sauli. Tena vita vilikuwa vikali sana juu ya Sauli, na wapiga upinde wakampata; hata akafadhaika sana kwa sababu ya wapiga upinde. Ndipo Sauli akamwambia yule mchukua silaha zake, Futa upanga wako, unichome nao, wasije watu hawa wasiotahiriwa wakanisimanga. Lakini huyo mchukua silaha zake akakataa; kwa sababu aliogopa sana. Basi Sauli akautwaa upanga wake, akauangukia. Na mchukua silaha zake alipoona ya kuwa Sauli amekufa, yeye naye akauangukia upanga wake, akafa. Hivyo Sauli akafa, na wanawe watatu; na nyumba yake yote wakafa pamoja. Kisha watu wote wa Israeli, waliokuwa huko bondeni, walipoona ya kuwa wamekimbia, na ya kuwa Sauli na wanawe wamekufa, wakaiacha miji yao, wakakimbia; nao Wafilisti wakaenda wakakaa humo. Hata ikawa siku ya pili yake Wafilisti walipokwenda kuwateka nyara hao waliouawa, walimwona Sauli na wanawe wameanguka juu ya mlima Gilboa. Wakamvua mavazi, wakamtwalia kichwa, na silaha zake, kisha wakapeleka wajumbe kwenda nchi ya Wafilisti pande zote, ili kutangaza habari kwa sanamu zao, na kwa watu. Wakaziweka silaha zake nyumbani mwa miungu yao, wakakikaza kichwa chake nyumbani mwa Dagoni.
1 Mambo ya Nyakati 10:1-10 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Basi Wafilisti wakapigana na Israeli. Waisraeli wakawakimbia, na wengi wakauawa katika mlima Gilboa. Wafilisti wakawafuatilia Sauli na wanawe kwa karibu, na wakawaua Yonathani, Abinadabu, na Malki-Shua. Mapigano yakawa makali kumzunguka Sauli na wakati wapiga mishale walipompata, wakamjeruhi. Sauli akamwambia mbeba silaha wake, “Futa upanga wako unichome nao, la sivyo hawa watu wasiotahiriwa watakuja na kunidhalilisha.” Lakini mbeba silaha wake akaogopa sana wala hakuweza kufanya hivyo. Kwa hiyo Sauli akachukua upanga wake mwenyewe na kuuangukia. Mbeba silaha wake alipoona kwamba Sauli amekufa, naye pia akauangukia upanga wake akafa. Kwa hiyo Sauli na wanawe watatu wakafa, pamoja na nyumba yake yote. Waisraeli wote waliokuwa bondeni walipoona kwamba jeshi limekimbia na kwamba Sauli na wanawe wamekufa, waliacha miji yao wakakimbia. Nao Wafilisti wakaenda na kuyamiliki. Kesho yake Wafilisti walipokuja kuwavua maiti silaha, walimkuta Sauli na wanawe wameanguka katika Mlima Gilboa. Wakamvua mavazi, wakachukua kichwa chake pamoja na silaha zake, wakawatuma wajumbe katika nchi yote ya Wafilisti kutangaza habari hizi miongoni mwa sanamu zao na watu wao. Waliweka silaha zake katika hekalu la miungu yao, na wakatundika kichwa chake katika hekalu la Dagoni.