Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Waroma 4:1-12

Waroma 4:1-12 BHN

Tuseme nini basi, juu ya Abrahamu baba yetu? Kama Abrahamu alikuwa amefanywa mwadilifu kutokana na bidii yake, basi, anacho kitu cha kujivunia mbele ya Mungu. Kwa maana, Maandiko Matakatifu yasema: “Abrahamu alimwamini Mungu, naye Mungu akamkubali kuwa mwadilifu.” Mfanyakazi hulipwa mshahara; mshahara wake si zawadi bali ni haki yake. Lakini mtu asiyetegemea matendo yake mwenyewe, bali anamwamini Mungu ambaye huwasamehe waovu, basi, Mungu huijali imani ya mtu huyo, akamkubali kuwa mwadilifu. Naye Daudi asema hivi juu ya furaha ya mtu yule ambaye Mungu amemkubali kuwa mwadilifu bila kuyajali matendo yake: “Heri wale waliosamehewa makosa yao ambao makosa yao yamefutwa. Heri mtu yule ambaye Bwana hataziweka dhambi zake katika kumbukumbu.” Je, hiyo ni kwa wale waliotahiriwa tu, ama pia kwa wale wasiotahiriwa? Ni kwa wale wasiotahiriwa pia. Kwa maana tumekwisha sema: “Abrahamu aliamini, naye Mungu akamkubali kuwa mwadilifu.” Je, Abrahamu alikubaliwa kabla ya kutahiriwa, ama baada ya kutahiriwa? Kabla ya kutahiriwa, na si baada ya kutahiriwa. Abrahamu alitahiriwa baadaye, na kutahiriwa huko kulikuwa alama iliyothibitisha kwamba Mungu alimkubali kuwa mwadilifu kwa sababu ya imani yake aliyokuwa nayo kabla ya kutahiriwa. Kwa hiyo, Abrahamu amekuwa baba wa wale wote ambao, ingawa hawakutahiriwa, wamemwamini Mungu, wakafanywa waadilifu. Vilevile yeye ni baba wa wale waliotahiriwa; lakini si kwa kuwa wametahiriwa, bali kwa sababu wanafuata njia ileile ya imani baba yetu Abrahamu aliyofuata kabla ya kutahiriwa.

Soma Waroma 4

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na Waroma 4:1-12

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha